KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UMOJA ...Inaendelea

Hakika amali moja (tendo moja la ibada) katika hakika halisia yake na sura (taswira) yake, ujira wake unatofautiana kwa kiwango kikubwa pale anapo itenda (amali hiyo) mtu akiwa peke yake na pale anapo itenda (amali hiyo hiyo) akiwa pamoja na wenzake. Hakika rakaa mbili za swala ya Alfajiri na rakaa nne za swala ya Adhuhuri, ni zile zile hazizidi kitu pale mtu anapo pendelea kuziswali pamoja na jamaa (kundi la waumini wenzake), kuliko kuziswali katika upeke yake. Pamoja na hivyo, kwamba idadi ya rakaa ni ile ile haizidi, lakini Uislamu umeurudufisha ujira wake kwa mara ishirini na kitu, pale mtu anapo simama mbele ya Allah pamoja na wenzake wakaabudu kwa pamoja, nyuma ya kiongozi mmoja.

Na huu ni ushakizi mkubwa unao msukuma mja kujumuika msikitini pamoja na waumini wenzake na kuacha kujitenga peke yake. Na unamsukuma mtu kujitoa kwenye upeke yake na kujichanganya na umma wake. Hakika Uislamu; dini na mfumo kamili wa maisha, unachukia na haupendi muislamu kujifungia kwenye wigo wa nafsi yake na kuwa mpweke katika fikra na hisia zake. Na kujitenga na maslahi yake binafsi na kutokushughulika na yale maslahi ya umma. Imepokewa katika hadithi: “Moyo wa mtu muumini usifanye mfundo kwenye mambo matatu; kufanya amali kwa ikhlaasi kwa ajili ya Allah, kuwanasihi viongozi wa Waislamu na kulazimiana na jamaa (kundi) yao. Kwani hakika dua yao inawazunguka kwa nyuma yao”. Al-Bazzaar-Allah amrehemu.

Lakini muislamu anatakiwa kujichanganya na jamii anayo ishi humo. Na ili kuliendea na kulifikia hilo, Allah akaweka sharia ya kuswaliwa swala tano za kila siku kwa jamaa na akaraghibisha kuzihudhuria misikitini na kuzikithirisha hatua katika kuziendea. Kisha tena akawalazimishia watu wa kijiji kidogo au kitongoji chenye kukaliwa, kukutana wote pamoja mara moja kila juma kwa ajili ya kuitekeleza swala ya Ijumaa. Si hivyo tu, kisha akauita mkusanyiko mkubwa zaidi kuliko ule wa swala ya Ijumaa katika kila juma, katika swala ya Eid. Na akafanya mahala pake pa kuswaliwa kuwa ni uwanja wenye wasaa ulio nje ya mji/kitongoji na akawaamrisha wanaume na wanawake hata wale walio katika ada yao ya mwezi, kwenda mahala hapo, ili manufaa yapate kutimia na kheri izidi. Kisha tena akatoa tangazo la kongamano kubwa mno, linalo wakusanya waumini wa rangi, jinsia, makabila na mataifa mbali mbali, kutoka Mashariki na Magharibi, Kaskazini na Kusini. Ili lipatikane kongamano kubwa hilo lisilo na mfano ulimwenguni, ndipo akaifaradhisha ibada ya Hija na kuifanya kuwa ni mojawapo ya nguzo tano za Uislamu. Na akaiwekea ibada hiyo mahala maalumu na kipindi maalumu cha kutekelezwa, ili kulifanya suala la kukutana baina ya jinsia za Waislamu kuwa ni jambo la faradhi.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akitahadharisha sana dhidi ya miisho na matokeo mabaya ya utengano na mfarakano. Na alikuwa katika ukaazi wake (kuwepo kwake mjini) na katika kusafiri kwake, akiusia kukusanyika na kuwa kitu kimoja. Imepokewa kutoka kwa Saeed bin Al-Musayyab-Allah amuwiye radhi: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Shetani hushughulika na mtu mmoja na wawili, wanapo kuwa watatu hashughuliki nao”. Maalik-Allah amrehemu.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikwisha ona katika safari yake, ya kwamba msafara unapo piga kambi mahala kwa ajili ya kupumzika, watu hutapanyika huku na huko, kama kwamba hapana mafungamano baina yao. Akachukizwa na mandhari ile na akakerwa nayo. Imepokewa kutoka kwa Abu Tha’alabah-Allah amuwiye radhi: Watu walikuwa wanapo piga kambi mahala, hutapanyika kwenye vijia vya majabalini na makorongoni. Hapo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Hakika kutapanyika kwenu kunatokana na shetani. Basi baada ya hapo hawakupiga kambi mahala, ila walichanganyika mpaka panasemwa: Lau ingeli kunjuliwa nguo (shuka) juu yao, basi ingeli waenea wote”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Hiyo ndio athari ya kuchanganyika kwa hisia na kubadilishana upendo na kukamatana kwa safu. Hakika watu kama hawakukusanywa pamoja na haki, basi watatapanywa na batili na kama hawakuunganishwa na ibada ya Rahmaani – Mwingi wa rehema – basi watachanwa chanwa na ibada ya shetani. Na kama hawakupendezwa na kuathiriwa na neema za Akhera, basi watahasimiana katika kugombea starehe zipumbazazo za Dunia.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Msirejee baada yangu (kuwa) makafiri (tena), mkiuana wenyewe kwa wenyewe”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Mtume wa Allah anakusudia kusema ya kwamba huu umwagaji damu, ni jambo la makafiri walio gawanyika makundi makundi yenye kuchinjana.

Uislamu umekuwa na sera laini katika kadhia nzima ya kukhitalifiana akili katika ufahamu na uoni wa mambo. Na ukampa mkosaji ujira mmoja kwa sababu ya kuitumia akili yake katika kulifahamu suala fulani, lakini akafahamu sivyo. Na mpatiaji akapewa ujira mara mbili, kwa kuitumia vema akili yake katika kufahamu na akafahamu ndivyo. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakapo fanya ijitihadi hakimu, akapatia basi ni wake ujira mara mbili. Na akifanya ijitihadi na akakosea, basi ni wake ujira mmoja”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Ndugu msomaji wetu mwema-Allah akurehemu-kupitia maelezo haya unaona ni namna gani rehema za Allah zinavyo fungamana na natija/matokeo ya fikra za waja wake, kwa kadiri ya kufungamana kwake (fikra hizo) na makusudio/nia tengenezi. Basi ni kwa nini uwezo wa mwanaadamu ukifanye finyu kile kilicho kunjuliwa na dini ya Allah?! Na ni kwa nini pawepo baina yao ukatili na utendana ubaya?!

Pale ambapo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo waamrisha mujahidina wa kutoka Madina, ya kwamba wasiswali swala ya Laasiri ila kwa Baniy Quraydhwah. Basi baadhi yao waliiawili (waliitafsiri) amri hiyo ya kwamba ni iwapo hautatoka wakati wa swala, kwa taawili hiyo wao wakaiswali Laasiri njiani, kabla ya kufika huko waliko amrishwa kwenda. Na kundi jengine likaichukulia nassi ya amri kwa maana yake ya dhaahiri, bila ya kuifanyia taawili, kwa maono yao hayo wakawa wameiswali swala ya Laasiri wakati wa kiza. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaukubali ufahamu wa makundi yote mawili, kisha akayapanga yote mawili safu moja na jeshi moja kumuelekea adui.

Hiyo ndio roho ya Uislamu katika kufumbua na kutatua khilafu (tofauti) za kielimu. Na hivyo ni pale ambapo hakuna pa kuikimbia khilafu hiyo wakati ambao dhamira zinakuwa njema. Ama pale khilafu itakapo fanywa kuwa ni windo la kuipatia Dunia na umaarufu, ikaletwa khilafu kwa sababu ya inda na chuki, hapo dini imesha potea (haipo).

Sheikh mmoja aliambiwa: Nenda kawawahi watu msikitini, wanakaribia kuuana. Akauliza: Wanataka kuuana kwa lipi? Akajibiwa: Kuna baadhi yao wanataka kuswali Tarawehe rakaa nane na wengine wanataka kuswali rakaa ishirini. Akauliza: Halafu ikawaje? Akaambiwa: Wanasubiri fat-wa yako. Akasema: Fat-wa yangu mimi ni kwamba msikiti ufungwe na usiswaliwe kabisa Tarawehe. Kwa sababu hiyo Tarawehe haivuki zaidi ya kuwa ni Sunna na umoja wa Waislamu ni FARADHI. Kwa hivyo kufanya hivyo ndio bora na ndio kuwa mbali na ghasia/fujo hatarishi zinazo weza kutokea kutokana na masuala hayo.

Ili kwenda sanjari na mafundisho ya Uislamu katika kuulinda/kuuepusha umma na masaibu ya mipasuko, maulamaa-Allah awarehemu-wametoa fat-wa ya kwamba hakulazimu kuuondosha munkari, iwapo uondoshaji wake utapelekea kwenye maharibiko makubwa zaidi. Kwani kuendelea kubakia kwa munkari huo ni madhara, lakini kutokea kwa maharibiko andamizi hayo ni madhara makubwa mno. Kwa ajili hiyo basi, kwa mujibu wa kanuni za Usuli litatendwa lile lenye madhara khafifu kati ya mambo mawili hayo ambayo yote yana madhara, lakini kwa kiwango tofauti. Hivi kwani ndugu msomaji huoni/hujui kwamba daktari haufanyii operesheni mwili, ila tu pale atakapo ona na kujiridhisha ya kwamba mwili huo unaimudu na kuiweza operesheni hiyo?! Na atakapo ona kupitia vipimo vyake ya kwamba operesheni hiyo itayahatarisha maisha ya mgonjwa, huacha kuifanya hata kama maradhi yataendelea kusalia mwilini mwa mgonjwa?!

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiwalisha kiapo Answaari “juu ya usikivu na utii katika uzito na wepesi, na katika hali ya machangamfu na machukivu, na juu ya kutupendelea sisi...”. Muslim-Allah amrehemu.

Likusudiwalo ni kwamba mtu mwema anatakiwa asijali na wala asipapatike kwa kulikosa fungu lake la Dunia. Utakapo fanyika uzembe/njama asipewe cheo/madaraka au akapunjwa/akadhulumiwa katika kiwango cha mshahara anao stahiki. Hazijazi pambizo za anga kwa makelele na ghasia. Kwani kughadhibika kwa ajili ya Dunia kwa namna hii imtiayo doa mtu, ni nembo ya wanafiki ambao Allah Atukukiaye amesema kuwakhusu: “NA MIONGONI MWAO WAPO WANAO KUSENGENYA KATIKA KUGAWA SADAKA. WANAPO PEWA WAO HURIDHIKA. NA WAKITOPEWA HUKASIRIKA”. [09:58]

Additional information