KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

VITA VYA UBULLAH

Kamanda Khalid Ibn Waleed-Allah amuwiye radhi-akaenda mpaka akakaribia Al-Ubullah, hapo akaligawa jeshi lake makundi matatu. Kundi la kwanza akampa uongozi wake Al-Muthana Ibn Haarith As-shaibaaniy, kundi la pili akamtawaza Adiy Ibn Haatim   At-twaiy kuwa amiri wake. Na lile la tatu likawa chini ya uongozi wake yeye mwenyewe. Akayatanguliza mbele yale makundi mawili, yeye akabakia na akawaambia wakutane Al-Hufair (Hili ni eneo lililopo kwenye njia itokayo Makah kwenda Basra, nalo liko karibu na Ubullah).

 

Mbabe wa ukanda huu hatari, alikuwa ni mmoja wa viongozi wa Fursi akiitwa Hurmuz. Hurmuz alikuwa akichukiwa sana na Waarabu kwa sababu ya kuwashambulia kwake mara kwa mara na kila mmoja alitaka kulipa kisasi kwake. Hurmuz alipo zisikia khabari za ujio wa kamanda Khalid na kwamba ameagana na vikosi vyake tangulizi kukutana Al-Hufair. Akatangulia yeye na jeshi lake kufika mahala hapo, kamanda Khalid nae akageuza muelekeo akalielekeza jeshi lake kwenda Kaadhwimah. Hurmuz akapata khabari, akaharakisha akatangulia kufika yeye hapo. Hapo jeshi la Waislamu halikuwa na uchaguzi ila kupiga kambi katika eneo kame; lisilo na maji. Khalid akaliambia jeshi lake: Piganieni nao maji, hakika Allah atayafanya kuwa mashukio ya lenye subira zaidi kati ya makundi mawili haya. Yeye akatoka mbele katikati ya safu akitaka mubaaraza (mpambano wa watu wawili) wa chini (sio wa juu ya mnyama). Hurmuz akamtokea, akashuka kutoka kwenye farasi wake, kamanda Khalid akamuingia maungoni. Wafursi walipo ona hivyo, wakataka kumuendea kinyume Khalid, wakamshambulia, lakini kitendo chao hicho hakikumzuia yeye kumuua kiongozi wao. Qa’aqaa alipo ona hivyo, akaliongoza jeshi la Waislamu na kufanikiwa kumuondoshea kamanda Khalid kiwingu cha Wafursi. Vita vikauma, mushrikina wakaendeshwa mbio na kushindwa.

Hivi ndivyo vita vya kwanza vilivyo jiri baina ya Waislamu na Wafursi. Baada ya ushindi huo, kamanda Khalid akapeleka khabari njema ya ushindi na khumsi (1/5) ya ngawira kwa Sayyidna Abubakar-Allah amuwiye radhi. Alifanya hivyo baada ya kugawanya nne ya tano (4/5) ya ngawira kwa wapiganaji. Akampa mpiganaji wa miguu fungu moja na mpiganaji wa farasi mafungu mawili.

Kamanda Khalid baada ya kumaliza kugawa ngawira, akamtuma    Al-Muthanna Ibn Al-Haarith kuwafuatia nyuma mushrikina walio kimbia. Hakuwafanyia maudhi wakulima kama walivyo usiwa na khalifa Abubakar-Allah amuwiye radhi. Khabari hizi za ushindwa zilipo mfikia mfalme wa Fursi aliye itwa Azdasheer aliye kuwa na makao yake Al-Madaain. Huu ulikuwa ndio mji wa wafalme wa Kifursi, mji huu ulikuwa kando kando ya mto Dajlah Kusini mwa Baghdad. Akawatumia Waislamu jeshi jingine likiongozwa na mmojawapo wa viongozi wa Fursi, aitwaye Qaarin Ibn Qaryaans. Huyu akaenda akawakusanya washindwa, akaja nao mpaka Thaniy kwenye maporomoko ya mto Dajlah karibu ya Basraa.

 

  VI.       Vita vya Thaniy:

         Qaarin akapiga kambi hapo Thaniy, kamanda Khalid akamuendea. Majeshi mawili haya yalipo kutana, Qaarin akatoka mbele akitafuta mubaaraza ili apate kulipa kisasi cha Hurmuz. Mpiganaji muislamu akamtokea akapambana nae na akamuua. Hapo tena jeshi la Waislamu likavaana na lile jeshi la mushrikina. Waislamu wakawaua mushrikina wengi, ukiachilia mbali wale walio ghariki mtoni. Baada ya kumalizika kwa mapambano, kamanda Khalid akatwaa kodi kutoka kwa wakulima na kuwafanya kuwa katika kundi la Ahlud-dhimma. Kisha akatuma khabari za ushindi na khumsi ya ngawira kwa khalifa Abubakar.

Mfalme wa Fursi hakukubali kushindwa, akapeleka jeshi jingine kwa Waislamu, likiongozwa na Al-Andru Za’az. Jeshi hili likafuatiwa nyuma na jeshi jingine likiongozwa na Jaadhawaihi. Majeshi yote mawili yakapiga kambi Al-Walajah. Vita vya Thaniy vilikuwa katika mwezi wa Swafar (Mfunguo Tano), mwaka wa 12 A.H./633 A.D. [Rejea TAARIKHUT-TWABARIY 2/312 & AL-BIDAAYA WAN-NIHAAYAH 6/344]

 

VII.       Vita vya Al-Walajah:

         Kamanda Khalid akayaendea majeshi yale wa Wafursi, Waislamu wakapigana nao mapigano makali kabisa mpaka kambi ya mushrikina ikasambaratika. Msambaratiko huo ukamuacha kamanda wa mujshrikina Al-Andru Za’az akiwa maiti. Khalid akawakamata vijana wa kabila la Bakri Ibn Waail walio kuwa wakipigana upande wa mushrikina, akawaua. Kaumu yao; yaani Manaswara wa Bakri wakamghadhibikia kamanda, wakakusanyika Ullaysi kujadili hatua ya kuchukua. Wakamuandikia waraka mfalme wa Fursi wakimuomba msaada wa jeshi litakalo wasaidia kupambana na Waislamu. Mfalme Azdasheer akalipokea ombi lao hilo kwa mikono miwili, akampelekea waraka Bahman Jaadhawaihi aliye shindwa    Al-Walajah. Akimuamrisha kwenda kujiunga na Manaswara wa Bakri kupigana dhidi ya Waislamu. Waraka huo ulipo mfikia, akamtanguliza mbele yake Jaabaan kwenda huko na yeye akaenda kwa mfalme Azdasheer ili kupata khabari na kumtaka ushauri. Alipo fika huko, akamkuta mfalme akiwa kitandani mgonjwa, akabaki hapo akisikilizia hali yake. [Rejea TAARIKHUT-TWABARIY 312,               AL-BIDAAYA WAN-NIHAAYA 6/345 & AL-MUNTADHWIM 4/102]

 

VIII.       Vita vya Ullaysi:

         Jaabaan yeye akaenda mpaka akafika kwenye jeshi la Wabakri, akapiga kambi pamoja nao Ullaysi. Hili ni eneo lililopo kando kando mwa mto Furaat, katika vitongoji vya Anbaar. Kamanda Khalid akawaendea akiwa na kikosi kidogo, akaingia katikati ya medani ya vita akitaka mpambano wa watu wawili (mubaaraza). Kiongozi mmoja wa Bakri akatoka mbele kupambana nae, wakapambana mpambano ulio malizika kwa kuua huyo kafiri. Hapo tena Waislamu kama mbogo aliye jeruhiwa wakawavaa mushrikina kwa nguvu moja na kasi kubwa. Waajemi hawa wakatoa upinzani mkubwa kwa kutazamia kwao kuja kwa Bahman kuwasaidia. Na Waislamu nao wakasimama imara mbele ya makafiri hawa, ili neno la Allah lipate kuwa juu. Basi haikufika Adhuhuri ila Wafursi walitimua mbio baada ya kuuawa wengi miongoni mwao. Kamanda Khalid akaigawa ngawira iliyo patikana kwa wapiganaji na akapeleka taarifa ya ushindi na khumsi ya ngawira kwa khalifa Abubakar-Allah amuwiye radhi. Vita hivi vilitokea katika mwezi wa Rabeel-Awwal (Mfunguo Sita), mwaka wa 12 A.H./Mei 633 A.D. [Angalia TAARIKHUT-TWABARIY 2/313, AL-BIDAAYA WAN-NIHAAYA 6/346 & AL-MUNTADHWIM 4/103]

Additional information