KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

KUVUA KATIKA TALAKA

Kama inavyo swihi talaka iliyo angikwa juu ya sifa fulani au sharti fulani, ndivyo inavyo swihi talaka iliyo ingiwa na uvuaji. Na muradi/makusudio ya kuvua katika talaka: Ni mume kukusanya zaidi ya talaka moja kwa tamko moja, kisha anatoa baadhi yake kwa kutumia ala/chombo cha kuvua, ambacho ni herufi “ILA”, kwa kusema kumwambia mke wake: “Wewe umeachwa talaka tatu, ILA talaka moja”, hapa ataachika talaka mbili. Au akamwambia: “Wewe umeachwa talaka tatu, ILA mbili”, hapa atakuwa ameachika talaka moja.

 

Kuswihi kwa talaka ya kuvua, ni kwa sababu uvuaji (Istithnaa) wa kinacho hesabiwa, ni muundo/mtindo lugha wa Kiarabu unao fuatwa (tumiwa) na umetumiwa na Qur-ani na Sunna (Hadithi) katika kuelezea maana mbali mbali na kudhibiti kiasi na idadi. Allah Ataadhamiaye amesema akihadithia juu ya Nabii Nuhu-Amani imshukie: “NA HAKIKA TULIMTUMA NUHU KWA WATU WAKE, NA AKAKAA NAO MIAKA ELFU ILA (kasoro) MIAKA KHAMSINI...” [29:14]

 

Kwa ajili/sababu ya kutumiwa kwake na Qur-ani, ndio kumejuzu kutumia uvuaji katika kuielezea talaka na kudhibiti idadi ya talaka zilizo kusudiwa kutolewa.

 

 

 

xii.            Sharti za kuswihi kuvua katika talaka:

 

         Ili uvuaji katika talaka uswihi, kumeshurutizwa kuchunga masharti yafuatayo:

 

1.         Mtoa talaka (mume) anuie kuunganisha uvuaji na maneno ya asili yenye kuvuliwa. Lau atakamilisha kutamka maneno yake ya asili, kisha ikampitikia akilini mwake kuvua sehemu/baadhi yake, hakutoswihi kuvua huko na talaka itatuka kama inavyo hukumiwa na maneno yake asili kabla ya kuyatundikia uvuaji.

 

2.         Tamko la kuvua liungane na tamko lenye kuvuliwa kwa kufuata ada ya mahala husika.

 

Angalia, lau atatenganisha baina ya matamko mawili hayo; lenye kuvua na lile lenye kuvuliwa, kwa kitambo kinacho zingatiwa na ada kuwa ni kitenganishi, kama vile dakika moja mathalan, uvuaji wake huo utakuwa ni batili. Na talaka itatuka kwa mujibu wa mahukumio ya tamko lenye kuvuliwa. Sura yake ni mume kumwambia mke wake: “Nimekuacha talaka tatu”, kisha akanyamaza kidogo halafu ndipo akasema: “ILA talaka moja/mbili”.

 

3.         Uvuaji usizamishe (usilingane/usizidi) kiasi/idadi ya kile kinacho vuliwa, kama vile kusema: “Nimekuacha talaka tatu ILA tatu”. Uvuaji kama huu, huzingatiwa kuwa ni puo (upuuzi) na hukumu itabakia kwa vile inavyo hukumiwa na tamko vuliwa; yaani hizo zitakuwa ni talaka tatu.

 

Baada ya hayo, sasa unapaswa kufahamu kwamba uvuaji katika maneno ya kukubali, huzingatiwa kuwa ni kukanusha. Na uvuaji katika maneno ya kukataa, huzingatiwa kuwa ni kuthibitisha, kwa sababu uvuaji hupewa kinyume cha hukumu ya asili ya chenye kuvua. Lau kama mume atasema: “Sikukuacha ILA talaka mbili”, zitakuwa talaka mbili.

 

 

 

xiii.            Dalili ya kuswihi kuvua katika talaka:

 

         Dalili ya kuswihi kuvua katika talaka, ni kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakaye acha huru mtumwa au akaacha mke na akavua, kunamuelea kuvua kwake huko”. Ibn    Al-Athiyr [AN-NIHAAYAH]

 

 

 

xiv.            Kumkabidhi mke mamlaka ya kujiacha:

 

         Kunaswihi mume kuyahamisha mamlaka ya kutoa talaka kutoka kwake kwenda kwa mke wake. Na uhamishaji huo, huwa katika daraja ya kummlikisha mke talaka.

 

 

 

xv.            Sharti za kutuka kwa talaka milikishwa:

 

         Ili talaka ya namna hii iswihi, kumeshurutizwa kupatikana kwa sharti zifuatazo:

 

                  1.          Talaka hiyo iwe ni ya kutinda (kukata), kwani hakuswihi kuitundika juu ya kitu/jambo fulani. Hivi ni kama vile mume kumwambia mke: “Ikifika kesho, basi jiache”.

 

                  2.          Mume mmilikishi talaka awe ni mukalafu (mtu mzima, mwenye akili timamu), kwani hauswihi umilikishi talaka wa mume mtoto au mwenda wazimu.

 

                  3.          Mke mmilikishwa pia awe mukalafu, kwani hauswihi umilikishwaji talaka wa mke mtoto au mwenda wazimu.

 

                  4.          Mke ajiache haraka mara tu baada ya kupewa mamlaka ya kujiacha, kwani lau atakuchelewesha huko kujiacha kwa kitambo kinacho likata tamko la “Qabuul” na “Ijaabu” ya ndoa, talaka hiyo haitaswihi.

 

 

 

xvi.            Dalili ya kujuzisha kumkabidhi mke mamlaka ya kujiacha:

 

         Hutolewa dalili ya kujuzisha kummilikisha mke talaka, kile kitendo cha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-cha kuwapa khiari wake zake wachague ama kuendelea kuishi naye au kuachwa. Na hilo ni pale ilipo shuka kauli yake Allah Ataadhamiaye: “EWE NABII! WAAMBIE WAKE ZAKO: IKIWA MNATAKA MAISHA YA DUNIA NA PAMBO LAKE, BASI NJOONI, NITAKUPENI KITOKA NYUMBA, NA KUKUACHENI MWACHANO MZURI”. [33:28]

Lau kuchagua kwao kuachwa kusingeli kuwa na athari yoyote, basi kule kupewa kwao khiari ya kuchagua, kusingeli kuwa na maana yoyote.

Additional information