KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

JAMVI LA RAMADHANI : KUISHI NA QURANI TUKUFU

Naam, katika jamvi letu la juma lililo pita tuliendelea kujifunza na kukumbushana kuhusiana na adabu za Qur-ani, tuzidi kumuomba Allah atuwezeshe kushikamana na kuzifanyia kazi adabu hizo ili tuvune matunda ya Qur-ani. Leo tena kwa kuwa tumesha tangulia kusema ya kwamba Ramadhani ni mwezi wa Qur-ani, ni vema tukaendelea kuishi na Qur-ani ambayo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anaitaja hivi: “Ndani ya Qur-ani kuna khabari za wa kabla yenu na khabari za wa baada yenu na hukumu ya matendo ya baina yenu”.

Qur-ani ambayo anamuusia swahaba wake Anas bin Maalik-Allah amuwiye radhi-kwa kumwambia: “Ewe mwanangu! Usighafilike na (usiache) kuisoma Qur-ani utakapo pambazukiwa na utakapo chwewa. Kwa sababu Qur-ani huupa uhai moyo ulio kufa, na humkataza (humzuia mtu) na machafu na maovu”.

 

Ni kwa kuyafahamu maneno hayo ya Bwana aliye Mkweli katika ayasemayo, ndio tunawaona wema walio tutangulia katika Imani wakiizengea na kuisoma sana Qur-ani ndani ya Ramadhani na nje yake. Hebu na tuwachukue wachache miongoni mwao ili wawe ni mfano kwetu sisi na pengine nasi tukaingiwa na wivu wa kuwaiga japo kwa sehemu ndogo.

 

 • Alikuwa Imamu Maalik bin Anas-Allah amrehemu-unapo ingia mwezi wa Ramadhani, huacha kusoma hadithi na kukaa na wadau wa elimu na hufata kusoma Qur-ani kwenye msahafu.

 • Na walikuwa Maimamu Abu Hanifa na Sha’abiy-Allah awarehemu-wakikhitimisha khitma sitini ndani ya mwezi wa Ramadhani, kwa kukhitimisha khitma mbili kila siku.

 • Na alikuwa Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-hufungua Qur-ani kwa kusoma Surat Al-Baqarah mpaka Suratil-Maaidah usiku wa kuamkia Ijumaa. Na usiku wa kuamkia Jumamosi husoma Surat An’aam mpaka Surat Huud. Usiku wa kuamkia Jumapili, husoma Surat Yusuf mpaka Surat Maryam. Usiku wa kuamkia Jumatatu husoma Surat Twaaha mpaka Surat Al-Qaswas. Usiku wa kuamkia Jumanne, Surat Ankabuut mpaka Surat Swaad. Usiku wa kuamkia Jumatano, husoma Surat Zumar mpaka Surat Ar-rahmaan na hukhitimisha usiku wa kuamkia Alkhamisi.

 

Hao ni baadhi ndogo tu ya watu walio muelewa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na wakaitambua thamani ya Qur-ani, wakashikamana na kuishi nayo na Qur-ani ikawavusha salama katika bahari kina hii Dunia hata wakatuachia leo utajo mwema. Hao ndio watu bora walio muelewa sana Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-pale alipo sema: “Hakika nyoyo hupata kutu kama kinavyo pata kutu chuma”. Wakauliza (Maswahaba): Ewe Mtume wa Allah! Ni kipi kitakashi chake? Akajibu: “Kusoma Qur-ani na kukumbuka mauti”.

 

Ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-ukiwa umeyaelewa maneno haya ya Bwana Mtume, basi bila ya shaka utakuwa umejua ya kwamba kuacha kusoma Qur-ani ni kuutia kutu moyo wako. Moyo ukiendelea kuingiwa na kutu ndipo inafikia mwanadamu hasikii la muadhini wala la mnadi swala, huna la Mungu wala la Mtume wake utakalo mwambia, akakuelewa. Kutu ni maradhi mabaya ya moyo ambayo dawa yake mujarabu ni kuisoma Qur-ani, tuwaige wema walio tutangulia, tushikamane na kuikumbatia Qur-ani yetu.

 

Ni kheri na neema kwetu iwapo tutakiri na kutambua ya kwamba yule aliye neemeshwa na Allah kuisoma Qur-ani yote au kuihifadhi yote, huyo amefikia lengo tukufu na daraja ya juu kabisa. Msomaji wa Qur-ani, Allah Mtukufu:

 

 • Humzagazia moyo wake kwa nuru ya Imani,

 • Humkinga na viza vya siku ya Kiyama,

 • Humuepushia shida mbali mbali,

 • Humuongozea kwenye njia yake iliyo nyooka,

 • Hukikunjua kifua chake kwa ajili ya Qur-ani, na

 • Huwaamuru Malaika wake kumuombea maghufira na rehema.

 

Kuishi na Qur-ani kwa kuisoma itakiwavyo, kuihifadhi na kuitumia ni sababu ya:

 

 • Kuamirika kwa nyoyo na majumba,

 • Kuenea kwa kheri na baraka katika kizazi, nyumba na kazi,

 • Kutoka na kukimbia mashetani majumbani,

 • Kunyanyuliwa na kuinuliwa daraja/heshima ya mdau wa Qur-ani duniani na akhera.

 

Tena elewa ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ametuamrisha tuipatie faida kila nukta/sekunde ya uhai wetu katika kumtii Allah, akasema: “Yapatie faida mambo matano kabla (hujafikwa na) mambo matano, (upatie faida):

 

 1. Uhai wako kabla ya umauti wako,

 2. Siha (afya njema) yako kabla ya maradhi yako,

 3. Faragha (nafasi) yako kabla ya mshughuliko wako,

 4. Ujana wako kabla ya uzee wako, na

 5. Utajiri wako kabla ya umasikini wako”. Al-Haakim [04/341] & Al-Baihaqiy [07/263]-Allah awarehemu.

 

Kipindi ambacho wapenzi wa Dunia wanashughulika na Dunia yao na tamu tamu zake zenye kuondoka na kumalizika. Wakitumia muda wao katika baraza/vijiwe vya kuteta na kuwasengenya watu, wakistarehe katika viwanja/sehemu zao za pumbao. Kipindi hicho wadau na wapenzi wa Qur-ani, wanatakiwa kuitumia kila pumzi yao kuishi kwa nyoyo na roho zao pamoja na kitabu cha Allah; kwa kukisoma, kukihifadhi, kukizingatia na kuyatendea kazi yaliyomo ndani yake.

 

Halafu tena tukubali na kufahamu ya kwamba nafsi ni yenye kuamrisha mno maovu, mabaya na machafu, ukiiachilia ukaacha kuishughulisha na mambo ya twaa, itakushughulisha wewe kwa kukufanya utende maasi. Na jua ya kwamba wakati ni mithili ya upanga, kama hukuutumia kukatia utakukata wewe mwenyewe. Basi jitahidi upeo wa uweza wako, kuupatia faida muda wa umri na maisha yako leo hapa duniani katika kukisoma, kukihifadhi na kuyafanyia kazi yaliyomo ndani ya Qur-ani ili uvune mavuno maridhawa mara mbili; leo duniani na kesho akhera.

 

Ndugu muislamu-Allah akurehemu-kuishi na Qur-ani ni kujiongezea fursa ya kuzidi na kuongezeka kwa imani yako. Yeyote anaye taka kuzidi imani yake siku baada ya siku, basi ashikamane na kitabu cha Allah kwa kukisoma na kukifanyia kazi, kwani Allah amekwisha tuambia: “Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Allah nyoyo zao hujaa khofu na wanapo somewa aya zake huwazidishia imani...”. Al-Anfaal [08]:02

 

Na akazidi kutuambia: “Na inapo teremshwa sura wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu sura hii imemzidishia imani? Ama wale walio amini inawazidishia imani, nao wanafurahi”. At-taubah [09]:124

 

Ndugu Muislamu-Allah akurehemu-unatawadha, ukakishika kitabu cha Allah, ukamlaani shetani, ukalitaja jina la Mola wako na ukaanza kukisoma kitabu hicho kwa mazingatio. Kupitia mazingatio hayo, unapo zisoma aya zinazo taja namna Allah alivyo wanusuru Mitume wake-Rehema na Amani ziwashukie-na ukazisoma aya zinazo elezea namna alivyo wafedhehesha makafiri, bila ya shaka itazidi imani yako kupitia aya hizo. Na unapo soma kuhusiana na ahadi ya Allah kwa waja wake waumini kuwaingiza peponi na kuwapa radhi zake na kwa upande mwingine unapo soma aya zinazo taja makamio ya Allah kwa makafiri kuwaingiza motoni na kuwashushia hasira zake, bila ya shaka aya hizo zitaizidisha imani yako.

 

Imepokewa kutoka kwa Jundub-Allah amuwiye radhi-amesema: Tulikuwa vijana tunao karibia baleghe kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-basi akawa anatufundisha imani kabla ya kutufundisha Qur-ani. Halafu tena ndio anatufundisha Qur-ani, kwa ajili hiyo basi ikatuzidishia imani”. NUZ-HATUL-HUDHWALAA [01/383]

 

Naam, ndugu yetu katika Imani-Allah akurehemu-sote tunapaswa kujua na kufahamu ya kwamba Qur-ani Tukufu ni dawa/tiba ya ukavu, ugumu, ukukutavu na ususuavu wa nyoyo. Unapo somewa au kusikia aya za Allah zikitajwa, ukawa hukataziki wala huamriki, huogopi wala hunyenyekei, hilo si jingine bali ni gonjwa baya na hatari la ususuavu wa moyo. Gonjwa hilo halina tiba nyingine zaidi ya kukikumbatia na kukisoma kitabu cha Allah, tusome na tuzingatie: “Allah ameteremsha hadithi nzuri kabisa, kitabu chenye kufanana na kukaririwa, husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Allah. Huo ndio uwongofu wa Allah, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Allah kupotea, basi hapana wa kumwongoa”. Az-zumar [39]:23

 

Naam, si jambo lenye kutiliwa shaka kwamba kila mtu anatamani kunasibika na mtu ambaye atajifakharisha mbele za wenzake kupitia nasabu ya mtu huyo, ama kutokana na utajiri wa mtu huyo, au kutokana na elimu yake au pia kutokana na uchaMngu au umaarufu alio nao mtu huyo. Na huko kujifakharisha na kujinasibu kwa mtu au vitu, ni sehemu au ndio raha ya maisha haya ya Dunia mpito, tusome kisha tuendelee: “Jueni ya kwamba maisha ya Dunia ni mchezo, na pumbao na kujifakhirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto...”. Al-Hadiid [57]:20

 

Ikiwa mtu anaona raha na fakhari kujinasibisha na mtu ambaye mwisho wake atakufa na kumuacha au vitu ambavyo hatimaye vitatoweka na wala havitamsaidia wakati wa kufa, kaburini na mbele ya Mola Muumba wake atakapo simamishwa kwa ajili ya hisabu na jazaa. Nini dhana na fikra yako kwa mtu ambaye anajinasibisha na Yule aliye umba mbingu na ardhi, je kuna sharafu na heshima kubwa kuliko heshima hiyo?!

 

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika Allah anao watu wake miongoni mwa waja. Wakauliza (Maswahaba): Ni kina nani hao, ewe Mtume wa Allah? Akajibu: Wadau wa Qur-ani, hao ndio watu wa Allah na wateule wake”. Ibn Maajah [215] & Ahmad [11870]-Allah awarehemu.

 

Upamoja ulioje huo wa kuwa pamoja na Allah Mola Muumba wa wote na vyote? Upamoja usio linganishwa na Dunia na vyote vilivyomo humo kithamani, upamoja usio ondoka, kumalizika na kuisha kama inavyo ondoka na kumalizika Dunia na vyake vyote. Kwani katika jumla ya ikramu ya Allah kwa waja wake wanao ishi na Qur-ani kwa kuisoma, kuihifadhi na kuifanyia kazi, ni Yeye kuwafanya wao kuwa watu wake wa karibu na wateule wake. Wakati ambapo wasanii wanajinasibu kwa usanii wao na matajiri wakijinasibu kwa utajiri wao, tahamaki wadau wa Qur-ani wanafuzu kwa kupata upamoja wa Mmiliki wa ufalme wa mbingu na ardhi na Mfalme wa wafalme wote.

 

Kwa fadhila, ubora na daraja hizo, ni kipi kinacho kuzuia ndugu muislamu kuwa mdau wa Qur-ani?! Tia nia ya kutinda Ramadhani hii iwe ni mwaka wa mapinduzi ya Qur-ani ndani ya moyo wako, ipe nafasi Qur-ani moyoni mwako, akilini mwako, matendoni mwako na maishani mwako. Na hilo halitapatikana ila tu kwa wewe kufanya jitihada na bidii kwa kadiri ya uweza wako kujifunza kuisoma Qur-ani ili uweze kusoma kama itakiwavyo, halafu tena ujifunze tafsiri yake ili upate kujua unacho kisoma na hapo ndipo utapata mazingatio, unyenyekevu na kuzidi imani yako.

 

Jamvi letu kumbushi kuhusiana na Ramadhani, kwa juma hili limetamatia hapa. Ukamilifu ni wake Mola Muumba ikiwa mmenufaika na jamvi la leo, na mapungufu ni yetu sisi waja kwa kushindwa kufikia malengo. Kwa pamoja tuinue mikono ya unyenyekevu tumuombe Allah: Mola wetu Mtukufu, ewe Mwenye Qur-ani yako! Turuzuku mahaba ya Qur-ani, tujaalie kuwa miongoni mwa wadau wa Qur-ani walio pata upamoja wako. Tuwezeshe kuishi na Qur-ani katika kila nukta ya maisha yetu. Pia tumuombe atkutanishe tena juma lijalo katika jamvi hili ili tuendelee kuitekeleza amri yake ya kukumbushana.

 

ALLAH ATUWEZESHE KUTENDA YALE AYAPENDAYO NA KUYARIDHIA.

 


 

 

Additional information