KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

KUMSAIDIA BABA/BABU KUJIZUIA NA MACHAFU

Kunamuwajibikia mtoto, awe ni wa kiume au yule wa kile, awe ni muislamu au kafiri, kumsaidia baba yake kupata kinga dhidi ya dhambi/uchafu wa zinaa, na mfano wa baba katika kadhia hii, ni babu, ni mamoja amekuwa ni babu kwa upande wa baba (babu mzaa baba), au ni kwa upande wa mama (babu mzaa mama). Hali kadhalika, ni mamoja amekuwa ni muislamu (babu huyo) au ni kafiri. Na huko kumsaidia ni kumpa mahari ya kuolea mwanamke huru (muungwana). Au amwambia: Oa mimi nitakupa mahari.

 

Lakini, ili hili la kumsaidia baba/babu kujizuia na zinaa limuwajibikie mtoto huyu, kumeshurutizwa kupatikana kwa sharti tatu hizi:

1.         Mtoto huyo awe ni mkwasi (mwenye uwezo) wa kutoa mahari hayo.

2.         Baba na mfano wake ni babu, awe mtwefu (asiye na uwezo) wa kutoa mahari.

3.         Baba/babu awe anakuhitajia huko kuoa, na hivi ni kuwa nafsi yake inatamani kuoa.

   Na wajihi wake: Ni kwamba huku kumsaidia baba/babu kujiepusha na zinaa kwa kumuwezesha kuoa, kunaingia katika mlango wa mahitaji yake muhimu; ya lazima, kama vile chakula na nguo.

Na ili asimuambalizie kwenye zinaa inayo pelekea katika hilaki na maangamivu na hili halirandani na utukufu wa daraja ya ubaba. Na hilo halimo katika wajihi wa kusuhubiana kwa wema kunako amrishwa na kauli yake Atukukiaye: “...LAKINI KAA NAO KWA WEMA DUNIANI...” [31:15]

 

Þ    Ndoa za makafiri:

         Ndoa za makafiri wao kwa wao, ni SAHIHI mbele ya macho ya Uislamu. Na dalili/ushahidi wa hili ni ile hadithi ya Ghailaan na wenginewe miongoni mwa walio silimu wakiwa na zaidi ya wake wanne. Hakika Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimuamuru kubakia na wake wanne tu na awataliki wale wengine.

Kwa kuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakumuuliza juu ya sharti za ndoa zao, kwa ajili hii basi hakutuwajibikii sisi kulipekua hilo. Na lau watasilimu, tutazikiri ndoa zao; hatutowafungisha ndoa upya kwa mujibu wa taratibu/sharti za Kiislamu.

 

Þ    Kusilimu kwa makafiri baada ya kufunga ndoa kwao:

         Mwanamume atakapo kuwa kafiri na akawa na mke kafiri, kisha wote wawili; mke na mume wakasilimu, ndoa yao hiyo ya ukafirini itadumu (itaendelea) katika Imani yao hii mpya (Uislamu). Hivi ndivyo ilivyo, kwa sababu ufarakano/utenganishi, hakika si vinginevyo hutokea kwa sababu ya ikhtilafu (tofauti) ya dini. Na wawili hawa haikukhitalifiana dini yao katika kipindi cha ukafiri, wala ndani ya Uislamu.

Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Abdullah Bin Abbas-Allah amuwiye radhi: “Kwamba mwanamume mmoja alikuja hali ya kuwa ni muislamu katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kisha akaja mkewe hali ya kuwa nae ni muislamu. Akasema (yule mwanaume): Ewe Mtume wa Allah! Hakika yeye (huyu mwanamke) alikuwa amesilimu pamoja nami, basi (naomba) umrejeshe kwangu. Mtume akamrudisha kwake”. Tirmidhiy [1144] & Abu Daawoud [2238]-Allah awarehemu.

Ama atakapo silimu mwanamume na mwanamke akaendelea kushikilia ukafiri;

(a)     Angalia, mwanamke huyo akiwa ni mtu wa kitabu (Myahudi au Mnaswara, itadumu ndoa yake (huyu muislamu) na mwanamke huyo, kwa sababu ya kujuzu muislamu kumuoa mwanamke Ahlu Kitaab.

(b)     Angalia, mwanamke huyo akiwa ni muabudu sanamu au mpagani na hakusilimu katika kipindi cha eda yake. Huvunjika ndoa baina ya wawili hawa tangu pale alipo silimu mwanamume.

(c)     Ama akisilimu ndani ya kipindi cha eda; yaani kabla ya kumalizika kwake, hakika hali ilivyo ndoa huendelea kusalia baina ya wawili hawa.

(d)     Lau mwanamke ndiye atakaye silimu na mwanamume akaendelea na ukafiri wake. Hakika hali ilivyo, watatenganishwa tangu kusilimu kwake huyu mwanamke, ila atakapo silimu mwanamume huyu ndani ya kipindi cha eda ya mwanamke huyu. Hakika hapo mwanamke huyu atarejeshwa kwa mwanamume huyo kwa nafsi ya ndoa iliyo tangulia.

Ama akirejea akasilimu baada ya kumalizika kwa eda yake, hakika hatarejeshwa kwake ila kwa ndoa mpya itakayo fungwa kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu.

Amrou Bin Shuaib amepokea kutoka kwa baba yake, ambaye nae amepokea kutoka kwa babu yake: “Kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimrejesha binti yake Zainabu kwa Abul-Aaswi Bin Rabee kwa mahari mpya na ndoa mpya”. Tirmidhiy [1142]-Allah amrehemu.

Additional information