KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UFUNGUZI WA MJI WA SHAMU

Tukirejea nyuma, tuliwaacha Waislamu huko Yarmouk wakiwa washindi, walio nusurika baada ya mapambano makubwa. Na amiri jeshi akiwa ni yule muaminifu wa uma huu; Abu Ubeidah Aamir Bin  Al-Jarraah Al-Aamiriy Al-Qurashiy (Mkuraishi wa ukoo wa Aamir), aliye shika uamiri baada ya kamanda panga la Allah; Khalid Bin      Al-Waleed Al-Makhzumiy Al-Qurashiy (Mkuraishi wa ukoo wa Makhzuum). Na wakati huo ilimfikia amiri jeshi habari ya kwamba Warumi walio timshwa mbio wameenda Fihli; eneo katika nchi ya Shamu palipo tokea mapambano baina ya Waislamu na Warumi. Na kwamba msaada mkubwa wa jeshi na zana umekuja Damascus kutoka kwa mfalme wa Urumi. Hapo ndipo amiri jeshi; Abu Ubeidah alipo muandikia waraka Sayyidna Umar akimtaka ushauri, aanze na upi kati ya miji miwili ile?

Sayyidna Umar nae akamjibu kupitia waraka wake, ya kwamba peleka kikosi Fihli ili kiwashughulishe watu wa hapo na wewe nenda Damascus, kwa kuwa hiyo ndio ngome ya Shamu na makao ya ufalme wake. Kamanda Abu Ubeidah akapeleka kikosi Fihli kama alivyo agizwa na Amirul-Muuminina, kilipo fika kikauzingira mji. Na akapeleka kikosi kingine baina ya Himswi na Damascus, ili kuzuia msaada wowote wa kijeshi kuingia Damascus. Na kingine akakipeleka baina ya Damascus na Palestina. Kisha ndipo yeye akatoka kuelekea Damascus, huku kikosi chake cha mbele kikiongozwa na kamanda Khalid Bin Al-Waleed. Na akamkaimisha Amrou Bin Al-Aaswi mamlaka ya uongozi wa Palestina na Jordan.

 

    ii.            Ufunguzi wa Damascus:

         Kamanda Abu Ubeidah alipo fika Damascus, watu wa mji wakajitia ngomeni. Waislamu wakawazingira, Abu Ubeidah akiwa upande mmoja na Khalid Bin Al-Waleed akiwa upande mwingine na mzingiro ukadumu kwa siku sabini. Siku moja wakati kamanda Khalid akiwa katika doria ya mzingiro wake usiku, alisikia makelele. Akamtuma askari wake kwenda kujua kulikoni, kwa sababu yeye alikuwa akipeleleza habari/hali za adui yake ili asipitwe na lolote na apate kuitumia fursa itakayo jitokeza. Jasusi wa kamanda Khalid akatambua kwamba kamanda wa mji amepata mtoto wa kiume na amefanya karamu kusherehekea. Katika karamu hiyo wanajeshi wakanywa pombe na kulewa sana. Kamanda Khalid akajiambia hii ni habari njema na ndio fursa adhimu ya kuitumia dhidi ya adui. Akaweka kamba upande wa ngazi za kuingilia ngomeni, akakwea yeye akiwa mbele akiwaongoza mashujaa, miongoni mwao akiwemo Qa’aqaa (kabla hajaelekea Iraq) na wengine wengi. Khalid akawaambia wapiganaji walio bakia chini: Mtakapo zisikia takbira zetu juu ya ngome, hapo nyie iendeeni milango ya ngome. Kamanda Khalid na wenzake walipo fika juu ya ukuta wa uzio, wakafunga kamba wakashuka chini na haraka wakaliendea lango kuu la ngome na kulifungua huku wakipiga takbira. Hapo ndipo jeshi la Waislamu likaingia ndani na mvumo wa takbira ukasikika kila upande kiasi cha kuwatia khofu watu wa mji ule. Wakatopokwa na ulevi wao wakiwa wanatetemeka hali ya kutomudu lolote.

Ukatoka ujumbe miongoni mwao, kwenda kuomba amani kwa kamanda Abu Ubeidah, nae akawapa amani na akaingia pamoja nao mjini ili kuwapa watu amani. Akakutana na kamanda Khalid katikati ya mji, yeye akiwa ametoa amani na Khalid akiendeleza vita. Abu Ubeidah akampasha Khalid habari ya suluhu, ndipo akaacha vita. Na ngome zilizo funguliwa kwa nguvu, zikapitishwa kwenye utaratibu wa suluhu, hivyo zote zikawa zimepata suluhu.

Kamanda Abu Ubeidah akapeleka taarifa ya ushindi kwa Sayyidna Umar. Kisha akampa Yazid Bin Abi Sufyaan ukhalifa wa mji, yeye akaenda kufungua pwani yake (Sweid, Irqah, Jubeil na Beirut). Na akamtuma Muawiya kwenda kuufungua mji wa Qaisariya, akaufungua. Ama kamanda Abu Ubeidah, yeye alielekea Fihli, kikosi chake cha mbele kikiongozwa na Khalid na vile vikosi viwili vya pembeni viliongozwa na Amrou Bin Al-Aaswi na Abu Ubeidah mwenyewe. Na kikosi cha farasi kiliongozwa na Dhwiraar Bin Al-Azwar Al-Asadiy, huku askari wa miguu wakiongozwa na Iyaadhw Bin Ghanam. Na hatamu za uongozi wa watu wote zilishikwa na Shurahbeela Bin Hasanah, akawaongoza mpaka akafika Fihli na kuuzingira mji. Usiku wakatoka Warumi wakitaka kuwashambulia Waislamu, lakini kamanda Shurahbeela alikuwa katika hali ya tahadhari muda wote na tayari kwa lolote linalo weza kutokea. Alikuwa hivyo kutokana na kuhadharishwa mara nyingi na Sayyidna Umar dhidi ya mashambulizi ya ghafla ya usiku kutoka kwa adui. Basi akapambana nao vikali usiku ule kucha na mchana wake kutwa. Ilipo ingia jioni, hima/ari na mori wa Warumi ukazimika, na wakaingiwa na ushindwa. Na pakakingamwa baina yao na mji wa Fihli kwa maji mengi waliyo kuwa wameyachimbua na kuitopesha ardhi ili yapate kuwa ni handaki lizungukalo mji. Waislamu wakawaendea kila upande mpaka wakawadhibiti na kufanikiwa kuutia mikononi mji wao. Amiri jeshi; kamanda Abu Ubeidah akampelekea amiri jeshi mkuu; Sayyidna Umar taarifa ya ushindi pamoja na khumsi ya ngawira. Kisha baada ya hapo akaunda vikosi viwili kutoka katika jeshi lake, akampa Shurahbeela Bin Hasanah uamiri wa kikosi kimoja na akampa amri ya kwenda Baisaan. Huu ni mji katika nchi ya Palestina, ulioko Kaskazini mwa mji wa Nablus. Na kikosi kingine akakipa amri ya kwenda Twabariya; jimbo la Jordan na kila kimoja kikaufungua mji kilio tumwa kwenda, kwa mtindo wa suluhu ya Damascus.

Ama Abu Ubeidah, yeye baada ya kuvipa majukumu vikosi viwili vile, alienda Himswi pamoja na Khalid. Walipo fika kwenye machunga ya Warumi, wakakutana na majeshi mawili yaliyo tumwa na Hiraqli kupambana na Waislamu. Jeshi moja likiongozwa na kamanda aitwaye Taudhar na lile la pili likiwa chini ya uongozi wa Shanshi Ruumiy. Kamanda Khalid akasimama mbele ya lile jeshi la kwanza na Abu Ubeidah akasimama na jeshi la pili. Kulipo pambazuka Khalid hakuiona athari yoyote ya Taudhar na jeshi lake, kumbe alimuacha Khalid  usiku akaelekea Damascus ili kujaribu kuurudisha mikononi mwao mji huo, akidhania kuwa hapana walinzi. Khalid akayajua makusudio yake, akamfuata na Yazid Bin Abi Sufyaan; amiri wa Damascus pia akatambua ujio wa Taudhar, kwa hivyo akajiandaa kupambana nae. Kwa hali hiyo, Taudhar akawa ametiwa kati na majeshi mawili yale, akapigwa vibaya yeye na jeshi lake hata wasiweze kuponyoka ila wachache tu.

Huku nyuma kamanda Abu Ubeidah akapambana na Shanshi na akamshinda, Khalid akarudi na kukuta udhia umesha malizwa.

 

  iii.            Ufunguzi wa Himswi:

         Kamanda Khalid akaondoka na kamanda mwenzake Abu Ubeidah kuelekea Himswi. Habari zao zilipo mfikia mfalme wa Urumi, alimtumia ujumbe kamanda wa Himswi akimuamuru kutoka mjini awafuate Waislamu. Basi akatoka na kwenda Ruhaa. Ama Waislamu wao wakapitia Ba’alabak na kuufungua mji huo na walipo fika Himswi wakauzingira. Wenyeji wake wakajitia ngomeni wakingojea msaada kutoka kwa mfalme Hiraqli. Lakini muda ulipo repa bila ya kujiwa na msaada walio utazamia, wakamwandikia Abu Ubeidah kumuomba suluhu kama ile aliyo fanya na watu wa Damascus, wakakubaliwa. Akampa Ubaadah Bin Swaamit ukhalifa wa Himswi, yeye akatoka kuelekea Humaata, wenyeji wake wakakutana nae wakiwa wanyenyekevu, akawaandikia suluhu kwa sharti ya kutoa kodi.

Additional information