"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

UNYENYEKEVU

Unyenyekevu unapatikanaje ndani ya swala?

Huoni kuwa ni upeo wa unyenyekevu usio ni mithali pale muislamu anapokiweka mavumbini kiungo chake kitukufu “Uso” kumsujudia Mola wake.

Tena wakalingana sawa katika unyenyekevu huu watu wote, wakubwa kwa wadogo, wanaume na wanawake, mabwana na watwana.

Hapana kichwa cho chote kinachoweza kuwa juu ya kichwa kingine katika rukuu na sujudi.

Ndani ya swala katika majumba ya Allah (Misikiti) mwanadamu hupata heshima na utukufu kuangalia matabaka na nyadhifa zao.

Swala kuwakumbusha viongozi/watawala usawa wao na wananchi wa kawaida pale wanaposimama safu moja, bega kwa bega, mguu kwa mguu, wakiwa nyuma ya Imamu mmoja.

 Mbali na nguzo tatu hizo, nguvu, upendo na unyenyekevu, swala ina hekima na manufaa mengi yasiyomalizwa kuzungumzwa na maneno ya kinywa cha binadamu mpungufu.

Katika jumla ya falsafa ya swala ni kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu juu ya neema zake zisizodhibitika alizotuneemesha :

“…………NA KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH, HAMTAWEZA KUZIHISABU BILA SHAKA MWANADHAMU NI DHALIMU MKUBWA ASIYE SHUKRANI (mwizi wa fadhila) “ (14:34).

Pia swala hujenga mahusiano na mawasiliano mazuri baina ya kiumbe (mja) na Muumba wake kwani mja huwa karibu zaidi na Mola wake anapokuwa ndani ya swala, ambamo humo hupata raha na utulivu wa moyo.

 Kadhalika swala humfinyanga muislamu kuwa ni mtu mwenye nidhamu.

Hii ni kwa sababu ndani ya swala muislamu hulazimika kumfuata Imamu wake kwa utaratibu maalumu ili swala yake ikubaliwe kitendo cha kurudiarudia utaratibu huu ndio humjengea muislamu tabia ya kuwa na nidhamu.

 Katika jumla ya mambo yanayoonyesha kwamba swala ina athari kubwa na nzuri katika kuwalea wanadamu na kudumisha tabia na maadili mema ni kitendo cha Nabii Ibrahim-Allah amshushie Amani- kumuomba Mola wake amjaalie yeye na kizazi chake kuwa ni wasimamishaji wa swala, aliposema:

MOLA WANGU! NIJAALIE NIWE MSIMAMISHAJI SWALA, NA KIZAZI CHANGU (pia  kiwe hivi) MOLA WETU ! NA UPOKEE MAOMBI YANGU”  (14:40).

 Swala ndio zana ya kumkumbusha mwanadamu hakika na ukweli kuwa yeye ni mja na mtumwa anayemilikiwa na Allah.

Aendelee kuukiri ukweli huu usio na mjadala, kila harakati na mishughulisho ya maisha inapomsahaulisha ukweli huu, swala hujitokeza na kumkumbusha tena, naye husema awapo ndani ya swala!

‘ WEWE TU NDIYE TUNAYEKUABUDU NA WEWE TU NDIYE TUNAYEKUOMBA MSAADA’ (1:5).

Kwa hiyo, swala humfanya mwanadamu kuyakinisha kuwa hakuna msaidizi wala mneemeshaji wa kweli ila ni Allah pekee.

Hata kama ataona katika maisha yake ya kila siku vitu/mambo/sababu ambazo kwa sura ya nje huonekana kuwa ndizo zinazomsaidia na kumneemesha.

Lakini ukweli unabakia pale pale  kwamba ni Allah pekee ndiye aliyemuumbia vitu, mambo au sababu hizo zote.

 Kazi inaposahaulisha mwanadamu na kumfanya aamini kuwa kazi ndio inayompatia riziki na kuisahau nguvu iliyo nyuma ya kazi, hapo ndipo huja swala na kufanya kazi yake.

 Ikamkumbusha kuwa msababishaji na muunganishaji wa riziki na kazi ni Allah pekee ambaye ni yeye tu ndiye mpaji riziki, Mneemeshaji, Msaidizi, Mwenye kudhuru na kunufaisha, Mtoa uhai na Mfishaji, KWA YAKINI ALLAH NDIYE MTOAJI WA RIZIKI MWENYE NGUVU, MADHUBUTI “ (51:58).