KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

MAZUNGUMZO BAINA YA MITUME NA KAUMU ZAO...Inaendelea/4

Hebu sasa tuhamie kwenye midahalo/majadiliano mengine, yaliyo tokea baina ya Mtume Hud-Amani imshukie-na kaumu yake, walio kuwa wakiyaabudu masanamu.  Na walikuwa maarufu kwa utajiri na nguvu ya mwili.

 

Mtume Hud-Amani imshukie-aliwaamrisha watu wake kumuabudu Allah Ataadhamiaye peke yake na kuitupilia mbali ibada ya masanamu waliyo izoea na kuirithi kutoka kwa wahenga wao. Basi je, ndugu msomaji unafikiri walimjibu nini? Hebu yasikilize yaliyo semwa na watopea wa upotevu katika kaumu yake, kama walivyo nukuliwa na Qur-ani Tukufu: “WAKASEMA WATUKUFU WA WALE WALIO KUFURU KATIKA KAUMU YAKE: SISI TUNAKUONA UMO KATIKA UPUMBAVU, NA HAKIKA SISI TUNAKUFIKIRIA KUWA WEWE NI KATIKA WAONGO”. [07:66]

Yaani: Walisema wale wenye vyeo na mamlaka katika kaumu ya Mtume Hud, kumwambia kwa namna ya kebehi na utovu wa adabu: Ewe Hud! Hakika sisi bila ya shaka, tunakuona wewe ni punguani, kwa sababu umeiacha dini ya wahenga na umetuletea dini mpya, tunaikataa na wala hatuikubali. Na sisi tunaitakidi kabisa kwamba wewe ni katika waongo. Hivyo ndivyo kaumu Hud walivyo mrudi Mtume wao, pale alipo waambia: Enyi watu wangu! Muabuduni Allah, nyinyi hamna mungu mwingine ila Yeye tu. Naye aliyakabili marejezo mabaya hayo ya watu wake kwa mantiki hekima na kwa kuilinda nafsi yake, kwa muundo unao simama juu ya hoja. Basi je, aliwaambia nini? “AKASEMA: ENYI WATU WANGU! MIMI SINA UPUMBAVU. LAKINI MIMI NI MTUME NILIYE TOKA KWA MOLA MLEZI WA VIUMBE VYOTE. NAKUFIKISHIENI UJUMBE WA MOLA WANGU MLEZI. NA MIMI KWENU NI MWENYE KUKUNASIHINI, MUAMINIFU. MNAONA AJABU KUKUFIKIENI MAWAIDHA KUTOKA KWA MOLA WENU MLEZI KWA MTU ALIYE MMOJA WENU NYINYI ILI AKUONYENI? NA KUMBUKENI ALIVYO KUFANYENI MSHIKE MAHALA PA KAUMU YA NUHU, NA AKAKUZIDISHENI KATIKA UMBO. BASI ZIKUMBUKENI NEEMA ZA ALLAH ILI MPATE KUFANIKIWA”. [07:67-69]

Basi ndugu msomaji mwema-Allah akurehemu-unaona kwamba Mtume Nuhu katika jawabu hili lenye busara alilo lielekeza kwa kaumu yake. Amejikanushia tuhuma za usafihi (upumbavu), kisha akawabainishia dhima (kazi) yake na tabia ya ujumbe wake. Halafu tena baada ya hayo, akawaambia ya kwamba yeye kwa muktadha wa udugu wake na wao, si jambo liingialo akilini yeye kuwaongopea au kuwahadaa wao. Na kwamba hakika si vinginevyo, yeye ni mtoa nasaha, muaminifu, anaye waongozea kwenye yanayo wanufaisha. Kisha akaanza kuwakumbusha uhalisia wao (wao ni nani) na neema za Allah zilizo juu yao na akawaamrisha kuzishukuru neema hizo, ili Muumba wao apate kuwaongezea.

Lakini wapi, watu maasi katika kaumu yake wakawa vipofu na viziwi, wasizione wala kuzisikia nasaha hizi, na wakamwambia kwa ghururi na jeuri iliyo pituka: “...JE! UMETUJIA ILI TUMUABUDU ALLAH PEKE YAKE, NA TUYAACHE WALIYO KUWA WAKIYAABUDU BABA ZETU? BASI TULETEE HAYO UNAYO TUAHIDI, UKIWA MIONGONI MWA WASEMAO KWELI”. [07:70]

Hivyo ndivyo walivyo khitimisha majadiliano yao kwa kutoa changamoto, vitisho na kwa kumbeza yeye na nasaha zake.

Na mahala pengine tunamuona akianzisha mazungumzo nao kwa kuwaamrisha kumuabudu Allah Ataadhamiaye peke yake, wasimshirikishe na yeyote/chochote. Na kwa kuwaambia ya kwamba yeye hahitaji ujira wowote kutoka kwao ukiwa kama malipo ya mahubiri yake hayo kwao. Na kwa kuwaongoza ya kwamba kumuomba kwao Muumba wao maghufira na kwa kutubia kwake, itakuwa ni sababu tosha ya wao kuzidishiwa utajiri juu ya utajiri walio nao, na nguvu nyingine ziada ya hizo walizo nazo. Hebu zisikilize aya za Qur-ani zikituhadithia hilo, inasema: “NA KWA KINA A’ADI TULIMTUMA NDUGU YAO HUD. AKASEMA: ENYI WATU WANGU! MUABUDUNI ALLAH! NYINYI HAMNA MUNGU ISIPO KUWA YEYE. NYINYI SI CHOCHOTE ILA NI WAZUSHI TU. ENYI WATU WANGU! SIKUOMBENI UJIRA KWA AJILI YA HAYA. HAUKUWA UJIRA WANGU ILA KWA YULE ALIYE NIUMBA. BASI HAMTUMII AKILI? NA ENYI WATU WANGU! MUOMBENI MSAMAHA MOLA WENU MLEZI, KISHA MTUBIE KWAKE. ATAKULETEENI MBINGU ZENYE KUNYESHA MVUA YA KUMIMINIKA. NA ATAKUZIDISHIENI NGUVU JUU YA NGUVU ZENU. WALA MSIGEUKE MKAWA WAKOSEFU”. [11:50-52]

Lililo kuwa likitazamiwa kwa kaumu yake, lau wangeli kuwa na akili, ni wao kumsikiliza yeye baada ya kuwalingania mara tatu na baada ya kuwabashiria na kuwakhofisha. Lakini wapi, wao waliikabili miongozo tukuka hii kwa kujikweza juu yake na kwa kumbeza, basi je walisema nini? “WAKASEMA: EWE HUD! HUJATULETEA DALILI WAZI. WALA SISI HATUIACHI MIUNGU YETU KWA KUIFUATA KAULI YAKO. NA WALA SISI HATUKUAMINI WEWE. SISI TUNASEMA: BAADHI KATIKA MIUNGU YETU IMEKUSIBU KWA BAA...” [11:53-54]

Yaani: Walimwambia Mtume na Mwongozi wao: Kwanza wewe hujatuletea hoja kinaishi zinazo turidhisha. Pili, sisi katu hatutoacha kuiabudu miungu yetu iliyo kuwa ikiabudiwa na baba zetu, kwa sababu tu ya maneno yako matupu; yasiyo na dalili! Tatu, sisi tutaendelea kukukhalifu, kwa sababu wewe kwetu ni katika watu waongo. Nne, sisi tunaitakidi ya kwamba kuacha kwako kuiabudu miungu yetu, kumeifanya baadhi ya miungu hiyo kukughadhibikia, na hilo likapelekea wewe kupatwa na uwendawazimu na uropokaji. Na wala wao hawakusema: MIUNGU YETU YOTE IMEKUSIBU KWA BAA, lakini wao walisema kama walivyo nukuliwa na Qur-ani: “BAADHI KATIKA MIUNGU YETU IMEKUSIBU KWA BAA”. Ikiwa ni kauli ya utisho kwake na dokezo ya kwamba lau miungu yote ingeli mghadhibikia, basi bila ya shaka ingeli muangamiza kabisa, tena mara moja.

Hivi ndivyo tunavyo waona wakimrudi Mtume na Muongozi wao kwa majawabu manne, wamepomoka katika majawabu hayo kutoka kwenye hali mbaya kuingia kwenye hali mbaya mno. Jambo linalo julisha jeuri na uovu wao ulio chupa mpaka. Basi je, ndugu msomaji mwema-Allah akurehemu-unafikiri nini ulikuwa msimamo wa Mtume huyu kwa kaumu yake? Msimamo wake kwao, ulikuwa ni msimamo wa mtu mwenye kujitenga mbali na ushirikina wao, mtoa changamoto kwenye jeuri yao na mwenye kumtegemea Allah Ataadhamiaye peke yake katika kumnusuru dhidi yao. Na Qur-ani imelinukuu jibu rejezi lake kwao: “...AKASEMA: HAKIKA MIMI NAMSHUHUDISHA ALLAH, NA NYINYI SHUHUDIENI, YA KWAMBA MIMI NAJITENGA MBALI NA HAO MNAO WAFANYA WASHIRIKA, MKAMWACHA YEYE. BASI NYOTE NYINYI NIPANGIENI VITIMBI, NA KISHA MSINIPE MUHULA! HAKIKA MIMI NIMEMTEGEMEA ALLAH, MOLA MLEZI WANGU NA MOLA MLEZI WENU. HAPANA KIUMBE YEYOTE ILA YEYE ANAMWENDESHA ATAKAVYO. HAKIKA MOLA WANGU MLEZI YUKO JUU YA NJIA ILIYO NYOOKA. NA IKIWA WATARUDI NYUMA, BASI MIMI NIMEKWISHA KUFIKISHIENI NILIYO TUMWA KWENU. NA MOLA WANGU MLEZI ATAWALETA WATU WENGINE BADALA YENU, WALA NYINYI HAMUMDHURU KITU YEYE. HAKIKA MOLA WANGU MLEZI NI MWENYE KUHIFADHI KILA KITU”. [11:54-57]

Yaani: Nabii Hud-Amani imshukie-alisema katika kuwarudi waasi katika kaumu yake: Hakika mimi ninamshuhudisha Allah ambaye hapana mola muabudiwa ila Yeye, na pia ninakushuhudisheni nyinyi, ya kwamba mimi ni mbali na kuabudu yeyote/chochote kisicho Yeye.

Kisha baada ya kujitenga na ushirikina wao huo, anaguria kwenye kuwapa changamoto kwa dhati ya moyo na utuvu wa nafsi, anawaambia: Haya mimi huyu mbele yenu, basi unganeni na miungu yenu hiyo ya uzushi, kisha nyote pamoja mnipige vita, hakika mimi siwaogopi nyinyi wala masanamu yenu,

Kisha baada ya hapo anahamia kwenye kubainisha ya kwamba sababu ya kuwaona wao na miungu yao si lolote/chochote, ni kwamba yeye ameyaacha mambo yake yote mikononi mwa Allah Ataadhamiaye. Ambaye hapana kinyama chochote kitambaacho juu ya ardhi, ila Yeye ndiye Mmiliki wake anaye kiendesha atakavyo.

Kisha anayakhitimisha majadiliano yake nao na majibu rejezi yake kwao, kwa kuwatahadharisha dhidi ya mwisho mbaya wa ghururi yao na kuishikilia kwao kufuru yao. Na akawabainishia ya kwamba ushikilia wao huo utawapelekea kwenye hilaki yao. Na utapelekea kuletwa kwa watu wengine watakao kuwa badala yao na kwamba katu ulimwengu huu hautabadilika kwa sababu ya kuangamizwa kwao. Kwani wao ni viumbe duni mno kuweza kubadili utaratibu maumbile wa Allah alio wapangia viumbe wake.

Na katika sehemu ya tatu, tunamuona akiukanya uasi/ujeuri wao na kujiona kwao kwa sababu ya nguvu walizo nazo, anawaambia: “JE! MNAJENGA JUU YA KILA MNYANYUKO KUMBUSHO LA KUFANYA UPUUZI? NA MNAJENGA MAJENGO YA FAKHARI KAMA KWAMBA MTAISHI MILELE! NA MNAPO TUMIA NGUVU MNATUMIA NGUVU KWA UJABARI. BASI MCHENI ALLAH NA NITIINI. NA MCHENI ALIYE KUPENI HAYA MNAYO YAJUA. AMEKUPENI WANYAMA WA KUFUGA NA WANA. NA MABUSTANI NA CHEMCHEM. HAKIKA MIMI NINAKUKHOFIENI ADHABU YA SIKU KUBWA”. [26:128-135]

Yaani: Baada ya Mtume Hud-Amani imshukie-kuwaamrisha watu wake kumuabudu Allah peke yake. Na akawabainishia ya kwamba yeye hahitaji ujira wowote kutoka kwao, ukiwa ni malipo ya mahubiri yake kwao. Akahamia kwenye kukana anasa na uasi walio nao, akawaambia: Nyinyi mnajenga majengo kwenye vilima kwa ajli ya pumbao na mchezo, ili majengo hayo yawe nembo, anasa na ghururi zenu. Na mnajenga makasri makubwa mno kama kwamba mtaishi milele bila ya kufa. Na mnapo taka kumfanyia uadui mtu, mnatumia nguvu kubwa na ukatili wa kutisha juu yake, bila hata ya kuwa na chembe ya huruma, upole waka sikitiko. Na ukiwa huo ndio mtindo wenu wa maisha, basi mimi nakukatazeni acheni kufanya hivyo. Na ninakutahadharisheni mwisho mbaya wa anasa hizi, ghururi na dhulma muifanyayo. Na ninakuamrisheni kumcha na kumuogopa Allah.

Mwenye kuyazingatia mazungumzo/majadiliano haya, yaliyo jiri baina ya Mtume Hud-Amani imshukie-na kaumu yake. Atayaona yamepambwa na hoja angavu, ujasiri nadra, nasaha kita nyoyo na uwazi fumbulizi kwa upande wa Mtume Hud. Naye akijibiwa kwa nguvu, ghururi na hali nzuri ya maisha ya kaumu yake. Ama kaumu yake, mazungumzo yao yalisimama juu ya msingi wa kumbeza Mtume wao, na kumpa wasifu wa upumbavu na uongo. Kama yalivyo simama juu ya kung’ang’ania ukafiri na ushirikina wao na kudai kwao ya kwamba miungu yao inanufaisha na inadhuru. Na kumpa changamoto Mtume wao kwa kutegemea nguvu zao, kiasi cha kufikia kusema: Nani ana nguvu kutushinda sisi?! Na mwisho wao ukawa ni maangamivu na hilaki.

Additional information