KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

MAVAZI NA MAPAMBO

Hakika asili/msingi katika hukumu za mavazi na mapambo, ni mamoja yawe ya mwilini au nguoni au mahala ni uhalali. Na hili ni kwa mujibu wa uenevu wa dalili ambazo zinazo beba neema ya Allah kwa waja wake. Katika vile alivyo waumbia na kuwaneemesha kwavyo ili wanufaike navyo katika maisha yao ya dunia, kwa kuvaa, kujipamba, kutumia na kuneemeka (kustareheka).

 

Amesema Allah Ataadhamiaye: "YEYE NDIYE ALIYE KUUMBIENI VYOTE VILIVYOMO KATIKA ARDHI..." [2:29] Na akasema: "...NA AKAKUPENI KILA MLICHO MUOMBA. NA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH HAMWEZI KUZIDHIBITI..." [14:34] Na amesema: "SEMA: NI NANI ALIYE HARIMISHA PAMBO LA ALLAH ALILO WATOLEA WAJA WAKE, NA VILIVYO VIZURI KATIKA RIZIKI. SEMA: HIVYO NI KWA WALIO AMINI KATIKA UHAI WA DUNIANI, NA SIKU YA KIYAMA VITAKUWA VYAO WAO TU. NAMNA HIVI TUNAZIELEZA ISHARA (aya)  KWA WATU WANAO JUA". [7:32] Na amesema: "ENYI WANAADAMU! TUMEKUTEREMSHIENI NGUO ZA KUFICHA TUPU ZENU, NA NGUO ZA PAMBO. NA NGUO ZA UCHAMNGU NDIO BORA. HAYO NI KATIKA ISHARA ZA ALLAH MPATE KUKUMBUKA". [7:26] Na amesema Atukukiaye akiwasumbulia waja wake kwa vile alivyo waumbia: "NA ALLAH AMEKUJAALIENI MAJUMBA YENU YAWE NI MASKANI YENU, NA AMEKUJAALIENI KUTOKANA NA NGOZI ZA WANYAMA NYUMBA MNAZO ZIONA NYEPESI WAKATI WA SAFARI ZENU NA WAKATI WA KUTUA KWENU. NA KUTOKANA NA SUFI ZAO NA MANYOYA YAO NA NYWELE ZAO MNAFANYA MATANDIKO NA MAPAMBO YA KUTUMIA KWA MUDA. NA ALLAH AMEKUFANYIENI VIVULI KATIKA VITU ALIVYO VIUMBA, NA AMEKUFANYIENI MASKANI MILIMANI, NA AMAKUFANYIENI NGUO ZA KUKUKINGENI NA JOTO, NA NGUO ZA KUKUKINGENI KATIKA VITA VYENU. NDIO HIVYO ANAKUTIMIZIENI NEEMA ZAKE ILI MPATE KUTII". [16:80-81]

Kutokana na dalili hizi na nyenginezo, tunajua kwamba asili katika kila kilicho aina ya kivazi na kipambo ni uhalali. Ila kilicho vuliwa katika hukumu hiyo kwa nassi (nukuu) makhsusi.

 

II.       Vilivyo vuliwa kutokana na uenevu wa uhalali:

         Vimevuliwa kutoka kwenye uenevu huu, vile ambavyo dalili zimethibiti juu ya kuharimishwa kwake na zikazuia utumizi wake. Na tutataja kwa ufupi baadhi ya vilivyo vuliwa kutoka katika uenevu wa uhalali na vikatwaa hukumu nyingine, nayo ni uharamu na uzuiwa.

 

III.    Kuharimishwa dhahabu na fedha katika matumizi yasiyo kuuza na kununua na yanayo fanana na mawili haya:

         Hakujuzu kutumia dhahabu na fedha katika aina yoyote ya matumizi yasiyo kuuza na kununua (biashara) na yenye kufanana na hayo mawili. Kwa hivyo basi, hakujuzu kutengeneza kwa kutumia madini ya dhahabu/fedha, vyombo vya kulia na kunywea. Wala kutengeneza kutokana navyo vyombo/zana za kuandikia, kujitia wanja au kupambia nyumba, kumbi, misikiti, maduka na vinginevyo. Ni sawa sawa vitu hivi vya dhahabu au fedha vitumiwavyo ni vidogo au vikubwa. Na kama ambavyo yameharimishwa matumizi ya dhahabu/fedha katika tuliyo yataja, ni haramu pia kuviweka tu hata bila ya kuvitumia. Kwa sababu kilicho harimishwa kukitumia ni haramu pia kukiweka tu.

 

IV.     Dalili ya kuharimishwa utumizi wa dhahabu na fedha:

         Na dalili za uharamu huu ni nyingi sana katika vitabu sahihi vya hadithi, miongoni mwake ni: Imepokewa kutoka kwa Ummu Salamah-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: "Atakaye kunywa kwa kutumia chombo cha dhahabu au fedha, hakika si vinginevyo anagumia tumboni mwake moto wa Jahanamu". Muslim [2065]-Allah amrehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Hudhayfa-Allah amuwiye radhi-amesema: Nilimsikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisema: "Msinywe katika vyombo vya dhahabu na fedha na wala msile katika sahani zake, kwani hivyo ni vyao wao (makafiri) duniani". Muslim [2067]-Allah amrehemu.

 

V.        Hukumu ya kutumia vyombo vilivyo tiwa koa la dhahabu au fedha:

         Ni haramu kutumia vyombo vilivyo tiwa koa la dhahabu kwa hali yoyote, ni mamoja limekuwa kubwa koa hilo au dogo. Na ni mamoja limetiwa koa mahala pa utumizi au penginepo.

Ama utiaji koa kwa kutumia madini ya fedha, angalia ikiwa fedha ni nyingi tena bila ya haja ni haramu. Na likiwa ni dogo au kubwa kwa ajili ya haja, kumejuzu kutumia chombo hicho, bila ya kujali fedha hiyo iko mahala pa utumizi au penginepo.

Na dalili ya kujuzu huku: Imepokewa kutoka kwa Aaswim Al-Ahwali, amesema: Niliiona hero (bilauri ya mti) ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa Anas Ibn Maalik-Allah amuwiye radhi. Na ilikuwa na mpasuko/mvunjiko, akaifunga kwa fedha. Anasema (mpokezi): Nayo ni hero nzuri, pana iliyo tengenezwa kwa aina ya mti mzuri. Anasema (mpokezi): Anas-Allah amuwiye radhi-akasema: "Nilimnywesha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika hero hii zaidi ya mara kadha kadha". Bukhaariy-Allah amrehemu.

 

VI.     Hukumu ya kutumia vyombo vilivyo chovywa dhahabu au fedha:

         Kupakaza dhahabu au fedha, kukiwa kuchache kiasi kwamba kitakapo yeyushwa/tiwa katika moto, hakipatikani chochote, ni halali. Na kama ni kwingi, kwa sura ya kupatikana kitu kitakapo tiwa motoni. Wakati huo hakujuzu kutumia chombo kilicho chovywa wala kukiweka tu.

Na ni haramu kupakaza kwa dhahabu/fedha dari za nyumba na viambaza (kuta) vyake, ujapokuwa kidogo mpako huo, hakipatikani kwao kitu utakapo tiwa katika moto.

Additional information