KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

HUKUMU YA MWANAUME AJNABIYA KUMUANGALIA MWANAMKE

Ni haramu kwa mwanaume aliye baleghe, mwenye akili timamu, mteuzi (mwenye khiari)-hata kama ni mzee au mshindwa (asiye weza lolote), kuangalia sehemu yoyote ya mwili wa mwanamke mkubwa ajinabiya. Kadhalika hilo ni haramu kwa kijana aliye karibia kufikia baleghe. Na mwanamke mkubwa katika mizani ya sharia, ni yule aliye fikia mpaka (umri) ambao hutamaniwa ndani yake, hata kama hajafikilia baleghe. Hata kama itakuwa hiyo sehemu iliyo angaliwa ni uso na vitanga vya mikono na hata kama hakutakuwa na fitina.

 

Na hali kadhalika ni haramu kwa mwanamke kumuangalia mwanaume pasina haja, Allah Ataadhamiaye amesema: “WAAMBIE WAUMINI WANAUME WAINAMISHE MACHO YAO, NA WAZILINDE TUPU ZAO. HILI NI TAKASO BORA KWAO. HAKIKA ALLAH ANAZO KHABARI ZA WANAYO YAFANYA. NA WAAMBIE WAUMINI WANAWAKE WAINAMISHE MACHO YAO, NA WAZILINDE TUPU ZAO...” [24:30-31]

Na imepokewa kutoka kwa Ummu Salamah-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilikuwa kwa Maimuna-Allah amuwiye radhi-nyumbani kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Mara tahamaki akaja Ibn Ummu Maktuum-Allah amuwiye radhi. Mtume wa Allah akasema: “Fichamaneni kutokana nae. Nikasema: Ewe Mtume wa Allah! Kwani yeye si kipofu, haoni na wala hatujui? Mtume wa Allah akasema: Je, na nyinyi ni vipofu?”. Tirmidhiy [2779]-Allah amrehemu.

Naam, hii ndio hukumu ya sharia. Na vile kulivyo harimika kuangalia, kumeharimika kugusa. Kwa sababu huko kugusa/kushika kunazidi kuona katika kusikia ladha na kuchochea matamanio.

Ama kumuangalia mtoto wa kike mdogo ambaye hajafikia kutamaniwa na kumuangalia mtoto wa kiume ambaye hajafikia baleghe. Hakika ya hali na shani, hakuharimiki kuangalia kwa wawili hao ila tupu tu. Hii ni kwa sababu kuwaangalia wawili hao, hapana ndani yake madhanio ya matamanio, kwa ajili hiyo si haramu.

 

Kuwaangalia maharimu:

         Kunamjuzia mwanaume kuwaangalia maharimu zake miongoni mwa wanawake, ila sehemu iliyo baina ya kitovu na magoti. Na kadhalika mwanamke ataangalia kwa maharimu zake miongoni mwa wanaume, ila sehemu iliyo baina ya kitovu na magoti.

 

Lini/wakati gani kunahalalika kumuangalia mwanamke ajinabiya?

         Jua na ufahamu ya kwamba maelezo yaliyo tangulia ya kuwa ni haramu kumuangalia mwanamke ajinabiya na kumgusa/kumshika. Hakika si vinginevyo, hilo ni pale ambapo hakuna haja inayo pelekea kufanya hivyo. Ama kukiwa na haja/dharura inayo pelekea kuangalia au kujgusa, hakika hilo huwa ni halali na wala hapana ubaya ndani yake. Na hiyo haja/dharura inadhihiri katika mambo yafuatayo:

1.           WAKATI WA KUFANYA DAWA/TIBA: Kwa sababu katika kuliharimisha hilo kuna uzito na ilhali Uislamu ni dini ya wepesi na uondoshaji wa uzito. Allah Ataadhamiaye amesema: “...WALA HAKUWEKA JUU YENU MAMBO MAZITO KATIKA DINI...” [22:78] Basi na paangaliwe zile sehemu ambazo anazo zihitajia tu.

Imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-kwamba Ummu Salamah-Allah amuwiye radhi-“alimuomba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ruhusa ya kupiga chuku. Mtume akamuamuru Abu Twaibah ampige chuku”. Muslim [2206]-Allah amrehemu.

Kwa mujibu wa hadithi hii, kunamuelea mwanaume kumganga (kumfanyia dawa) mwanamke katika hali ya dharura na pakiwa hapana mwanamke mwenzake anaye weza kutoa huduma hiyo ya utibabu. Na hali kadhalika kunamuelea mwanamke nae kumganga mwanaume pakiwa hapana mwanaume mwenzake na pakawa na dharura. Lakini pamoja na ruhusa hiyo itokanayo na dharura, mwanaume asimgange mwanamke ila pawepo na maharimu wa mwanamke huyo mgonjwa, au mume wake au mwanamke mwingine aliye muaminifu.

Na atakapo patikana tabibu (daktari) muislamu, basi hapo asiye muislamu hapewi nafasi ya kumtibia mgonjwa muislamu.

2.           WAKATI WA MUAMALA: Yaani wakati wa kuuza/kununua, hii ni iwapo kuna haja ya kumjua mwanamke huyo na ikawa hajulikani ila kwa njia ya kumuona tu.

3.           WAKATI WA USHAHIDI: Yaani wakati wa kuchukua/kutoa ushahidi, kwa sababu haja inapelekea kumuona mtolewa ushahidi dhidi yake (mshtakiwa) au mtolewa ushahidi nufaishi (malalamikaji).

4.           WAKATI WA KUSOMA/KUJIFUNZA: Na ruhusa hii ni katika yale mambo ambayo ni wajibu kujifunza/kuyajua au yamesuniwa kuyajua. Kwa ajili ya manufaa ya kisharia yanayo patikana ndani yake.

Kutakapo ruhusiwa kuangalia (kwa ajili ya posa)/kugusa (kwa ajili ya tiba n.k.) sehemu zilizo tajwa, hakika si vinginevyo huruhusiwa kwa kadri ya haja tu. Kwa sababu huko kuangalia, hakika si vinginevyo kumehalalishwa kwa ajili ya dharura au haja tu. Na kisharia, hiyo dharura na hiyo haja, hukadiriwa kwa kiasi ambacho kinacho weza kuondosha madhara na kutekeleza lengo.

Additional information