KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

JAMVI LA RAMADHANI : “TUIKARIBISHE NA TUIPOKEE RAMADHANI KWA TWAA /3”

 

Juma hili kwa auni na uwezeshi wake Allah tutajifunza adabu/taratibu za usomaji wa Qur-ani Tukufu. Lakini kabla hatujaanza kuzielezea adabu hizo, tunaendelea kusisitiza ya kwamba Qur-ani Tukufu ni maneno yake Mola yaliyo teremshwa na Malaika Jibrilu-Amani imshukie-kwa Mtume Muhammad-Rehema na Amani zimshukie. Allah Mtukufu anasema: “Na ikiwa mmojawapo wa washirikina akikuomba ulinzi, basi mpe ulinzi apate kusikia maneno ya Allah (Qur-ani)...”. At-taubah [09]:06

 

 

Tukishatambua na kukiri ya kwamba Qur-ani ni maneno ya Allah, sasa tukubali kwamba kuisoma Qur-ani ni wajibu wa kila muislamu, kama alivyo sema Mola Mtukufu: “...basi someni kilicho chepesi katika Qur-ani...”. Al-Muzzammil [73]:20

 

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia: “Isomeni Qur-ani, kwani hakikayo itakuja siku ya Kiyama hali ya kuwa ni yenye kuwaombea watu wake”. Muslim-Allah amrehemu.

 

Ndugu muislamu-Allah akurehemu-fahamu na ufahamikiwe ya kwamba kuihama, kuipuuza, kutoshughulika na kutokuisoma Qur-ani, ni kuipinga amri ya Allah na Mtume wake. Qur-ani Tukufu ni kitabu chako ulicho shushiwa wewe ili kiwe ni mwongozo na katiba katika maisha yako, ukishikamana nayo utaishi kama atakavyo mwenye Dunia yake na ukiipuuza utahiliki na kuangamia. Ni wajibu wetu kujifunza, kuisoma na kuishi na Qur-ani na katika kuutekeleza wajibu huo ni vema tukafahamu ya kwamba usomaji wa Qur-ani una adabu/taratibu zake ambazo msomaji anapaswa kuzijua na kuzifuata. Kwani ni kwa kuzifuata adabu/taratibu hizo ndipo kisomo chake hicho kitabariki na atapata ujira kwa ukamilifu. Zifuatazo sasa ni baadhi ya adabu/taratibu hizo, tuzisome, tuzielewe na kisha tuzifanyie kazi:

 

 1. Nia njema: Tulikusudialo kwa nia njema hapa ni msomaji wa Qur-ani kuwa na ikhlasi katika usomaji wake, aisome Qur-ani kwa ajili ya Allah tu na wala asiisome kwa ajili ya kusifiwa au kupata pesa. Tutambue ya kwamba amali yoyote ikikosa Ikhlasi; kwa kutendwa pasina kumkusudia Allah peke yake, amali hiyo haikubaliwi na wala haipokelewi na Allah. Cha kutangulizwa katika amali ni Ikhlasi na mengine yawe ni matokeo na wala yasiwe ndio makusudiwa. Kuwa na Ikhlasi katika amali ni amri yake Allah kama alivyo sema katika kitabu chake kitukufu: “Nao hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Allah kwa kumtakasia Dini (Ikhlasi), wawe waongofu...”. Al-Bayyinah [98]:05

 

Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema hivi kuhusiana na Ikhlasi: “Hakika Allah Mtukufu haikubali amali ila tu ile ambayo imetakata kwa ajili yake tu na pakakusudiwa dhati yake tu”. Nasaaiy [3140]-Allah amrehemu.

 

Ndugu yetu muislamu-Allah akurehemu-kwa muktadha wa aya na hadithi tulizo kunukulia hivi punde, ni wajibu wa msomaji wa Qur-ani kuwa na ikhlasi katika kusoma kwake na aepuke kuisoma Qur-ani ili kuwaonyesha watu kuwa yeye anajua, yeye ndiye bingwa, yeye ana sauti nzuri. Kufanya hivyo itakuwa ni riya ambayo haitamzawadia ila sifa na kupata vilivyomo mikononi mwa watu lakini mbele ya Allah atakuwa ni muflisi. Lakini nia yake iwe tu ni kupata ujira na thawabu zilizo ahidiwa kupata mwenye kusoma Qur-ani. Hali kadhalika, anuie katika kusoma kwake:

 

 • Kupata uwongofu kutoka katika kitabu hicho,

 • Kukifanyia kazi anacho kisoma,

 • Kufuata na kutumia hukumu zake; maamrisho na makatazo. Penye amri akaamrika na penye makatazo akakatazika, na

 • Kujifunza namna ya kumridhisha Mola Muumba wake.

 


 

 1. Kutaraji kupata thawabu:

 

Muislamu anatakiwa aisome Qur-ani kwa nia ya kutaraji kupata ujira wa usomaji wake kutoka kwa Allah aliye Mtukufu na atafute kupata ujira ulioa ahidiwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-pale alipo sema: “Atakaye soma herufi moja katika kitabu cha Allah, atapata yeye kwa (herufi moja) hiyo jema moja na jema moja kwa kumi mfano wake. Sisemi kwamba ‘Alif Laam Miim’ hiyo ni herufi moja, lakini Alif ni herufi moja, Laam ni herufi na Miim ni herufi nyingine”. Tirmidhiy [2910]-Allah amrehemu.

 


 

 1. Kusoma Qur-ani akiwa katika hali ya twahara:

 

Muislamu kukisoma kitabu cha Allah hali ya kuwa ana twahara, jambo hilo humpatia ujira mkubwa zaidi kuliko kukisoma pasina kuwa na twahara. Hatusemi kwamba muislamu haruhusuwi kuisoma Qur-ani akiwa hana twahara; kwa maana ya udhu. Anaweza kusoma, lakini pasina kuushika msahafu bali atasoma kile alicho kihifadhi moyoni mwake. Wawili hawa; huyu anaye soma Qur-ani akiwa na twahara na yule anaye isoma akiwa hana twahara, katu hawalingani kiujira. Kwa hivyo basi, ili uhodhi ujira mkubwa, jitahidi kusoma Qur-ani ukiwa na twahara.

 


 

 1. Kujitwaharisha kwa ajili ya kuushika/kuugusa msahafu:

 

Katika jumla ya adabu za Qur-ani, ni muislamu kuhakikisha kuwa ana twahara kabla ya kukishika au kukigusa kitabu cha Allah, kwani Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ametuambia: “Hasiishike/hasiiguse Qur-ani ila aliye twahara”. Twabaraaniy [12/313]-Allah amrehemu.

 

Naam, ijapo kuwa baadhi ya Wanazuoni-Allah awarehemu-wamejuzisha kuushika/kuugusa msahafu pasina udhu. Lakini lililo bora ni muislamu kutawadha kabla ya kuushika/kuugusa msahafu, kwani jambo hilo ndilo linalo mpelekea mtu kuwa na unyenyekevu zaidi na kuwavutia malaika kuhudhuria ili kuisikiliza Qur-ani.

 


 

 1. Kuelekea Kibla wakati wa kusoma Qur-ani:

 

Muislamu kuelekea Kibla wakati wa kusoma Qur-ani, si sharti ambalo ni lazima litimizwe kwanza ndipo aweze kusoma Qur-ani, la hasha. Lakini tu, Wanazuoni wetu walio tusomesha na kutuonyesha thamani ya Qur-ani-Allah awarehemu-wanatuambia kuelekea Kibla wakati wa kusoma Qur-ani, jambo hilo humpelekea mno mtu kuwa na unyenyekevu na hudhuri ya moyo.

 


 

 1. Kusoma Qur-ani akiwa amekaa kitako:

 

Naam, hili pia sio sharti, bali tu Wanazuoni wetu wameona ya kwamba mtu kusoma akiwa amekaa kitako, hilo humpelekea mno kuwa na heshima na kitabu chake Mola na ni katika jumla ya kuyatukuza na kuyaheshimu matukufu yake. Pamoja na hivyo, mtu akisoma Qur-ani huku anatembea, amesimama wima au amelala, inajuzu. Kwa sababu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Alikuwa akimdhukuru Allah katika hali zake zote”. Muslim [373]-Allah amrehemu.

 


 

 1. Kupiga mswaki kabla ya kuanza kusoma Qur-ani:

 

Muislamu anatakiwa kupiga mswaki kabla ya kusoma Qur-ani ili iwe nzuri harufu ya kinywa chake ambamo humo yanatoka maneno ya Allah. Imepokewa katika Hadithi ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakapo amka mmoja wenu kuswali usiku, basi na apige mswaki. Kwani mmoja wenu anapo soma (Qur-ani) ndani ya swala yake, Malaika huweka kinywa chake karibu na kinywa chake (mswaliji), hakitoki kinywani mwake chochote ila huingia kwenye kinywa cha malaika”. Al-Baihaqiy [02/381]-Allah amrehemu.

 

Ndugu muislamu-Allah akurehemu-hizo ndizo fadhila kubwa sana za mtu kuamka kuswali usiku na fadhila za kuisoma Qur-ani katika swala za usiku. Kwa hivyo basi, kunampasa kila muislamu kulichunga jambo hilo.

 


 

 1. Kuisoma Qur-ani kwa utaratibu na utungo:

 

Ili muislamu azihodhi fadhila adhimu na ujira maridhawa kutokana na kuisoma Qur-ani, anapaswa kuisoma Qur-ani kwa utuvu, utaratibu na utungo. Hilo litapatikana kwa kuzitamka herufi kwa usahihi kutoka kwenye matokeo yake na kuchunga na kufuata hukumu za usomaji ambazo ni somo na fani kamili inayo jitegemea (TAJWEED). Tutambue kuisoma Qur-ani kwa utuvu, utungo na utaratibu ni amri yake Mola pale alipo tuambia: “...na soma Qur-ani kwa utaratibu na utungo”. Al-Muzzammil [73]:04

 


 

 1. Kuisoma Qur-ani kwa sauti nzuri:

 

Miongoni mwa adabu za Qur-ani, ni muislamu kuisoma Qur-ani kwa sauti nzuri, yenye kupendeza na kumvutia msikilizaji. Na kufanya hivyo hakupungui kuwa ni kulitekeleza agizo la Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-pale alipo uambia umma wake: “Ipambeni Qur-ani kwa sauti zenu, kwani sauti iliyo nzuri inaizidhishia Qur-ani uzuri”. Al-Haakim [01/768] & Ad-Daaramiy [3501]-Allah awarehemu.

 

Na akasema tena Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Allah hajapatapo kutoa idhini ya jambo/kitu kiasi alicho mpa idhini mtume (idhini ya) sauti nzuri anayo rindima kwa kuisoma Qur-ani, akiidhihirisha kwayo (hiyo sauti nzuri)”.

 

Usiku mmoja Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-alichelewa kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamuuliza: “Ni lipi lililo kuchelewesha?” Akajibu: Kilicho nichelewesha ni kisomo cha mtu ambaye sijapatapo kuisikia sauti nzuri kuliko yake. Mtume akainuka akamsikiliza kwa kitambo, kisha akasema: “Huyo ni Salim; huru wa Abu Hudhaifa. Kila sifa njema ni zake Allah ambaye amewaweka katika umati wangu watu kama yeye”.

 

Ndugu muislamu-Allah akurehemu-kwa mujibu wa maneno hayo ya Bwana Mtume, kunampasa kila msomaji wa Qur-ani kujitahidi kuisoma kwa sauti nzuri kwa kadiri ya uweza wake, kwani Malaika huhudhuria kuisilikiza Qur-ani pale inapo somwa. Si hivyo tu, hata watu na majini pia hupenda kumsikiliza msomaji mwenye sauti nzuri. Kwa hivyo basi, sauti nzuri huwavutia watu na viumbe wengine wa Allah kuisikiliza Qur-ani na kupitia huko kuisikiliza wakapata kuzingatia na kuifanyia kazi.

 


 

 1. Qur-ani impe msomaji wake huzuni na unyenyekevu:

 

Msomaji wa Qur-ani anapaswa kuwa na unyenyekevu wakati anapo isoma Qur-ani na aingiwe na huzuni au ajikalifishe kuwa na huzuni na unyenyekevu. Lakini asifanye hivyo kwa riyaa wala kwa kutafuta sifa na kujionyesha mbele za watu. Bali analo takiwa kufanya, ni yeye kuivuta huzuni na unyenyekevu kwa kuzipeleka fikra zake kwenye Qur-ani anayo isoma. Aone kuwa anasoma maneno matukufu ya Allah, auone utukufu na ukubwa wa mwenye maneno yake ili kutimie kufaidika kwake na Qur-ani Tukufu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mzuri kushinda watu wote kwa kisomo (cha Qur-ani), ni yule ambaye anapo soma, unamuona ya kwamba yeye anamuogopa Allah”.

 


 

 1. Kulia au kujiliza wakati wa kuisoma Qur-ani:

 

Ndugu muislamu-Allah akurehemu-fahamu ya kwamba msomaji wa Qur-ani anatakiwa kulia kadiri awezavyo wakati anapo isoma Qur-ani na kama hakuweza kulia basi na ajilize. Allah Mtukufu anasema: “...wanapo somewa aya za Mwingi wa rehema, huanguka kusujudu na kulia”. Maryam [19]:58

 

Na akasema tena Mola Muumba na Mlezi wetu: “...hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu. Na wanasema: Sub-haana Rabbinaa. Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe. Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidishia unyenyekevu”. Al-Israa [17]:107-109

 

Na mahala pengine akasema Allah: “Na wanapo sikia yaliyo teremshwa kwa Mtume, utaona macho yao yanachururika machozi kwa sababu ya haki waliyo itambua...”. Al-Maaidah [05]:83

 


 

Ewe ndugu Muislamu-Allah akurehemu-fahamu na utambue ya kwamba hakika si vinginevyo, kulia huku na unyenyekevu huu ulio tajwa katika aya tulizo kunukulia. Haupatikani ila tu kwa msomaji au msikilizaji kujawa na hisia za utukufu/ukubwa wa Allah ndani ya fikra, moyo na mwili wake wote wakati anapo kisoma kitabu cha Allah au anapo sikiliza maneno ya Allah yakisomwa. Na kwamba Yeye Allah ndiye aliye zungumza naye kupitia hiyo Qur-ani anayo isoma wakati huo. Na ikiwa kunyenyekea na kulia huko kunafahamisha jambo, basi hakika jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kuwa ni dalili ya moyo wa msomaji/msikilizaji kuwa hadhiri wakati wa kusoma/kusomwa Qur-ani Tukufu. Tumewaona watu wangapi wakilia kutokana na kuguswa na Kaswida/nyimbo yenye maudhui na mirindimo ya huzuni, basi ni katika mlango wa ubora mtu kulia wakati anapo soma/somewa Qur-ani.

 

Naam, ewe ndugu yetu mwema-Allah akurehemu-hilo ndilo jamvi letu la juma hili, tunatumai kwa uwezo wake Allah ya kwamba jamvi lako litakuwa linazidi kukusogeza karibu zaidi na kitabu cha Allah, ukaribu utakao kudhaminia amani, furaha na salama katika maisha haya ya ulimwengu huu wa mpito na yale ya milele yasiyo na ukomo. Tumuombe Mola wetu Mtukufu aturuzuku mahaba ya kushikamana, kukipenda na kuishi na kitabu chetu Qur-ani katika kila nukta na kipengele cha maisha yetu. Na pia tuzidi kumuomba atupe uhai na uzima tukutane tena katika jamvi letu la juma lijalo, tuendelee kuishi na adabu/taratibu za Qur-ani. Muwezeshaji wetu Mkuu ni Allah na Yeye ndiye Mbora wa Wawezeshaji wote.

 

Additional information