KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UTAKASIFU WA NIYA (IKHLAASI)...Inaendelea

Ijapo kuwa nia ya kweli inamzawadia mdau wake kabuli hii yenye wasaa, hakika nia inayo ingizwa ikachanganyika na amali njema katika sura yake ile ile. Inaweza kuibadilisha amali njema hiyo kuwa maasi yanayo pelekea kwenye jangwa la moto: “BASI, OLE WAO WANAO SWALI. AMBAO WANAPUUZA SWALA ZAO; AMBAO WANAJIONYESHA, NAO HUKU WANAZUIA MSAADA”. [107:04-07]

 

Hakika swala pamoja na riyaa imekuwa ni kosa na baada ya kuikosa roho ya ikhlaasi, imekuwa ni taswira mfu; isiyo na kheri yoyote. Na hali kadhalika zaka, nayo ikitolewa na moyo ufanyao ukarimu kwa ajili tu ya Allah na ujiwekeao akiba kwake, hutakabaliwa. Na kama haikuwa hivyo, basi hiyo ni amali iliyo batilika: “ENYI MLIO AMINI! MSIHARIBU SADAKA ZENU KWA MASIMBULIZI NA MAUDHI, KAMA ANAYE TOA MALI YAKE KWA KUWAONYESHA WATU, WALA HAMUAMINI ALLAH WALA SIKU YA MWISHO. BASI MFANO WAKE NI KAMA MFANO WA JABALI AMBALO JUU YAKE PANA UDONGO, KISHA LIKAPIGWA NA MVUA KUBWA, IKALIACHA TUPU. BASI HAWATAKUWA NA UWEZA WOWOTE KWA WALIVYO VICHUMA...” [02:264]

Hakika moyo ulio kosa ikhlaasi, hauwezi kuotesha kabuli ya amali, mfano wa mwamba ulio funikwa na mchanga usivyo weza kutoa mimea. Hebu ione thamani ghali ya ikhlaasi na baraka yake, inachanganyika na amali chache (kidogo) basi inaikuza mpaka inafikia uzani wa jabali. Na amali nyingi (kubwa) inakosa ikhlaasi, basi inakosa hata thamani ya uzani wa vumbi mbele za Allah. Ni kwa ajili/sababu hiyo, ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Ipe ikhlaasi (itakasie nia) dini yako, itakutoshea amali kidogo (chache)”. Al-Haakim-Allah amrehemu.

Inadhihiri kwamba tofauti ya ujira ulio wekwa kwa kutenda mema, kuanzia kumi mpaka maradufu ya mia saba na kuendelea, inarejea kwenye siri ya ikhlaasi iliyo sitirika ndani ya mvungu wa moyo wa mtendaji. Na siri hiyo haichomozei yeyote hata akaijua ila Mjuzi wa siri na ya dhaahiri. Kwa kadiri ya usafi (utakati) wa siri na ukunjufu wa manufaa huandikwa ziada.

Na sio dhaahiri ya mtu wala dhaahiri ya maisha ya Dunia, ndio ambayo Allah huipa radhi zake. Kwani hakika Allah Ataadhamiaye huwalaki waja wake wanyenyekevu, watakasifu wa nia na huwatakabalia kile wanacho jikurubishia kwake nacho. Ama yasiyo haya, katika mapambo ya Dunia na taklifu za wanaadamu, hizo hazina thamani mbele yake na wala haziangalii. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Hakika Allah haangalii viwili wili vyenu wala sura zenu, lakini anaziangalia nyoyo zenu na matendo yenu”. Muslim-Allah amrehemu.

Na katika hadithi nyingine amesema: “Itakapo fika siku ya Kiyama italetwa Dunia, kisha kitachambuliwa humo kilicho kuwa cha Allah na kilicho kuwa kwa asiye Allah kitupwe katika moto wa Jahannamu”. Al-Baihaqiy-Allah amrehemu.

Basi yeyote yule atakaye yafungamanisha maisha yake na kweli halisi hizi, bila shaka huyo amestarehe katika maisha yake na amefanya maandalizi ya marejeo yake kwa Mola Mlezi wake. Kwa hivyo basi, hakimdhuru alicho kikosa duniani wala hakimuhuzunishi alicho kitanguliza Akhera. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakaye fariki Dunia hali ya kuwa ana ikhlaasi kwa Allah pekee, asiye na mshirika na akasimamisha swala na akatoa zaka, huyo ameifariki na ilhali Allah yu radhi naye”. Ibn Maajah-Allah amrehemu.

Na huu ni usadikisho wa kauli yake Allah Atukukiaye: “NAO HAWAKUAMRISHWA KITU ILA WAMUABUDU ALLAH KWA KUMTAKASIA DINI, WAWE WAONGOFU, NA WASHIKE SWALA, NA WATOE ZAKA. NA HIYO NDIO DINI MADHUBUTI”. [98:05]

Na miale ya ikhlaasi huenea mno ndani ya nafsi pale mja anapo kamatana nayo khasa katika shida/matatizo makubwa. Kwani mahala hapo pa mkwamo, ndipo ambapo mwanaadamu hujivua na upotovu wake na akanyenyekea kutokana na makosa/madhambi yake. Na akasimama kwenye uwanja wa Allah hali ya kuwa ni mwenye kujitupa kwake, akiitarajia rehema yake na akiichelea adhabu yake. Qur-ani Tukufu imeisawirisha fazaa na kupapatika kwa mwanaadamu wakati anapo hemewa, asijue la kufanya wala pa kukimbilia. Na kujitupa kwake kwa Mola Mlezi wake akimuomba msaada, amuokoe na masaibu yaliyo msibu: “SEMA: NI NANI ANAYE KUOKOENI KATIKA GIZA LA NCHI KAVU NA BAHARINI? MNAMWOMBA KWA UNYENYEKEVU NA KWA SIRI, MKISEMA: KAMA AKITUOKOA NA HAYA BILA YA SHAKA TUTAKUWA MIONGONI MWA WANAO SHUKURU. SEMA: ALLAH HUKUOKOENI KUTOKA HAYO, NA KUTOKA KILA MASHAKA, NA KISHA NYINYI MNAMSHIRIKISHA!” [06:63-64]

Bila ya shaka ikhlaasi kama hii, ni hali tokezi inayo mtokea mja akiwa mkwamoni. Na hizi hali zinazo mtokea mtu, kisha zikamuondoka, sio hulka. Na Allah-utakati wa mawi ni wake-anacho taka kwa waja wake, ni wao kumjua Yeye ukweli wa kumjua na wamkadirie haki ya uweza wake katika raha/furaha na shida/dhiki zote. Na wakufanye kumtakasia nia Yeye (Ikhlaasi) kutulizane ndani ya mwendo wao, wasikate mafungamano/mawasiliano naye na wala wasimkusudie kwa matendo yao mwingine asiye Yeye.

Na joto la Ikhlaasi hupungua kidogo kidogo kila vinapo charuka ndani ya nafsi virusi vya umimi (kujipendelea), kupenda kusifiwa, kutaka heshima/madaraka na kujikwaza na kujifakharisha. Huwa hivyo, kwa sababu Allah Ataadhamiaye hupenda amali iliyo takata, isiyo na taka zichafuazo: “HAKIKA DINI SAFI NI YA ALLAH TU...” [39:09]

Na tabia ya jambo tukufu ni kama tabia ya tunda lililo iva (bivu), ili libakie salama, safi na utamu wake, ni lazima liepukane na yale yote yanayo weza kulisababishia kuharibika na kuoza. Na Uislamu umekwisha itangaza wazi chuki yake kubwa dhidi ya riyaa katika amali njema na ukaizingatia na kuichukulia kuwa ni kumshirikisha Allah; Mola Mlezi wa viumbe vyote. Na lililo haki kutajwa, ni kwamba riyaa ni maradhi hatari mno kwa amali. Riyaa ikisha tawala na kukamilisha kazi yake ndani ya nafsi kama vinavyo fanya vijidudu na virusi vya maradhi, huwa ni aina ya ushirikina unao mbwagia motoni mdau (muumini) wake. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Uchache wa riyaa, ni shirki. Na atakaye wafanyia uadui mawalii wa Allah, bila ya shaka huyo amejitokeza kupigana na Allah. Hakika Allah anawapenda wema, wachaMngu ambao wakitoweka hawakosekani na wakiwepo hawajulikani. Nyoyo zao hao ni taa za uwongofu, hutoka katika kila ardhi yenye kiza”. Al-Haakim-Allah amrehemu.

Na imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi: Mtu mmoja alisema: Ewe Mtume wa Allah! Hakika mimi ninashika msimamo, ninaikusudia dhati ya Allah nami ninataka Yeye aone mahala pangu (nilipo). Basi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakumjibu mpaka ikateremka: “MWENYE KUTARAJI KUKUTANA NA MOLA WAKE MLEZI BASI NA ATENDE VITENDO VYEMA, WALA ASIMSHIRIKISHE YEYOTE KATIKA IBADA YA MOLA WAKE MLEZI”. [18:110]

Hakika si vinginevyo, vita vya Uislamu dhidi ya riyaa na ndugu zake, miongoni mwa maradhi yanayo tokana na kukosekana kwa Ikhlaasi, vimekuwa vikali mno kwa sababu hayo ni fisadi inayo ua kabisa amali za mja. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Allah atakapo wakusanya wale wa mwanzo na wa mwisho kwa ajili ya siku ya Kiyama, siku isiyo na shaka, atalingana mlinganiaji: Yeyote aliye mshirikisha yeyote katika ibada yake aliyo itenda kwa ajili ya Allah, basi na akachukue thawabu zake kwa huyo. Kwani hakika Allah ni Mkwasi wa washirika katika kushirikishwa”. Tirmidhiy-Allah amrehemu.

Additional information