KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA KUBWA ZA KIYAMA: JUA KUCHOMOZEA KWENYE MACHWEO YAKE

 

Mpendwa mwana jukwaa-Allah kurehemu-na akuongoze kutambua ya kwamba jua kuchomoza kutokea upande wa Magharibi badala ya Mashariki kama yalivyo maumbile ya ulimwengu tangu kuumbwa kwake, jambo hilo ni katika jumla ya zile alama kubwa za Kiyama zilizo tajwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Ujio wa alama hii kubwa ya Kiyama umethibiti pasina shaka ndani ya Qur-ani Tukufu na katika Sunna, alama hiyo ndio inayo tajwa na kukusudiwa na kauli yake Mola Muumba wetu pale alipo sema: “.... Siku zitakapo fika baadhi ya ishara za Mola wako Mlezi, kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake...”. Al-An’aam [06]:158

 

 

Naam, aya inakusudia kusema ya kwamba siku zitakapo tokea baadhi ya alama za Kiyama, wakati huo basi kuamini kwa mtu kafiri hakutamfaa na wala hakutamsaidia kumuondolea adhabu inayo andamia ukafiri wake. Na hali kadhalika twaa (utiifu kwa Mola kwa kutekeleza maamrisho na kuacha makatazo) haitamfaa mtu aliye kuwa asi; mtenda maasi na hakupata kutenda matendo mema hapo kabla.

 

Imamu Twabariy-Allah amrehemu-amesema: “Yaani (aya inakusudia kusema ya kwamba) kuamini kwa watu walio kuwa wakimshirikisha Allah kabla ya ujio wa alama hiyo kubwa, yenye utisho kutokana na amri yake Allah. Basi hukumu ya kuamini kwao huko ni kama ile ya hukumu ya kuamini wakati wa kusimama kwa Kiyama (hapo Imani itafaa nini?!)”. [Rejea TAFSIIR AT-TWABARIY 16/266]-Allah amrehemu.

 

Na Hadithi nyingi zilizo sahihi, zimefahamisha ya kwamba muradi na mapendeleo ya ibara “baadhi ya ishara” iliyo tajwa ndani ya aya tuliyo inukuu punde, ni kuchomoza kwa jua kutokea kwenye machweo yake (upande wa Magharibi badala ya Mashariki). Na hiyo ndio kauli ya Wanazuoni wengi wa fani ya Tafsiri ya Qur-ani Tukufu. [Rejea TAFSIIR AL-QURTUBIY 07/145]-Allah amrehemu.

 

Na hivi ndivyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anavyo itaja na kuielezea alama hiyo ambayo ni katika jumla ya alama kubwa zinazo ashiria kukaribia mno kwa ile saa ya Kiyama, haya na tumsikilize. Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakitosimama (hakitatokea) Kiyama mpaka kwanza jua lichomoze kutokea kwenye machweo yake. Basi litakapo chomoza na watu wakaliona, wote wataamini na wakati huo ni pale ambapo  {kuamini hapo hakutomfaa mtu kitu, ikiwa hakuwa ameamini kabla yake, au amefanya kheri katika Imani yake}”. SAHIH AL-BUKHAARIY [4636]

 

Na jambo lililo rasmi kama lilivyo thibiti kwenye maana ya aya tuliyo tangulia kuinukuu, ni kwamba jua litakapo chomoza kutokea upande wa Magharibi (machweo yake), wakati huo haitakubaliwa imani ya mtu ambaye hakuwa ameamini kabla ya hapo kama ambavyo haitakubaliwa toba ya mtu asi; mtenda madhambi. Itakuwa hivyo kwa sababu kuchomoza jua kutokea kwenye machweo yake, hiyo ni aya/alama kubwa itakayo onwa iyaana (dhaahiri shaahiri) na kila mtu atakaye kuwa hai katika zama hizo. Kwa ajili hiyo basi, zitafichuka kwao kweli halisia na watashuhudia vitisho na mambo ya ajabu ambayo hawakupata kuyaona hapo kabla, hayo sasa ndio yatakayo washurutisha kukiri na kumuamini Allah na aya/ishara zake. Imepokewa kutoka kwa Imraan bin Huswein-Allah amuwiye radhi-ya kwamba yeye amesema: “Hakika si vinginevyo, haitakubaliwa toba wakati wa kuchomoza jua kutokea kwenye machweo yake mpaka uje ukelele mmoja, basi na wahiliki (wafe) katika ukelele huo watu wengi. Basi yeyote atakaye silimu na akatubu katika wakati huo, kisha akafa, haitakubaliwa toba yake. Na atakaye tubia baada ya hapo (baada ya kuchomoza kwa jua na kutokea kwa ukelele, huyo) itakubaliwa toba yake”. [Rejea: FAT-HUL-BAARIY 11/354]

 

Na kauli hiyo ya Ibn Huswein inatiwa nguvu na ile riwaya iliyo pokewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa bi. Aysha-Allah awawiye radhi-amesema: “Itakapo tokea ya mwanzo ya zile alama kubwa (za Kiyama), watazuiwa malaika waandishi (kuandika matendo ya waja), zitatupwa kalamu (za kuandikia amali) na viwiliwili vitatoa ushahidi wa matendo”. [Rejea: AL-MUSWANNAF 38754]

 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tambua na ujue ya kwamba muradi na mapendeleo ya ibara “ya mwanzo ya zile alama kubwa”  hapa ni kule kuchomoza jua kutokea kwenye machweo yake. Ama zile alama zilizo kabla ya huku kuchomoza kwa jua, hakika hadithi zinafahamisha juu ya kukubaliwa kwa toba na imani. Imamu Jariir Twabariy-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Abdillah bin Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema: “Toba ni yenye kukunjuliwa muda wa kuwa jua halijachomoza kutokea kwenye machweo yake”. [Rejea TAFSIIR AT-TWABARIY 08/103]

 

Na linalo dhihirika kutokana na baadhi ya rejea za hadithi, ni kwamba kipindi cha mabadiliko ya ulimwengu katika kuchomoza kwa jua kutokea upande wa machweo yake, kitachukua muda mrefu. Hilo limeashiriwa kwenye riwaya iliyo pokewa na Abdullah bin Amrou-Allah awawiye radhi-kutoka kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Baada ya kuchomoza jua kutokea kwenye machweo yake, watu watabakia kwa kipindi cha miaka mia moja na ishirini”. [Rejea: UMDATUL-QAARIY 27/218]

 

Additional information