KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UKATIKATI WA MATUMIZI NA KUJIZUIA NA MACHAFU

Uislamu kama dini na mfumo sahihi na kamili wa maisha kwa wanaadamu wote, katika jumla ya mafundisho yake umekusanya sehemu ya maongozi/sera zinazo fungamana na maisha ya Waislamu kwa khususi na watu wote kwa uenevu. Maongozi ambayo lengo lake ni kuratibu mambo yao ya kimwili na kinafsi na baki ya mipango yao mingine wanayo iendea mbio katika maisha haya mafupi ya Dunia hii ipitayo. Ili mambo/mipango yao hiyo isiwayumbishe na kuwapelekea kwenye maisha ya uruhubani (useja) ugharikishao wala kwenye mfumo choyo uthaminio mali na pesa. Maongozi/sera hizo za Uislamu zinasimama juu ya misingi ya ukatikati na ulinganifu ambazo utekelezaji wake ni mwepesi uwezwao.

 

Hakika Uislamu katika mafundisho yake unalinganisha na unakutanisha mahitaji ya mwili pamoja na yale ya nafsi. Na huzuia dhulma ya kimojawapo dhidi ya kingine na unaona katika uratibu wa haja za viwili hivyo kuna msaada kwa mtu katika kutekeleza majukumu yake katika maisha haya na yale yajayo (ya baada ya kufa). Na hizi falsafa mbali mbali zilizo chipuka ulimwenguni kama vile ujamaa, ukomunisti na kadhalika, ambazo zimebuniwa na watu ili wapate kuishi ndani ya wigo wake pale walipo ukosa muongozo wa mbinguni. Falsafa hizi hazikufanikiwa na wala hazijafanikiwa katika suala zima la kuoanisha baina ya mahitaji dharura ya mwili na shauku za roho. Na baina ya dhamana ya Akhera ambako tutakwenda baada ya maisha haya na uangalizi wa Dunia ambamo tumeanzia safari yetu ya Akhera. Baadhi ya falsafa hizo zimejengwa juu ya msingi wa kukibomoa kiwiliwili, kwa madai ya kwamba roho haiwezi kuwa katika muelekeo sahihi, ila tu pale itakapo jinasua na pingu za mwili. Na baadhi nyingine zimelenga anasa na starehe za mwili.

Lakini katika Uislamu katu hutoukuta humo uruhubani (useja) anao wadhiki watu kiasi cha kushindwa kuyamiliki maumbile yao na kuteseka na shida/ugumu wake. Kama ambavyo hutokuta humo uhayawani ulio simama juu ya msingi wa kuchezea matamanio maovu ya nafsi na kuyatii mapondoko ya nafsi.

Na tunapaswa kuutaja ukweli halisia mkataa katika kadhia/suala hili, nao ni kwamba maisha ya muumini msadiki nyumba ya Akhera, si kama maisha ya kafiri ambaye anauzingatia umri wake juu ya mgongo wa ardhi hii, kuwa ndio Dunia na Akhera yake pamoja. Ndio fursa yake ya mwanzo na ya mwisho ya kukidhi/kutimiza makusudio na mipango yake na kuyafikia malengo yake. Na wengi wa wanao kosa utawa wao na wanao fuata mawazo yao na wanaishi kwa ajili tu ya kustarehe, hao ndio miongoni mwa watu wa pote (kundi) la mwisho. Au wao hao ndio wakamiwao kupata adhabu iwapo hawatarejea kwenye utambuzi wao na wakaacha upotevu wao. Na hao ndio ambao Allah Ataadhamiaye anawazungumzia kupitia kauli yake: “HAKIKA ALLAH ATAWAINGIZA WALIO AMINI NA WAKATENDA MEMA KATIKA BUSTANI ZIPITIWAZO NA MITO KATI YAKE. NA WALIO KUFURU HUJIFURAHISHA NA HULA KAMA WALAVYO WANYAMA, NA MOTO NDIO MAKAAZI YAO”. [47:12]

Na anasema: “HUENDA IKAWA WALIO KUFURU WAKATAMANI WANGE KUWA WAISLAMU. WAACHE WALE, NA WASTAREHE, NA IWAZUGE TAMAA. WATAKUJA JUA”. [15:02-03]

Ama mtu muumini yeye huigawa mipango na matashi/matakwa yake kwenye maisha yake haya na marejeo yake (Akhera) kwa Mola Muumba wake. Na hujitafutia kheri kwa manufaa ya nafsi yake leo Duniani na kesho Akherani. Na Qur-ani Tukufu imekwisha tufundisha ya kwamba kuzirondea neema na mafanikio katika maisha yote mawili; ya Dunia na ya Akhera, ni miongoni mwa dhikri kubwa kabisa kumdhukuru Allah. Allah Atukukiaye anasema: “NA MKISHA TIMIZA IBADA ZENU BASI MTAJENI ALLAH KAMA MLIVYO KUWA MKIWATAJA BABA ZENU AU MTAJENI ZAIDI. NA WAPO BAADHI YA WATU WANAO SEMA: MOLA WETU MLEZI, TUPE DUNIANI! NAYE KATIKA AKHERA HANA SEHEMU YOYOTE. NA KATIKA WAO WAPO WANAO SEMA: MOLA WETU MLEZI, TUPE DUNIANI MEMA, NA AKHERA MEMA, NA UTULINDE NA ADHABU YA MOTO! HAO NDIO WATAKAO PATA SEHEMU YAO KWA SABABU YA YALE WALIYO YACHUMA. NA ALLAH NI MWEPESI WA KUHISABU”. [02:200-202]

Na yamepokelewa katika kunasihiwa Qaarun maelezo yanayo sisitiza kuyafanyia kazi/kuyashughulikia maisha yote mawili pamoja. Kwani Dunia ndio njia ya kuifikia Akhera na usahihi wa njia ni dhamana ya kufanikiwa/kupata makusudiwa. Kama ambavyo uratibu wa vitangulizi unavyo pelekea kwenye kupata natija itakiwayo. Kutokea hapo ndipo maongozi ya Allah kwa Qaarun yakazikusanya maana zote hizo: “NA UTAFUTE, KWA ALIYO KUPA ALLAH, MAKAAZI YA AKHERA. WALA USISAHAU FUNGU LAKO LA DUNIA. NAWE FANYA WEMA KAMA ALLAH ALIVYO KUFANYIA WEMA WEWE. WALA USITAFUTE KUFANYA UFISADI KATIKA ARDHI. HAKIKA ALLAH HAWAPENDI MAFISADI”. [28:77]

Kwa kuwakia (kujengea) kanuni hizi zilizo kunjuliwa fikrani mwako, ewe msomaji mwema, ndipo Uislamu unamuusia mtu kutokuwa mtumwa wa tumbo lake, anaye ishi Duniani ili tu apate kula. Na anapambazukiwa na kuchwewa akiwa hana lengo lolote ila kukusanya mezani kwake anuwai (aina mbali mbali) za vyakula. Basi atakapo kusanya mezani hapo vilivyo vinono na vitamu, hapo hufurahi na hutua moyo wake. Na ikiwa kinyume na hivyo, hapo hubadilika sura akawa mnyonge na akafura kwa hasira na akaitakidi kwamba qadari ya Allah imemtupa mkono.

Hakika ya watu wanao rondea kushiba na kujaza matumbo na wanavumbua aina mbali mbali za mapishi na anuwai za kupata urojo, hao hawana sifa ya kupata kazi tukufu. Na wala hima zao pweteshi haziwastahikishi kwenye jihadi au kujitoa muhanga. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Watu washibao mno Duniani, ndio watakao kuwa na njaa kali siku ya Kiyama”. Al-Bazzaar-Allah amrehemu.

Na ni jambo lijulikanalo wazi hata na mtu asiye na elimu, kwamba idadi kubwa ya maradhi makubwa na magonjwa hemezi, inatokana na tumbo kusongwa na chakula isicho weza kukisaga. Ni kwa ajili hiyo basi, ndio imekuja kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika hadithi: “Mwanaadamu hajapatapo kujaza chombo chenye madhara mno (kwa afya yake), kuliko tumbo lake...”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Na suala la mtu kupunguza kiasi cha vyakula, halitimii kwa kuvipa nyongo tu vyakula hivyo au kujizuia bila ya maana ifahamikayo. La hasha, lakini njia sahihi, ni mtu kuifungamanisha hima yake na hamu/tamaa ya kupata kitu bora, kisha akahangaika kukipata. Hapo ndipo hilo litamuondosha kwenye anuwai za pumbao na tamu tamu rahisi.

Ilitokezea siku moja Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamfanyia dhifa mtu mmoja kafiri. Akaamuru mbuzi akamwe, akayanywa maziwa yake, akakamwa mbuzi mwengine akayanywa maziwa yote, mpaka akanywa kamwa za mbuzi saba, akalala. Alipo pambazukiwa asubuhi akasilimu, Mtume wa Allah akaamuru akamwe mbuzi, akayanywa maziwa yake yote, kisha akapewa maziwa ya mbuzi mwengine, basi hakuweza kuyamaliza. Ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Hakika muumini bila ya shaka hunywa katika tumbo moja na kafiri hunywa katika matumbo saba”. Muslim-Allah amrehemu.

Na ilikuwa hivyo, kwa kuwa mtu yule alishindwa na fikra pale alipo hisi khofu ya kutoka kwenye wigo wa jaahiliya kuingia kwenye wigo wa nuru. Na pale alipo ujua wajibu wake mpya kwa Mola wake Mlezi, majukumu ya dini yake na hesabu ya Akhera yake. basi kukawa kuinuka kwa hima yake katika kuasisi/kuanzisha maisha matukufu kuliko yale yaliyo pita, kuna athari kubwa katika kujizuia kwake kuongeza ziada ya alicho pewa/letewa (maziwa).

Na lililo la haki kusemwa, vyakula ladhidhi na tamutamu za Dunia zimewekwa mahala pa watu kushindana na kuonyeshana, kwa kiwango fedheheshi tunacho kiona katika zama zetu hizi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika maakuli ya mwana Adamu yamefanywa kuwa ni mfano wa Dunia, pale anapo yatia viungo na chumvi, basi angalia mwisho wake utakavyo kuwa (hayo maakuli)”. Ahmad-Allah amrehemu.

Na katika upokezi mwengine: “Hakika Allah amepiga mfano wa kile kitokacho kwa mwanaadamu (kinyesi) kuwa ndio mfano wa Dunia”.

Maneno haya, kwa mtu mwenye upeo mfupi wa kuona mambo, anaweza akashindwa kufahamu eleweko lake na akadhania ya kwamba yanakusudia kumtenga mwanaadamu na maisha ya Dunia. Na yanamuhimiza kuacha mazuri yake (hiyo Dunia) na kuzihama neema zake. Kitu kama hicho hakikusudiwi/hakilengwi na Uislamu, kwani kuharimisha halali ni sawa na kuhalalisha haramu, hilo ni kosa baya kabisa. Na haki ya Allah kwa muislamu, ni haramu kutoishinda subira yake na halali kutoishinda shukrani yake.

Ama haki yake katika kuishi na kuzistarehekea kheri (mazuri) zake, hilo halina shaka ndani yake: “SI DHAMBI JUU YA WALIO AMINI NA WAKATENDA MEMA KWA WALIVYO VILA (ZAMANI) MAADAMU WAKICHAMNGU NA WAKIAMINI NA WAKITENDA MEMA, KISHA WAKACHAMNGU NA WAKAFANYA MAZURI. NA ALLAH HUWAPENDA WAFANYAO MAZURI”. [05:93]

Na tumekwisha usikia ukarimu wa baba wa Mitume Ibrahimu kwa wageni wake, alifanya haraka kuwachinjia kondoo aliye nona na akamuandaa mezani bila ya kuuliza au kusubiri: “AKENDA KWA AHALI YAKE NA AKAJA NA NDAMA ALIYE NONA. AKAWAKARIBISHA, AKASEMA: MBONA HAMLI?” [51:26-27]

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake katika maisha yao binafsi, walikuwa wakikomea kwenye kauli yake Allah Ataadhamiaye: “ENYI MLIO AMINI! MSIHARIMISHE VIZURI ALIVYO KUHALALISHIENI ALLAH, WALA MSIKIUKE MIPAKA. HAKIKA ALLAH HAWAPENDI WAKIUKAO MIPAKA”. [05:87]

Na mwili una mahitaji mengi, wapevu wa akili wamekongamana ya kwamba kuyapunguza mahitaji hayo, kuna madhara kwa mwili. Kwa hivyo basi, kila mfumo unao yatenga mahitaji ya mwili, Uislamu u mbali mno nao. Na mashambulizi yaliyo elekezwa na Uislamu kwenye mfumo uthaminio mali/pesa, hakika si vinginevyo unalenga ujazatumbo wa watanuzi wa maisha na uvimbiwa wa wazoefu wazamao kwenye matamanio yao.

 

Additional information