KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

MWANZO WA KADHIA YA WARUMI

Mamlaka/Ufalme wa Urumi ndio mamlaka ya pili kubwa ambayo ilikuwa ikijiranikiana na nchi za Kiarabu kwa upande wa Kaskazini. Na la mwanzo lililo tokea baina ya ufalme huu na Waislamu, ni waraka wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alio muandikia Hirakli; mfalme wa Urumi. Katika waraka huo alikuwa akimlingania kuingia katika Uislamu. Habari ya waraka huu na maelezo ya Abu Sufyan kuhusiana nao, tumeitaja katika sehemu ya kwanza ya Sira; Sira ya Mtume wa Allah. Pia unaweza kurejea Sahih Bukhaariy hadithi nambari [4553] na Sahih Muslim, hadithi nambari [1773].

 

Waraka huo, ukafuatiwa na waraka mwingine ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimuandikia Al-Haarith Bin Abi Shamri; mfalme wa kabila la Ghassaan katika jimbo la Bulqaa, katika nchi ya Sham. Nae huyu ndiye aliye kuwa liwali/balozi wa mfalme Qaiswar katika nchi za Kiarabu, akimlingania ndani ya waraka huo kuingia katika Uislamu. Huyu alipo fikiwa na waraka huo wa Mtume wa Allah, alipandwa na mori wa kutenda dhambi ulio msukuma kutaka kumshambulia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Ikamjia amri kutoka kwa Qaiswar akimkataza kuitekeleza azma yake hiyo.

Katika mwaka wa nane wa Hijrah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliandaa jeshi chini ya uamiri jeshi wa Zaid Bin Haarith kwenda Sham. Hivi ndivyo vita vya “Mu’utah”, Warumi wakalikusanyia jeshi hili la Waislamu, kundi kubwa lenye zaidi  ya askari laki moja kupambana nao. Katika mpambano huo, amiri jeshi Zaid, kamanda Ja’afar Bin Abi Twalib na Abdallah Bin Rawaahah, walikufa shahidi. Uongozi wa jeshi ukatwaliwa na panga la Allah; Sayyidna Khalid ambaye akawa ndio sababu ya kuliokoa na hilaki. Habari ya vita hivi, tumeitaja kwa ukunjufu katika Sehemu ya Kwanza ya Sira; Sira ya Mtume wa Allah.

Katika mwaka wa tisa wa Hijrah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alijiandaa kuipiga Dola ya Urumi. Akafika Tabuuk, hapo akajiwa na Gavana wa Aylah; Yohana Bin Ru’ubah na magavana wa Jarbaa na Adhrumi, wakatoa kodi. Habari za Yohana zilipo mfikia mfalme Hirakli, akatoa amri auawe na kusulubiwa kwenye jimbo lake.

Na katika ule mwaka ambao Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alifariki Dunia, alikuwa amekiandaa kikosi chini ya aumiri wa Usaamah Bin Zaid Bin Haarithah. Kielekee Ubnaa na Qudhwaa kwa ajili ya kuchukua kisasi kwa mauaji ya baba yake. Mtume wa Allah akafariki kabla ya kutoka kwa Sayyidna Usaamah na kikosi chake. Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-alipo tawazwa kuwa khalifa kushika nafasi iliyo achwa wazi na Mtume wa Allah, alikiandaa tena kikosi hicho. Sayyidna Usaamah akaenda mpaka akafika Ubnaa, akayashambulia vikali kabisa makabila ya Qudhwaa, kisha akarejea Madinah na ushindi mnono.

Khalifa Abubakar-Allah amuwiye radhi-alipo funga bendera za vikosi vya vita katika tukio la Dhil-Qiswah. Miongoni mwa bendera hizo, alifunga bendera ya kamanda Khalid Bin Said Bin Al-Aasw na akamuagiza kuelekea kwenye viunga vya Sham. Kisha akamuamuru kuwa auni (msaada) ya Waislamu wa Taimaa, asiondoke katika mji huo ila kwa mri yake na wala asipigane ila na atakaye muanza. Habari za kamanda huyu zikamfikia Hirakli; mfalme wa Urumi. Akamuandalia jeshi la Waarabu washirika wa Urumi wa pande za Bahraa, Sulaihi, Kalbi, Lakhmi, Judhaamu na Ghassaan. Kamanda Khalid alipo fikiwa na habari za jeshi hilo, haraka akaliendea na kulikuta kwenye kambi yao kabla halijatoka. Jeshi la washirika wa Urumi likasambaratika kutokana na mshtuko ulio lipata baada ya kujiwa ghafla na jeshi la Waislamu. Kamanda Khalid akatoa taarifa ya tukio hilo kwa Amiri jeshi mkuu; Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-kwa ajili ya kupata maelekezo. Amiri jeshi mkuu baada ya kupata taarifa hiyo ya kamanda wake, akamuandikia waraka akimuagiza kusonga mbele. Nae kamanda Khalid akasonga mbele kama alivyo agizwa na mkuu wake, njiani akakutana na mmoja wa makanda wa Kirumi aitwaye Mahaani, akapambana nae na kufanikiwa kumsambaratisha.

Kutokana na upinzani huu wa njiani, kamanda Khalid Bin Said Bin   Al-Aasw, akamuandikia waraka Amiri jeshi mkuu kumuomba msaada. Kuanzia hapo ndipo Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-alipo anza rasmi kuishughulikia kadhia ya Sham. Na wakati huo walikuwa wamewasili kwake watimuliwa wa Yemen na Ikrimah Bin Abi Jahli nae akaja na alio ambatana nao kutoka Tihaama na Bahrein. Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-akamtumia ujumbe Amrou Bin Al-Aasw ambaye alikuwa liwali wa zaka za koo za Saad na Hudhaim za kabila la Qudhwaah. Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-alimpeleka huko siku ile aliyo funga bendera pale Dhil-Qiswah. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa amemuahidi uliwali wa huko, Sayyidna Abubakar akamuandikia waraka usemao: “Hakika mimi nilikuwa nimekurejesha kwenye kazi ambayo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikutawalisha mara moja na kukuahidi mara nyingine. Nilifanya hivyo kwa ajili ya kutekeleza ahadi za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nawe umekwisha shika wadhifa huo. Nami hakika ningependelea kukuweka katika nafasi ambayo hiyo ni bora kwako Duniani na Akhera. Ila kama wewe unaona nafasi uliyo nayo ni bora zaidi kwako (basi, salia hapo)”. Liwali Amrou Bin Al-Aasw, alipo wasiliwa na waraka wa Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-akaandika waraka akimjibu Amiri wa waumini, akasema: “Hakika mimi ni mmoja kati ya mishale ya Uislamu na wewe ndio mtupaji na mkusanyaji mishale hiyo baada ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Basi angalia ulio shadidi, uogopwao na bora kabisa ya mishale hiyo, uutupe (uulenge) huo (panapo stahiki)”.

Amiri wa Waumini; Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-alipo pata majibu mazuri hayo, yenye utayarifu wa utumishi kwa Uislamu na utii kwa kiongozi. Akamuagiza liwali Amrou kuja kwake kwa ajili ya kupangiwa kazi nyingine. Liwali Amrou hakusita kutekeleza agizo hilo la mkuu wake, akaitika na kufika. Hapo ndipo Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-akaviandaa vikosi vinne vya jeshi ambapo alimpa Amrou uamiri wa mojawapo ya vikosi hivyo. Na akamuagiza kwenda Palestina, hili wakati huo lilikuwa ni jimbo la Sham kwa upande wake wa Kusini. Kikosi cha pili uongozi wake ulishikwa na Shurahbeelah Bin Hasanah ambaye alikuwa anatokea Iraq, yeye huyu alipelekwa Jordan. Hili pia lilikuwa jimbo la Sham lililo pewa jina la mto wa huko unao anzia kwenye Ziwa Twabariyah na kuishia katika Ziwa Mfu. Hatamu za kikosi cha tatu, zilishikwa na Yazid Bin Abi Sufyaan, huyu alipelekwa Al-Bulqaa. Hili nalo lilikuwa ni jimbo la Sham na akapewa ndugu yake Muawiyah kuwa msaidizi wake. Na kile kikosi cha nne, uamiri wake alipewa muaminifu wa umma huu; Abu Ubeidah Bin Al-Jarraah ambaye alipelekwa Himswi.

Maamiri wanne hawa wakaondoka kwa baraka za Allah kwenda kutekeleza majukumu waliyo twisha na Amiri wa Waumini; Sayyidna Abubakar-Allah awawiye radhi wote. Kamanda mkuu Sayyidna Abubakar alikuwa akiwaaga maamiri na askari kwa kuwasindikiza umbali mdogo kwa miguu. Huku akiwausia kwa wasia ambao ndani yake kuna utengenevu wa Dunia na Akhera yao. Katika jumla ya hazina ya wasia ulio rithiwa kutoka kwake, ni ule wasia wake adhimu alio mpa Yazid. Na tumependelea tuuandike wote hapa kwa ukamilifu, kwa sababu ya nasaha maridhawa zilizomo humo ambazo zinamlazimu kila amiri jeshi kuzifuata. Na ufuatao ndio wasia wake huo:

“Hakika mimi nimekutawaza uamiri jeshi ili nikutahini na kukujaribu. Basi ukiitenda vema kazi yako (hii mpya), nitakurejesha katika kazi yako na nitakuongeza. Na ukitenda vibaya nitakuuzulu (nitakuondosha kwenye madaraka). Basi ni juu yako kumcha Allah, kwani hakika Yeye anaiona batini (ndani) yako kama unavyo onwa kwa dhaahiri (nje) yako. Na hakika mbora wa watu kwa Allah, ni yule mwingi wao mno kwa kutawalia mambo kwa ajili yake. Na mkaribu mno wa watu kwa Allah, ni yule mwingi wao mno kwa kujikurubisha kwake kwa amali yake. Na bila ya shaka mimi nimekutawaza kazi ya Khalid (huyu ni Bin Said Bin Al-Aasw ambaye mwanzo alipelekwa Sham na Sayyidna Abubakar). Na jiepushe na aibu za jahilia, kwani hakika Allah anazichukia na anawachukia wadau wake. Na utakapo liendea jeshi lako, basi suhubiana nalo kwa wema na anza nao kwa lile lililo bora na waahidi kulipata.

Na utakapo waidhi, basi fupisha kwani maneno mengi husahaulika. Na itengeze nafsi yako, watu watakutengenekea. Swali swala kwa nyakati zake kwa kutimiza rukuu na sijida zake na unyenyekevu ndani yake. Na watakapo kujia wajumbe wa adui yako, basi wakarimu na uchachishe ukaaji wao mpaka waondoke kambini kwako wakiwa hawajui lolote. Na wala usiwaweke muda mrefu hata wakaweza kuona mapungufu yako na wakaijua kazi yako. Wafikishie kwenye utajiri wa kambi yako na zuia watu kuzungumza nao mbele yako, wewe ndio utawalie mazungumzo yao. Na wala usiifanye siri yako kama dhaahiri yako, likachanganyika jambo lako. Na utakapo taka ushauri, basi kuwa mkweli katika maneno yako, utapewa ushauri wa kweli. Na wala usimpe mtoa ushauri hazina yote ya habari zako, usije ukaijiwa mbele yako.

Piga soga usiku na watu wako, zitakujia habari mbali mbali na zitafichuka siri mbele yako. Wakithirishe walinzi wako na watawanye katika kambi yako. Na wakague mara nyingi kwa ghafla katika malindo yao bila ya wao kujua. Basi yeyote utakaye mkuta ameghafilika na lindo lake, muadabishe kwa wema na muadhibu pasi na kupitiliza katika adhabu. Na wapangie zamu baina yao mchana na usiku na uifanye  zamu ya mwanzo ya usiku kuwa ndefu zaidi kuliko ile ya mwisho. Kwa sababu hiyo ndio nyepesi ya zamu mbili hizo kwa ajili ya ukaribu wake na mchana.

Na wala usichelee kumuadhibu mstahiki wa adhabu na wala usikosee katika adhabu hiyo na wala usiifanyie haraka. Usiwasahau watu wa kambi yako, usije ukaiharibu na wala usiwapeleleze ukawafedhehesha. Na wala usiulizie siri zao kwa watu, tosheka na dhaahiri yao. Na wala usikae na watu wa hovyo hovyo, bali kaa na wadau wa ukweli na utekelezaji. Kuwa mkweli/imara/thabiti unapo kutana na adui vitani na wala usiwe mwoga, wakawa waoga watu wako. Na jiepushe na khiana katika ngawira, kwani hiyo (khiana) hukurubisha ufakiri na kukimbiza ushindi”.

Majeshi yakaendelea kwenda mpaka yakafika Sham. Kamanda Amrou Bin Al-Aasw yeye akapiga kambi Palestina, Shurahbeelah yeye alipiga kambi Jordan. Kamanda Yazid kambi yake ilikuwa ni Al-Bulqaa, ama Abu Ubeidah yeye alipiga kambi Al-Haabiyah. Habari za ujio wa makamanda hawa zilipo gonga ngoma za masikio ya Hirakli; mfalme wa Urumi, aliwaambia watu wake: “Mimi rai yangu naona mfanye suluhu na Waislamu. Kwani wallah, nyinyi kufanya nao suluhu kwa nusu ya mazao yanayo patikana Sham na nyinyi mkabakia na nusu yake pamoja na nchi yenu. Kufanya hivyo ni bora kwenu kuliko (kupigana nao) wakakushindeni kwenye nchi ya Sham na nusu ya nchi ya Urumi. Kwa jeuri na kiburi topea walicho kuwa nacho, wakaitupilia mbali rai hiyo ya mfalme wao, hata akaenda kupiga kambi Himswi, huu ni mji wa Kisham ulioko Mashariki mwa mto Al-Aaswiy. Hapo akatoa amri ya kukusanywa majeshi, ikakusanyika idadi kubwa ya Warumi kuitika amri ya mfalme wao. Akampelekea kila kamanda wa Waislamu idadi ya majeshi inayo zidi idadi ya wanajeshi Waislamu alio nao. Kamanda Amrou Bin Al-Aasw akawashauri makamanda wenzake kukusanyika pamoja. Wakampelekea Amiri jeshi mkuu: Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi-habari za hali ilivyo. Yeye akatoa ushauri kama ule ulio tolewa na kamanda Amrou, akasema: “Hakika watu (wenye imani) kama nyinyi hawashindwi kwa sababu ya uchache (wao). Hakika si vinginevyo, hushindwa kwa sababu ya (kutenda) madhambi, basi jiepusheni nayo (msije mkashindwa)”.

Additional information