KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UFUNGUZI WA MISRI

Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi-katika kipindi cha ziara yake ya Shamu, aliombwa na Amrou Bin Al-Aaswi ruhusa ya kwenda kuifungua Misri. Na akamtajia kheri zake na kwamba nchi hiyo ni nguvu kubwa ya mamlaka ya Urumi na enzi hizo ilikuwa ni mfuasi/mshirika wake. Ikitawaliwa na gavana Mrumi aliye kuwa akiishi Iskandaria (Alexandria). Sayyidna Umar akampeleka huko Amrou na jeshi kubwa kama alivyo omba, baada ya kuondoka akampelekea kikosi kingine chini ya Zubeir Bin Al-Awwaam. Wote kwa pamoja wakaingia kwa kupitia mlango wa Alyoun, wakapita kwenye vijiji vya mshambani mpaka wakatokea Misri.

Huko wakakabiliwa na Al-Jaathiliyq Abu Mariam akiwa na askofu aliye tumwa na mfalme Muqauqis ili kuihami nchi. Amrou alipo fika walipo, wakamuanza kwa vita. Amrou akawaambia: Msifanye haraka, ngojeni mpaka tukupeni maelezo na anijie Al-Jaathiliyq na askofu. Wawili hawa wakatoka upande wao na wakaenda kuitika wito wa Amrou. Walipo fika, akawalingania kuingia katika Uislamu au watoe kodi na akawapasha habari ya usia wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa watu wa Misri kwa sababu ya Haajir; mama yake Nabii Ismail. Imepokewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisema: “Hakika nyinyi mtaifungua Misri nayo ni ardhi ambayo panaitwa humo Qiraatw. Basi mtakapo ifungua, watendeeni wema watu wake, kwani wao wana dhima na udugu au dhima na ukwe”. Muslim [2543]-Allah amrehemu.

Wakasema (Al-Jaathiliyq na askofu): Udugu wa mbali huo, hauungwi udugu kama huo ila na Mitume tu, basi tunaomba utupe amani mpaka tutakapo rudi tena kwako. Amrou akasema: Mtu kama mimi, si mtu wa kudanganywa, lakini nakupeni siku tatu tu ili mpate kufikiri. Wakasema: tuongeze. Nae akawaongeza siku moja. Haoo wakaondoka, wakarudi kwa Muqauqis; kiongozi wa Maqibtw na Artwaboun; gavana wa Kirumi, wakawaeleza ile habari ya Waislamu. Huyu Artwaboun akakataa kusikia habari yoyote ila kuingia vitani na Waislamu. Akawashambulia Waislamu kwa kushtukiza usiku, wakamshinda na jeshi lake na hivyo kumlazimisha kukimbilia Alexandria. Waislamu wakapiga kambi katika mji wa Ainus-shamsi, wakauzingira. Kamanda Amrou akampeleka Abrahah Bin Swabaahi kuuzingira mji wa Farmaa na Auf Bin Maalik akapelekwa kuuzingira mji wa Alexandria. Wenyeji wa nchi wakaandikiana nae nyaraka na wakangojea kuona kitakacho fanywa na Waislamu hapo Ainus-shamsi. Na baada ya kuzingirwa kwa kipindi, wenyeji wa miji hiyo wakaridhia kufanya suluhu na kutoa kodi. Na wakavipitisha katika mapito ya suluhu, vile vilivyo twaliwa kwao kwa nguvu na wakashurutiza kurejeshwa kwa mateka.

 

Ibn Al-Aaswi akamtumia ujumbe Amirul-Muuminina kumueleza hilo, nae akalikubali na akawaandikia mkataba, na hii ndio picha/taswira yake:

 

KWA JINA LA ALLAH, MWINGI WA REHEMA, MWENYE KUREHEMU.

 

         Hii ndio amani iliyo tolewa na Amrou Bin Al-Aaswi kwa watu wa Misri, juu ya nafsi zao, mali zao, mila zao, makanisa yao, misalaba yao, bara na pwani yao. Kisiingiliwe chochote katika hivyo na wala visivunjiwe heshima yake na wala Wanubi wasiishi pamoja nao. Na kumewapasa watu wa Misri kutoa kodi watakapo kongamana na suluhu hii na kukoma ziada ya mto wao. Watoe dirham elfu khamsini. Na watabeba dhima ya makosa ya jinai yatakayo fanywa na wezi wao. Akikataa yeyote miongoni mwao kuitika, wataondoshewa jazaa kwa kadiri yao, na hatakuwa na dhima yetu yule aliye kataa.

 

Na Mrumi au Mnubi atakaye ingia katika suluhu yao hii, basi huyo kumemstahikia kupata kile wakipatacho na kumemlazimu kile kinacho walazimu. Na atakaye kataa na akachagua kundoka, basi huyo yuko katika amani mpaka afikilie mahala pake pa amani au atoke katika mamlaka yetu.

 

Iko juu ya yaliyomo ndani ya mkataba huu, ahadi ya Allah na dhima yake, dhima ya Mtume wake, dhima ya khalifa; Amirul-Muuminina na dhima za Waumini. Na Wanubi walio itika wasaidiwe ili wasishambuliwe na wala wasizuiwe kufanya biashara ya ndani na ile ya nje.

 

Wameushuhudia mkataba huu:

 

Zubeir, Abdullah na Muhammad; watoto wa Amrou.

 

Na umeandikwa na:

 

Wardaan na Hudhwar.

 

[TAARIKHUT-TWABARIY 02/515 na AL-BIDAAYA WAN-NIHAAYA 07/112]

 

 

 

Watu wote wa Misri wakaingia kwenye suluhu hii. Halafu Waislamu wakafikia kwenye hema lililo kitwa na Amrou, nao wakapiga mahema yao pembezoni mwake katika lile eneo ambalo walikuwa wameizingira Misri kutokea hapo. Na wakauhama mji unao kaliwa na Muqauqis na Sayyidna Amrou akajenga msikiti wake mashuhuri katika mji alio uanzisha.

 

 

 

    ii.            Ufunguzi wa Alexandria:

 

         Kadhia ya suluhu ilipomalizika, Sayyidna Amrou-Allah amuwiye radhi-akaondoka kuelekea Alexandria. Yakamkusanyikia baina yake (Alexandria) na Fustwaatw, makundi ya Warumi na Waqibtw, akapambana nayo na kuyashinda. Akaingia na kupiga kambi nje ya Alexandria na akawataka wenyeji wake kuingia kwenye suluhu kama ile waliyo funga watu wa Misri, wakakataa. Basi akaufungua kwa nguvu mji wao na akazitwaa ngawira mali zake na wao akawafanya kuwa chini ya dhima ya Dola ya Kiislamu (Ahlud-dhima). Na wakati wa vita vile Warumi walikuwa wamechukua mali nyingi kutoka kwa Waqibtw wa mashambani, basi wakaja kwa Sayyidna Amrou na wakasema: Sisi hatukuingia vitani, lakini mali zetu zilitwaliwa kwa kutenzwa nguvu. Basi Sayyidna Amrou akawarejeshea ile mali waliyo itambua kuwa ni yao baada ya kuthibitisha kwa ushahidi.

 

Misri ilipo kwisha funguliwa na kuwa chini ya himaya ya Kiislamu na Warumi wakaondoka kurudi Costantinia, mfalme Muqauqis na Waqibtw wakauridhia ule mkataba wa suluhu ulio fungwa na Sayyidna Amrou na akambakisha Muqauqis kwenye kiti chake cha utawala. Na Waislamu waliendelea kumpa kiongozi huyu heshima yake stahiki na wakawa wanamtaka ushauri kwa matatizo yanayo wasibu hadi kifo chake. Na mfalme huyu alikuwa akikaa Alexandria na mara nyingine akikaa Manfi.

Na kwa ufunguzi/ushindi huu wa Misri, yakawa yamekoma mapambano baina ya Waislamu-Allah awawiye radhi-na Warumi katika kipindi cha ukhalifa wa Sayyidna Umar. Walizitwaa wilaya (majimbo) mbili; Shamu na Misri na sehemu muhimu ya Kusini mwa Urumi (Al-Anaadhwoul). Kwa ujumla waliidhofisha nguvu ya Warumi na wakaitapanya dola yao.

Additional information