KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

WANAWAKE WALIOHARAMISHWA KWA MUDA

Wanawake walio harimishwa kuwaoa kwa uharamu wa muda tu, hao ni wale walio harimishwa kwa mtu kwa mojawapo miongoni mwa sababu. Itakapo ondoka sababu hiyo, uharamu nao huondoka na kurudi uhalali. Basi mtu atakapo funga kifungo cha ndoa na mmoja miongoni mwa wanawake hao, kifungo hicho huwa ni baitili. Wanawake hao ni hawa wafuatao:

 

         1.     Kuwachanganya/kuwakusanya pamoja madada wawili (mtu na dada yake) katika ndoa moja. Ni mamoja ndugu wawili hao wamekuwa ni wa nasabu/damu au ni ndugu wa kunyonya. Na ni sawa sawa amefunga nao ndoa wote kwa pamoja au kwa nyakati mbili tofauti.

 

Atakapo funga nao ndoa wote wawili kwa pamoja, ndoa itabatilika kwa wote wawili. Na atakapo funga nao ndoa mmoja baada ya mwingine, itabatilika ile ndoa ya pili.

 

Atakapo kufa yule wa kwanza au kutalikiwa na eda yake ikamalizika, kumemuhalalikia kufunga ndoa na dada wa marehemu/mtalikiwa. Allah Ataadhamiaye amesema: “...NA KUWAOA PAMOJA DADA WAWILI ISIPO KUWA YALE YALIYO KWISHA PITA. HAKIKA ALLAH NI MWENYE KUSAMEHE MWENYE KUREHEMU”. [04:23]

 

         2.     Kuwachanganya mwanamke na shangazi yake, mwanamke na mama yake mdogo/mkubwa, mwanamke na binti ya dada yake au binti ya kaka yake au binti ya mwanawe wa kiume (mjukuu) au binti ya mwanawe wa kike, katika ndoa moja.

 

Mafaqihi-Allah awarehemu-wameweka kanuni inayo dhibiti wanawake ambao ni haramu kuwaoa pamoja katika ndoa moja, wakasema: (Kunaharimika kukusanya pamoja baina ya kila wanawake wawili ambao lau mmoja wao angeli kuwa ni mwanaume, kusingeli mjuzia kumuoa yule mwngine). Na kanuni hii inawahusu wanawake wote tulio wataja.

 

Dalili/ushahidi wa hili: Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hapakusanywi (kwa pamoja) baina ya mwanamke na shangazi yake, wala baina ya mwanamke na khaloo wake (mama mdogo/mkubwa)”. Bukhaariy [4820] & Muslim [1408]-Allah awarehemu.

 

 

 

Hekima/Falsafa ya uharimisho huu:

 

 

 

         Hekima ya kuharimisha kuwakusanya pamoja baina ya walio tajwa, ni ile mifundo na chuki inayo patikana baina ya ndugu kwa sababu ya wivu unao jitokeza baina ya wake wenza.

 

Amepokea Ibn Hibban-Allah amrehemu-(Kwamba  Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekataza mwanamke kuozeshwa pamoja na shangazi au khaloo. Na akasema: Hakika nyinyi mtakapo fanya hivyo, kwa yakini kabisa mtaukata udugu wenu).

 

Imepokewa kutoka kwa Isa Ibn Twalhah-Allah amrehemu-amesema: (Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekataza kuozwa mwanamke pamoja na ndugu yake, kwa kuchelea kuukata udugu). [Angalia NAILUL-AUTWAAR 6/147]

 

Atakapo kufa mmoja miongoni mwao au kutalikiwa na eda yake ikamalizika, huhalalika kumuoa yule mwingine.

 

         3.       Mwanamke aliye zidi juu ya wake wane:

 

Hakujuzu mtu kuongeza mke wa tano kwa wakeze wanne waliopo kwake mpaka amtaliki mmoja miongoni mwa wanne hao na eda yake imalizike au afe. Angalia, atakapo kufa au kuachwa, atahalalikiwa kumuoa yule wa tano, Allah Atukukiaye amesema: “...BASI OENI MNAO WAPENDA KATIKA WANAWAKE, WAWILI AU WATATU AU WANE...” [04:03]

 

Amepokea Abu Daud-Allah amrehemu-na wengineo kutoka kwa Qays Ibn Al-Haarith-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilisilimu nami nikiwa na wake wanane, nikamtajia hilo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Chagua wanne miongoni mwao”.

 

         4.       Mwanamke mshirikina muabudu sanamu:

 

Huyu ni yule asiye na kitabu cha mbinguni, atakapo silimu huhalalika kuolewa na muislamu. Allah Atukukiaye anasema: “WALA MSIWAOE WANAWAKE WASHIRIKINA MPAKA WAAMINI. NA MJAKAZI MUUMINI NI BORA KULIKO MSHIRIKINA HATA AKIKUPENDEZENI...” [0:221]

 

 

 

TANBIHI:

 

(a)    Hakumjuzii mwanamke muislamu kuolewa na mwanaume asiye muislamu, vyovyote itakavyo kuwa dini yake. Kwa sababu mume ana utawala juu ya mke na hapana utawala wa kafiri juu ya muislamu. Na kwa sababu yeye huyu mwanamke wa Kiislamu haipati amani dini yake kwa mwanaume huyo, kwa kuwa yeye haiamini. Allah Ataadhamiaye anasema: “...WALA ALLAH HATAWAPA MAKAFIRI NJIA YA KUWASHINDA WAUMINI”. [04:141] Na akasema: “...WALA MSIWAOZE (binti zenu) WANAUME WASHIRIKINA MPAKA WAAMINI. NA MTUMWA MWANAMUME MUUMINI NI BORA KULIKO MSHIRIKINA HATA AKIKUPENDEZENI. HAO WANAITIA KWENYE MOTO, NA ALLAH ANAITIA KWENYE PEPO NA MAGHAFIRA KWA IDHINI YAKE. NAYE HUZIBAINISHA AYA ZAKE KWA WATU ILI WAPATE KUKUMBUKA”. [02:221]

 

Atakapo silimu, atahalalikiwa kumuoa mwanamke huyo muislamu. Na atakapo muoa kabla ya kusilimu kwake, ndoa hiyo huwa batili na ni wajibu kuwatenganisha haraka. Na ikipatikana jimai ndani ya ndoa hiyo batili, hiyo huwa ni zinaa.

 

(b)   Kunamjuzia muislamu kumuoa mwanamke myahudi au mnaswara, kwani huenda ndoa hiyo ikawa ndio sababu ya kusilimu kwa wanawake hao na jamaa zao.

 

Na wala hakujuzu kwa mumewe huyu muislamu kumlazimisha kubadili dini yake au kumdhiki katika utekelezaji wa ibada yake. Allah Ataadhamiaye anasema: “...NA CHAKULA CHA WALIO PEWA KITABU NI HALALI KWENU, NA CHAKULA CHENU NI HALALI KWAO. NA PIA WANAWAKE WEMA MIONGONI MWA WAUMINI NA WANAWAKE WEMA MIONGONI MWA WALIO PEWA KITABU KABLA YENU, MTAKAPO WAPA MAHARI YAO. MKAFUNGA NAO NDOA, BILA YA KUFANYA UHASHARATI WALA KUWAWEKA KINYUMBA...” [05:05]

 

 

 

         5.       Mwanamke aliye olewa:

 

Hakujuzu kwa mtu kufunga ndoa na mwanamke mwenye mume ilhali akingali katika hifadhi yake mume huyo. Mpaka afe mume huyo au amtaliki na imalizike eda yake. Atakapo kufa au kumtaliki na eda yake ikamalizika, kumehalalika kumuoa. Allah Atukukiaye amesema katika kuwataja wanawake walio haramu kuwaoa: “NA WANAWAKE WENYE WAUME...” [04:24] – Yaani ni haramu kwenu kuwaoa wake za watu wote; waungwana na wasio waungwana.

 

         6.       Mwanamke aliye katika eda:

 

Hakumjuzii mtu kumuoa mwanamke ambaye bado yuko katika eda, bila ya kuangalia ni eda ya talaka au ni ile ya kufiwa. Eda yake itakapo malizika kumehalalika kumuoa, Allah Atukukiaye anasema: “...WALA MSIAZIMIE KUFUNGA NDOA MPAKA EDA IFIKE MWISHO WAKE...” [02:235]

 

         7.       Mwanamke aliye achwa talaka tatu:

 

Hakumjuzii mume wake kumrejea mpaka aolewe na mume mwingine kwa ndoa sahihi ya kisheria, kisha mume huyu wa pili amuache na eda yake imalizike. Yatakapo patikana yote hayo, ndipo kutamjuzia yule mume wake wa kwanza kumrejea kwa kumuoa upya kwa mujibu wa sheria na kwa ridhaa yake mke. Allah Ataadhamiaye anasema: “NA KAMA AMEMPA T’ALAKA (ya tatu) BASI SI HALALI KWAKE BAADA YA HAYO MPAKA AOLEWE NA MUME MWINGINE. NA AKIACHWA BASI HAPANA UBAYA KWAO KUREJEANA WAKIONA KUWA WATASHIKAMANA NA MIPAKA YA ALLAH. NA HII NI MIPAKA YA ALLAH ANAYO IBAINISHA KWA WATU WANAO JUA”. [02:230]

 

Na imepokewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-Mke wa Rifaa Al-Quradhwiy alikuja kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Nilikuwa nimeolewa na Rifaa akanitaliki na akaikata kabisa talaka yangu (akaniacha talaka tatu). Nikaolewa na Abdul-Rahmaan Ibn Zubeir, hakika si vinginevyo yeye jogoo halipandi mtungi. Mtume akauliza: “Unataka kurudi kwa Rifaa? Hapana, mpaka uionje asali yake naye aionje asali yako”. Bukhaariy [2496] & Muslim [1433]-Allah awarehemu.

 

   

 

Additional information