KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

DALILI/USHAHIDI WA KUFUFULIWA...Inaendelea

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tambua ya kwamba Kitabu chetu; Qur-ani Tukufu katika kuthibitisha mwanaadamu kurejeshwa upya kwa Mola na maisha ya pili baada ya haya ya kwanza hapa duniani. Qur-ani imepita mapito ya kiakili yaliyo katika upeo wa uwazi na wepesi kufahamika na kila aliye na siha ya akili. Katika jumla ya mapito hayo ya Qur-ani ni pamoja na:

  1. Kutolea dalili/ushahidi wa kufufuliwa kupitia kufufuliwa katika maisha haya kwa baadhi ya walio kufa:

     

 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tukiendelea kufahamishana na kujifunza dalili/ushahidi unao thibitisha kufufuliwa kwa wafu ndani ya Qur-ani, leo tujue na tukubali ya kwamba kwa mujibu wa Qur-ani zipo baadhi ya jamii za wanaadamu katika zama tofauti za Historia. Jamii hizo zilipata bahati ya kushuhudia kurudi tena uhai kwenye miili iliyo sambaratikia mavumbini na kwenye mifupa iliyo kwisha chakafuka kiasi cha kupeperushwa na upepo. Si hivyo tu, bali walishuhudia pia uhai unao tambaa kwenye vitu vigogofu. Allah Mtukufu ametuhadithia sehemu ya miujiza hiyo angavu; iliyo onekana dhaahiri shaahiri na kila aliye kuwa na macho, katika jumla ya miujiza hiyo ni kwamba kaumu (watu) ya Nabii Musa-Amani imshukie-ilimwambia Mtume wao: “...Hatutakuamini mpaka tumwone Allah wazi wazi. Ikakunyakueni radi nanyi mnaangalia. Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru”. Al-Baqarah [02]:55-56

 

Na ilitokea mtu mmoja katika Bani Israili kuuawa na kila kabila likawa linalituhumu kabila jingine kwa mauaji hayo, ili kuondosha mzozo huo na ili kupata kumjua muuaji, Mtume wao kupitia wahyi alio shushiwa, aliwaamuru kuchinja ng’ombe, wakamchinja lakini baada ya kuhoji sana sifa za ng’ombe huyo wa kuchinjwa. Baada ya kumchinja, Mtume wao akawaamuru wampige muuliwa na sehemu ya ngozi ya ng’ombe huyo, pale pale Allah akamuhui (akamrejesha kuwa hai tena) nao wakishuhudia, akawatajia aliye muua. Hilo ndilo analo litaja Allah aliye na utukufu kupitia kauli yake, tusome na tuzingatie: “Na mlipo muuwa mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na Allah ni Mwenye kuyatoa hayo mliyo kuwa mkiyaficha. Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo ng’ombe). Ndivyo hivyo Allah huwahuisha wafu, na anakuonyesheni ishara zake ili mpate kufahamu”. Al-Baqarah [02]:72-73

 

Na Yeye aliye Mtukufu akatuambia kuhusiana na wale maelfu walio kimbia kutoka kwenye makaazi yao kwa kuchelea kufikwa na mauti, Allah akawafisha na kisha akawahuisha, tusome: “Hukuwaona wale walio toka majumbani kwao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Allah akawaambia: Kufeni! Kisha akawahuisha. Hakika Allah ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru”. Al-Baqarah [02]:243

 

Na Yeye aliye na utukufu na ukuu akatuhadithia kuhusiana na yule aliye pita kwenye mji ulio geuka na kuwa magofu matupu; wakaazi wake wote wamekufa, na akastaajabu ni namna gani Allah ataweza kuwahuisha walio kuwa wakiishi hapo baada ya kufa na kutoweka kabisa katika uso wa ardhi. Akiwa katika mawazo na fikira hizo, Allah akamfisha kwa kipindi cha miaka mia moja, kisha akamfufua. Alipo ulizwa amekaa (amekufa) kwa muda gani, akadhania ya kwamba yeye hakukaa ila kwa siku moja tu au sehemu ya siku. Ili kumjulisha amekaa kwa muda gani, baada ya kumuhuisha Allah akamuhuishia punda wake aliye kuwa akimtumia kusafiria, huku yeye akiwa anaangalia uwezo wa Allah namna gani anavyo warejeshea uhai viumbe. Kwanza akaona mifupa ikijikusanya na kujiunda, kisha ikavikwa nyama, halafu umbo hilo likapuliziwa roho na punda akawa hai tena kama alivyo kuwa hapo awali. Ama tukija kwenye chakula chake alicho kuwa nacho safarini, katika miaka yote hiyo, kilibakia vile vile bila ya kuharibika, kuoza wala kutoa harufu kiasi cha kutolika. Na huo ni muujiza mwingine unao fahamisha na kuonyesha uwezo mkuu wa Allah katika kufisha na kuhuisha, yote hayo yanatajwa na Allah katika Kitabu chake Kitukufu kupitia kauli yake Yeye aliye Mtukufu: “Au kama yule aliye pita karibu na mji ulio kwisha kuwa magofu tu, akasema: Ataufufuaje Allah mji huu baada ya kufa kwake? Basi Allah alimfisha yeye muda wa miaka mia. Kisha akamfufua. Akamuuliza: Je, umekaa muda gani? Akajibu: Labda nimekaa siku moja au baadhi ya siku. Akamwambia: Bali umekaa miaka mia wewe. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na muangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu, iangalie hii mifupa yake jinsi tunavyo inyanyua kisha tunaivisha nyama. Basi yalipo mbainikia alinena: Najua kwamba Allah ni Mwenye uweza juu ya kila kitu”. Al-Baqarah [02]:259

 

Na pia tusisahau ya kwamba Nabii Ibrahimu-Amani imshukie-alimuomba Mola wake amuonyeshe namna anavyo wahuisha (wafufua) wafu, na hivi ndivyo ilivyo kuwa kama alivyo tuhadithia Allah Mtukufu: “Na alipo sema Ibrahim: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyo fufua wafu. Allah akasema: Kwani huamini! Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akamwambia: Twaa ndege wane na uwazoeshe kwako, kisha uweke juu ya kila kilima sehemu, kisha wete, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Allah ni Mtukufu Mwenye nguvu, na Mwenye hekima”. Al-Baqarah [02]:260

 

Katika aya hiyo, Allah Mtukufu alimuamuru Mtume wake Ibrahimu kuwachukua ndege wanne, awachinje, kisha atapanye viungo vyao kwenye majabali kadhaa; mguu huku, kichwa kule, utumbo hapa na kama hivyo. Kisha awaite akiwa anawaamrisha kujikusanya, basi ikawa kila kiungo kinamjia na kukaa mahala pake kilipo kuwepo kabla ya kuchinjwa na kukatwa katwa. Kulipo kamilika kujikusanya kwake, hapo ndipo Allah akavivizia roho viungo hivyo vilivyo jikusanya baada ya kutapanyika, na ndege wale wakaondoka, wakaruka wakijianikiza angani.

 

Kama vile haitoshi, Nabii Isa-Amani imshukie-alikuwa akitengeneza ndege wa udongo na kisha akiwavivizia roho na wakawa ndege hai kwa idhini yake Allah na hali kadhalika alikuwa akiwahuisha walio kufa, wakawa hai tena kwa idhini ya Allah. Kwani yeye aliwaambia kaumu yake: “Na ni Mtume kwa Wana wa Israili kuwaambia: Mimi nimekujieni na Ishara kutoka kwa Mola Mlezi wenu, ya kwamba nakuundieni kwa udongo kama sura ya ndege. Kisha nampuliza anakuwa ndege kwa idhini ya Allah. Na ninawaponesha vipofu wa tangu kuzaliwa na wakoma, na ninawafufua maiti kwa idhini ya Allah, na ninakwambieni mnacho kila na mnacho kiweka akiba katika nyumba zenu. Hakika katika haya ipo ishara kwenu ikiwa nyinyi ni wenye kuamini”. Aali Imraan [03]:49

 

Na pia tukumbuke ya kwamba As-haabul Kahfi (watu wa pangoni), Allah Mtukufu aliwalaza pangoni kwa kipindi cha miaka mia tatu na miezi tisa, kisha wakaamshwa kutoka katika usingizi wao huo baada ya muda mrefu huo, tukumbuke pamoja kisa kizima namna kilivyo kuwa kama kinavyo simuliwa na Qur-ani Tukufu: “Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadhaa wa kadhaa. Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lilio hisabu sawa muda walio kaa”. Al-Kahfu [18]:11-12

 

Akaendelea kusema katika aya ile ya 19: “Na kwa namna hii tuliwainua usingizini wapate kuulizana wao kwa wao. Alisema msemaji katika wao: Mmekaa muda gani? Wakasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku. Wakasema: Mola wenu Mlezi anajua zaidi muda mlio kaa. Hebu mtumeni mmoja wenu na hizi fedha zenu ende mjini, akatazame chakula chake kipi kilicho bora kabisa akuleteeni cha kukila. Naye afanye mambo hayo kwa busara, wala asikutajeni kabisa kwa yeyote”. Al-Kahfu [18]:19

 

 

Additional information