KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA KUBWA ZA KIYAMA: DAJJAAL ATATOKEA WAPI ?

 

Kwa mujibu wa ilivyo elezwa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ni kwamba Dajjaali atatokea pande za Mashariki, kwenye eneo la Khuraasaani, kupitia kwa Wayahudi wa Aswbihaani. Kuanzia hapo basi, ataenda ulimwenguni kote, hatauacha mji/nchi ila atapita na kuingia humo, isipokuwa miji miwili tu, Makka na Madina. Hataweza kupenya na kuingia kwenye miji mitakatifu hiyo, kwani itakuwa inalindwa na Malaika watakao mzuia kuingia kwa amri yake Allah na kwa hekima anazo zijua Yeye Mwenyewe.

 

 

Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-amesema: Alituhadithia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Dajjaali atakuja akitokea kwenye upande wa Mashariki wa ardhi (Dunia), unao itwa Khuraasaani”. Tirmidhiy & Al-Haakim-Allah awarehemu.

 

Na imepokewa kutoka kwa Anas-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Dajjaali atatokea kwa Wayahudi wa Aswbihaani, akiambatana na Wayahudi sabini elfu”. Ahmad-Allah amrehemu.

 

Na huku kutoka kwa Dajjaali kutafuatia ushindi wa Imamu Mahdiy dhidi ya Warumi, ushindi huo utamkera mno na kumchochea Dajjaali kutoka kwenye maficho yake, kama ilivyo kuja katika hadithi: “...hakika yeye atatoka kwa sababu ya ghadhabu...”. SAHIH MUSLIM [7543]-Allah amrehemu.

 

Ila tu ni kwamba mwanzo tu atakapo toka, ataanza na kuhubiri imani, dini, swala na uchaMngu ili kuwachombeza watu wampende, wamkubali na wamfuate. Na ataendelea kupata makundi ya watu mpaka atafika Koufa nchini Iraq, hapo ndipo atakapo anza kudai utume, kwa madai yake hayo watu watagawanyika; wapo watakao mkubali an wengine watakamkataa na kujitenga nae. Na baada ya hapo, sasa ndio atadai uungu kuwa yeye ndiye Mungu Mwenyezi, kuyaandamia madai yake hayo zitadhihiri wazi alama za ukafiri na udajali wake.

 

Al-Haafidh Ibn Hajar-Allah amrehemu-amesema: “Ama kwa suala la wapi atatokea. Ni upande wa Mashariki, kwa kauli ya kutinda”. Rejea [FAT-HUL-BAARIY 13/328]

 

Na Imamu Ibn Kathiir-Allah amrehemu-amesema: “Mwanzo wa kudhihiri kwake kutakuwa ni Aswbihaani, katika kitongoji kinachoitwa Al-Yahuudiyyah”. Rejea [AN-NIHAAYAH 01/128]

 

Naam, hayo yaliyo semwa ndivyo sawa khasa, lakini kudhihiri kwa jambo lake kwa Waislamu kutakuwa wakati ambapo atakapo fika mahala paliopo baina ya Iraq na Shamu (Syria). Imekuja katika hadithi iliyo pokewa na Nawaasi bin Sam’aan: “Hakika yeye ni mwenye kutokea kwenye eneo la mpaka baina ya Shamu na Iraq, basi atafanya ufisadi upande wa kulia na atafanya ufisadi upande wa kushoto. Enyi waja wa Allah! Thibitini (katika imani yenu)”. Muslim [2937]-Allah amrehemu.

 

  • Wafuasi wa Dajjaali.

 

Ndugu mwanajukwaa letu-Allah akurehemu na akunufaishe na jukwaa hili-sote kwa pamoja tukae kwa utulivu, umakini na usikivu, tumsikilize Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akitutajia na kutuelezea wafuasi wa Dajjaali. Kwa mujibu wa hadithi zilizo pokewa, ni kwamba sehemu kubwa ya wafuasi wa Dajjaali watakuwa ni Wayahudi, Waajemi (wasio Waarabu), Waturuki na mchanganyiko wa watu wengine, wengi wao wakiwa ni mabedui (wakaazi wa jangwani) na wanawake.

 

Imepokewa kutoka kwa Anas bin Maalik-Allah amuwiye radhi-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Watamfuata Dajjaali katika Wayahudi wa Aswbihaani sabini elfu wakiwa wamevaa mavazi maalumu ya kijani”. Muslim [18/85]-Allah amrehemu.

 

Na katika upokezi wa Imamu Ahmad: “...sabini elfu wakiwa wamevaa mataji”. Ahmad [Rejea FAT-HUL-BAARIY 13/238]-Allah amrehemu.

 

Na Wayahudi wanamtambua Dajjaali kwa jina la “Masihi mwana wa Dawoud”, nao wanadai ya kwamba yeye atatoka katika zama za mwisho na utawala wake utafika bara na baharini na itatembea pamoja naye mito. Nao wanadai ya kwamba yeye Dajjaali ni mojawapo ya aya/ishara/dalili za uwepo wa Allah na ndiye atakaye warejeshea utawala wao. [Rejea LAWAAMI’UL-ANWAAR AL-BAHIYYAH 02/112]

 

Na ama kule kusemwa kwamba wengi wa wafuasi wake ni katika mabedui, ni kwa sababu ya kutawaliwa kwao na ujinga na kwa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-iliyomo katika hadithi ndefu iliyo pokewa na Abu Umaamah-Allah amuwiye radhi: “... na hakika miongoni mwa fitina zake (huyo Dajjaali) ni yeye kusema kumwambia bedui: Unaonaje, nikikufufulia baba yako na mama yako, utakiri kwamba mimi ni Mola Mlezi wako? Aseme (huyo bedui): Ndio, basi watamtokea yeye mashetani wawili wakiwa katika sura ya baba yake na mama yake, wamwambie: Ewe mwanangu! Mfuate, hakika yeye ndiye Mola Mlezi wako...”. Ibn Maajah & Al-Haakim-Allah awarehemu.

 

Na ama kule kusemwa kwamba wengi wa wafuasi wake ni wanawake, ni kwa sababu hali yao wao ni kubwa mno kuliko ya mabedui kutokana na kuathirika kwao haraka na jambo au maneno na kutawaliwa na ujinga.

 

Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atashukia Dajjaali kwenye ardhi hii ya kinamasi (swampland) katika jangwa la Marqanaah, na wengi watakao toka kumfuata watakuwa ni wanawake. Kiasi cha kufikia mwanaume kurejea kwa mwandani wake (mkewe), mama yake, binti yake, dada yake na shangazi yake na kuwafunga kamba, kwa kuchelea wasije kutoka kumfuata”. Ahmad [5353]-Allah amrehemu.

 

Additional information