KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ADABU YA MAZUNGUMZO

Neema ya bayana (fasaha ya maelezo), ni miongoni mwa neema tukufu kabisa ambazo Allah Atukukiaye amemneemesha nazo na kumtukuza kwa sababu yake mwanaadamu juu ya viumbe wengine: “ARRAH’MAN, MWINGI WA REHEMA. AMEFUNDISHA QUR’ANI. AMEMUUMBA MWANAADAMU, AKAMFUNDISHA KUBAINI”. [55:01-04]

 

Na kwa kadiri ya utukufu wa neema, huwa kubwa haki yake na kuwajibisha kuishukuru neema husika na kukanya kuikufuru. Na Uislamu tayari ulikwisha wabainishia watu namna ya kufaidika na neema hii iliyo tolewa bure kwao. Na ni jinsi gani watakavyo yafanya maneno yao yanayo tamkwa na ndimi zao mchana kutwa, kuwa ni njia ya kuwapelekea kwenye kheri ilinganiwayo na Uislamu. Umefanya hivyo kwa sababu watu wengi hawatindikiwi na maneno na wala ndimi zao haziachi kutukutishwa na maneno. Utakapo anza kuyahesabu waliyo yasema, utayakuta ni puo lenye kupotea bure au zogo lenye kudhuru na wala hilo silo ndilo lengo la Allah kuziumba ndimi na kuzitia vinywani mwa waja wake. Na wala kipawa faidishi hakithaminiwi kwa kuyafanya hayo: “HAKUNA KHERI KATIKA MENGI YA WANAYO SHAURIANA KWA SIRI, ISIPO KUWA YULE ANAYE AMRISHA KUTOA SADAKA, AU KUTENDA MEMA, AU KUPATANISHA BAINA YA WATU. NA MWENYE KUFANYA HAYO KWA KUTAKA RADHI YA ALLAH, BASI TUTAKUJA MPA UJIRA MKUBWA”. [04:114]

Uislamu umelishughulikia na kulipa umuhimu mkubwa suala la mazungumzo (maneno) na mitindo/namna za kuyafikisha kwa walengwa. Kwa sababu maneno yanayo toka kwa mtu yeyote, yanaashiria (yanaonyesha) hakika (ukweli halisia) ya akili yake na tabia ya hulka yake. Na kwa sababu njia/namna za mazungumzo katika jamii fulani, uhukumu kiwango chake jumla na upeo wa maadili mema katika mazingira ya jamii husika.

Mtu anapaswa kujiuliza kabla ya kuzungumza na watu wengine:

F          Je, kuna ulazima wa kuzungumza? Akikuta lipo linalo pelekea kuzungumza, basi na azungumze na kama si hivyo, basi kukaa kimya ni bora zaidi kwake kuliko huko kuzungumza. Na kuacha kwake kuzungumza pale/wakati ambapo hapana dharura (lazima) ya kuzungumza, ni ibada yenye ujira maridhawa.

Abdullah Bin Masoud-Allah awawiye radhi-amesema: “Naapa kwa yule ambaye hapana Mola aabudiwaye kwa haki ila Yeye, hapana juu ya mgongo wa ardhi kitu kinacho hitajia mno kutiwa gerezani kwa muda mrefu kuliko ulimi”. Twabaraaniy-Allah amrehemu.

Na amesema Abdullah Bin Abbas-Allah awawiye radhi: “Mambo matano ni bora zaidi kwao (hao waja) kuliko farasi wenye ubora wa hali ya juu kabisa; Usizungumze lisilo kuhusu, kwani huo ni ufedhuli na wala hautosalimika na uzushi! Na wala usilizungumze lile linalo kuhusu mpaka ulipatie mahala pake, kwani huenda mzungumzaji wa lenye kumuhusu akaliweka mahala si pake, ikampata aibu! Na wala usibishane na mtu mpole wala mtu safihi (mpumbavu), kwani huyu mtu mpole atakuchukia na yule safihi atakuudhi! Na mtaje ndugu yako asipo kuwapo kwa yale ambayo wewe unapenda akutaje kwayo. Na msamehe kutokana na yale unayo penda yeye akusamehe! Na tenda matendo ya mtu mwenye yakini kwamba yeye ni mwenye kulipwa ujira kwa wema (autendao) na ni mwenye kuadhibiwa kwa uovu”. Ibn Abi Dunyaa-Allah amrehemu.

Muislamu hayawezi hayo ila pale atakapo umiliki ulimi wake na akazitawala barabara hatamu zake, akaufudikiza pale panapo lazimu kukaa kimya na akaudhibiti pale panapo taka kuzungumza. Ama wale wanao buruzwa na ndimi zao, hakika si vinginevyo zinawaburuzia kwenye maangamivu yao.

Hakika ubwabwaji ni makelele yanayo ondosha akili ongofu. Na wengi wale ambao hukaa mabarazani (vijiweni), wakafungulia bomba la maneno, humfanya msikilizaji wao kutinda ya kwamba wao hawayatoi maneno yao kutoka katika mwamko hai au fikra zilizo enda kina. Na huenda akadhania kwamba kuna kitenganishi baina ya akili ya mzungumzaji na hayo maneno yanayo mtoka.

Mtu anapo taka kuzikusanya fikra zake na kuyadurusi (review) matendo yake, hukimbilia kwenye ukimya (kutokuzungumza). Lakini pia anapo taka kuiona (kuitambua) nafsi yake na kuiweka sawa (kuipanga) akili yake, huyakimbia mazingira yenye makelele (ya mjini) akaenda mashambani kuliko kimya au huenda kwenye kiunga kilicho tulivu. Kwa ajili hii basi, ikawa hapana budi Uislamu uusie kukaa kimya na ukakuhesabu kuwa ni miongoni mwa njia za malezi bora. Kwani katika jumla ya nasaha za Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa Abu Dharri, alimwambia: “Jilazimishe na ukimya mrefu, kwani huo ni kimbizo la Shetani na ni msaada kwako katika suala la dini yako”. Ahmad-Allah amrehemu.

Naam, ni kweli kwamba ulimi uachiliwao ni kamba iliyoko mkononi mwa shetani, akimsarifu mwenyewe kama atakavyo. Mtu atakapo kuwa hayamiliki mambo yake, kinywa chake huwa ni lango la kuingilia ndani makatazwa ambayo huuchafua moyo wake na kuongeza juu yake mapazia ya mghafala. Na ilhali Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekwisha sema: “Haitosimama sawa imani ya mja mpaka usimame sawa moyo wake na wala hautosimama sawa moyo wake mpaka usimame sawa ulimi wake”. Ahmad-Allah amrehemu.

Na hatua ya mwanzo kabisa ya usimama sawa huu uelezwao, ni mtu kujipangusa mikono yake na lile lisilo muhusu na wala asijitose katika lile ambalo hatoulizwa: “Sehemu ya uzuri wa imani ya mtu, ni kule kuacha kwake lisilo muhusu”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Na kuwa mbali na puo/upuuzi ni katika jumla ya nguzo za kufaulu na Qur-ani Tukufu imelitaja hilo baina ya nguzo mbili miongoni mwa nguzo lazima za Uislamu, ambazo ni swala na zaka: “HAKIKA WAMEFANIKIWA WAUMINI, AMBAO NI WANYENYEKEVU KATIKA SWALA ZAO, NA AMBAO HUJIEPUSHA NA MAMBO YA UPUUZI, NA AMBAO WANATOA ZAKA”. [23:01-04]

Uislamu umayechukia mambo ya upuuzi/porojo/uchekeshaji, kwa sababu mambo hayo yanaupoteza umri katika lile ambalo mwanaadamu hakuumbwa kwa ajili yake. Kwani mwanadamu ameumbwa awe mtu mwenye juhudi/bidiii na uzalishaji ili auamirishe uliwengu wake kwa manufaa ya akhera yake. Na sio kuupoteza muda wake katika mambo yasiyo na faida kwake si katika dini yake tu, bali hata katika dunia na akhera yake. Na kwa kadiri ya kujiepusha muislamu na mambo hayo ya upuuzi, ndio huwa daraja/nafasi yake mbele ya Allah.

Imepokewa kutoka kwa Anas Bin Maalik-Allah amuwiye radhi-amesema: Alikufa mtu mmoja, mtu mwingine akasema na ilhali Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akisikia: Furahia kupata pepo! Mtume akasema: “Pengine wewe hujui, huenda yeye alilizungumza lisilo muhusu au alikifanyia ubakhili kisicho mpunguzia”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Na mpiga porojo kwa sababu ya mawasiliano dhaifu baina ya fikra zake na matamshi yake, huongea bila ya mpango (hupayuka payuka). Pengine likamtoka neno ambalo likawa ndio sababu ya maangamivu yake na likaudamirisha (uharibu) mustakabali wake. Na pamesemwa: Mwenye kukithiri porojo zake, hukithiri makosa yake.

Na mshairi mmoja amepata kusema:

Hufa kijana kutokana na kwao la ulimi wake,

     Na wala mtu hafi kutokana na kwao la mguu wake.

 

Na imekuja katika hadithi sahihi: “Hakika mja huweza kuzungumza neno, halisemi ila kwa lengo la kuwachekesha watu, ataporomoka nalo mbali kuliko umbali uliopo baina ya mbingu na ardhi. Na hakika mtu huteleza zaidi kwa ulimi wake kuliko anavyo teleza kwa miguu yake”.

Additional information