KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

TUTAFAKARI PAMOJA: JE, SWAUMU, KISIMAMO NA AMALI ZETU TULIZO TENDA NDANI YA RAMADHANI, ZIMEKUBALIWA NA ALLAH AU LA?

Mpendwa Muislamu!

Naam, ni wajibu wa kila mmoja wetu kumshukuru Allah kwa neema ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ametujaalia kuudiriki mwanzo na mwisho wake, akatuwezesha kufunga, kusimama usiku, kusoma Qur-ani na kutenda baki ya amali nyingine za kheri, ijapokuwa kwa mapungufu makubwa yatokanayo na ubinadamu wetu. Tumuombe na tumbembeleze atutakabalie pamoja na mapungufu yetu hayo ambayo ayajuaye zaidi ni Yeye pekee.

 

 

Ni vema na ni kheri kwetu ikiwa tutatambua na kukubali ya kwamba kama Ramadhani ilikuwa ni mtihani wa Mola kwetu sisi waja wake, basi bila ya shaka walio faulu katika mtihani huo ni wale ambao walikuwa ndani ya mchana wa Ramadhani wanafunga, wanaswali na wanasoma Qur-ani. Na usiku wake walikuwa wakisujudu na kurukuu kwa kulia na kwa kunyenyekea. Na wakati wa karibu na kuzama kwa jua na ule wa maladaku, walikuwa wakileta Tasbihi, Tahalili, Istighfaari na Dhikri. Wao hao hawakuuacha mlango wowote ule wa kheri yoyote ile ila waliingia humo kwa kadiri ya uwezo wao. Lakini pamoja na yote hayo, bado nyoyo zao zina uoga na khofu kutokana na kutokujua, je amali zao hizo zimepokelewa na kukubaliwa na Mola wao au hazijakubaliwa?! Na je, walizitenda kwa ajili tu ya Allah Mola Muumba wao (Ikhlaasi) au ndani yake ilikuwemo japo chembe ndogo tu ya riyaa?!

 

Mpendwa Muislamu!

 

Sisi na wewe-Allah atuongoze kufahamu ya kwamba wema walio tangulia walikuwa na wasiwasi zaidi wa kukubaliwa kwa amali zao kuliko hiyo amali yenyewe, Allah Mtukufu anawataja kwa kauli yake: “Na wale ambao wanatoa walicho pewa na hali nyoyo zao zinaogopa, kwa kuwa watarejea kwa Mola wao Mlezi”. Al-Muuminuna [23]:60

 

Katika jumla ya hao wema walio tangulia, ni Sayyidna Aliy bin Abi Twalib-Allah amuwiye radhi-na hivi ndivyo anavyo sema kuhusiana na suala zima la wasiwasi wa kukubaliwa kwa amali, tumsikilize: “Kuweni nyinyi na hima kubwa mno katika kukubaliwa kwa amali (mlizo zitenda) kuliko hizo amali (zenyewe), kwani nyinyi hamjaisikia kauli yake Allah Mtukufu: {...hakika si jenginelo, Allah huwapokelea wachaMngu”. Al-Maaidah [05]:27

 

Na swahaba Fudhwaala bin Ubeid-Allah amuwiye radhi-amesema: Mimi kujua kuwa Allah amenitakabalia amali sawa na uzito wa chembe ndogo ya hardali, hilo linapendeza mno kwangu kuliko Dunia nzima na vyote vilivyomo humo, kwa kuwa Allah Mtukufu anasema: {...hakika si jenginelo, Allah huwapokelea wachaMngu”.

 

Hali kadhalika swahaba Ibn Masoud-Allah awawiye radhi-alikuwa akipiga yowe katika usiku wa mwisho wa mwezi wa Ramadhani kwa kusema: “Yaa laiti! Ni nani huyo aliye takabaliwa, tukampongeza. Na ni nani huyo aliye nyimwa kabuli, tukamfanyie taazia!”.

 

Na kongole na pongezi ni zako wewe uliye takabaliwa amali zako. Na ewe uliye ruka patupu, Allah aufanye mwepesi msiba wako. Ewe ndugu yetu mwema-Allah akurehemu-hebu tujiulize na tuwe wakweli wa nafsi zetu, ni nani miongoni mwetu aliye shughulishwa na hisia hizi; hisia za kukubaliwa au kutokukubaliwa kwa amali zake?! Tena tuzidi kujiuliza, ni nani miongoni mwetu aliye utukusa ulimi wake kumuomba Allah amtakabalie swaumu na ibada zake alizo zitenda ndani ya Ramadhani?! Kwa mujibu wa mapokeo, wema walio tangulia walikuwa wakimuomba Allah awafikishe Ramadhani miezi sita kabla ya Ramadhani. Kisha wakimuomba awatakabalie Ramadhani yao ndani ya kipindi kisicho pungua miezi sita baada ya Ramadhani. Tumuombe Allah, Mola wetu Mkarimu, kwa ihsani na ukarimu wake atuandike kwenye diwani la walio fuzu katika Ramadhani hii.

 

Mpendwa Muislamu!

 

Huenda ukawa unajiuliza, nitajuaje kama mimi ni miongoni mwa hao walio fuzu au wale walio feli katika Ramadhani hii? Ikiwa hivyo ndivyo, basi wala usiwe na wasiwasi, jipime kupitia alama hizi za kukubaliwa kwa amali tutakazo kutajia hivi punde na kisha ndio utajua kama wewe umefaulu au umefeli. Haya, tunasema huku tukitaraji msaada wake Allah: Katika jumla ya alama zinazo onyesha kukubaliwa kwa amali ya mja, ni pamoja na:

 

  1. Kuendelea kutenda mema aliyo kuwa akiyatenda ndani ya Ramadhani: Baada ya Ramadhani, Muislamu akaendelea na kudumu kuyatenda yale yote mema mazuri aliyo kuwa akiyatenda ndani ya Ramadhani. Akadumu na swala tano kwa nyakati zake tena kwa jamaa kama alivyo kuwa ndani ya Ramadhani, akaendelea kushikamana kuisoma, kujifunza na kuizingatia Qur-ani, akaendelea kuwafanyia ihsani masikini, wajane, mayatima na wanyonge wengine. Akaendelea kupupia kula halali na kujiepusha na haramu kama alivyo kuwa ndani ya Ramadhani, akadumu na kuitumia vema pumzi yake kama alivyo fanya ndani ya Ramadhani. Na .... na .... Tambua na ufahamu ewe ndugu mwema, ya kwamba kudumu na kuendelea na mema mazuri hayo baada ya Ramadhani, hilo halipungui kuwa ni dalili na kielelezo cha mja kupata radhi ya Allah. Na Allah anapo mridhia mja wake, basi humpa taufiki ya kuendelea kutenda twaa (maamrisho) na kuacha maasia (makatazo).

  2. Kukunjuka moyo na kuhisi ladha unapo fanya ibada: Baada ya Ramadhani, Muislamu akaendelea kufanya ibada na ilhali moyo wake ukiwa mkunjufu na akaihisi ndani yake ladha na tamu ya ibada. Tena akawa na furaha kwa kutenda kheri (mema) na kujiepusha na shari (maovu/mabaya), akawa hivyo kwa kutambua ya kwamba muumini wa kweli ni yule ambaye anaye furahiswa na jema analo litenda na kuumizwa hisia zake na ovu baya alilo litenda. Hiyo pia, ni alama ya kukubaliwa kwa amali za mja na kufuzu ndani ya Ramadhani.

  3. Kuendelea kutubia kwa madhambi aliyo yatenda: Baada ya Ramadhani, Muislamu akaendelea kuleta toba kutokana na madhambi aliyo kwisha yatenda, kwa makusudi au kwa bahati mbaya, kwa dhaahiri au kwa siri, kwa kujua au kwa kutokujua. Hilo ni katika jumla ya alama kubwa zinazo julisha kupata kwake radhi za Allah Mtukufu na hakuna kufuzu kukubwa zaidi ya kupata radhi za Allah. Haya, mimi na wewe tujikague na kujitazama uhusiano wetu na ibada ukoje baada ya Ramadhani, hapo ndipo hatutahitaji mtu wa kutuambia tumefaulu au tumefeli.

  4. Kuwa na khofu ya kutokukubaliwa kwa amali za Ramadhani: Baada ya Ramadhani, Muislamu akawa na khofu na wasiwasi juu ya kukubaliwa kwa amali zake njema alizo zitenda ndani ya Ramadhani, na akaendelea kumuomba Mola wake amtakabalie, hiyo ni dalili ya imani. Na huko ni kuwaiga maswahaba wa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-ambao walikuwa wakimuomba Allah awatakabalie amali zao kwa kipindi cha miezi sita. Na Allah akurehemu ikiwa utatambua kwamba kuwa na imani ni kielelezo cha kufuzu kwa mja.

 

Mpendwa Muislamu!

 

Jipe mwenyewe alama zako ulizo zipata katika mtihani wako wa Ramadhani, kupitia vigezo hivyo hapo juu, halafu ndio utajua kama UMEFAULU au UMEFELI katika Ramadhani hii. Na ukijitambua kuwa umefaulu, basi tahadhari kughurika na kufaulu kwako huko. Kwani huenda nafsi yako ikakunong’oneza kwamba wewe una shehena kubwa ya mema/thawabu mithili ya jabali kubwa unalo lijua wewe. Au madhambi yako yote yamekwisha futwa na umekuwa msafi na mweupe kama ile siku uliyo zaliwa na mama yako. Kabisa usikubali kutoa mwanya huo kwa nafsi yako na utambue ya kwamba nafsi na shetani havitoacha kukushakiza ili ukithirishe kufanya maasi na madhambi, na hapo ndipo utakapo angamia. Allah atuhifadhi sote na ghururi za nafsi na shetani – Aamin!

 

Kila unapo fanya amali njema, mshukuru Allah aliye kuwezesha na endelea kufanya amali na ujione kama hujafanya chochote hata ustahiki kupata neema za Allah. Na jiepushe na vibomoa amali kama riyaa na nduguze.

 

Mpendwa Muislamu!

 

Sasa umewadia ule wakati wa kulikunja jamvi letu la Ramadhani kwa mwaka huu wa 1441H/2020 na hayo yaliyo kujia tangu kabla kidogo ya Ramadhani mpaka leo hii, ndio tuliyo wezeshwa na Allah kukumbushana kupitia jamvi letu hili. Tulilo patia ni kwa taufiki yake Allah Mola Muwezeshi na tulilo kosea linatokana na mapungufu ya kibinaadamu, kwani ukamilifu ni wake Allah pekee. Sote kwa pamoja tumuombe Mola wetu amruzuku kila mwana jamvi hili elimu, maarifa, ufahamu na busara inayo ambatana na matendo. Hali kadhalika tumbembeleze atupe nguvu za kuitekeleza ile amri yake iliyo kuja kupitia kauli yake tukufu: “Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie yakini (mauti)”. Al-Hijri [15]:99

 

EID MUBAARAK WAKULLU AAMUN WA ANTUM BIKHEIR!

 

 

Additional information