KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

TALAKA

Neno “talaka”, lina maana mbili kuu; maana katika lugha na maana katika sheria. Twendapo na maana ya talaka kilugha, ni: kuacha huru, kufungua, kurudisha kwenye asili, kuvunja. Na talaka kisheria: Ni kufungua/kuvunja kifungo cha ndoa kwa tamko la talaka na mfano wa tamko hili.

 

 

    ii.            Dalili ya kushariiwa kwa talaka:

         Asili/msingi katika uweko wa sheria ya talaka, ni kitabu     (Qur-ani), Sunna (Hadithi) na Ijmaa. Ama Qur-ani, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “T’ALAKA NI MARA MBILI. KISHA NI KUKAA KWA WEMA AU KUACHANA KWA VIZURI...” [02:229]

Yaani, talaka ni mara mbili. Baada ya kila talaka mume ana haki ya kukaa naye kwa kumrejea kabla ya kwisha siku za eda, au kumrejesha katika dhamana yake kwa kumwoa upya. Na katika hali hiyo makusudio yake yanapasa yawe ni kukaa naye kwa uadilifu na kumtendea wema, au kuachana kwa ihsani na heshima bila ya kuhasimiana.

Na kauli yake Atukukiaye: “EWE NABII! MTAKAPO WAPA T’ALAKA WANAWAKE, BASI WAPENI T’ALAKA KATIKA WAKATI WA EDA ZAO...” [65:01]

Yaani, mkitaka kuwapa talaka wanawake, basi wapeni talaka kwa kukabiliana na eda zao (yaani wakati wa twahara kabla ya kuwaingilia).

Ama katika Sunna, ni kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Halali ichukizayo mno mbele za Allah Ataadhamiaye, ni talaka”. Abu Daawoud [2178] & Ibn Maajah [2018]-Allah awarehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Nilikuwa na mwanamke nimpendaye na baba yangu (Sayyidna Umar) alikuwa akimchukia (mke wangu huyo). Baba yangu akaniamuru nimtaliki, mimi nikakataa. Akalitaja hilo (akamshtakia) Mtume-Rehema na Amani zimshukie. (Mtume) akasema: “Ewe Abdullah Bin Umar! Mtaliki mkeo”. Tirmidhiy [1189], Ibn Maajah [2088] & Abu Daawoud [5138]-Allah awarehemu.

Ama Ijmaa, limekongamana neno la Wanazuoni juu ya uweko wa sheria ya talaka na hakuna yeyote miongoni mwao aliye khalifu.

 

  iii.            Falsafa ya kushariiwa kwa talaka:

         Asili katika ndoa, ni kuendelea kwa maisha ya kindoa baina ya mke na mume. Na Allah-utakasifu wa mawi ni wake-ameiwekea ndoa hukumu nyingi na adabu/taratibu nyingi. Ili kuiendeleza, kudhamini usalia wake na kukuza mafungamano ya kindoa baina ya mume na mke. Ila kwamba adabu na hukumu nyingi hizi hutokezea kutokuchungwa na wote wawili, mume na mke au mmoja wao. Hivi ni kama vile mume kutokujishughulisha na uchaguzi mzuri wa mke kama alivyo elekezwa na Sheria. Au mume na mke wote pamoja au mmoja wao kutolazimikiana na adabu/taratibu za tangamano la ndoa walizo rasimiwa na dini isiyo na taklifu. Kwa ajili hiyo hutuka baina yao ukorofi, kisha ukorofi huu huzidi kukua kiasi cha kutokutoa nafasi ya usuluhishi. Na wala hauachi njia ya kuelewana na kuishi pamoja baina ya mume na mke. Hapo ndipo kwa kuizingatia hali hii, ikawa hapana budi kuweka kanuni ya tahadhari itakayo kimbiliwa katika hali kama hii. Kwa lengo la kufungua kifungo cha ndoa kwa namna ambayo haki za upande wowote hazitapotea. Kanuni hii itatumika tu muda wa kuwa maisha ya ndoa yameshindikana kabisa baina ya wawili hawa, Allah Ataadhamiaye anasema: “NA WAKITENGANA ALLAH ATAMTOSHELEZA KILA MMOJA KATIKA WAO KWA UKUNJUFU WAKE. NA ALLAH NI MKUNJUFU MWENYE HIKIMA”. [04:130]

- Yaani, ikiwa suluhu haikumkinika na ikawa chuki au karaha ndio ndio imeshika nguvu zaidi, basi kunalazimika kufarikiana (kuachana). Na wakifarikiana Allah atawatosheleza kila mmoja wao kutokana na ukunjufu wa rehema na fadhila zake. Na riziki ziko katika mikono ya Allah, na Yeye ndiye Mwenye hikima na hupanga mambo yote kwa mipango yake.

Basi ikiwa mume ataitumia kanuni hii kama njia ya mwisho kwenye dharura kama hii, basi hiyo ni tiba ya dharura isiyo kwepeka ingawa mara nyingi huwa chungu kumeza. Ama akiitumia ili kutimiza purukushani zake za kupitishia matamanio maovu yake, basi kanuni hiyo kwake huwa ni halali chukivu mno mbele za Allah Ataadhamiaye. Na Allah Ataadhamiaye ndiye amjuaye mtengenezaji na mfanya fisadi na kwake ndio marejeo ya huyu (mtengenezaji) na yule (mfanya fisadi).

Kutokana na maelezo tuliyo yataja, tunatiwa nguvu kwamba kuwekwa kwa sheria ya talaka kwa namna ambayo zilivyo pangwa hukumu na natija zake na sheria ya Kiislamu. Kunahesabiwa na kuchukuliwa kuwa ni miongoni mwa fahari ya Sheria ya Kiislamu. Na ni dalili kubwa inayo onyesha kwamba hukumu za sheria hii zinarandana mrandano timilifu na umbile la mwanaadamu na haja za kimazingira alizo nazo huyu mwanaadamu. 

Additional information