KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UNADHIFU, UMARIDADI NA SIHA...Inaendelea/3

Hakika ushughulikiaji wa Uislamu katika suala zima la usafi na afya, ni sehemu ya ushughulikiaji wake wa nguvu ya Waislamu; ile ya kimaada na kidesturi. Kwa mantiki hiyo basi, Uislamu unahitaji viwiliwili ambavyo inapita ndani ya mishipa yake damu ya afya na ikawajaza wenye viwiliwili hivyo, murua na nguvu tendaji. Kwani viwiliwili kondefu haviyawezi magumu ya harakati za maisha na mikono yenye kitete haiwezi kuleta kheri yoyote.

 

Kiwiliwili kizima, chenye siha njema, kina athari si tu katika kutafakari, lakini katika suala zima la mtu kwenda sanjari na maisha na watu. Na risala ya Uislamu ni pana mno katika malengo yake na ni ngumu katika umbile lake, kuweza kuishi katika umma mchovu, wenye maradhi, usio weza lolote.

Ni kwa ajili hiyo basi, ndipo Uislamu ukayapiga vita maradhi na ukaweka vikingamizi mbele ya viini vya maradhi, ili usienee pamoja navyo udhaifu, unyong’onyevu na kukorofika. Na kwa ajili hiyo, ikanyonywa kupitia vitu hivyo nguvu ya nchi na ya watu wake.

Na Uislamu umezikithirisha sababu za kinga kupitia kanuni za unadhifu wa daima ilizo ziweka kama sheria, kama ulivyo kwisha ona. Kisha kupitia maisha ratibu iliyo yarasimu ambayo Muislamu analazimika kuyafuata. Kwa hivyo basi, anaamka Alfajiri, anajiepusha kukesha katika puo na pumbao, na anajihami na mitelezo ya matamanio maovu. Na hufanya ukatikati/uwastani katika vyakula, hujiepusha na haramu katika maisha yake na mwenendo wake mzima. Na huijadidisha nguvu ya utendaji wake kupitia swala kila siku na swaumu kila mwaka.

Na wala usisahau ya kwamba kuwa mbali na maasi ni ngome kubwa dhidi ya maradhi mabaya. Mtu atakapo tumbukia katika makucha ya maradhi, kunamuwajibikia kupata suluhisho/ufumbuzi ili asalimike nayo. Na Uislamu unawaongoza watu kutafuta dawa mujarabu zitakazo waondoshea machungu ya maradhi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Allah hakuteremsha ugonjwa wowote, ila aliuteremshia dawa (yake)”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na amesema: “Hakika Allah ameteremsha maradhi pamoja na dawa na akauwekea kila ugonjwa dawa. Basi jigangeni/jitibuni na wala msifanye dawa kwa vilivyo haramu”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Na amesema: “Hakika kila ugonjwa unayo dawa (yake), basi dawa itakapo sibu ugonjwa, (mgonjwa) atapona kwa idhini ya Allah”. Muslim-Allah amrehemu.

Na Uislamu umeharimisha kwenda kutafuta tiba kwa makuhani/wapiga ramli/watazamiaji, kwani kila elimu inao wadau wake wanao ijua vema na ni wajibu kuwasikiliza. Ama wale madajali (waongo wakubwa) ambao wanajiingiza kwenye mambo yasiyo wapasa, basi si vema kwa muislamu kuwaendea au kuyasadiki wanayo yasema. Imepokewa kutoka kwa Uqbah bin Aamir: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: “Atakaye angika/tundika (vaa) hirizi/hazima, Allah asimtimizie (aliyo yakusudia)...” Al-Haakim-Allah amrehemu.

Na amepokea pia Uqbah: Kwamba msafara wa ujumbe wa watu kumi ulikuja kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kula kiapo cha utii na ufuasi. Mtume akawalisha kiapo cha utii watu tisa na akaacha kumlisha kiapo hicho mtu mmoja miongoni mwao. Wakamuuliza: Ana nini huyo? Akajibu: Hakika amefunga hirizi kwenye kifupa panya chake. Mtu yule akaikata hirizi ile. Hapo ndipo Mtume akamlisha kiapo cha utii, kisha akasema: “Atakaye angika (hirizi), bila ya shaka huyo amefanya shirki”. Ahmad-Allah amrehemu.

Na miongoni mwa njia za kinga zilizo madhubuti ambazo zimewekwa na Uislamu, ni kule kuwajibisha kwake kukidhi haja (kujisaidia) katika maeneo yaliyo andaliwa kwa ajili ya hilo. Ili mabaki yatokanayo na vyakula yaende chini sehemu ya mbali na yasiweze kuchafua vyanzo vya maji na wala yasiweze kunajisi njia tupitazo na mahala tukaamo. Basi, lau Waislamu wangezi lazimisha nafsi zao kufuata adabu/utaratibu huu ulio tukuka. Wangeli okoka na kuzihepa shida/dhiki na mateso ya magonjwa yanayo zivunja nguvu zao na kuudhoofisha umoja wao. Imepokewa kutoka kwa Jaabir: kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Kwamba yeye (Mtume) alikataza kukojoa kwenye maji yaliyo tuama”. Muslim-Allah amrehemu.

Na pia imepokewa kutoka kwake: Amekataza (Mtume) kukojoa kwenye maji yatembeayo”. Twabaraaniy-Allah amrehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Muaadh: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Yaogopeni matatu yasababishayo laana; kujisaidia haja kubwa kwenye vyanzo vya maji, majiani na kwenye vivuli”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Yaani ni kwamba mambo matatu hayo yanawaletea laana watendaji wake. Na mtu anaye jisaidia katika njia wapitayo watu, ni mtu aliye filisika kimurua, kwani yeye anatenda kitendo kinacho chochea kichefu chefu, kukirihisha, kuudhi na kuleta ghadhabu. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekwisha sema: “Atakaye wafanyia maudhi Waislamu katika njia zao, imemuwajibikia laana yao”. Twabaraaniy-Allah amrehemu.

Na katika riwaya/upokezi mwingine: “Atakaye weka haja yake kwenye mojawapo ya njia za Waislamu, basi na iwe juu yake laana ya Allah, malaika na watu wote”.     Al-Baihaqiy-Allah amrehemu.

Na mambo haya yaliyo katazwa, yote ni chanzo cha kuenea kwa magonjwa yanayo zunguka miongoni mwetu Waislamu, kwa kuwa watu wameyapuuzia kwa ajili hiyo basi likawafika balaa.

Na Uislamu umekwisha weka kanuni kinga za kiafya, basi yatakapo tokea maradhi ambukizi katika jamii fulani, mji huo hutiwa mzingironi, mzingiro huo ukazuia kutoka na kuingia kwenye mji huo. Hili linafanyika ili kudhibiti utanukaji wa wigo wa maradhi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mtakapo usikia mripuko wa tauni kwenye mji fulani, basi msiingie kwenye mji huo. Na utakapo ripuka kwenye mji mliomo, basi msitoke humo”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Uislamu umewaliwaza wakaazi wa mji ulio kumbwa na maradhi na ukawapendezeshea kukaa humo, kwani raghba (hamu kubwa/shauku) ya uokovu huwapambia wengi kutoka humo kwa njia ya uficho. Na raghba hiyo katika kuhodhi salama ya mtu binafsi, huiingiza nchi nzima kwenye hatari kubwa sana. Ni kwa ajili hiyo basi, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “...hapana mja anaye kuwa ndani ya mji ulio na tauni, akabakia humo asitoke, ilhali akiwa mwenye kusubiri akitaraji malipo kutoka kwa Allah. Huku akijua ya kwamba halimsibu ila lile alilo andikiwa na Allah, ila atakuwa na ujira mithili ya ujira wa shahidi”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na pengine baadhi ya majasiri wakajasiri kusafiri kwenda kwenye mji ulio kumbwa na maradhi ambukizi, na wakatoa hoja ya kwamba kuogopa uambukizi ni udhaifu katika yakini au ni kuikimbia hukumu iliyo kwisha pitishwa. Hilo ni kosa ambalo halipungui kuwa ni ulemavu wa akili, kwani khalifa wa pili; Sayyidna Umar bin Al-Khatwaab alikataa kusafiri kwenda Shaamu pale ulipo ripuka humo ugonjwa wa tauni, akaambiwa: Unaikimbia qadari ya Allah? Akajibu: Tunaikimbia qadari ya Allah, ili kuikimbilia qadari (nyingine) ya Allah.  

Hakika kutwaa/kufuata sababu ni jambo la haki, nalo hilo ni sehemu ya qadari kama anavyo sema Sayyidna Umar. Na Uislamu umeweka sheria ya kujikinga dhidi ya maradhi ya kuambukiza, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Kabisa asiende mgonjwa kwa aliye mzima”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na akasema: “Mkimbie mwenye ukoma kama unavyo mkimbia simba”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Na hakika ya hali ilivyo, pamoja na kuwa uambukizi ni haki (kweli upo), ila tu ni kwamba sisi tunapaswa kujua ya kwamba si kila uambukizi, husibu. Kwani mtu anaweza kubeba viini/virusi vya maradhi na yeye asipatwe na maradhi yanayo sababishwa/enezwa na viini maradhi hivyo, kwa sababu ndani yake imo nguvu kinga maalumu. Tena husalimika nayo na kuyagurishia kwa mtu mwingine.

Additional information