KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

KUUNGA UNDUGU

Hakuna njia/sababu inayo ingia akilini, inayo wapelekea watu kuishi kwa kutengana na kukatana pande. Bali sababu/njia zinazo simama juu ya mantiki ya haki na hisia salama, huwatia watu hisia za kuhurumiana na kuoneana sikitiko. Na huwaandalia jamii kamilifu inayo tawaliwa na upendo na amani. Na Allah Ataadhamiaye amezirejesha nasaba na jinsia zote za watu wote kwa wazazi wawili, ili aunde kutokana nao makutano ya mafungamano na maungano: “ENYI WATU! HAKIKA SISI TUMEKUUMBENI (nyote) KUTOKANA NA MWANAMUME (mmoja) NA MWANAMKE. NA TUMEKUJAALIENI KUWA NI MATAIFA NA MAKABILA ILI MJUANE. HAKIKA ALIYE MTUKUFU ZAIDI KATI YENU KWA ALLAH NI HUYO ALIYE MCHAMNGU ZAIDI KATIKA NYINYI. HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUJUA, MWENYE KHABARI”. [49:13]

 

Kwa hivyo basi kujuana/kuzoeana – na si kutengana/kukatana pande – ndio msingi wa mafungamano baina ya jamii ya wanaadamu. Na wakati mwingine hupata kutokezea vikwazo vinavyo uzuia mjuano/mzoeano huu wa wajibu kupita katika mapito yake na kuyaendesha maisha kwa athari zake njema. Na katika kuzongana watu katika vyanzo vya riziki na katika kutofautiana kwao katika kuifahamu kwao haki, kunaweza kuzusha mizozo na kutokea mgongano. Pamoja na kwamba matukio mabaya haya, hayatakiwi kusahaulisha hekima ya kuumbwa kwa watu na kuiamirisha (kuiendeleza na kuistawisha) ardhi kwa juhudi ratibiwa zao.

Na kila kiungo kinacho uimarisha mzoeano/mjuano huu na kuondosha vikwazo kwenye njia ya kuufikia, basi hicho ni kiungo kinacho pasa kujengwa na kunufaika na khususi zake. Na Uislamu haukuwa ni kiunganishi kinacho jumuisha pamoja baina ya kundi dogo au kubwa la watu, pakesha. Lakini Uislamu ni jumla ya hakika zinazo weka nyanja sahihi baina ya watu na Mola Muumba wao, kisha baina ya watu wote, wao kwa wao.

Na kuondokea hapo basi, wadau wa Uislamu na wabeba risala yake wanapaswa kuuhisi utukufu wa akida (imani) ambayo kupitia hiyo Allah amezifungua nyoyo zao na akayakusanya juu yake mambo yao. Na wautawalishe mjuano huu juu ya akida hiyo kama inavyo stahiki, kwa kuutunza na kuuenzi. Hakika huo ni mjuano unao ufanya upya udugu shirika ulio baina ya watu wote na unauthibitisha ubaba wa kimaada unao komelea kwa Adam, kwa ule ubaba wa kiroho unao rejea kwenye mafundisho ya dini zote yaliyo fupishwa kwenye risala ya Uislamu. Na kwa ajili hiyo basi, dini halisi inakuwa ndio msingi wa udugu na kishiko imara kinacho waunganisha wafuasi wake walioko Mashariki na Magharibi, Kaskazini na Kusini. Na inawaundia pamoja na utofauti wa nchi na zama, umoja ulio kita mizizi, wenye jengo refu lisilo yumbishwa na tufani wala dhoruba kali. Na udugu huo ndio roho ya imani iliyo hai na ndio mlango wa hisia za ndani anazo kuwa nazo muislamu kwa ndugu zake kiasi cha kumfikisha kujiona kuwa yeye anaishi kwa ajili yao na wao wanaishi kwa ajili yake. Wanakuwa kama kwamba wao ni matawi yaliyo pukutika kutoka kwenye mti mmoja mkubwa au wanakuwa kama roho moja iliyomo kwenye viwiliwili tofauti.

Hakika umimi/ubinafsi ulio kithiri ni janga kwa mwanaadamu na ni dubwana la maadili mema yake. Ubinafsi/umimi huo unapo mtawala mtu, huzifuta na kuziondosha kheri zake na kumea shari zake mahala pake. Na humfunga kwenye wigo finyu ambamo haujui humo ila shakhsiya (dhamira dhati) yake tu basi na wala hapatwi na furaha au huzuni ila tu kwa sababu ya kheri au shari inayo mgusa. Ama Dunia yenye ukunjufu na mabilioni ya watu, basi yeye hawajui wao ila katika mipaka inayo mfikishia kupitia kwao kutimiza malengo yake.

Hakika Uislamu umeupiga vita umimi/ubinafsi dhaalimu huo kwa silaha ya udugu adilifu na ukamfahamisha mwanaadamu ya kwamba maisha si yake peke yake na kwamba maisha hayaendi kwa mtu mmoja yeye peke yake. Kwa hivyo basi, atambue ya kwamba wako watu wengi kama yeye. Pale anapo zikumbuka haki zake zilizo juu yao na maslahi yake yaliyoko kwao, akumbuke pia na haki zao zilizo juu yake na maslahi yao yaliyoko kwake. Na ukumbukaji wa hayo humvua mtu ubinafsi wake mdogo na humpelekea kumfikiria mwingine pale anapo jifikiria yeye, kwa ajili hiyo basi hatajifanya yeye kuwa zaidi/juu kuliko wengine.

Katika jumla ya haki za mwanaadamu mwenzio zilizo juu yako, ni wewe kuchukia yeye kufikwa na madhara na ukafanya haraka kumuondoshea madhara hayo kwa kadiri ya uweza wako. Akipatwa na lenye kumkera na kumtia maudhi, unashirikiana naye katika machungu yatokanayo na kero/maudhi hayo na ukaonyesha huzuni zako. Ama wewe kuwa mfu wa hisia, usiye jali eti kwa kuwa janga halikukutokea wewe, kwa hivyo halikuhusu. Huo ni mwenendo mbaya ulio katikiwa na mafungamano ya hisia za udugu ulio wafunika wanaadamu wote. Udugu unao ziunganisha nyoyo za waislamu na kumfanya mtu kuugulia kwa machungu yanayo mpata mwenzake, kwa usadikisho wa kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Mfano wa waislamu katika kupendana kwao, kuoneana sikitiko kwao na kuhurumiana kwao. Ni mithili ya mwili mmoja, kinapo ugua kiungo chake kimoja, hushirikiana nacho katika kukesha (kwa maumivu) na homa, viungo (vyote)”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na uchungu wa kweli ni ule unao kupelekea na kukusukuma kuondosha dhiki za ndugu zako, hutulii mpaka ziondoke huzuni na wingu lake. Utakapo faulu katika hilo, utanurika uso wako na itapata raha dhamira yako. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Muislamu ni ndugu ya muislamu, hamdhulumu na wala hamsaliti. Atakaye kuwa katika haja ya ndugu yake, Allah atakuwa katika haja yake (naye). Na atakaye muondoshea (mtatulia) muislamu shida, Allah atamuondoshea kwa (sababu yake) shida miongoni mwa shida za siku ya Kiyama. Na atakaye msitiri muislamu, Allah atamsitiri siku ya Kiyama”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Na katika jumla ya alama za udugu mwema, ni wewe kumpendelea manufaa ndugu yako na uyafurahikie manufaa yake kama unavyo yafurahikia manufaa yako wewe. Na utakapo toa juhudi katika kupatikana kwa manufaa hayo, kwa yakini utakuwa umejikurubisha kwa Allah kwa twaa tukufu mno na yenye thawabu maridhawa. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-ya kwamba yeye alikuwa amekaa itikafu ndani ya msikiti wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akajiwa na mtu, akamsalimia kisha akaketi, Ibn Abbas akamuuliza: Ewe fulani wee! Mbona nakuona umejawa na huzuni? Akajibu: Naam (nina huzuni), ewe mwana wa ami yake Mtume wa Allah! Fulani ana haki ya walaa (uacha huru) kwangu, na (naapa) kwa utukufu wa mwenye kaburi hili (Mtume) mimi siwezi kuitekeleza. Ibn Abbas akamwambia: Je, unaonaje nikienda kuzungumza naye (ili akusamehe)? Akajibu: Ukipenda (mimi sina neno).

Anasema (mpokezi): Ibn Abbas akavaa viatu na kisha akatoka msikitini. Yule mtu akamuuliza: Je, umesahau kuwa wewe ulikuwa katika itikafu? Akamjibu: Hapana (sijasahau), lakini mimi nilipata kumsikia mwenye kaburi hili, ambaye hajafariki muda mrefu – na macho yake yakabubujika machozi – akisema: “Atakaye ishughulikia haja ya ndugu yake na akaitekeleza, ni bora kwake yeye kuliko itikafu ya miaka kumi. Na atakaye kaa itikafu siku moja kwa kutaka radhi za Allah Ataadhamiaye, Allah ataweka baina yake na moto, mahandaki matatu yenye umbali wa baina ya Mashariki na Magharibi”. Al-Baihaqiy-Allah amrehemu.

Hadithi hii inatoa taswira ya namna ambavyo Uislamu unavyo yaenzi mafungamano ya udugu mwema na namna unavyo zipa heshima ya juu kabisa aina mbali mbali za huduma (tumishi) za umma ambazo jamii inazihitajia ili kuzikita nguzo zake na kulilinda jengo lake. Tunamuona Ibn Abbas akiona bora kuiacha itikafu yake na hali ya kuwa itikafu ni ibada menyu, yenye daraja tukufu mbele ya Allah, kwa sababu ibada hiyo inamzamisha mja muda wake wote ndani ya swala, swaumu na dhikri. Tena ibada hiyo anaitenda ndani ya msikiti wa Mtume wa Allah ambao ujira wa amali itendwayo humo hurudufishwa mara alfu kuliko ujira wa amali hiyo hiyo ndani ya misikiti mingine. Lakini pamoja na yote hayo, ufahamu wa Ibn Abbas katika kuuelewa Uislamu kama dini na mfumo wa maisha unao randana na maumbile ya mwanaadamu, ukamsukuma kuiacha ibada hiyo, ili kwenda kutoa huduma kwa muislamu anaye hitajia msaada. Hivyo ndivyo maswahaba walivyo jifunza kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na huo ndio udugu wa kweli, udugu wa imani. Allah awawiye radhi maswahaba wote wa Mtume wa Allah, nasi atupe ufahamu kama wa kwao katika kuifahamu dini yake. Aamin!

Additional information