|
Kisha akamteua Qa’aqaa bin Amrou kuwa mjumbe/mpatanishi baina yake
na Twalhah na Zubeir na akamwambia: Nenda kawaitie kwenye masikizano
na jamaa (umoja wa umma) na waase juu ya hatari kubwa ya
faraka/utengano. Halafu tena akamuuliza: Haya hebu niambie,
utawafanya nini wale watako kujia kutoka upande wa wawili hao, ambao
hawana wasia? Akajibu: Tutakutana nao kwa vile/namna uliyo amrisha.
Na wakituletea yale ambayo sisi hatuna rai yako katika kadhia hiyo,
tutajitahidi kwa rai yetu na tutazungumza nao kama tunavyo sikia na
kuona kuwa inafaa. Akasema Sayyidna Aliy: Wewe ndio mstahiki hasa wa
hili. [TAARIKHUT-TWABARIY 03/29, AL-FITNATU WA WAQ’ATUL-JAMAL sah.
145 & AL-KAAMIL 03/122 & AL-MUNTADHWAM 05/75].
Mjumbe wa Amani wa Imamu Aliy; Qa’aqaa akawasili Basrah, akaianza
kazi aliyo tumwa kwa kuonana kwanza na mama wa waumini, akamuuliza:
Ewe mama wa waumini! Ni lipi lililo kuleta kwenye mji huu? Akajibu:
Ewe mwanangu! (Lililo nileta huku) ni kufanya suluhu baina ya watu
(Waislamu). Akamwambia: (Ikiwa hilo ndilo lililo kuleta) basi naomba
uwaitishe Twalhah na Zubeir ili upate kusikiliza maneno yangu na yao.
Akawatumia ujumbe wa wito, nao wakaitika, walipo fika Qa’aqaa
akasema: Mimi nimemuuliza mama wa waumini ni lipi lililo mleta huku,
akasema amekuja kufanya suluhu baina ya watu. Basi je, na nyinyi
mnasemaje (ni lipi lililo kuleteni)? Je, nyinyi mnamfuata mama au
mnamkhalifu? Wakajibu: Tunamfuata. Akawaambia: (Ikiwa msemavyo
ndivyo) basi hebu nielezeni hiyo njia ya usuluhishi, kwani wallah
sisi tukiijua, hapana shaka tutakubali suluhu. Na kama tutaikataa
(kwa kuwa si ya haki), haitofaa (kuwa ndio njia ya suluhu). Wakasema:
(Njia yenyewe ni kuwakamata na kisha kuwahukumu) wauaji wa Uthman,
kwa sababu kuachwa kwa jambo hili (bila ya hatua yoyote stahiki),
kutakuwa ni kuacha (kuifuata) Qur-ani. Akawaambia: Nyinyi mmekwisha
waua wauaji wa Uthman katika watu wa Basrah. Na nyinyi kabla ya
kuwaua watu hao, mlikuwa karibu mno na msimamo (wa haki) kuliko
mlivyo leo, mmewaua watu mia sita! Kwa ajili hiyo basi,
wakaghadhibika kwa ajili yao watu elfu sita, wakajitenga nanyi na
wakajitoa kundini mwenu. Na mkataka (kumuua) Hurquusw bin Zuheir,
akahamiwa dhidi yenu na watu elfu sita. Basi lau mngeli waacha,
mngeli yaacha mnayo yasema na mngeli wapiga vita na wale walio
jitenga nanyi, bila ya shaka mngeli wanusuru na kuwashinda. Basi lile
mlilo lichelea na mkalitia nguvu kwalo jambo hili, hilo ni kubwa
kuliko hilo nionalo mnalichukia. Na ikiwa nyinyi mtawazuilia na mji
huu ukoo wa Mudhwar na Rabeea, watajumuika katika kukupigeni vita na
kukutupeni mkono, ili kuwanusuru hao kama walivyo jumuika hawa dhidi
ya wadau wa tukio hili kubwa na dhambi kubwa.
Mama wa waumini naye akasema: Je, wewe unasemaje? Akajibu: Mimi
ninasema hakika dawa ya jambo hili ni kutulizwa na likitulia watu
wataona athari yake. Na iwapo nyinyi mtafunga baia kwetu, hiyo
itakuwa ni alama ya kheri, bishara, rehema na kudiriki kisasi. Na
ikiwa nyinyi mtakataa ila kulikuza jambo hili na kutumia nguvu, basi
hiyo itakuwa ni alama ya shari. Basi hebu ifadhilisheni mno afya
mtakayo ruzukiwa na kuweni nyinyi funguo za kheri kama mlivyo kuwa.
Na wala msituambalizie kwenye balaa nanyi mkaiingia balaa hiyo, kwa
hivyo ikatupiga mweleka sisi na nyinyi pia. Na ninamuapia Allah haya
ndiyo maneno niyasemayo mimi na ninakuiteni kwayo. Nami ninachelea
kutotimia mpaka Allah aitwae haja yake kwa umma huu, ambao zimekuwa
chache starehe zake na umefikwa na mabalaa yaliyo ufika. Kwani hakika
jambo hili lililo tokea, si kama kadhia ya mtu kumuua mwenzake, wala
kundi la watu kumuua mtu mmoja na wala kabila zima kumuua mtu mmoja.
Wakasema (hadhira): Kwa yakini umesibu (umepatia/umesema ndivyo
khasa) na umetenda wema. Iwapo Aliy atarejea naye akiwa na rai/maoni
kama ya kwako, suala hili litatengenea.
Bwana Qa’aqaa akarejea kwa Imamu Aliy na kumpasha khabari ya
yaliyojiri katika utumwa wake. Khabari hiyo ikampendeza na
kumfurahisha na kaumu ikakurubia kufanya suluhu. Na ujumbe wa watu wa
Basrah ukaja kwa ndugu zao katika watu wa Koufa, ili wapate kuijua
rai ya ndugu zao hao (katika kizungumkuti hiki kilicho wakumba
Waislamu). Wakawakuta watu wote wa Koufa wamekongamana juu ya suluhu
na wala hata kusiwapitikie akilini mwao kupigana na ndugu zao. Basi
wakarejea Basrah na wakawaelezea wakaazi wake khabari hii ya
kufurahisha. Imamu Aliy akainuka kuwakhutubia Waislamu, akaanza kwa
kumuhimidi na kumsifia Allah. Kisha akataja ubaya wa jaahiliya
sambamba na saada/wema wa Uislamu na neema ya Allah juu ya umma kwa
kuufanya kuwa jamaa (moja) chini ya khalifa baada ya Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kisha chini ya khalifa aliye mfuatia
(mtangulizi wake), kisha aliye mfuatia huyo. Kisha tena ndipo lilipo
tokea tukio hili, lililo letwa kwa umma na watu waitakayo na kuiendea
mbio Dunia hii. Watu walio mfanyia hasadi mtu aliye pewa neema na
Allah na wakataka kuurejesha Uislamu na mambo nyuma huko yaliko toka.
Na Allah ni Mtimizaji wa jambo lake. Ehee, fahamuni ya kwamba mimi
ninaingia safarini kesho na kabisa asiingie safarini pamoja nasi
yeyote aliye msaidia Uthman kwa lolote katika mambo ya watu. Waacheni
masafihi wasaidiane wao kwa wao.
Wasabai (wafuasi wa Abdullah bin Sabai) walipo yasikia maneno yaliyo
semwa na Imamu Aliy, wakajuta na wakaona ya kwamba madhara ya suluhu
hiyo yatawarudia wao, kwani kama itatimia suluhu hiyo natija yake
itakuwa ni wao kuuawa. Kwa kuliona hilo, wakashauriana wafanye nini
ili kuizuia suluhu hiyo kufanikiwa. Akasema kiongozi wao aliye
mpotevu na pandikizi katika Uislamu: Enyi watu wangu! Hakika utukufu
wenu umo katika kuwaparaganya watu. Sikilizeni, kesho watakapo kutana
watu, basi nyinyi simikeni (anzisheni) vita na wala msiwape nafasi
hata finyu ya kuchunguza/kutafakari kulikoni. Kwa hivyo basi, wale
ambao nyinyi mko pamoja nao hawatakuwa na njia ya kujizuia kupigana.
Na Allah atamshughulisha Aliy, Zubeir na Twalhah na wote walio na
fikra kama zao (za suluhu), wayasahau yote muyachukiayo. Basi wote
wakakongamana juu ya rai yake na huku watu wakiwa hawajui lolote
linalo endelea.
Kulipo pambazuka, Imamu Aliy akaenda mahala pa maagano na Twalhah na
Zubeir wakamuendea, majeshi mawili hayo yakakutana nje ya mji wa
Basrah. Imamu Aliy akaulizwa na baadhi ya watu wake kuhusiana na nini
cha kufanya. Akajibu: Kufanya suluhu na kuzima kichochea fitina,
huenda Allah akalikusanya jambo la umma huu na kuuepusha na vita.
Akauliza: Na kama wakito liitika hilo? Akajibu: Tutawaacha muda wa
kuwa na wao watatuacha. Akauliza (tena): Na kama hawakutuacha?
Akajibu: Tutajilinda/tutajitetea. Akauliza: Je, wanayo wao haki
katika kadhia hii kama ule wajibu walio nao? Akajibu: Naam (wanayo).
Akainukiwa na mtu mwingine, akauliza: Je, unaona watu hawa wanayo
hoja katika damu hii (ya Sayyidna Uthman), ikiwa wamemkusudia Allah
katika hilo? Akajibu: Naam (wanayo hoja). Akazidi kuuliza: Je, wewe
unaona kuwa unayo haki ya kuakhirisha kisasi? Akajibu: Naam (ninayo).
Akaendelea kuuliza: Basi je, hali yetu na hali yao itakuwaje kesho
iwapo tutaonjwa (na Allah kuingia vitani)? Akajibu: Hakika mimi
ninatarajia kutouawa miongoni mwetu wala miongoni mwao yeyote aliye
utakasa moyo wake kwa ajili ya Allah, ila Allah atamuingiza peponi.
Kisha akasema: “Enyi watu! Wamilikisheni watu hawa mikono na ndimi
zenu, wasije wakatutangulia, kwani mkhasimiwa wa kesho ni yule aliye
khasimiwa leo”.
Halafu tena Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-akawatumia mjumbe Twalhah
na Zubeir awaambie ya kwamba: Ikiwa nyinyi mngali bado na fikra mlizo
kuwa nazo wakati mnaachana na Qa’aqaa, basi jizuieni (bakieni huko
huko) mpaka tuje tupige kambi na tulikague suala hili. Wakaitika.
Kisha akatoka Zubeir baina ya majeshi mawili yale akiwa amempanda
farasi wake, Imamu Aliy akaambiwa: Zubeir huyoo yuwaja! Akasema
Imamu: Ama hakika yeye ni mpapia mno wa watu wawili hao kukumbuka,
pindi anapo tajiwa Allah. Na Twalhah naye akatoka pia, Imamu Aliy
naye akatoka kwenda kukutana nao mpaka zikakabiliana shingo za
wanyama wao. Imamu Aliy akawaambia: Naapa, hakika nyinyi mmekwisha
andaa silaha na watu (askari wapiganaji). Ikiwa nyinyi mmekwisha
andaa udhuru wa kukuokoeni mbele ya Allah, basi mcheni Allah
(muogopeni) na wala msiwe kama yule mwanamke anaye uzongoa uzi wake
baada ya kwisha usokota ukawa mgumu. Je, mimi sikuwa ndugu yenu
katika dini yenu, mkiharimisha kumwagwa damu yangu nami nikiharimisha
damu zenu? Basi je, kuna tukio lililo tokea ambalo limekuhalalishieni
nyinyi kumwaga damu yangu? Twalhah akasema: Wewe uliwakusanya watu
dhidi ya Uthman (wakamuua). Imamu Aliy akawalaani wauaji wa Sayyidna
Uthman, halafu akasema: Hivi wewe haukula baia kwangu? Akajibu:
Nilikubai na ilhali kukiwa na upanga shingoni mwangu. Kisha Imamu
Aliy akamkumbusha Zubeir mambo mengi ili kuulainisha kwayo moyo wake,
akamwambia: Unaikumbuka ile siku uliyo pita ukiwa pamoja na Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa Baniy Ghaanim. Mtume akaniangalia
kisha akacheka nami nikamchekea. Wewe ukamwambia: Mwana wa Abu
Twaalib haachi tu fakhari yake! Mtume wa Allah akakuambia: “Si
mwenye kujifakharisha, kabisa kwa yakini wewe utampiga vita na ilhali
ukiwa unamdhulumu”. [TWABARAANIY katika TAARIKH yake 03/37]
Taathira ya maneno ya Amirul-Muuminina; Sayyidna Aliy-Allah amuwiye
radhi-ikawa ni kurejea kwa Zubeir ilhali akiapa ya kwamba yeye
hatapigana vita na Aliy. Na khususan pale alipo jua ya kwamba Ammaar
bin Yaasir yu pamoja na Aliy na ilhali Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-alikwisha mwambia: “Utauliwa na kikundi kilicho asi”.
Bukhaariy [447] & Muslim [2915, 2916]-Allah awarehemu.
Kama kwamba yeye amekwisha hisi ya kwamba yeye amekosea katika
Ijitihadi yake, kwa kuwa yeye anafanya amali kwa ajili ya Allah, huwa
karibu mno kurejea kwenye haki na kuongokea kwenye swawaabu (ilivyo
ndivyo/sawa) huwa ni kwepesi mno. Basi kila mmoja katika wao akarejea
kwa watu wake na wote wakiwa hawana shaka na suluhu. Na wakalala
usiku wa shwari kwa sababu ya natija ambayo wanakaribia kuifikia.
|