Utangulizi:
- Neno la Awali
Sifa na Shukurani zote njema ni zake Mola Muumba wetu ambaye ametuambia katika Kitabu chake Kitukufu: “Enyi watu! Hakika Sisi tumekuumbeni kutokana na mwanamume na mwanamke. Na tumekujaalieni kuwa ni mataifa na makabila ili mjuane. Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allah ni huyo aliye mchaMngu zaidi katika nyinyi. Hakika Allah ni Mwenye kujua, Mwenye khabari”. Ewe Mola wa haki! Mrehemu, mpe Amani na mbariki mwanaadamu kamili; Bwana wetu Muhammad pamoja na Aali zake, Maswahaba wake na wote walio muamini na kumfuata.
Kabla ya lolote, tuendelee kuzielekeza shukurani za dhati zenye kusuhubiana na taadhima pamoja na unyenyekevu mkubwa kwa Allah ambaye Yeye ndiye anaye tuwezesha kuungana nawe katika jukwaa letu hili la kila juma. Jukwaa lenye dhima ya kukumbushana yale yaliyo ya muhimu katika dini na maisha yetu ya kila siku, kwa ajili ya ustawi wa maisha yetu haya ya mpito na yale ya milele kule Akhera, ambako huko ndiko yaliko marejeo yetu sote. Tumuombe Allah atudumishie neema hii na atuwezeshe kuishukuru kwa kuyatendea amali yale anayo tuwafikisha kukumbushana, kwani hiyo ndio namna bora kabisa ya kuishukuru neema.
Ndugu yetu mwema, mpenzi na mshiriki wa jukwaa hili-Allah akurehemu-tumuombe Allah atunufaishe sote na fursa hii aliyo tupa kupitia jukwaa letu hili la kila juma. Kwa auni na msaada wake Allah, watumishi na washirika wako katika Dini; WEBSITE UISLAMU, tunakusudia kuanza kukuletea mfululizo wa makala zitakazo izungumzia familia ya Kiislamu; muundo, mjengo na mpango wake.
Sote kwa pamoja tunapaswa kufahamu ya kwamba Familia katika mtazamo wa Uislamu si tu ni njia/chombo cha kuzalisha na kuendeleza kizazi cha wanaadamu na mahala pa kukidhi matamanio ya kijinsia. Bali familia ndio tofali la mwanzo na msingi mkuu ambao jamii kama jengo bali hata taifa hujengwa juu yake. Kwa maneno mengine tunaruhusika kusema ya kwamba kutengenea kwa jamii na hata taifa, kunategemea kwa kiasi kikubwa kutengenea na kunyooka kwa familia zetu. Hivyo ni sawa na kusema, jamii bora na taifa lenye maadili ni zao litokanalo na familia bora iliyo asisiwa juu ya maadili mema na utu bora. Na familia bora haiwezi kupatikana kupitia kanuni zitokanazo na fikra za mwanaadamu; kiumbe dhaifu, bali hujengwa kutokana na sheria ya Allah; Mola Muumba na sheria fafanuzi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kwa muislamu tayari ameshawekea taratibu na sheria ambazo akizifuata zinamdhaminia kupata familia iliyo bora, sheria tayari zipo lake yeye ni kuzifuata tu.
Ni kutokana na umuhimu huo mkubwa wa familia, ndio Qur-ani Tukufu na Sunna zikaiwekea familia sheria, hukumu na taratibu za kuiendesha na kuiongoza. Ni kwa sababu hizo ndipo tunapo isoma Qur-ani, tunakuta imesheheni hukumu za ndoa, talaka, wasiya, mirathi, ulezi, unyonyeshaji, huduma za familia na baki ya hukumu nyingine zinazo hakikisha ubora, uimara na uthabiti wa familia. Ufafanuzi wa hukumu mama hizo, utaupata ndani ya Sunna na Sira ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Dhima kuu ya hukumu zote hizo ni kujenga familia bora, yenye watu wenye utu na dini, ili kutokana na familia hiyo ipatikane jamii bora na hatimaye taifa lenye maadili mema.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-fahamu na ujue ya kwamba mtungo wa familia katika sheria ya Kiislamu, ni utaratibu ulio kamilika, wenye hukumu zinazo suhubiana na mwanaadamu maisha yake yote; tangu kabla ya kuzaliwa kwake, baada ya kuzaliwa na mpaka anaingia kaburini. Hukumu hizo zinachunga maslahi ya mtu binafsi, familia na jamii yake. Si hivyo tu, bali hukumu hizo zimebeba ufumbuzi na suluhisho la matatizo yote yanayo jitokeza katika maisha ya kila siku ya familia.
Makala hizi zitagusia na kuzungumzia kwa kiasi tutakacho jaaliwa na kuwezeshwa na Allah maeneo makuu yafuatayo:
- Ndoa, tutaanza nayo kwa kuzingatia kwamba familia ya Kiislamu hupatikana kupitia ndoa halali na si vinginevyo. Tutaiangazia ndoa na vipengele na vipera vyake vyote chini ya mwangaza wa Qur-ani na Sunna. Kisha
- Watoto, hawa ndio tunda na zao kuu la ndoa. Tutaangalia malezi yao ya kimwili na kiroho na vipengele vyake vyote na wajibu wa wazazi katika kuwalea, kuwaadabisha na kuwaelimisha kwa mujibu wa muongozo, sera na mtaala wa Qur-ani na Sunna ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Kwa ujumla, makala hizi zinalenga kumfahamisha msomaji wake na umma mzima wa Kiislamu, juu ya nyumba (familia) ya Kiislamu yenye mafanikio; nguzo zake, sifa za vifaa vya ujenzi wake, viunganishi vinavyo imarisha na kuzifanya madhubuti nguzo zake. Samani (furniture) zinazo ipamba nyumba hiyo, pambaja (provisions/victuals) zinazo dhamini uhai na ustawi wa wana kaya (wakaazi wa nyumba hiyo).
Naam, Makala hizi zinakusudia kuishi na familia tangu ikiwa ni fikra tu za mmojawapo wa wenza wawili wa maisha, ziambatane nayo (hiyo familia) katika safari yake ndefu mpaka kupatikana kwa matunda yake yanayo tarajiwa kwa idhini yake Allah. Makala hizi hazitaiacha familia peke yake na matatizo yake katika safari hiyo, bali zitasimama nayo kama mlinzi muaminifu, mshauri mtoa nasaha na muongozi mwenye hekima.
Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tunataraji kwa maneno haya ya utangulizi, utakuwa umeelewa na kupata taswira ya kile kinacho lengwa na kukusudiwa na makala hizi zinazo tarajia kukujia hivi punde kwa uwezo wake Allah, kwani ni Yeye pekee ndiye Muwezeshaji wa kila kitu. Tunataraji pia kutoka kwenu dua, ili Allah atuwezeshe kuandika hayo tunayo yakusudia, kwa sababu mada hii ni pana na ni ngumu kuliko uwezo wa akili na maarifa yetu. Mwisho tuseme kama walivyo sema Malaika:
﴿… سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنْتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ٣٢
“Sub-haanaka! Wewe umetakasika! Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyo tufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hikima”. Al-Baqarah [02]:32
Na mwisho kabisa, huu sasa ni wakati wa kumuomba Allah Mtukufu; Mola Mjuzi wa wote, vyote na kila kitu: Tunakuomba Mola Mlezi wetu utupe Ikhlasi (utakasifu wa nia) na wepesi katika utayarishaji na uandishi wa makala hizi. Na uzikunjue fahamu za wasomaji wetu wazisome makala hizi na kisha wazizingatie na kuzifanyia kazi kwa manufaa yao na yetu sisi leo hapa duniani na kesho tutakapo rejea kwako. Na kwa rehema na fadhila zako utujumuishe sisi, wasomaji wetu, wazazi wetu, waalimu na masheikh zetu, wapendwa wetu na jamia Waislamu katika kundi la watakao fuzu kuingia katika pepo yako. Na zishushe rehema na amani kwa mja na Mtume wako; Muhammad, Aali, Sahaba na umma wake woote.
Tukutane juma lijalo katika muendelezo wa Utangulizi kabla ya kuzianza makala zetu, in shaa Allah.
Ni sisi ndugu zenu katika utumishi wa dini;
WEBSITE UISLAMU.