"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

IBADA YA ITIKAFU

MAANA YA ITIKAFU:

Kilugha neno “Itikafu” lina maana kuu mbili, kama zifuatazo:

Kuzuia, na

Kukaa.

Kisheria “Itikafu” ni: Kitendo cha kukaa msikitini kwa mfumo maalumu uambatanao na nia ya kujikurubisha kwa Allah, kwa kutekeleza ibada mbali mbali.

HUKUMU YA ITIKAFU:

Itikafu ni ibada ya SUNAH katika wakati wo wote na imekokotezwa sana katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Na itikafu kwa upande mwingine inaweza kuchukua hukumu ya UWAJIBU, hii ni iwapo mtu atajiwajibishia mwenyewe.

Mtu atakaposema nimenuia kukaa itikafu siku moja au mbili iwapo nitapata mtoto mathalan. Katika mazingira haya itikafu itakuwa imekwisha kuwa wajibu juu yake.

Kwa sababu ya msingi usemao:(Kutekeleza nadhiri ni wajibu). Imepokelewa kwamba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Mwenye kutia nadhiri ya kumtii Allah, basi na amtii”. Bukhaariy

DALILI YA ITIKAFU:

Ibada hii ya itikafu imethibiti ndani ya Qur-ani Tukufu, suna ya Mtume na Ijmaa ya wanazuoni. Allah Mtukufu anasema:

“…WALA MSICHANGANYIKE NAO, NA HALI MNAKAA ITIKAFU MISIKITINI. HIYO NI MIPAKA YA ALLAH, BASI MSIIKARIBIE…” [2:187]

Yaani Allah Mtukufu anawaamrisha waja wake waumini kutokuwaingilia wake zao katika kipindi chote cha kukaa kwao itikafu msikitini.

Na katika sunah, imepokewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema:

“Mtume-Rehema na amani zimshukie-alikuwa akikaa itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani…” Bukhaariy & Muslim

SHARTI ZA KUSIHI ITIKAFU:

Ili itikafu ya mja isihi kisheria ni wajibu zipatikane sharti zifuatazo:-

Nia, kwa sababu amali zote hufungama na nia kama ilivyothibiti katika hadithi sahihi.

Twahara ya hadathi kubwa. Itikafu haisihi kwa mtu mwenye janaba, mwenye hedhi na mwenye nifasi.

Itikafu ifanyike msikitini kwa ushahidi wa kauli tukufu ya Allah: “…WALA MSICHANGANYIKE NAO, NA HALI MNAKAA ITIKAFU MSIKITINI…”

TANBIHI:

Mwanamke ana haki ya kukaa itikafu msikitini kama aliyo nayo mwanamume. Ila tu haki yake hii ni lazima ipate idhini ya mumewe akiwa ni mke wa mtu. Au walii wake kama si mwanandoa. Na sharti akae itikafu katika mahala palipotengwa kwa ajili ya wanawake msikitini humo. Hii ni kwa sababu wakeze Mtume-Allah awawiye radhi-walikuwa wakikaa itikafu msikitini na katika mahala palipotengwa kwa ajili yao.

YENYE KUBATILISHA ITIKAFU:

Ibada ya itikafu huwa ni batili mbele ya sheria, iwapo muhusika wa ibada hii atafanya mojawapo ya mambo haya:-

Kumuingilia mkewe.

Kutoka msikitini bila ya dharura ya msingi.

Kuondokewa na akili kwa kupatwa na wazimu, kulewa na baki ya mambo mengine.

Kupatwa na hedhi au nifasi.

TANBIHI:

Kutoka msikitini kwa ajili ya kwenda kukidhi haja ya kimaumbile kama kukidhi haja ndogo/kubwa.

Kukoga na kununua mahitaji yake ya lazima mithili ya chakula, kinywaji na mengineyo. Haya yote hayabatilishi ibada ya itikafu, kwani imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa anapokaa itikafu haingii nyumbani ila kwa haja ya mwanadamu”. Bukhaairy & Muslim

YALIYOSUNIWA KUTENDWA NA MKAA ITIKAFU:

Mwenye kukaa itikafu ni suna kwake kukithirisha:-

Ibada mbali mbali za suna.

Kusoma Qur-ani Tukufu.

Kuleta nyiradi mbali mbali (kumdhukuru Allah kwa wingi)

Kuleta istighfaari (kumuomba Allah msamaha wa dhambi).

Kumswalia Bwana Mtume.

Kuomba dua.

Na baki ya mambo mengine ya twaa ambayo yanamkurubisha mja na kumuunga na Mola wake.

USIKU WA CHEO/MTUKUFU (LAYLATUL-QADRI).

Kama ambavyo Allah Mtukufu amemkirimu Mtume wake katika mwezi wa Rajabu kwa kumpeleka safari tukufu ya Israa na Miiraji.

Na kama ambavyo amemkirimu katika mwezi wa Shaabani kwa kumbadilishia Qiblah kutoka msikiti wa Baytul-Maqdis kwenda msikiti mtukufu wa Makah.

Ndivyo hivyo amemkirimu katika mwezi wa Ramadhani kwa kumpa usiku mtukufu. Uliotukuzwa na kupewa hishima ya kushushwa Qur-ani Tukufu ndani yake. Kuhusiana na hili Allah Mtukufu anasema:

“ HAKIKA TUMEITEREMSHA (Qur-ani) KATIKA LAYLATUL-QADRI (usiku wenye hishima kubwa). NA JAMBO GANI LITAKALOKUJULISHA (hata ukaujua) NI NINI HUO USIKU WA LAYLATUL-QADRI? HUO USIKU WA HISHIMA (huo) NI BORA KULIKO MIEZI ELFU. HUTEREMKA MALAIKA NA ROHO MUAMINIFU (JibriIi) KATIKA (usiku) HUO KWA IDHINI YA MOLA WAO KWA KILA JAMBO. NI AMANI (usiku) HUO MPAKA MAPAMBAZUKO YA ALFAJIRI”. [97:1-5]

WAKATI WAKE:

Laylatul-Qadri inatarajiwa sana kuwa inapatikana katika kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani. Ni kwa ajili hii ndio kukasuniwa kukaa itikafu ndani ya kumi hili la mwisho ili kuuzengea usiku huu mtukufu. Usiku ambao ibada ifanywayo humo ni bora zaidi kiujira kuliko ibada ya miezi alfu moja isiyo na Laylatul-Qadri.

Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikaa itikafu katika kumi la mwisho la Ramadhani na akisema: “Izengeeni (itafuteni) Laylatul-Qadri katika kumi la mwisho la Ramadhani”.

Na katika riwaya yake nyingine, Bibi Aysha amesema: “Alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-linapoingia hilo kumi (la mwisho) uhuhisha usiku. Na akawaamsha wakeze na akajipinda na kujifunga kibwebwe (katika kufanya ibada) mpaka Allah alipomfisha. Kisha wakeze wakakaa itikafu baada yake”.

KUUHUHISHA USIKU HUU KWA IBADA:

Kuuhuhisha usiku huu kwa kufanya aina kwa aina za ibada ni suna. Kwa sababu hivyo ndivyo alivyofanya Bwana Mtume, wakeze na maswahaba wake.

Na hekima ya kuuhuhisha usiku huu kwa ibada ni kuikumbuka neema ya Allah kwa waja wake. Neema ya kushushwa Qur-ani Tukufu ndani yake, muongozo wa watu uliosheheni kheri za ulimwengu na akhera yao.

Ikiwa Allah Mtukufu ameutukuza usiku huu wa cheo hata akashusha sura nzima ndani ya Qur-ani kwa jina la usiku huu. Basi ni wajibu wetu sisi kama waislamu kuujua utukufu, cheo, hishima, umuhimu na thamani ya usiku huu kwetu.

Tulionyeshe hili kwa kupupia kuuhuhisha usiku huu kwa kila aina za ibada na kujikurubisha kwa Allah. Muislamu mwenye akili, mkamilifu wa imani ni yule anayeuzengea usiku huu na kuuhuhisha kwa ibada.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakayesimama (kufanya ibada) usiku wa Laylatul-Qadri kwa imani na kutaraji malipo ya Allah, atafutiwa dhambi zake zilizotangulia”. Bukhaariy & Muslim

 

ZAKAATUL-FITRI.

ZAKAATUL-FITRI NI NINI?

Zakaatul-fitri ni kile chakula au thamani ya chakula hicho anachokitoa mtu ndani ya mwezi wa Ramadhani na kuwapa mafakiri na wenye shida kabla ya Eidil-Fitri.

NINI HUKUMU YAKE?

Zakaatul-Fitri ni FARDHI mbele ya kundi kubwa la wanazuoni (jopo la wataalamu wa fani ya Fiq-hi). Ufaradhi huu unatokana na hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema:

“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-AMEFARADHISHA Zakaatul-Fitri ya Ramadhani. Pishi ya tende au pishi ya shayiri, kwa mtumwa na muungwana, mwanamume na mwanamke, mtoto na mkubwa katika waislamu. Na ameamrisha itolewe kabla ya watu kutoka kwenda kuswali (yaani swala ya Eid)”. Bukhaariy & Muslim

Bwana Mtume ameifaradhisha Zakaatul-Fitri na kuamrisha itolewe katika mwaka ule ule uliofaradhishwa swaumu ya Ramadhani. Yaani katika mwezi wa Shaaban, mwaka wa pili wa Hijrah.

NINI FALSAFA/HEKIMA YAKE?

Zakaatul-Fitri imefaradhishwa kwa hekima nyingi, miongoni mwake ni:-

Kuwasaidia wenye shida katika siku ya sikukuu ili furaha ienee kwa watu wote.

Kuunga mapungufu na kuziba makosa yanayoweza kuwa yamemtokea mtu katika swaumu yake.

Haya tunayafahamu kupitia hadithi ya Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema:

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifaradhisha Zakaatul-Fitri ili kumtwaharisha mfungaji kutokana na maneno na matendo machafu. Na ili iwe chakula kwa masikini, atakayeitoa kabla ya swala basi hiyo ndiyo zaka yenye kukubaliwa. Na atakayeitoa baada ya swala, basi hiyo ni sadaka kama sadaka nyinginezo”. Abuu Daawoud

INAMUWAJIBIKIA NANI?

Zakaatul-Fitri ni wajibu kwa kila muislamu, mwenye uwezo wa kutoa hata kama hamiliki kiwango cha zaka ya fardhi. Mwenye kumiliki chakula chake na familia yake cha siku ya Eid, kinachozidi hapo ni wajibu akitoe kama Zakaatul-Fitri.

Atajitolea yeye mwenyewe na watu wote ambao chakula chao cha kila siku kinamuwajibikia yeye.

Hawa ni pamoja na wanawe ambao bado wanamtegemea yeye, wazazi wake, mkewe na wale wote walio chini ya ulezi wake kwa njia ya wajibu na wala sio kwa njia ya ihsaani/ khiari.

NINI KITOLEWACHO?

Zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazoweka wazi alichowaamrisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-maswahaba wake kukitoa kwa ajili ya Zakaatul-Fitri. Miongoni mwa hadithi hizo ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Abuu Saaid Al-khudriy-Allah amuwiye radhi-amesema:

“Tulikuwa wakati alipokuwa miongoni mwetu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-tukimtolea Zakaatul-Fitri kila mkubwa na mdogo. Kibaba cha chakula, au kibaba cha shayiri, au kibaba cha zabibu au kibaba cha maziwa ya unga”. Bukhaariy & Muslim

Na imepokelewa kutoka kwa Abdillah Ibn Tha’alabah-Allah amuwiye radhi-amesema:

“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikhutubu siku moja au mbili kabla ya Eid akasema: Toeni kibaba cha ngano, au kibaba cha tende au cha shayiri. (Mtoleeni) kila muungwana au mtumwa, mkubwa au mtoto”. Abuu Daawoud

Mafaqihi wamesema mazingatio katika kutoa ni kuangalia chakula rasmi cha mahala husika, chakula kitumiwacho katika dhifa na shughuli zao mbali mbali.

Na kibaba kwa kipimo cha kilogramu ni sawa na ¾ ya kilogramu moja. Hiki ndicho kipimo kinachopaswa kutolewa kwa kila kichwa kimoja.

ITOLEWE LINI?

Wakati bora kabisa wa kutoa Zakaatul-Fitri ni ule usiku wa kuamkia siku ya Eid. Na ni wajibu itolewe kabla ya kuswaliwa swala ya Eid.

Na wajibu wa kutoa haupomoki/hauondoki kwa sababu ya kuchelewa kutoa. Bali itakuwa ni deni iliyo katika dhima ya aliyewajibikiwa kutoa.

Na itamlazimu kulipa deni hilo hata mwishoni mwa umri wake, kwa sababu aliwajibikiwa na akafanya uzembe kutoa. Na haisihi kuchelewa kutoa bila ya dharura na ni haramu kisheria.

Kwa sababu ucheleweshaji huu unapelekea kupotea kwa lengo la utoaji wake ambalo ni kuondosha uhitaji wa masikini katika siku ile ya furaha.

Ambao Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amelizungumzia suala lao kwa kusema: “Watosheeni na udhalili wa kuomba katika siku hii”. Yaani siku ya Edil-Fitri.

APEWE NANI?

Wanaopaswa kupewa Zakaatul-Fitri ni wale wale wenye sifa ya kupewa Zaka ya faradhi ambao wametajwa katika kauli yake Allah:

“SADAKA HUPEWA (watu hawa): MAFAKIRI NA MASIKINI NA WANAOZITUMIKIA NA WANAOTIWA NGUVU NYOYO ZAO (juu ya Uislamu) NA KATIKA KUWAPA UUNGWANA WATUMWA NA KATIKA KUWASAIDIA WENYE DENI NA KATIKA (kutengeneza) MAMBO ALIYOAMRISHA ALLAH NA KATIKA (kupewa) WASAFIRI (walioharibikiwa) NI FARDHI INAYOTOKA KWA ALLAH, NA ALLAH NI MJUZI (na) MWENYE HEKIMA”. [9:60]

Lakini masikini na mafakiri ndio walengwa khasa wa Zaakatul-Fitri kuliko mafungu mengine yaliyotajwa.