"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

MINBARI YA IDD

Assalaam Alaykum !

Leo tena Nasaha zako za wiki inakuletea Mimbari ya Eid, karibu ujikumbushe na kuongeza maarifa yako juu ya swala ya Eid na siku yenyewe Eid kwa ujumla.

SWALA YA EID

1) HUKUMU YAKE NA WAKATI WA KUSWALIWA

Swala ya Eid mbili, Eidil-Fitri { Eid ya mfunguo mosi baada ya Ramadhani} na Eidil-adh-haa {Eid ya mfunguo tatu baada ya Hijja}au kama tulivyozoea kuiita "Eid kubwa" na "Eid ndogo" ni SUNNA MUAKKADAH. Mwenyezi Mungu ameamrisha katika kauli yake:

"HAKIKA TUMEKUPA KHERI NYINGI. BASI SWALI KWA AJILI YA MOLA WAKO NA UCHINJE ( kwa ajili ya Mola wako)"[108: 1-2]

Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie- aliswali swala hii na akadumu nayo mpaka anakufa. Na isitoshe amewaamrisha maswahaba bali umma mzima kuiswali na ili kulisisitiza hilo akawapa ruhusa wanawake na watoto kuhudhuria swala hii.

Swala hii ni nembo miongoni mwa nembo za uislamu ambayo hudhihirisha imani na ucha Mungu.

Tukivipekuwa vitabu vya historia hatutashindwa kuona kuwa Eid ya kwanza kuswaliwa na Bwana Mtume ilikuwa ni Eidil-Fitri katika mwaka wa pili wa Hijra.

Wakati wa swala ya Eid huingia tangu kuinuka kwa jua mpaka kupinduka kwake kwake yaani baina ya saa 1:30 Asubuhi mapaka saa 6:00 Mchana.

Katika kipindi chote hiki inaweza kuswaliwa swala ya Eid, LAKINI ni vema / bora swaala ya Eidil-Adh-haa ikaswaliwa mwanzo wa wakati yaani saa 1:30. Hii ni kwa ajili ya kuwapa watu fursa ya kutosha kwenda kuchinja wanyama wao wa UDHUHIA. Swala ya Eidil - Fitri ni ni kinyume chake, hii ni bora ikacheleweshwa kuswaliwa ili kuwapa watu fursa ya kuweza kutoa zakatul-fitri (sadaka ya Fitri).

Hivyo ndivyo alivyokuwa akifanya Bwana Mtume. Amesema Jundub-Allah amuwiye radhi –

"Mtume-Rehema na Amani zimshukie - alikuwa akituswalisha swala ya Eidil-Fitri il-hali jua likiwa limepanda kiasi cha (mtupo wa) mikuki miwili na swala ya Eidil-Adh-haa kiasi cha mkuki mmoja". Al-Haafidh.

2) ADABU/ TARATIBU ZINAZOTAKIWA KUFUATWA KATIKA SIKU YA EID.

  1. Muislamu anatakiwa katika siku za Eid akoge, ajitie manukato (mwanamume) na avae nguo nzuri za kupendeza. Mwongozo huu unatokana na kauli ya Anas Ibn Maalik - Allah amuwiye radhi,

" Alituamrisha Mtume wa Allah - Rehema Na Amani zimshukie - katika Eid zote mbili tuvae nguo nzuri sana tuwezazo (kuzipata), tujitie manukato mazuri sana tuyapatayo na tuchinje mnyama mwenye thamani kubwa tuwezavyo" Al – Haakim. " Na Mtume wa Allah - Rehema na Amani zimshukie - alikuwa akivaa burda (kishali) cha rangi ya wino (light blue) katika Eid zote" As - Shaafiy.

  1. Ni suna kula kwanza kabla ya kwenda kuswali swala ya Eidil-Fitri kama ambavyo si suna mtu kula kabla ya kuswali swala ya Eidil - Adh-haa bali suna ni kuswali kwanza ndipo ale kama ilivyithibitishwa kutoka kwa Bwana Mtume.

 

  1. Kuleta Takbira kwa wingi tangu usiku wa Eid zote mbili. Takbira za Eidil - Fitri huendelea mpaka baada ya swala tu, muda wake huwa umeisha. Ama zile za Eidil-Adh-haa hudumu mpaka siku ya mwisho ya kuanikwa nyama {Alasiri ya mwezi 13 - Mfunguo tatu}

Takbira za Eid ni kusema:-

ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR ALLAAHU AKBAR . LAA ILAAHA ILLAL-LAAH WALLAAHU AKBAR . ALLAAHU AKBAR WALILLAAHIL-HAMDU. ALLAAHU AKBAR KABIYRAA . WAL-HAMDU LILLAHI KATHIYRAA. WASUB-HAANALLAAHI BUKRATAN WA ASWIYLAA. LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU WAHDAU. SWADAQA WA’ADAU. WANASWARA ‘ ABDAU . WA A’AZZA JUNDAU WAHAZAMAL - AHZAABU WAHDAU. LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU. WALAA NA-'BUDU ILLAA IYYAAU MUKHLISWIYNA LAHUD - DIYN WALAU KARIHAL- KAAFIRUUN.

ALLAAHUMMA SWALLI ALAA SAYYIDNAA MUHAMMAD WA ALAA AALI SAYYIDNAA MUHAMMAD . WA ALAA ASW-HAA BI SAYYIDNAA MUHAMMAD WA ALAA ANSWAARI SAYYIDNAA MUHAMMAD WA ALAA DHURRIYATI SAYYDINAA MUHAMMAD . WASALLIM TASLIYMAN KATHIRYRAA.

Takbira hizi ni kwa mujibu wa Mwenyezi Mungu Mtukufu;

" NA MTAJENI ALLAH KATIKA ZILE SIKU ZINAZOHISABIWA" [ 2; 203 ]

Na kauli yake ,

"HAKIKA AMEKWISHAFAULU ALIYEJITAKASA (na mabaya ) . AKAKUMBUKA JINA LA MOLA WAKE NA AKASALI" [ 87; 14 -15 ]

Na kauli yake;

"....NA KUMTUKUZA ALLAH KWA KUWA AMEKUONGOZENI ...." [ 2: 185 ]

  1. Ni suna kwenda msikitini kwa njia moja na kurudi kwa njia nyingine isiyokuwa ile ya kwendea. Amesema Jaabir - Allah amuwiye radhi –

" Alikuwa Mtume - Rehema na Amani zimshukie - alibadili njia inapokuwa siku ya Eid " Bukhaariy

  1. Ni suna swala ya Eid kuswaliwa uwanjani mahali pa wazi ila kama kuna dharura ya mvua na kadhalika, hapo ndipo inaweza kuswaliwa msikitini. Hii inatokana na kudumu kwake Mtume kuiswali jangwani kama ilivyopokewa na Bukhaariy na Muslim.

 

  1. Kadhalika ni suna waislamu kupeana mikono siku ya Eid. Muislamu amwambie nduguye ( TAQABBALALAAHU MINNAA WA MINKA ) (Mwenyezi Mungu atutakabalie sisi na nyinyi ibada yetu.). Hivi ndivyo ilivyopokelewa kwamba maswahaba wa Mtume wlikuwa wanapokutana siku ya Eid huambizana:

           " Taqabbalal-laahu Minnaa waminkum" Ahmad.

  1. Hakuna makosa kutanua katika malaji, vinjwaji na pumbao la halali,. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume - Rehema na Amani zimshukie-aliyosema katika Eidil - Adh-haa. " Masiku ya kuanikwa nyama ni masiku ya kula na kunywa na kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu" Muslim.

Masiku ya kuanikwa nyama ni mwezi 11, mwezi 12 na mwezi 13- Mfunguo 3. Na kwa kauli ya Anas - Allah amuwiye radhi; Mtume wa Rehema na Amani zimshukie - alipofika Madina aliwakuta wana siku mbili maalum za kucheza na kufurahi. Mtume akawaambia;

" Mwenyezi Mungu amekubadilishieni siku mbili hizo kwa ( kukupeni ) siku mbili bora zaidi kuliko hizo; siku ya Eidil- Fitri na Eidil - Adh-haa" Nasaai.

Na kwa kauli ya Mtume alipomwambia Abu Bakri alipowakemea wajakazi wawili waliokuwa wakiimba mashairi nyumbani kwa Mama Aysha siku ya Eid:

"Ewe Abu Bakr kila watu wana sikukuu yao, na leo ni sikukuu yetu" Bukhaariy

MAWAIDHA YA EID

Ndugu zanguni waislamu, Asslaam Alaykum!

Himda njema zote zinamstahikia Allah na Rehema na Amani zimuendee Nabii Muhammad, Maswahaba na aali zake.

Ama baad

Ndugu zanguni waislamu, sote tunakubaliana kwamba siku ya Eid ni siku ya furaha, ni siku ambayo mmehalalishiwa kula na kunywa mchana baada ya kumalizika kwa mfungo mtukufu wa Ramadhani. Ni siku ya watu kuvaa vizuri.

Hebu itegee sikio pamoja nami kauli yake Mtume - Rehema na Amani zimshukie:

" Inapokuwa siku ya Eidil-Fitry, malaika hukaa mwanzoni mwa njia wakalingana: Damkeni enyi waislamu, enendeni kwa Mola Mkarimu aneemeshaye kisha hulipa thawabu juu ya neema hizo.

Mmeamrishwa kusimama usiku kuswali (taraweh) mkasimama na mliamrishwa kufunga mchana mkafunga. Na mkamtii Mola wenu pokeeni zawadi zenu.

Wanapomaliza kuswali hunadi mwenye kunadi. Eeh hakika Mola wenu amekwisha kusameheni, basi rejeeni majumbani mwenu hali ya kuwa mmeongoka. Nayo ni siku ya zawadi na siku hii huitwa mbinguni siku ya zawadi"

Siku ya Eid ni siku ya mahafali. Waislamu wamehitimu mafunzo yao ya mwezi mmoja katika Chuo Kikuu cha Ucha -Mungu (Swaumu).

Leo ndio siku ya kukabidhiwa na kutunukiwa vyeti wahitimu na leo ndio siku kila mtu atajua matokeo ya mafunzo yake kama amefaulu au amefeli. Hili litajulikana kutokana na namna atakavyoisherehekea siku yake hii ya Eid.

Ndugu zanguni wapenzi, Katika kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani tunapata fundisho moja kubwa sana, nalo ni kwamba , kama vile tulivyoshuhudia mwanzo wa mwezi wa Ramadhani na leo hii tunashuhudia kumalizika kwake.

Tujiulize na tutafakari hili linaashiria nini ? Ikiwa hili linatoa ishara ya kitu/jambo, basi jambo hilo litakuwa si jingine bali ni kwamba tujue kwa yakini kuwa kila chenye mwanzo hakina budi kuwa na mwisho isipokuwa ALLAH pekee YEYE ndiye asiye na mwanzo wala mwisho.

Tuukiri na kuukubali ukweli huu usiopingika, tujue na tufahamu kuwa kama ambavyo kila mmoja wetu alikuwa na siku yake ya kuja kwake katika ulimwengu huu, kadhalika anayo siku imngojeayo ya kuondoka kutoka katika ulimwengu huu umalizikao. Tusome na tuzingatie:

"KILA KILICHOKO JUU YAKE (ardhi na mbingu) KITATOWEKA (kitaondoka). INABAKI DHATI YA MOLA WAKO ( tu mwenyewe) MWENYE UTUKUFU NA HISHIMA" [55: 26-27]

Ndugu zanguni, tujiandae vema na siku hii ngumu, nzito ambayo haikwepeki, hatuna budi tutakutana nayo.

Siku hii ndio mwanzo wa safari ya kuhudhurishwa mbele ya mahakama yenye uadilifu, haki na usawa, kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa kwa mujibu wa amali zetu tulizozitenda hapa duniani bila kudhulumiwa mtu. Kinachofuata baada ya hapo;

"...KUNDI MOJA LITAKUWA PEPONI NA KUNDI JINGINE MOTONI" [ 42:7].

Kuwa katika kundi la peponi au motoni , huu ni uchaguzi wako mwenyewe na hili litategemea jinsi utakavyozichanga karata za maisha yako katika ulimwengu huu. Utavuna pepo/moto kwa akili, nguvu na mali yako mwenyewe. Tuiogope ndugu zanguni siku hii;

" NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOCHUMA; NAO HAWATADHULUMIWA[2:281]

Naam, mwezi wa Ramadhani umemalizika na bila shaka utatushuhudia mbele za Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa yote mema / mabaya tuliyoyatenda ndani yake.

Katika mwezi huu mtukufu sote tumeshuhudia jinsi misikiti ilivyokuwa ikijaa waumini katika swala zote za fardhi hata swala nzito na ngumu ya alfajiri.

Misikiti ilikuwa ikiamrishwa kwa kusoma sana Qur-ani Tukufu, na kudhukuriwa sana Allah. Takriban wakati wote usiku na mchana utawakuta waumini misikitini wakifanya namna kwa namna ibada , na utaviona vikundi vya ilmu, waumini wasomeshana.

Yote haya tumeyaona ndani ya mwezi wa Ramadhani, leo mwezi umemalizika na yote yamemalizika, huyaoni tena hadi Ramadhani ya mwakani panapo uhai na majaliwa.

Eh! Hasara, msiba na majuto yaliyoje kwa waja hawa, kana kwamba walikuwa wanauabudu mwezi wa Ramadhani na sio mola wa mwezi wa Ramadhani. Mwezi ukiisha hakuna tena kuswali, kufunga, kusoma Qur-ani wala.... wala....

Hii ni dalili na ishara ya wazi ya kutokukubaliwa swaumu na amali zao nyingine walizozitenda ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Kwani amali ya mja ikikubaliwa na kupokelewa, Mola humzidishia mja huyo taufiki na kutengenea, hapo ndipo utamuona kila siku anazidi kuendelea kumtii Mola wake.

Ndugu zangu waislamu, ni muhali kabisa kwa mtu aliyefunga kwa ikhlaaswi, halafu leo baada ya swala ya Eid akawa anauaga msikiti, haswali tena hadi Ramadhani ya mwakani ambayo hana dhamana nayo.

Ikiwa hivi swaumu ya mja huyu haikumfikisha kwenye lengo lake ambalo ni kumuandaa mja kuwa mcha Mungu. Tusome na tuzingatie

" ENYI MLIOAMINI ! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH" [2:183].

Ni ukweli usiopingika kwamba mtu hawezi kuwa mcha Mungu bila ya kushikamana na swala tano.

Ndugu zanguni, Mwenyezi Mungu aliwaamrisha Malaika pamoja na Iblisi ambaye alikuwamo kundini wamsujudie Nabii Adamu - Rehema na Amani zimshukie - hali ya kumuamkia.

Iblisi kwa ushupavu na upasito aliokuwa nao alikataa kuitekeleza amri ya Mola wake. Ni kwa sababu hii tu, Mwenyezi Mungu akamfukuza na kumtoa huko alikokuwa na akamtenga mbali na rehema zake (akamlaani) na kesho akhera ataingia motoni ikiwa ni jazaa ya inadi na kibri chake.

Basi wewe ndugu yangu mpenzi usotaka kuswali, hujioni kuwa wewe ni mbaya zaidi kuliko Iblisi ?

Pengine utauliza kwanini ? Hii ni kwa sababu Iblisi alikataa kumsujudia Nabii Adamu (sijida ya maamkizi si ya ibada), wewe usioswali una kataa kusujudia sijida ya ibada ya yule aliye muumba Nabii Adamu. Iblisi alikataa kusujudia mara moja tu, wewe usioswali unakataa kusujudia mara 34 kila siku.

Hebu angalia tena adhabu aliyopewa Iblisi kwa kuacha sijida moja tu, hii inamaanisha mwenye kuacha sijida 34 kila siku anastahiki kupata adhabu kali zidi kuliko aliyopewa Iblisi, sikwambii tena usioswali wiki au zaidi.

Eeh ! Ndugu yangu kiumbe dhaifu wee! Ionee huruma nafsi yako, acha ukaidi, huiwezi adhabu ya Mola wako. Badili mwenendo wako sasa kabla hujachelewa. Tusome na tuzingatie

"....NA BILA SHAKA ADHABU YA AKHERA NI KALI ZAIDI NA INAYOENDELEA SANA" [ 20:127 ]

Pia kuna khatari kubwa ya kuwa kafiri mtu asioswali. Isikize kwa makini kauli hii ya Bwana Mtume - Rehema na Amani zimshukie " YE YOTE atakaye acha swala kwa makusudi, bila shaka atakuwa amekufuru".

Ndugu zanguni waislamu inasikitisha sana jinsi waislamu tunavyoisherehekea sikukuu. Siku ya Eid ndiyo siku ambayo waislamu wenyewe wanautukanisha uislamu na kuudhihirishia ulimwengu kwamba akthari/aghlabu ya wafanyao mabaya ni waislamu.

Mtu alikuwa hawezi kukesha msikitini kufanya ibada, siku ya Eid atakesha kwenye ulevi, atakunywa hadi atajimwagia, eti anasherehekea kumalizika kwa mfungo mtukufu wa Ramadhani, Sub-hanallah, na huyu si mwingine bali ni yuleyule muislamu tuliyekuwa naye msikitini katika kipindi chote cha Ramadhani.

Huyu haisherehekei Eid bali anausherehekea moto wa Jehannam na huyu ndiye mtu aliyefeli vibaya kabisa katika mafunzo yake katika Chuo Kikuu cha Ucha Mungu (swaumu) Siku ya Eid ndiyo siku ambayo utaona madada zetu wamevaa mavazi ya ajabu ajabu na kuwa kama mbuzi wasio na mchunga kwa kuuza utu wao.

Ili muradi siku ya Eid, watu watashindana katika kumuasi Mola wao. Wote hawa nawaasa kwa kauli hii ya Allah

" AMA YULE ALIYEASI NA AKAPENDA ZAIDI ( akayafadhilisha maisha ) YA DUNIA. BASI KWA HAKIKA JAHANAMU NDIYO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE NA AMA YULE ALIYEOGOPA KSIMAMISHWA MBELE YA MOLA WAKE, AKAIKATAZA NAFSI YAKE NA MATAMANIO (maovu) BASI (huyo) PEPO NDIO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE. [ 79: 37-41]

Ndugu zangu waislamu funga ya Ramadhani imemalizika LAKINI hii haiaaamaanishi kuwa muislamu hana tena fursa ya kufunga hadi Ramadhani ya mwakani. La hasha bali anayo fursa ya kujipendekeza na kujikurubisha zaidi kwa Molaa wake kwa kufunga funga mbalimbali za suna.

 Miongoni mwa funga hizo za suna ni kufunga siku sita za mfunguo mosi (shawwal). Imepokelewa hadithi na Abu Ayyuub - Allah amuwiye radhi- kwamba Mtume - Rehema na Amani zimshukie - amesema,

" Atakayeufunga mwezi wa Ramadhani, halafu akaufuatishia siku sita za mfunguo mosi itakuwa kama kufunga mwaka mzima" Muslim.

Ndugu zanguni, hayo ndiyo malipo na ujira adhimu wa funga ya Ramadhani iambatanayo na funga ya siku sita za mfunguo mosi.

Tumeweza kufunga mwezi mzima, tutashindwa kufunga siku sita! Ikiwa tuna nia ya kujipendekeza na kujikurubisha kwa Mola wetu Mtukufu hatutashindwa haya shime ndugu zanguni.

Mwisho tunakutakieni Waislamu wote popote mlipo ulimwenguni kheri, baraka,amani furaha na radhi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika sikukuu yenu hii ya Eid. Tunawapongezeni nyote kwa kusema;

Wasalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakatu.