"Mwenyezi Mungu akimtakia kheri Mja humfahamisha (humpa elimu) kwenye dini" Hadith Tukufu

UTANGULIZI

i) MAANA YA JOSHO

Neno JOSHO/KUKOGA ni matokeo ya tafsiri ya neno la kiarabu GHUSLU.

Neno hili lina maana mbili; ya kilugha na kisheria.

Kwa mtazamo wa kilugha josho/kukoga ni kuyatiririsha maji kwenye kitu chochote kile kiwacho. Josho kisheria ni kitendo cha kuyapitisha maji mwili mzima kwa nia maalum.

 

ii) HUKUMU NA DALILI YA JOSHO:

Josho kisheria ni WAJIBU/FARDHI kwa kila muislamu akipatwa na mojawapo wa mambo yatakayomlazimisha kukoga kama vile janaba kwa jimai au kukoga, hedhi, nifasi, uzazi na mengineyo kama tutakvyoeleza huko mbele.

Ulazima huu akipatwa na mambo haya ni juu ya kila muislamu, mwenye akili timamu na mwenye uwezo wa kulitekeleza josho hilo. Dalili na ushahidi wa josho ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu :

"NA MKIWA NA JANABA BASI OGENI" [5:6]. Na amesema tena "NA WANAKUULIZA JUU YA HEDHI; WAAMBIE HUO NI UCHAFU. BASI JITENGENI NA WANAWAKE WAKATI WA HEDHI (zao). WALA MSIWAKARIBIE MPAKA WATWAHIRIKE" [2:222]

Josho ni jambo la kisheria, liwe ni josho la nadhafa au josho la faradhi/wajibu. Na dalili za usheria wa josho zinapatikana ndani ya Qur-ani Tukufu, Sunna ya Mtume (Hadithi) na Ijmaai.

Miongoni mwa dalili za josho katika Qur-ani Tukufu :

"HAKIKA ALLAH HUWAPENDA WANAOTUBU NA HUWAPENDA WANAOJITAKASA .." [2:222].

Yaani watu wanaojiepusha na kujilinda na hadathi/uchafu wa kimaada na kimaana/najisi za dhahiri na zile za batini. Katika jumla ya dalili za josho katika suna ni ile hadithi iliyopopkelewa na Abu Hurayrah – Allah amuwie radhi – amesema, amesema Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie –

"Ni haki ya kila muislamu kukoga siku moja katika juma, akaosha kichwa na mwili wake"

Bukhariy na Muslim. Mapendeleo na muradi wa neno haki ni kwamba haifai kwa muislamu kuacha, na wanazuoni wameichukulia siku hiyo kuwa ni siku ya ijumaa.

Ijmaa ya wanazuoni mujitahidi imekongomana na kukubaliana kwamba kukoga kwa ajili ya nadhafa ni jambo lililosuniwa na kukoga kwa ajili ya kusihi ibada ni wajibu na hakuna hata mwanachuoni mmoja aliyelipinga kongamano hili.

 

iii) FALSAFA/HEKIMA YA JOSHO :

Josho katika sheria lina hekima/falsafa na faida nyingi, miongoni mwa hizo ni kama zifuatazo :

 

1.      Kupata thawabu – Hii ni kwa sababu josho kwa maana na mtazamo wa kisheria ni IBADA kwa kuwa ndani yake kuna kutekeleza amri ya sheria na kuitumia hukumu ya sheria.

Kwa hivyo lina hili la utekelezaji amri na hukumu ya sheria ujira adhimu/mkubwa.

Ni kwa mantiki hii ndio Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – akatuambia : "Twahara ni nusu ya imani" Muslim.

Ni vema ikaeleweka wazi kuwa twahara imekusanya udhu, josho, tayammum na mengineyo.

 

2.      Kuwa nadhifu – Muislamu anapokoga, mwili wake hutakasika na kuwa msafi.

Usafi huu ni kinga kubwa ya vijidudu vinavyoweza kusababisha maradhi kama vile upele na humfanya muislamu anukie vema, kitu ambacho humkurubisha na watu kwani watu humteta mtu mchafu anukaye.

Imepokelewa kutoka kwa Bi Aisha – Allah amuwie radhi – kwamba amesema : Watu (maswahaba) walikuwa wakifanya kazi na hawakuwa na watumishi/vibarua wakawa na harufu mbaya ya jasho. Wakaambiwa na Mtume

"Lau mngalikuwa mnakoga siku ya Ijumaa".

Na katika upokezi mwingine Mtume – Rehema na Amani zimshukie –

"Lau mngalikuwa mnajitwahirisha kwa ajili ya siku yenu hii (yaani Ijumaa)". Bukhaariy na Muslim.

 

3.      Kuwa mchangamfu na kupata nguvu.

Mwili wa mwanadamu anapokoga huwa na nguvu mpya na kurudia kuwa katika hali ya uchangamfu baada ya ulegevu na uchovu ambao humsababisha uvivu na kutokujisikia kufanya jambo lolote zaidi ya kubweteka bwete!

Hili la kujisikia kuchoka na mwili kunyong’onyea hupatikana zaidi mara tu baada ya tendo la kujamiiana.

Kwa maneno ya jumla, falsafa ya josho twahara na nadhafa ambavyo hivi humuandaa mtu/mja na kumuweka katika nafasi nzuri ya kuwasiliana na kuzungumza na Mola Muumba wake ndani ya swala akiwa katika hali njema kabisa.