"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

UTANGULIZI

i) MAANA YA UDHU :

Tamko/Neno udhu linafasirika katika lugha ya kiarabu kama wema, uzuri na ung'avu.

Ama maana ya udhu katika istilahi ya wanazuoni wa fani ya Fiq-hi;

udhu ni twahara inayotumia maji, twahara hii inahusisha viungo maalum vya mwili, baadhi yake hukoshwa kama mikono, uso na miguu na vingine hupakwa maji kama vile kichwa.

 

ii) HUKUMU YA UDHU NA DALILI YAKE :

Udhu kwa maana tulivyoieleza ni FARDHI/WAJIBU katika kusihi na kukubalika kwa ibada ya swala kwani hapana swala bila ya udhu kwa maneno mengine, tunaruhusika kusema kuwa udhu ndio msingi mkuu na imara wa ibada ya swala.

Udhu ndani ya Qur-ani unapatikana katika kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema :


"ENYI MLIOAMINI! MNAPOTAKA KUSWALI, BASI OSHENI NYUSO ZENU NA MIKONO YENU MPAKA VIFUNDONI, NA MPAKE VICHWA VYENU, NA (osheni) MIGUU YENU MPAKA VIFUNDONI ..." [5:6]

Ama dalili na ushahidi wa udhu katika suna ni ile kauli yake Mtume wa Mwenyezi Mungu aliposema "Allah haikubali swala ya mmoja wenu atakapohuduthu/atakapotengukiwa na udhu mpaka atawadhe (tena)" Bukhariy na Muslim.

 

iii) UBORA/FADHILA ZA UDHU :

Zimepokelewa hadithi kadhaa kutoka kwa Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie - katika kutaja na kuonyesha ubora na fadhila za udhu. Miongoni mwa hadithi hizo ni hizi zifuatazo :

1.Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na Amani zimshukie –

 "Yeyote atakayetawadha vyema (kama alivyoelekezwa na sheria), hutoka madhambi yake mwilini mpaka chini ya kucha zake" Muslim.

2. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu - Rehema na Amani zimshukie - :

"Hakika umati wangu wataitwa siku ya Kiyama (mbele ya Mola wao) hali ya kuwa wang'avu wa nyuso, mikono na miguu kutokana na athari ya udhu, basi yeyote yule awezaye kurefusha mipaka ya viungo vyake (katika kutawadha) na afanye hivyo." Muslim.