KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

KUZINGIRWA KWA SAYYIDNA UTHMAN

Kisha baada ya mahojiano hayo ambamo waasi walishikilia kuwa Sayyidna Uthman ndiye mwandishi wa waraka ule, na yeye akikataa kuuandika wala kuutambua kwa kiapo. Waasi waliendelea kuung’ang’ania msimamo wao, wakamzingira Amirul-Muuminina na swahaba na mkwe wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliye bashiriwa pepo. Mzingiro ulio mkubwa mno, kiasi hata cha kumzuia kuswali kwenye msikiti wa Mtume wa Allah.

Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-akatuma ujumbe wa wito kwa Sayyidna Aliy, Twalhah na Zubeir, nao wakaitika wito. Walipo fika, akawatokea akasema: Enyi watu wangu! Kaeni nyote! Basi wote, mtaka amani na mtaka vita miongoni mwao, wakaketi. Walipo kaa, akasema: Enyi watu wa Madina! Ninakuagieni kwa Allah na ninamuomba akupeni khalifa bora baada yangu. Halafu akaendelea kusema: Ninakuapieni kwa Allah, je mnajua ya kwamba wakati alipo fishwa Umar, nyinyi mlimuomba Allah akuteulieni na akukusanyeni kwa aliye mbora wenu. Je, sasa mnasema ya kwamba Allah hakuyajibu (maombi yenu)? Mmekuwa dhaifu juu yake na ilhali nyinyi ndio wadau wa haki yake! Au mnasema imeingia unyonge kwa Allah dini yake, kwa hivyo Yeye hajali ni nani atawaliaye dini (yake) kwa sababu ya kutapanyika watu wake siku hiyo? Au mnasema (jambo) hilo (la uteuzi wa khalifa) halikufanyika kwa shura na hakika si vinginevyo ulikuwa ni udikteta? Kwa ajili hiyo basi, Allah akauachia umma mambo yake pale ulipo muasi na usitake ushauri katika uongozi. Au mnasema kwamba Allah hakuujua mwisho wa jambo langu (uongozi)? Ninakuapieni Allah, je nyinyi mnajua kwamba mimi nina utangulizi katika kheri na mguu wa kheri, mguu wa Allah uko kwangu. Kwa haki ya kila aliye kuja baada yangu aujue ubora wake huo (mguu wa kheri) kwangu. Basi hebu taratibuni, msiniue, kwani ilivyo khasa si halali ila kuwaua watu watatu; Mwanaume aliye zini baada ya kuwa na ngome, au aliye kufuru baada ya imani au aliye iua nafsi pasina haki. Kwani hakika mtakapo niua, mtakuwa mmeuweka upanga juu ya shingo zenu, kisha Allah hatakuondosheeni ikhtilafu abadan.
Waasi wakasema (baada ya kumsikiliza Sayyidna Uthman): Ama uliyo yataja, yaani istikhara iliyo fanywa na watu baada ya Sayyidna Umar, kisha wakakutawaza wewe kuwa khalifa, hakika kila alilo lifanya Allah ni kheri. Lakini (pamoja na yote hayo) amekufanya wewe kuwa ni mtihani alio watahini kwao waja wake. Na ama uliyo yataja, yaani utangulizi wako kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakika wewe ulikuwa hivyo na umekuwa mstahiki wa utawala. Lakini umeyazua unayo yajua na sisi hatutaacha kusimamisha haki juu yako kwa kuichelea fitina kubwa inayo kuja. Na ama kusema kwako kwamba si halali kuua ila watu watatu; hakika sisi tunakuta katika dini yah Allah zaidi ya hao watatu ulio wataja wewe. (Tunakuta) kumuua aliye eneza ufisadi (uharibifu) katika ardhi (nchi), kumuua aliye fanya dhuluma (jeuri), kisha kumpiga vita kwa dhuluma yake. Na kumuua aliye zuia kitu/sehemu ya haki na anaye pigana kumlinda. Nawe umekwisha fanya dhuluma, umezuia haki na umefanya udikiteta juu ya haki. Na hujalipa kisasi cha ulio wadhulumu na umeufanyia ukiritimba uongozi wetu. Na kama unadai kwamba hujatufanyia udikiteta juu ya uongozi, basi hakika wale walio simama dhidi yako na kukuzuia, ama watakupiga kwa kung’ang’ania kwako uongozi. Basi lau utajiuzulu, wataondoka na kuacha kukupiga vita.
Sayyidna Uthman hakuwajibu na akabakia nyumbani kwake asitoke nje. Na wengi miongoni mwa watu wa Madina walikuja wakaizunguka nyumba yake ili kumuondoshea hatari ya waasi wale. Sayyidna Uthman akawaamuru waondoke, basi wakaondoka ila wachache, miongoni mwao (hao wachache walio bakia) alikuwamo Hassan bin Aliy, Ibn Abbas, Ibn Zubeir na Muhammad bin Twalhah.
Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-alikuwa akichukia sana vita kutokea Madina katika zama za uongozi wake. Basi akawa anajiepusha na hilo kwa kadiri alivyo weza, kiasi cha kufikia kuwakataza hata watu wake wa nyumbani kuchomoa panga zao. Na akawa anawarepeshea muda wale wapinzani na akiwakithirishia khutba. Na akiwatumia Aliy bin Abi Twaalib mara baada ya mara akiwausia kuachana na madai yao, lakini wapi hawakukatazika. Si hivyo tu, bali kila alipo wafungia mlango mmojawapo wa fitina, wao walifungua mlango mwingine. Wakamzuilia maji khalifa wa Waislamu, Sayyidna Aliy akawaendea wakati wa magharibi, akawaambia: Enyi watu nyie! Hakika hili mnalo lifanya sasa, halifanani na mambo ya Waislamu na wala (halifanani) na mambo ya makafiri – (yaani mlifanyalo halitendwi na makafiri seuze na Waislamu!) Basi (kama kweli nyinyi ni waislamu), msimkatie maji wala chakula, kwani hutekwa Warumi na Wafursi (nao wote ni washirikina), basi pamoja na hivyo bado hupewa chakula na maji. Waasi wakasema: Hapana wallah, wala (hatutadondosha hata) tone la machozi (kwa kufa kwake kwa kiu). Imamu Aliy akaondoka baada ya jitihada zake za kuwashawishi waasi kugonga mwamba. [AL-BIDAAYA WAN-NIHAAYAH 03/192, TAARIKHUT-TWABARIY 02/672, AL-FITNATU WA WAQ’ATUL-JAMAL sahifa 66, AL-MUNTADHWAM 05/54 & AL-KAAMILU FIT-TAARIKH 03/63]
Akaja mama wa waumini (mke wa Mtume wa Allah); Habibah bint Abi Sufyaan, akiwa amechukua chombo kidogo cha kuwekea maji. Waasi wakaupiga uso wa nyumbu wake, akasema (Ummul-Muuminina): Hakika wasiya wa Baniy Umayyah uko kwa mtu huyu, kwa ajili hiyo basi nimependa kuja kumuuliza kuhusiana nao, ili mali za mayatima na wajane zisije zikapotea bure. Waasi wakasema: Mwongo wee! Wakaikata kamba ya nyumbu wake kwa upanga, (nyumbu) akafanya ukorofi na mama wa waumini akakurubia kuanguka, watu wakamdaka na kumpeleka nyumbani kwake.
Baada ya kuzuiliwa maji, Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-akawachungulia watu, akawaambia: Ninakuapieni kwa Allah, je nyinyi mnajua kwamba mimi ndiye niliye kinunua kisima cha Rouma kwa mali yangu, ili watu wapate maji matamu (yasiyo ya chumvi). Na nikaifanya ndoo yangu (katika kuteka maji humo) ni sawa na yeyote katika waislamu (hilo mnalijua)? Wakajibu: Naam (tunalijua). Akawaambia (kama mnalijua) basi kwa nini mnanizuia kunywa mpaka ninafuturu kwa maji ya bahari (maji chumvi)? Kisha akaendelea kusema: Ninakuapieni kwa Allah, je nyinyi mnajua ya kwamba mimi nilinunua ardhi kadha, nikaitoa kwa msikiti (huu wa Mtume)? Wakajibu: Naam (tunajua). Akasema: Basi je, mnamjua yeyote aliye zuiliwa kuswali humo kabla yangu? Halafu akaendelea kusema: Ninakuapieni kwa Allah, je nyinyi mnajua ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema kadha kadha kunikhusu mimi? Akataja mambo kadhaa katika sifa zake za pekee si kwa kuonyesha ufakhari, bali kwa njia ya ukumbusho. Maneno yake hayo yakawaathiri watu wengi miongoni mwao mpaka wakamwambia: Taratibu ewe Amirul-Muuminina! Hapo ndipo shetani wa fitina hii alipo paaza sauti yake na kusema: Huenda hivyo ni vitimbi vyake kwenu (ili apate kuokoka). Kauli yake hiyo ikawazidishia mori wa dhuluma na uasi.
Mama wa waumini (mkewe Mtume wa Allah); Bi. Aysha akatoka kwa ajili ya ibada ya Hija, na alikuwa amekimwa kukaa Madina pamoja na fitina ile. Na akamtaka kaka yake Muhammad bin Abibakar afuatane naye, akakataa kwa sababu naye alikuwa ni miongoni mwa waasi walio jitoa kwenye utii wa Amirul-Muuminina, Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi. Handhwalah yule mwandishi akamwambia: Mama wa waumini (dada yako) anakutaka ufuatane naye, wewe unakataa kumfuata. Lakini unakubali kuwafuata mbwa mwitu wa Waarabu kwenye jambo lisilo halali?! Na hakika jambo hili ikiwa litafikia kwenye ugombezi, watakushinda Baniy Abdi Manaaf.

Additional information