2. Awamu za kujengwa kwa Al-Ka’aba.

SIRA YA MTUME WA ALLAH; FALSAFA NA MAFUNDISHO YAKE”

Mpendwa msomaji wetu-Allah akurehemu-baada ya kujifunza kwa mukhtasari tarekhe ya kuasisiwa na kujengwa kwa mji mtukufu wa Makka, leo tena kwa auni na uwezeshi wake Allah, tuiangalie Al-Ka’aba na awamu za kujengwa kwake. Huku tukizingatia ya kwamba Al-Ka’aba ndio kibula cha Waislamu wote, kwa hivyo basi ni wajibu wa kila muislamu kuijua na kuitambua kuwa ni katika jumla ya matukufu yake Mola. Ili apate kuiadhimisha, kuienzi na kuitukuza, kwa kutambua: “Ndio hivyo! Na anaye tukuza ibada za Allah, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo”.

Kwa jina lake Allah tunasema hali ya kutaraji msaada wake, tukianzia na:

Awamu ya kwanza:

Kwa mujibu wa waandishi wa Tarekhe, kwa mara ya kwanza Al-Ka’aba ilijengwa na Malaika. Hayo ni kwa mujibu wa ilivyo pokewa na Al-Azraqiy-Allah amrehemu. [Rejea AKHBAARU MAKKA 01/02]

Awamu ya pili:

Baada ya kujengwa na Malaika, Al-Ka’aba ilijengwa kwa mara ya pili na baba yetu Mtume Adam-Amani imshukie. Hayo ni kwa mujibu wa riwaya ya Imamu Baihaqiy na wengineo-Allah awarehemu. [Rejea DALAAILUN-NUBUWWAH 02/45]

Awamu ya tatu:

Baada ya Nabii Adam-Amani imshukie, Al-Ka’aba ilijengwa tena na watoto wake. Hayo yanatajwa na riwaya ya Al-Azraqiy na wengineo kutoka kwa Wahab Ibn Manbah. [Rejea AKHBAARU MAKKA 01/08]

Na Imamu Suhailiy-Allah amrehemu-ametaja ya kwamba aliye ijenga katika watoto wa Nabii Adam ni Shiith. [Rejea AR-RAUDHWU AL-UNFU 01/221]

Awamu ya nne:

Hii ndio awamu iliyo jengwa Al-Ka’aba na Mtume Ibrahim na mwanawe Ismail-Amani iwashukie-kama tulivyo eleza katika somo lililo tangulia.

Awamu ya tano na sita:

Al-Ka’aba ilijengwa kwa mara ya tano na sita na Waamaaliqa kisha Wajurhum kama ilivyo nukuliwa na Shaamiy kutokana na riwaya ya Ibn Abi Shaibah na Is-haaq bin Raahawaihi katika Musnad yake. Na Ibn Jariir, Ibn Abi Haatim na Al-Baihaqiy katika Ad-Dalaailu Aliy. Amesema Suhailiy: “Na pamesemwa: Ya kwamba Al-Ka’aba ilijengwa mara moja au mbili katika utawala wa Jurhum, kwa sababu mkondo wa maji uliozesha ukuta wake. Na huo haukuwa ujenzi kamili ila ukarabati wa kuta zilizo pata nyufa. Na aliye fanya ukarabati huo ni Aamir Al-Jaaroud…”. [Rejea AR-RAUDHWU AL-UNFU 01/222]

Awamu ya saba:

Katika awamu hii, Al-Ka’aba ilijengwa na babu yake Mtume aitwaye Quswayi Ibn Kilaab. Amesema Shaamiy-Allah amrehemu: “Hilo limenukuliwa na Zubeir Ibn Bakri katika kitabu An-Nasab…”. [Rejea SUBULUL-HUDAA WAR-RASHAAD 01/192]

Awamu ya nane:

Katika awamu hii ya nane, Makuraishi ndio walio ijenga tena Al-Ka’aba wakati Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akiwa na umri wa miaka thelathini na mitano. Na hili tutakuja kulielezea kwa ukunjufu katika somo linalo jitegemea katika kipengele kinacho elezea: Ushiriki wa Mtume katika ujenzi wa Al-Ka’aba.

Awamu ya tisa:

Aliye ijenga tena Al-Ka’aba katika awamu hii, ni Bwana Abdullah bin Zubeir kama ilivyo pokewa na Imamu Bukhaariy na Muslim na wasio wao. [Rejea SUBULUL-HUDAA WAR-RASHAAD 01/192 – 196]

Awamu ya kumi:

Hajjaaj bin Yusuf ndiye aliye ijenga tena Al-Ka’aba katika awamu ya tisa kwa amri ya khalifa wa Baniy Umayyah; Abdul-Malik bin Marwaan. Hayo ni kwa mujibu wa ilivyo pokewa na Imamu Muslim-Allah amrehemu. [Rejea SAHIH MUSLIM 02/971]

Awamu ya kumi na moja:

Katika awamu hii, Al-Ka’aba ilijengwa na Sultan Muraad Khaan anaye tokana na ukoo wa Uthmaan mnamo mwaka 1040 – 1630 A.H. Hayo yametajwa na Muhammad Aliy bin Alaan katika Risala yake kwa njia ya kunukuu. [Rejea IKHBAARUL-KIRAAM BIAKHBAARIL-MASJIDIL-HARAAM cha Sh. Ahmad bin Muhammad Al-Makkiy]

Na sababu inayo tajwa katika ujenzi huu ni kubomoka kwa baadhi ya sehemu za Al-Ka’aba kutokana na mafuriko makubwa yaliyo tokea zama hizo.

Tanbihi:

Aya za Qur-ani na Hadithi Sahihi zilizo pokewa na Imamu Bukhaariy na wengine-Allah awarehemu-zinafahamisha ya kwamba, wa mwanzo kabisa kuijenga Al-Ka’aba ni Nabii Ibarahim na mwanawe Ismail-Amani iwashukie. Na palikuwa mahala hapo ilipo jengwa Al-Ka’aba ni eneo lenye ukuu na utukufu, lililo juu ya eneo linalo pazunguka. Na lilikuwa ni eneo linalo julikana na Malaika na Mitume walio tangulia na kilikuwa ni kitongoji chenye sharafu (hadhi) na taadhima tangu kale mpaka alipo kuja Nabii Ibrahim akaweka misingi yake na akaijenga.

Tutie nanga hapa kwa juma hili, tumuombe Allah atufahamishe haya tuliyo someshana na atupe uhai na uzima tukutane juma lijalo kwa muendelezo wa darsa hizi za Sira ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *