Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

ADABU/TARATIBU NA SUNNA ZA SWAUMU NDANI YA RAMADHANIFA

Faida

ADABU/TARATIBU NA SUNNA ZA SWAUMU NDANI YA RAMADHANI


Ndugu Muislamu uliye wafikiwa na Allah kuingia ndani ya ibada hii tukufu ya swaumu ya mwezi wa Ramadhani, leo tena kwa auni yake Allah Ataadhamiaye tunakutana katika muendelezo wa makala zetu maalumu za Mimbari ya Ramadhani. Mimbarini kwetu leo tutazungumzia Adabu na Sunna za swaumu ya Ramadhani. Wewe kama mfungaji unapaswa kuyajua na kuyafahamu mambo yanayo fungamana na swaumu, ili kupitia mambo hayo swaumu yako iweze kufanikiwa na upate kuhodhi ujira adhimu walio ahidiwa wafungaji.

Ewe ndugu Muislamu!

Fahamu ya kwamba ibada ya swaumu inazo adabu/taratibu ambazo muislamu amesuniwa kujipamba nazo katika kipindi chote cha kuitekeleza ibada hii ya swaumu. Katika jumla ya adabu na sunna hizo ni kama zifuatavyo:

  1. KULA DAKU:

Kula daku ewe ndugu muislamu, kwani huko kula daku ni katika jumla ya taratibu na sunna za swaumu zilizo fundishwa na kutekelezwa na mwenyewe Mtume wa Allah. Na pia kula daku ni agizo la Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kupitia kauli yake: “Kuleni daku, kwani hakika imo ndani ya daku baraka”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Na pia amesema Bwana Mtume: “Kipambanuzi baina ya swaumu yetu na swaumu ya watu wa kitabu, ni kula daku”. Muslimu-Allah amrehemu.

Na bora ya chakula cha daku ni tende, kwani imekuja katika hadithi ya Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Bora ya daku la muumini ni tende”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Na kadhaalika amesema: “Hakika Allah na Malaika wake wanawaswalia walaji daku”. Ibn Hibbaan.

Zitoshe nukuu hizi katika kukuonyesha umuhimu wa kula daku na kukuhimiza juu ya hilo. Basi na jitahidi ewe mfungaji kula daku ijapo kuwa kwa kunywa funda ya maji au kwa kula kokwa ya tende, kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kula daku ni baraka, kwa hivyo msikuache wala kwa mmoja wenu kunywa funda moja la maji, kwani hakika Allah na Malaika wake wanawaswalia walaji wa daku”. Ahmad-Allah amrehemu.


  1. Kuchelewesha kula daku:

Ndugu mfungaji!

Fahamu ya kwamba katika jumla ya Sunna za swaumu ni kuchelewesha kula daku mpaka karibu ya kuingia kwa Alfajiri. Kufanya hivyo hakupungui kuwa ni kumfuata Mtume wako-Rehema na Amani zimshukie-kwani imepokewa katika hadithi ya Anas-Allah amuwiye radhi: “Ya kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na Zaid bin Thaabit walikula daku, walipo maliza kula daku lao, Mtume aliinuka kwenda kuswali, akaswali. Tukamuuliza Anas kulikuwepo na muda gani baina ya kumaliza kwao kula daku na kuingia kwao kwenye swala. Akajibu kiasi cha muda wa mtu kusoma aya khamsini”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Ndugu mfungaji! Katika kuitekeleza kwako Sunna hii, tahadhari kula, kunywa au kufanya lolote katika yanayo funguza swaumu baada ya kuchomoza/kuingia kwa alfajiri, kwani huo ndio mwanzo wa swaumu.


  1. Kuharakia kufuturu:

Ndugu mfungaji!

Ni Sunna kwako kuharakia kufuturu mara tu baada ya kuthibitika kuchwa/kuzama kwa jua, kwani huo ndio mwisho wa swaumu. Sunna hii imethibiti kupitia kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Watu hawataacha kuwa katika kheri muda wa kuharakia kufuturu”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Na ni Sunna mfungaji kufuturu kabla ya kuswali swala ya Maghribi kama ambavyo ni Sunna kufuturu kwa kula tende na akitopata hizo tende basi japo kwa kunywa funda za maji. Na akivikosa vyote hivyo, basi na afuturu kwa kula chakula au kinywaji chochote halali alicho kipata. Hivyo ndivyo alivyo fanya mbora wa wafungaji wote; Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Anas-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akifuturu kwa kula tende mbichi na akizikosa basi kwa tende kavu, kabla ya kuswali. Na akitozipata, basi hupiga funda za maji”. Ahmad & Abu Daawoud-Allah amrehemu.


  1. Kuomba sana dua:

Ndugu muislamu!

Fahamu ya kwamba dua ya mfungaji lillaah hairejeshwi patupu, basi usiipoteze fursa hii adimu na adhimu ambamo ndani yake dua za wafungaji haziruki patupu. Muombe Allah ewe mfungaji, kwa uyatakayo miongoni mwa kheri na neema za Dunia na Akhera. Na muombe Allah ndani ya kipindi chote cha ufungaji mpaka wakati wa kufuturu. Imepokewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Dua tatu hazirejeshwi patupu; dua ya mzazi kwa mwanawe, dua ya mfungaji na dua ya msafiri”. Al-Baihaqiy-Allah amrehemu.

Na ni Sunna kwa mfungaji anapo futuru kuomba kwa dua aliyo kuwa akiiomba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah amuwiye radhi: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa anapo futuru husema: DHAHABA DHWAMAU WAB TALLATIL-URUUQ WA THABATAL-AJRU, INSHAALLAH – kiu kimeondoka, mishipa imelowana na ujira umethibiti pindipo atakapo Allah”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Ndugu mfungaji! Ukiwafikiwa kuyatekeleza mambo haya tuliyo yataja, hiyo itakuwa ni kheri kubwa kwako uliyo wepesishiwa na Allah, basi yapapie kwa maslahi na manufaa yako mwenyewe.


  


 | Tuandikie |