KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

BASRAH

Mwanzoni mwa awamu ya ukhalifa wa Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-gavana wa Basrah alikuwa ni Abu Mousa Al-Ash’ariy. Akaushikilia wadhifa huo mpaka mwaka wa ishirini na tisa, Sayyidna Uthman akamuuzulu na akamtawaza kushika mahala pake Abdullah bin Aamir, bin Kuraiz, bin Rabeeah, bin Abdi Shamsi. Na akamkusanyia jeshi la Abu Mousa na jeshi la Abil-Aaswi At-thaqafiy kutoka Oman na Bahrein.

 

Na katika enzi za ugavana wake (Abdullah bin Aamir), watu wa Faaris walimuasi amiri (kiongozi) wao; Ubeidullah bin Ma’amar. Ubeidullah akawaendea na kukutana nao kwenye lango la kuingilia Istwakhri, likauawa na kuendeshwa mbio jeshi lake. Khabari hiyo ilipo mfikia gavana Ibn Aamir, akawaendea na jeshi kubwa, akapambana nao mpambano mkali mpaka akafanikiwa kuwasambaratisha na akaufungua mji wa Istwakhri kwa nguvu. Na akakiendea kitongoji cha Daarabajardi ambacho wakaazi wake walifanya uhaini, nacho akakifungua. Wakati akiwa hapo ikamjia khabari ya kwamba watu wa Istwakhri wamefanya uhaini tena, akarudi tena na akaufungua mji kwa mara ya tatu na wakauawa wengi miongoni mwa viongozi/wenye heshima wa wakaazi wa huko. Kisha akatusha mshindo mkuu kwa watu wa Faaris ambao ulimuondoshea udhalili. [TAARIKHUT-TWABARIY 01/392, TAARIKHU AL-KHULAFAA Sah. 155]

Na katika enzi zake pia, aliuwa Yazdajrid; mfalme wa Fursi, akiwa ndio mfalme wao wa mwisho [TAARIKHUT-TWABARIY 01/93].

Na khabari zilizo pokewa katika kuelezea namna alivyo uawa, zinagongana. Ila tu ni kwamba waandishi wa Sira/Tarekh wanakongamana ya kwamba yeye aliuawa peke yake akiwa ametupwa mkono na watu wake, huku ufalme huo mkubwa usimsaidie kwa chochote. Na wakakongamana ya kwamba aliuawa na mtu asiye muarabu. Na alikuwa akitamani wakati huo ya kwamba yeye angeli angukia mateka mikononi mwa Waarabu Waislamu, kwani wao walikuwa hawauawi, kwa hivyo akaishi kwa amani chini ya kivuli cha Uislamu. Lakini atalipataje hilo na ilhali uovu unapo shindwa haurudi tena!

Mnamo mwaka wa thelathini na moja, gavana Abdullah bin Aamir alisonga mbele kwenda kuufungua mji wa Khuraasaan ambao watu wake waliasi baada ya kufariki kwa Sayyidna Umar. Alipo fika Twabasain, nayo ni milango miwili ya kuingilia mji wa Khuraasaan, wakaazi wake wakampokea kwa kutaka suluhu. Akawapa suluhu, kisha huyoo akasonga mbele kuelekea Qahastaan, akakabiliana na wakaazi wake na akapambana nao mpaka wakalazimika kuingia ngomeni mwao. Alipo fika mjini, wakaazi wake wakataka suluhu, akawaandikia suluhu kwa sharti la kutoa dirham laki saba kila mwaka. Halafu huyoo akaelekea Naisaabouri, wakaazi wake wakafanya nae suluhu kwa kuahidi kutoa dirham milioni moja kila mwaka. [TAARIKHUT-TWABARIY 02/547]

Kisha hapo akampeleka Al-Ahnaf bin Qays kukiongoza kikosi vita kwenda Twakhaaristaan. Halafu baada yake aende Murou Raudh, huko akakabiliwa na kundi kubwa la washirikina, akawaendesha mbio. Na akampeleka Al-Aqra’a bin Haabis At-tamimiy, kuliendea kundi la Wafursi lililoko Al-Jauzijaan, na akamuusia yeye na watu wake, akasema: “Enyi ukoo wa Tamim! Pendaneni na peaneni, mambo yenu yatatengenea. Na anzeni na jihadi ya matumbo yenu na tupu zenu, itatengenea dini yenu. Na wala msiweke mifundo, itasalimika jihadi yenu”.

Basi wakasonga mbele watu wale, mpaka wakakutana na adui, wakawapeleka puta na kuwashinda. Halafu tena Al-Ahnaf akaufungua mji wa Twaaliqaan kwa njia ya suluhu na akasonga mbele kuelekea Balkhi, huko nako wenyeji wakafanya ane suluhu kwa makubaliano ya kutoa dirham laki tatu. Kisha huyoo akaelekea Khawaarizm, lakini hakuweza kuufungua mji huo kutokana na upinzani mkali alio kumbana nao, akarudi.

Baada ya kazi nzito hiyo ya ufunguzi wa miji, gavana Abdullah bin Aamir akarejea baada ya kuikamilisha kazi hiyo mikubwa kwa mara ya pili. Akaambiwa: Allah hajafungua kupitia kwa yeyote kama alivyo ifungua kupitia kwako miji ya Faaris, Karmaan, Sajistaan na Khuraasaan. Akasema: Hapana ubaya, kabisa nitaifanya shukrani yangu kumshukuru Allah kwa kuniwafikisha hilo, kutoka mimi ilhali nimenuia umra hapa hapa nilipo, nikahirimie umra kutokea Naisaabouri.

Na baada ya miaka mitatu ya uongozi wa Abdullah bin Aamir katika mji wa Basrah, ilimfikia khabari ya kwamba kuna mtu mmoja aliye fikia kwa Hakeem bin Jabalah Al-Abdiy ana rai zisizo kubaliwa. Ibn Aamir akatuma watu kumuita, alipo kuja mbele yake akamuuliza: Wewe ni nani? Akajibu: Mimi ni miongoni mwa watu wa kitabu niliye upenda Uislamu na kukaa karibu yako. Akamwambia: Ni lipi litakalo nijulisha hayo, hebu niondokee. Akaondoka huyoo mpaka Koufa, huko nako akatimuliwa. Akaelekea Hijaazi na Shaamu, nako akafukuzwa. Basi akaenda Misri, huko ndiko aliko jenga kiota chake, akataga mayai na kuyaangua vikatoka vifaranga. Mtu huyo alikuwa ni Abdullah bin Sabai na mama yake ni Saudaa, na alikuwa ni Muyahudi halafu akasilimu kiuwongo akiwa na dhamira chafu. Na alikuwa na rai mbovu, miongoni mwa rai zake alikuwa akisema: Ninamshangaa anaye sadiki kurudi kwa Isa ulimwenguni na akashindwa kusadiki kurudi kwa Muhammad! Na huo ndio ulio kuwa mwanzo wa madhehebu ya “Raj-a” – imani ya urejeo. Na alikuwa akisema kwamba Imamu Aliy ndiye wasii wa Muhammad na aliporwa haki yake (ya ukhalifa) na wale walio utawalia kabla yake. Kwa hivyo basi, lililo la wajibu kwa Waislamu ni kupambana ili kuirejesha haki kwa wastahiki wake. Na waliyafuata madhehebu yake hayo, wengi miongoni mwa ambao zilichetuka akili zao. Na hiyo ikawa ni mojawapo ya sababu zilizo pelekea kukatika kwa fimbo ya utii wa Dola/khalifa na kuchangukana kwa umma wa Kiislamu. Umma ambao haunufaishwi ila na mshikamano na umoja na haudhuriwi ila na mchangukano na mfarakano.

Additional information