KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA KUBWA ZA KIYAMA: KUPULIZWA KWA BARAGUMU...Inaendelea

 

Naam, ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-ni juma jingine tena, kwa uwezo wake Mola Muumba na Mlezi wetu, tunakutana kwenye jukwaa letu hili la kila juma. Juma hili kwa auni na uwezeshi wake Allah, tunaendelea na somo letu la juma lililo pita ambapo tulianza kuiangalia alama andamizi ya zile alama kubwa za Kiyama. Alama hiyo inazingatiwa kuwa ndio alama ya mwisho, hakuna tena maisha wala ulimwengu baada ya kutokea kwake. Alama hiyo si nyingine ila ni kule kupulizwa kwa baragumu.

 

 

Haya na tuendelee na jukwaa letu, tayari tumeshajifunza juma lililo pita na tumeshajua baragumu ni nini na nani aliyepewa jukumu la kulipuliza. Tumeyajua yote hayo kupitia aya za Qur-ani na kauli za Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Leo tuendelee na darsa la jukwaa letu kwa kujiuliza: Baragumu litapulizwa siku gani miongoni mwa siku saba za juma? Kuhusiana na swali hili, tayari Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikwisha tuambia ya kwamba Kiyama kitasimama (kitatokea) siku ya Ijumaa na ndani ya siku hiyo ya Ijumaa watu watafufuliwa, akasema: “Hakika katika bora ya siku zenu, ni siku ya Ijumaa. Ndani ya siku hiyo aliumbwa Adam, ndani yake alikufa. Na ndani yake litapulizwa baragumu na ndani yake utakuwa ufufuo. Basi kithirisheni kuniswalia ndani yake (siku hiyo), kwani swala yenu huonyeshwa kwangu. Hakika Allah ameiharamishia ardhi kula miili ya Mitume”. Ahmad, Abu Daawoud & Nasaai [SAHIH AL-JAAMI’I 2212]-Allah awarehemu.

 

Na akasema tena Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Nilionyeshwa siku na nikaonyeshwa ndani ya siku hizo, siku ya Ijumaa. Tahamaki nikaiona (hiyo Ijumaa) ni mithili ya kioo cheupe na katikati yake kuna doa jeusi. Nikauliza: Ni nini hiki? Nikajibiwa: (Hiyo ni) Saa (Kiyama)”.Twabaraaniy [SAHIH AL-JAAMI’I 4000]-Allah amrehemu.

 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-kama tunafuatana pamoja na kama unakumbuka, tumesema huko katika darsa zilizo tangulia ya kwamba baragumu litapulizwa mara mbili na Malaika Israafilu; pulizo la kufa kila kilicho hai na kumalizika kwa ulimwengu na pulizo la kufufuliwa. Sasa tujiulize: Kitapita kitambo gani baina ya mapulizo mawili hayo? Swali hili juu ya muda ambao utakao pita baina ya pulizo la kumaliza kila kitu na lile la ufufuo, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekwisha lieleza hilo. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurairah-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Baina ya mapulizo mawili hayo kuna arobaini”. Wakauliza: Ewe Abu Huraira! Ni siku arobaini? Akajibu: Nimekataa. Wakauliza (tena): Ni miezi arobaini? Akajibu: Nimekataa. Wakauliza (kwa mara nyingine): Ni miaka arobaini? Akajibu: Nimekataa”. Bukhaariy [11/551] & Muslim [2955]-Allah awarehemu.

 

Na imepokewa kutoka kwa Ibn Masoud-Allah awawiye radhi: “Kisha atasimama Malaika mpuliza baragumu baina ya mbingu na ardhi na kupuliza baragumu. Na hilo baragumu ni pembe. (Baada ya kupuliza), hatobakia kiumbe yeyote mbinguni wala ardhini ila atakufa isipo kuwa yule atakaye mtaka Mola Mlezi wako. Kisha utakuwepo baina ya mapulizo mawili hayo muda ambao Allah atataka uwe”. FAT-HUL BAARIY [11/370]-Allah amrehemu.

 

Imamu Qurtubiy-Allah amrehemu-amesema katika kuizungumzia kauli ya Abu Huraira katika hadithi “Nimekataa”: Kauli/neno hilo lina tafsiri mbili:

 

1.       “Nimekataa”– huenda anakusudia kusema: Nimejizuia kubainisha hilo. Na tafsiri ya kauli hiyo ni kwamba yeye alikuwa na ujuzi wa hilo, yaani alilisikia kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

 

2.       “Nimekataa”huenda anakusudia kusema: Nilikataa kumuuliza juu ya hilo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na tafsiri ya kauli yake hiyo ni kwamba yeye hakuwa na ujuzi wa hilo.

 

Kati ya tafsiri mbili hizo, ile ya kwanza ndio ina nguvu zaidi na hakika si vinginevyo yeyehakulibainisha hilo kwa kuwa hakuona haja ya kufanya hivyo, na kwa sababu hilo si miongoni mwa ubainifu na uwongofu alio amrishwa kuufikisha. [AT-TADHKIRAH 01/320]

 

Haya na tuendelee na darsa letu, sote bali kila muislamu anaamini na anakubali uwepo wa siku ya Kiyama kama anavyo amini na kukubali kupulizwa kwa baragumu. Tuendelee kuongeza maarifa yetu juu ya hilo baragumu kwa kujiuliza: Je, baragumu litapulizwa mara mbili tu kama tulivyo tangulia kusema au ni zaidi ya hizo mara mbili?

 

Pamekhitalifianwa baina ya Wanazuoni-Allah awarehemu-katika idadi ya mipulizo ya baragumu. Al-Hafidh Ibn Hajar na Imamu Qurtubiy-Allah awarehemu-madhehebu yao wao ni kwamba Malaika Israafilu atalipuliza baragumu mara mbili tu. Mpulizo wa kwanza ni ule wa kumaliza uhai wa ulimwengu na vyote vilivyomo humo na ule wa pili ni kwa ajili ya ufufuo. Lakini madhehebu ya Imamu Ibn Al-Arabiy, Ibn Taimiyah, Ibn Kathiir na As-safaarayiniy-Allah awarehemu-itakuwa ni mipulizo mitatu. Wa kwanza ni mpulizo wa fadhaa(muhangaiko), wa pili ni wa kufisha na wa tatu ni wa kufufua. Watu wa madhehebu ya kwanza, dalili yao ni ile kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Baina ya mapulizo mawili hayo kuna arobaini”. Ama wale wenye madhehebu ya mipulizo mitatu, dalili yao ni kwamba Allah Mtukufu ametofautisha baina ya mipulizo hiyo mitatu kupitia kauli yake: “Na siku litapo pulizwa baragumu, watahangaika waliomo mbinguni na katika ardhi, ila amtakaye Allah. Na wote watamfikia nao ni wanyonge”. An-Namli [27]:87

 

Huo ni mpulizo mmoja, halafu akataja mipulizo miwili katika neno lake: “Na litapulizwa baragumu, wazimie waliomo mbinguni na waliomo katika ardhi, isipo kuwa yule aliye mtaka Allah. Kisha litapulizwa mara nyingine. Hapo watainuka wawe wanangojea”. Az-zumar [39]:68

 

Additional information