KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA KUBWA ZA KIYAMA: HALI YA WAISLAMU KIPINDI CHADAJJAAL

 

Ndugu mwenza wetu katika jukwaa letu hili-Allah akurehemu-baada ya kuzitazama na kuzielezea nguvu na uwezo atakao kuwa nao Dajjaali na ambao ndio utakao kuwa sababu ya fitina kwa wenye nyoyo zenye maradhi ya upungufu wa Imani na Tauhidi. Juma hili kwa msaada wake Allah, tuiangalie itakavyo kuwa hali ya Waislamu katika kipindi atakacho ondokea Dajjaali.

 

 

Kipindi kidogo cha kabla ya kutokea kwa Dajjaali, Waislamu watakuwa na sauti na nguvu kubwa yenye kuogopewa ulimwenguni. Na inavyo elekea ni kwamba ujio wa Dajjaali si kwa jingine ila ni kuja kuiangamiza nguvu hiyo. Ni ndani ya kipindi hicho cha kabla ya ujio wa Dajjaali, ndimo ambamo Waislamu wataingia makubaliano ya amani na ushirika na Warumi (Wakristo kiimani). Wote kwa pamoja; Waislamu na Wakristo wale watapambana na kumshambulia adui yao na kumshinda, halafu ndipo vitaripuka vita baina ya Waislamu na Wakristo (wafia msalaba).

 

Imepokewa kutoka kwa Dhu Mukhbiri-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Mtafanya makubaliano ya amani na Warumi, nyinyi na wao mtapigana na adui (mshirika) aliye nyuma yenu, mpate ushindi (dhidi yake), ngawira na kusalimika naye. Kisha mtaondoka (kwenye medani ya vita) mpaka mpige kambi kwenye nyika yenye vilima, hapo mmojawapo wa Wakristo ataunyanyua juu msalaba, aseme: Msalaba umeshinda. Basi aghadhibike mmoja wa Waislamu augonge (huo msalaba na kuuvunja), hapo ndipo Warumi watafanya khiana (kwa kuvunja makubaliano waliyo afikiana nanyi), wajikusanye kwa ajili ya kufanya mauaji ya halaiki”. [SUNAN ABU DAAWOUD]

 

Wapokezi wengine wakaongezea ibara: “Hapo Waislamu watazichupia silaha zao, watapambana na Allah atakikirimu kipote kile kwa kufa mashahidi”.

 

Naam, ndugu mwanajukwaa mwenzetu-Allah akurehemu-bila ya shaka chini ya kivuli cha maneno yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-unaiona nguvu ya Waislamu katika kipindi hicho. Kwa sura ambayo wao watapigana na kushinda, watachukua ngawira na kurejea wakiwa salama. Na utaona kwa kiwango kikubwa namna watakavyo shikamana na dini yao, kwani pale yule mwana msalaba atakapo unyanyua juu msalaba akidai kwamba ule ushindi ambao Waislamu walishiriki katika kupatikana kwake, ni ushindi wa msalaba. Hapo ndipo atakapo simama muislamu mwenye ghera (uchungu wa Imani) na dini yake, augonge na kuuvunjilia mbali msalaba ule. Kikundi kile cha Waislamu kitakacho kuwepo mahala pale, kitazirukia silaha zao na kupambana na Warumi pasina kujali uchache wao. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anakishuhudia kikundi kile ya kwamba wao ni mashahidi walio kufa kwa ajili ya dini ya Allah na kwamba Allah amewakirimu kwa hilo (la kuifia dini). Na khiana hiyo ya Warumi na yatakayo jiri baada yake ndio yatakuwa sababu ya kutokea kwa mauaji ya halaiki. [Rejea AL-QIYAAMATUS-SWUGHRAA 226-227]

 

Additional information