|
Ama wito wa tatu uliomo ndani ya aya hizi, ni kauli ya Allah
Atukukiaye: “ENYI WATU WA KITABU! MBONA MNAZIKATAA ISHARA (aya) ZA
ALLAH ILHALI NYINYI MNASHUHUDIA?”
Yaani: Kwa nini mnazikataa aya za Allah Ataadhamiaye ambazo mnazo
somewa na Mtume wake Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-na ilhali
nyinyi mnaujua ukweli na usahihi wake kwa ujuzi wa yakini, kama ujuzi
wa kushuhudia na kuona kwa macho. Na ilhali pia nyinyi mnajua ya
kwamba yeye Muhammad ni mtume kweli kama mnavyo wajua watoto wenu,
kuwa ni damu zenu.
Na ulizo lililomo ndani ya kauli yake Allah Ataadhamiaye: “MBONA
MNAZIKATAA”, linabeba dhima ya dhana nzima ya kuwaumbua na
kuistaajabu hali yao na ukanushi walio nao wa kuzikataa aya za Allah
pamoja na kuujua ukweli wake.
Na imo ndani ya wito huu ishara inayo onyesha ya kwamba elimu/ujuzi
walio pewa, ulikuwa unawataka na kuwapelekea wao kuharakia kuamini na
sio kuzikufuru aya za Allah. Aya ambazo zinazo fahamisha juu ya
ukweli wake na zimo humo hoja na miujiza aliyo waletea wao
Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Kisha Allah-utakati wa mawi ni wake-akawaelekezea wito wa nne,
akawakataza humo kuchanganya baina ya haki na batili na kuificha
haki, baada ya kuwa alikwisha wakataza kuzikanusha aya, akasema:
“ENYI WATU WA KITABU! MBONA KWELI MNAIVISHA UWONGO, NA KWELI
MNAIFICHA NA ILHALI MNAJUA?”
Yaani: Enyi watu wa kitabu! Kwa nini mnaichanganya haki iliyo wazi
ambayo imetamkwa na vitabu vya mbinguni na akili zilizo salimika.
Mnaichanganya haki hiyo na batili mnayo izua nyinyi wenyewe ili
kuyaridhisha matamanio yenu?
Na katika kukaririwa kwa wito na herufi ulizi, imo ziada ya kuwaumbua
na kuikanusha itikadi na msimamo walio nao na kuidunisha hali yao.
Hivyo ni kwa kuwa wao wamekusanya aina mbaya kabisa ya mambo mabaya
ambayo la mbele na kubwa lao, ni kule kukanusha na kuzikataa kwao aya
za Allah. Na kuchanganya kwao haki na batili na kuificha haki kwa
yule aitakaye.
Na walinganiaji (wahubiri) wa upotevu, wanazo njia mbili wanazo
zitumia katika kuwapotosha watu;
Ya kwanza: Njia ya kuichanganya haki na batili, kiasi cha
kutokujulikana haki ni ipi na batili ni ipi. Na njia hii ndio inayo
ashiriwa na kauli yake Ataadhamiaye: “MBONA KWELI MNAIVISHA
UWONGO”.
Ya pili: Njia ya kuikataa/kuipinga haki na kuificha ili isiweze
kudhihiri na njia hii ndio inayo ashiriwa na kauli yake Ataadhamiaye:
“NA KWELI MNAIFICHA”.
Watu wa kitabu walizitumia njia mbili hizi zote, katika kuwakengeusha
watu na dini ya Uislamu. Kwani baadhi yao walikuwa wakiziawilisha
(wakizifasiri) nukuu (nassi) za vitabu vyao zinazo fahamisha juu ya
ukweli wa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-tafsiri potofu ambayo
huichanganya haki na batili. Wanafanya hivyo ili kuwatia fikra watu
kwamba Muhammad si ndiye mtume aliye kuwa akingojewa kama alivyo
tabiriwa ndani ya Taurati na Injili. Na wengine walikuwa wakitia
shubuha kwenye haki, ili wapate kuwatumbukiza madhaifu wa imani
katika uhemewa na uzingazinga. Na wengine walikuwa wakificha au
kuondosha nassi (nukuu za maneno ya Allah zilizomo katika vitabu vya
mbinguni), zinazo fahamisha ukweli wa Mtume-Rehema na Amani
zimshukie-au zile zisizo wafikiana na matashi/maslahi yao.
Na kauli yake: “NA ILHALI MNAJUA”, hii ni sentensi ya hali.
Yaani: Na ilhali nyinyi mnajua ya kwamba mnacho kificha na mnacho
watatiza watu, ndicho haki na kweli. Au na ilhali nyinyi ni katika
watu wenye ujuzi na elimu ya vitabu vilivvyo tangulia, na wala
hainasibu mtu aliye hivyo kuificha haki na kuichanganya na batili. Na
kijapo kuwa kitendo hicho (cha kuficha haki), huhesabiwa kuwa katika
jumla ya madhambi makubwa hata kama kosa hilo limetendwa na mtu wa
kawaida (asiye mwanachuoni). Basi bila ya shaka kitendo hicho hicho,
pale kitakapo fanywa na mwanachuoni mweledi, mwenye uwezo wa
kupambanua baina ya haki na batili, huwa ni kibaya mno na ufisadi
wake huwa ni mkubwa mno na hatima yake huwa ni ukorofi mkubwa sana.
Ndugu msomaji wetu-Allah akurehemu-kutokana na maelezo yote yaliyo
tangulia, itakubainikia namna ambavyo Qur-ani Tukufu ilivyo tusimulia
namna mbali mbali za shubuhaati za watu wa kitabu. Na kuwarudi kwa
namna inayo batilisha shubuha hizo, kwa kutumia mantiki sahihi na kwa
majadiliano salama, yanayo zikinaisha akili. Na yanayo wazidishia
watu wa haki ithibati zaidi juu ya ithibati yao na imani zaidi juu ya
imani yao waliyo nayo.
Ndugu msomaji mwema-Allah akurehemu-hii ni mifano teule katika jumla
ya mazungumzo/majadiliano, yaliyo jiri pamoja na watu wa kitabu, kama
yalivyo nukuliwa na Qur-ani Tukufu.
|