KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

NGUZO ZA KIFUNGO CHA NDOA

Ndoa kama taasisi/kiwanda mama cha kuzalisha na kuiendeleza jamii bora ya kizazi cha wanaadamu wenye utu na maadili, ina nguzo tano kama zifuatavyo:

       I.       Nguzo ya kwanza: Tamko la ndoa (swigha):

Tunakusudia kwa ibara “Tamko la ndoa”: IJAABU (Tamko la kutoa/kukabidhi) itokayo kwa walii wa mke. IJAABU ni ile kauli ya walii kumwambia mume mtarajiwa: “Nimekuoza binti yangu” au “Nimekufungisha ndoa na binti yangu”. Na kwa upande wa pili ni QABUUUL (tamko la kupokea/kustakabadhi) itokayo kwa muoaji (mume). Qabuul ni kauli ya mume mtarajiwa kumwambia walii wa mke: “Nimemuoa binti yako” au “Nimefunga ndoa na binti yako”.

 

 

Kunasihi kutangulia tamko la mume (Qabuul) mbele ya tamko la walii (Ijaabu), hii ni kwa sababu kutangulia na kuchelewa ni sawa sawa katika kufidisha makusudi/madhumuni.

 

 

 

Þ       Hekima/Falsafa ya kushariiwa kwa tamko la ndoa:

 

         Hekima iliyopo ni kwamba kwa kuwa kifungo cha ndoa ni miongoni mwa vifungo ambavyo hapana budi ipatikane ndani yake radhi ya wafunga kifungo wawili/pande mbili. Na kwa kuwa hiyo radhi yenyewe ni jambo lililo fichikana, la moyoni mwa mtu, halichomozewi na yeyote zaidi ya muhusika wake. Hapo ndipo sheria ilipo lizingatia tamko la ndoa ambalo ndio ile “Ijaabu” na “Qabuul”, kuwa ni dalili ya dhaahiri ya radhi iliyomo ndani ya nafsi ya kila mmoja wa wana kifungo.

 

 

 

Þ       Sharti za tamko la ndoa:

 

         Zimeshurutizwa katika tamko la ndoa sharti zifuatazo:

 

                       1.       Liwe kwa tamshi la ndoa au kuoa: Na kwa maneno/ibara zichimbukanazo kutokana na isimu/nomino mbili hizi. Kama vile walii wa binti kusema kumwambia muoaji (mume mtarajiwa): “Nimekuoza” au “Nimekufungisha ndoa”. Na kauli ya mume kumjibu walii: “Nimekubali kumuoa” au “Nimekubali kufunga nae ndoa”.

 

Na hakika si vinginevyo, yameshurutizwa matamko ya “ndoa”, “kuoa” na yanayo chimbuka kutoka katika matamko mawili hayo. Kwa sababu matamko mawili hayo ndio matamko yaliyo wekwa katika lugha na sheria juu ya kufahamisha kifungo cha ndoa. Na matamko mawili haya ndio yaliyo tumika katika nukuu (nassi) za Qur-ani na Sunnah (Hadithi). Katika Qur-ani Tukufu matamko hayo yametumika katika kauli zifuatazo za Allah Ataadhamiaye: “...BASI OENI MNAO WAPENDA KATIKA WANAWAKE, WAWILI AU WATATU AU WANE...” [04:03]  “...BASI ZAID ALIPO KWISHA HAJA NAYE TULIKUOZA WEWE, ILI ISIWE TAABU KWA WAUMINI KUWAOA WAKE WA WATOTO WAO WA KUPANGA...” [33:37]

 

Na katika Sunnah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Enyi kusanyiko la vijana! Atakaye weza miongoni mwenu kuishi na mke (gharama za ndoa na siha ya jimai), basi na aoe....”.

 

 

 

                       2.       Kufumbuliza tamko la ndoa au kuoa katika Ijaabu na Qabuul: Angalia, lau walii atasema kumwambia muoaji: “Nimekuoza binti yangu”. Yule muoaji nae akasema: “Nimekubali” tupu tupu tu bila ya kuongezea neno “kumuoa”, ndoa haijafungamana; yaani kisheria bado hapana ndoa hapo. Na kinyume chake, lau muoaji atamwambia walii: “Nioze binti yako”, walii akasema: “Nimekubali”, akakomelea hapo tu, bila ya kuongeza neno “kukuoza”, pia ndoa haijafungamana. Ndoa haikufungamana kwa sababu wawili hao; muoaji na walii hawakuyafumbuliza matamko ya ndoa au kuoa.

 

 

 

Kufunga ndoa kwa lugha isiyo Kiarabu.

 

         Kunasihi kufunga ndoa kwa lugha za Kiajemi, nazo ni zile lugha zote zisizo Kiarabu; yaani ukikiweka kando Kiarabu. Kwa mantiki hii basi, lau Ijaabu na Qabuul zitapatikana kwa lugha ya Kiajemi, kifungo cha ndoa kitasihi hata kama walii na muoaji wanajua lugha ya Kiarabu. Ndoa itasihi kwa kuzingatia maana.

 

 

 

Kufunga ndoa kwa matamko fumbo/ficho (kinaaya):

 

         Hakusihi kufunga ndoa kwa matamko fumbo; yasiyo beba maana ya wazi wazi na ya moja kwa moja ya dhana ya ndoa/kuoa, kwa lugha yoyote ile iwayo. Na matamko fumbo ni yale ambayo yanabeba kwa wakati mmoja, maana ya ndoa na kitu kingine. Haya ni pamoja na walii kusema: “Nimekuhalalishia binti yangu” au “Nimekupa hiba binti yangu”. Ndoa haitasihi, kwa sababu matamko fumbo yanahitajia nia, na ijulikanavyo nia mahala pake ni moyoni. Na kifungo cha ndoa kimeshurutiziwa uwepo wa mashahidi na ni jambo lijulikanalo wazi kwamba mashahidi hawayachomozei yaliyomo nyoyoni. Hata waweze kushuhudia ikiwa wafunga ndoa wamenuia ndoa au jambo jingine.

 

 

 

Kufunga ndoa kwa maandishi:

 

         Kama ambavyo ndoa isivyo fungamana kwa matamko fumbo, ni hivyo hivyo haifungamani kwa maandishi. Ni sawa sawa wafunga ndoa wamekuwapo katika kifungo hicho au hawapo.

 

Kwa maana hii basi, lau walii wa mke atamuandikia muoaji aliyepo hapo au ambaye hayupo: “Nimekuoza binti yangu”. Na waraka (maandishi hayo) ukamfikia mume nae akausoma, kisha akasema: “Nimekubali kumuoa binti yako”. Ndoa hiyo haitasihi, kwa sababu maandishi ni katika jumla ya matamko fumbo na ndoa haifungamani kwa matamko fumbo.

 

 

 

Ishara ya bubu yenye kufahamika:

 

         Ama ishara ya bubu yenye kufahamisha, na hii ni ile ambayo muradi wake unafahamika na watu wote; wenye elimu/ujuzi wa lugha ya bubu na wasiyo nao. Hakika bila ya shaka ndoa inafungamana kwa kupitia ishara hiyo, kwa sababu ishara hiyo inashuka (inakaa) katika daraja (mahala) la tamko fumbulizo.

 

Ama ishara yake itakapo kuwa imefichikana kiasi cha kutokufahamika ila tu na watu maalumu; wenye utambuzi wa ziada wa lugha ya bubu. Ndoa haitafungamana kwa kutumia ishara hiyo, kwa sababu wakati huo ishara hiyo inakaa mahala pa matamko fumbo. Na ndoa haifungamani kwa matamko fumbo.

 

 

 

                       3.       Ijaabu kuungana (kushikamana) na Qabuul: Na katika jumla ya sharti za tamko la ndoa ni Ijaabu ya walii kuungana na Qabuul ya muoaji. Basi lau walii wa mke atasema: “Nimekuoza binti yangu”, kisha muoaji akanyamaa kwa muda mrefu, halafu ndipo akasema: “Nimekubali kumuoa”. Ndoa haitasihi, kwa sababu ya uwepo wa kipambanuzi/kitenganishi kirefu baina ya Ijaabu na Qabuul. Kitenganishi ambacho kinalifanya suala la walii kughairi ndoa kuwa ni jambo liwezekanalo. Ama kinyamao kifupi, kama vile kile cha kupumua au kupiga chafya, hicho hakidhuru katika kusihi kwa ndoa.

 

 

 

                       4.       Kubakia kwa ustahiki wa wafunga ndoa mpaka kutimia kwa Qabuul: Lau walii wa mke atasema: “Nimekuoza binti yangu”, lakini kabla ya kupatikana kwa Qabuul ya muoaji walii akapatwa na wazimu au akazimia. Muoaji akakubali, ndoa haikusihi.

 

Na kadhalika, lau muoaji atasema: “Nioze binti yako”, kisha mara tu baada ya kutamka hayo, akazimia kabla ya walii wa mke kusema: “Nimekuoza”. Ijaabu hiyo itakuwa batili na ndoa haitasihi hata kama Qabuul imepatikana. Kwa sababu ya kukosekana kwa ustahiki wa mmoja wa wafunga kifungo cha ndoa kabla ya kutimia kwa kifungo hicho.

 

 

 

                       5.       Tamko la ndoa liwe ni la kutinda/kukata: Kwa hivyo basi, hakusihi kukiegemeza kifungo cha ndoa kwa mustakabali (muda ujao) wala kukitundikia sharti. Basi lau walii wa mke atasema: “Utakapo fika mwezi wa Ramadhani, hakika nimekuoza binti yangu”. Mume mtarajiwa nae akasema: “Nimemuoa”, ndoa haijasihi. Na lau walii wa mke atasema: “Ikiwa binti yangu amefaulu mtihani, basi hakika nimekuoza”. Muoaji akasema: “Nimekubali kumuoa”, pia ndoa haitasihi, kwa sababu kifungo cha ndoa ni wajibu kiwe cha kutinda. Zinaandamia juu yake athari zake tangu pale kinapo fungwa. Kwa ajili hiyo basi, kukiegemeza na mustakabali au kukitundikia sharti, kunapelekea kuzichelewesha hukumu za ndoa mpaka wakati ujao au mpaka kupatikana kwa sharti. Na hilo linapingana na muktadha wa kifungo cha ndoa.

 

 

 

                       6.       Tamko la ndoa liwe huru: Kwa sharti hili basi, hakusihi kuiwekea ndoa muda maalumu, kama vile mwezi mmoja au mwaka mmoja. Au muda usio julikana, kama vile ujio wa mtu ambaye hayupo. Angalia, lau walii wa mke atasema: “Nimekuoza binti yangu kwa muda wa mwezi mmoja/mwaka mmoja/mpaka kuja kwa fulani”. Mume akasema: “Nimekubali kumuoa”, ndoa haitafungamana katika sura zote hizi, kwa sababu hiyo ni katika jumla ya ndoa za mut’a zilizo harimishwa.

 

Imepokewa kutoka kwa Sabrah Al-Juhaniy-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye alikuwa pamoja na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema (Mtume): “Enyi watu! Hakika mimi nilikuwa nimekupeni ruhusa ya kustarehe na wanawake kwa ndoa ya mut’a (ya muda maalumu). Hakika Allah ameiharimisha (ndoa) hiyo mpaka siku ya Kiyama, basi yeyote mwenye mke aliye tokana na ndoa hiyo na amuache huru na wala msitwae chochote katika vile mlivo wapa”. Muslim [1406]-Allah amrehemu.

 

 

 

Ndoa ya mpeano/nipe nikupe iso mahari (shighaari):

 

         Haisihi ndoa ya mpeano, nayo ni walii wa mke kusema kumwambia mtu: “Nimekuoza binti yangu kwa sharti na wewe unioze binti yako, na utupu wa kila mmoja wao ndio mahari ya mwingine”. Na aseme yule mtu mwingine: “Nimemuoa binti yako na nimekuoza binti yangu kwa masharti uliyo yataja”.

 

Na sababu ya ubatili wa ndoa hii, ni kule kuitundikia ndoa ya kila mmoja wa waolewa kwa mwenzake na utundikaji unafisidi kifungo cha ndoa, kama tulivyo tangulia kueleza. Na pia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekataza ndoa hiyo ya mpeano (Shighaari).

Imepokewa kutoka kwa Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi: “Kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekataza shighaari, na hiyo shighaari: Ni mtu kumuoza binti yake kwa mtu kwa sharti nae amuoze yeye binti yake, na hapana baina ya wawili hao mahari”. Bukhaariy [4822] & Muslim [1415]-Allah awarehemu.

Additional information