KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA KUBWA ZA KIYAMA: UJIO WA NABII ISA...Inaendelea

 

Allah Mtukufu anasema: “Na hawi katika watu wa kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao”. An-Nisaa [04]:159

 

Katika kuitafsiri kauli hiyo yake Allah na kumtaja mlengwa wa maneno hayo, imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas na Said bin Jubeir-Allah awawiye radhi: “Na hawi katika watu wa kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake...”. amesema: Ni kabla ya kufa kwa Nabii Isa-Amani imshukie.

 

 

Na amesema Abu Maalik: Hilo (litakuwa) kabla ya kushuka kwa Nabii Isa na kabla ya kufa kwake-Amani imshukie-hatasalia yeyote katika watu wa kitabu ila atamuamini. Na kauli hii ndio kauli ya haki ingawa zimetajwa tafsiri nyingi kuielekea aya hii, lakini bora ya kauli zote hizo kwa usahihi ni kauli hii. Ambayo inasema baada ya kushuka kwa Nabii Isa-Amani imshukie-hatasalia yeyote katika watu wa kitabu ila atamuamini kabla ya kufa kwake. Na hiyo ndio kauli sahihi, kwa sababu ndio inayo kusudiwa na mtiririko wa aya katika kuelezea ubatili wa madai ya Mayahudi katika kuuliwa na kusulubiwa kwa Nabii Isa. Allah akaeleza ya kwamba suala halikuwa hivyo kama walivyo dai wao, bali hakika si vinginevyo wao walishabihishiwa mtu mwingine, wakamuua huyo mshabihishwa pasina kutanabahi. Kisha Allah akamnyanyua kwake Mtume wake na kwamba yeye yuko hai na atashuka ulimwenguni kabla ya siku ya Kiyama, kama linavyo fahamishwa hilo na Hadithi nyingi mutawatiri. Atakapo shuka, atamuua Masihi wa upotevu (Dajjaali), atavunja misalaba na kuwauwa nguruwe. Na ataondosha kodi kwa kutoikubali na kuipokea kutoka kwa waumini wa dini isiyo Uislamu, kwani hatokubali ila Uislamu au upanga tu; mtu asilimu na akikataa auawe.

 

Na muradi na makusudiwa ya haya yote tuliyo yaeleza kuhusiana na kuwepo na kuishi mbinguni kwa Nabii Isa-Amani imshukie, na kwamba atashuka ulimwenguni kabla ya siku ya Kiyama. Ni yeye kuja kuwakadhibisha hawa Mayahudi na Manaswara ambao wamesema kauli tofauti tofauti, zenye kupingana juu yake, ambazo hazina ukweli. Mayahudi na Manaswara, wote wakachupa mipaka katika kumuelezea. Mayahudi wakamsingizia na kumzushia yeye na mama yake mambo mabaya na machafu. Na Manaswara wakampachika sifa asizo kuwa nazo, wakamuondosha kwenye daraja ya utume na kumpandisha kwenye daraja ya uungu, wakasema yeye ndiye Mungu Mwenyezi. Allah ametakata na kuepukana mbali mno na hayo wanayo yasema na hapana Mola apasaye na afaaye kuabudiwa kwa haki ila ni Yeye tu”. [Rejea MUKHTASAR TAFSIIR IBN KATHIIR 01/462-463]

 

Dalili na ushahidi wa kushuka kwa Nabii Isa-Amani imshukie-ndani ya Qur-ani.

 

Ndugu mwana jukwaa-Allah akurehemu-tambua na ufahamu ya kwamba kadhia ya kushuka kwa Nabii Isa-Amani imshukie-katika zama za mwisho, imethibiti pasina shaka ndani ya Qur-ani Tukufu na Sunna. Na huko kushuka kwake ni miongoni mwa alama kubwa za Kiyama.

 

Allah Mtukufu anasema: “Na alipo pigiwa mfano wa mwana wa Mariamu, watu wako waliupiga ukelele. Wakasema: Miungu yetu kwani si bora kuliko huyu? Hawakukupigia mfano huo ila kwa ubishi tu. Bali hao ni watu wagomvi. Hakuwa yeye (Isa) ila ni mtumwa tuliye mneemesha na tukamfanya ni mfano wa wana wa Israili. Na tungeli penda tungeli wafanyia miongoni mwenu Malaika katika ardhi wakifuatana. Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama. Basi usiitilie shaka, na nifuateni. Hii ndio njia iliyo nyooka”. Az-Zukhruf [43]:5761

 

Yaani, likusudiwalo kuelezwa na aya ni kwamba kushuka kwa Nabii Isa-Amani imshukie-kabla ya siku ya Kiyama, hiyo ni mojawapo ya alama zinazo julisha kukaribia mno kwa ile Saa ya Kiyama.

 

Na amepokea Imamu Ahmad-Allah amrehemu-kwa sanadi yake inayo kwenda mpaka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-katika kuitafsiri aya hii “Na kwa hakika yeye ni alama ya Saa ya Kiyama”. Amesema: “Huko ni kutoka kwa Nabii Isa mwana wa Mariamu-Amani imshukie-kabla ya siku ya Kiyama”. Ahmad [04/329]-Allah amrehemu.

 

Na kwa sababu ya umuhimu wa maudhui haya ya ujio wa Nabii Isa-Amani imshukie-ndio Qur-ani Tukufu ikatawala na kubeba dhima ya kuzirudi (kuzijibu) shubuha zilizo zushwa na kupikwa na Mayahudi wakidai kumuua na kumsulubu Nabii Isa.Ndipo Allah Mtukufu akasema: “Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Allah, nao hawakumuua wala hawakumsulubu, bali walifananishiwa tu. Na hakika walio khitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuua kwa yakini. Bali Allah alimtukuza kwake, na hakika Allah ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima. Na hawi katika watu wa kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao”. An-nisaa [04]:157-159]

 

Aya zote hizi, kama ambavyo zinavyo fahamisha ya kwamba Mayahudi hawakumuuana wala hawakumsulubu Nabii Isa-Amani imshukie-kama linavyo tajwa hilo na kauli yake Mola: “Pale Allah alipo sema: Ewe Isa! Mimi nitakutwaa kwangu (kwa roho na mwili), na nitakunyanyua kwangu, na nitakutakasa na wale walio kufuru...”. Aali Imraan [03]:55

 

Basi pia, aya hizo zinajulisha ya kwamba wamo miongoni mwa watu wa kitabu ambao watakao muamini Nabii Isa-Amani imshukie-katika zama za mwisho. Na hilo litakuwa wakati ule wa kushuka kwake ulimwenguni baada ya kunusuriwa na Allah dhidi ya kuuliwa na Mayahudi na kabla ya kufa kwake. Kama linavyo thibitishwa hilo na hadithi nyingi sahihi zilizo kuja kwa njia ya tawatiri.

 

Dalili na ushahidi wa kushuka kwa Nabii Isa-Amani imshukie-ndani ya Sunna (Hadithi).

 

Ama kwa upande wa Sunna, zimepokewa hadithi nyingi sahihi zinazo fumbuliza wazi ujio na kushuka kwa Nabii Isa-Amani imshukie-katika zama za mwisho, miongoni mwa hadithi hizo, ni pamoja na ile iliyo pokewa kutoka kwa:

 

Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mkononi mwake, hakika kabisa anakurubia kukushukieni Mwana wa Mariamu akiwa ni hakimu muadilifu, basi ataivunja misalaba, atawauwa nguruwe na ataondosha kodi. Na mali itatapakaa kiasi cha kufikia kutokukubaliwa na mtu (akipewa) na mpaka ifikie sijida moja kuwa ni  bora kuliko Dunia na vilivyomo humo”.

 

Kisha akasema Abu Huraira: Na someni mkipenda (kauli yake Allah): “Na hawi katika watu wa kitabu ila hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye siku ya Kiyama atakuwa shahidi juu yao”. Bukhaariy [06/490-491] FAT-HUL-BAARIY & Muslim [02/189-191] SHAR-HUN-NAWAWIY.

 

Na imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Litaendelea kuwa katika umati wangu kundi linalo pigana upande wa haki, likinusurika mpaka siku ya Kiyama. Akaendelea kusema: Basi atashuka Isa mwana wa Maryamu-Amani imshukie-(kwenye kundi hilo), atasema Amiri wao (kumwambia Nabii Isa): Tuswalishe. (Nabii Isa) atamjibu: Hapana, hakika baadhi yenu nyinyi ni maamiri kwa wenzenu, hiyo ni takrima ya Allah kwa umma huu”. Muslim [03/193-194] SHAR-HUN-NAWAWIY.

 

Na imepokewa kutoka kwa Abu Huraira-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mitume ni kama ndugu ambao mama zao ni wake wenza; mama zao ni tofauti na itikadi yao ni moja. Na mimi ni mbora wa watu wote kwa Isa mwana wa Mariamu, kwani hapakuwepo baina yangu na yeye mtume yeyote (aliye letwa kati yetu). Na hakika yeye atashuka na mtakapo muona, basi mtambueni”. Ahmad [02/406] & Al-Haakim [02/595]-Allah awarehemu.

 

Additional information