KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

MAZUNGUMZO BAINA YA MITUME NA KAUMU ZAO...Inaendelea

Na ifananayo na aya hizi na ile midahalo iliyomo humo, iliyo jiri baina ya Mitume na kaumu zao, ni kauli yake Allah Ataadhamiaye: “NA WAPIGIE MFANO WA WAKAAZI WA MJI WALIPO WAFIKIA WALIO TUMWA. TULIPO WATUMIA WAWILI, WAKAWAKANUSHA. BASI TUKAWAZIDISHIA NGUVU KWA MWINGINE WA TATU. WAKASEMA: HAKIKA SISI TUMETUMWA KWENU. WAKASEMA: NYINYI SI CHOCHOTE ILA NI WATU KAMA SISI. NA MWINGI WA REHEMA HAKUTEREMSHA KITU. NYINYI MNASEMA UWONGO TU. WAKASEMA: MOLA WETU MLEZI ANAJUA KWAMBA HAKIKA SISI TUMETUMWA KWENU. WALA SI JUU YETU ILA KUFIKISHA UJUMBE ULIO WAZI. WAKASEMA: SISI TUMEAGUA KUWA NYINYI NI WAKOROFI. IKIWA HAMTAACHA BASI KWA YAKINI TUTAKUPIGENI MAWE, NA MTAPATA ADHABU CHUNGU KUTOKA KWETU. WAKASEMA: UKOROFI WENU MNAO WENYEWE! JE! NI KWA KUWA MNAKUMBUSHWA? AMA NYINYI NI WATU WALIO PINDUKIA MIPAKA”. [36:13-19]

 

Maana ya aya: Ewe Mtume Mtukufu! Ifanye hali ya wakaazi wa mji huu kuwa ni mfano kwa washirikina wa Makka, katika kushikilia na kung’ang’ania ukafiri na inadi (jeuri). Na watahadharishe ya kwamba mwisho wao utakuwa kama mwisho wa hao walio watangulia. Ambao mwisho wao ulikuwa ni kutwaliwa na ukelele mkali, tahamaki hao wamezimia, kwa sababu wao waliwakadhibisha Mitume.

Allah Ataadhamiaye aliwapelekea wakaazi wa mji ule, wajumbe (Mitume) wawili, nao wakaupa mgongo wito wao. Ndipo Allah Atukukiaye akampeleka mjumbe wa tatu pamoja na wale wajumbe wawili wa mwanzo, ili huyu awaongezee nguvu na asaidiane nao katika kufikisha neno la haki. Wajumbe wale watatu wakalitangaza suala lao na wakawaambia wale wakaazi wa mji: Hakika sisi tumetumwa kwenu nyinyi na si kwa wengine, basi tutiini katika haya tunayo kuitieni, katika kumuabudu Allah Ataadhamiaye peka yake na katika wajibu wa kujipamba na tabia njema.

Lakini wale wakaazi wa mji wakawaambia Mitume wao kwa namna ya ukanushi na kujikweza: Nyinyi si lolote ila ni wanaadamu kama sisi tu na wala nyinyi hamna ubora wowote juu yetu. Katika madai yao haya ni kama kwamba ubinaadamu unakinzana na utume; yaani mwanaadamu hawezi kuwa mtume.

Kisha kama kwamba hayo hayatoshi wakaongeza kusema: Na Allah Mwingi wa rehema hakuteremsha chochote, enyi Mitume! Na hamkuwa nyinyi ila ni waongo tu katika huko kudai kwenu kwamba mmetumwa kwetu.

Hivi ndivyo wakaazi wa mji ule walivyo wakabili Mitume wao kwa kuupa mgongo mlingano (wito) wao, kwa kujikweza juu yao, kwa kuyakanusha waliyo wapelekea na kwa kuwapa wasifu wa uwongo katika yale wanayo yasema. Lakini Mitume watukufu waliukabili usafihi huo kwa upole na subira kama ilivyo hali ya mwenye kuamini ukweli wake, wakawaambia wale wakaazi wa mji: Ni Mola wetu Mlezi peke yake ndiye ajuaye ya kwamba hakika sisi tumetumilizwa kwenu nyinyi na yatosha kabisa kujua kwake na hukumu yake. Na baada ya hayo, si juu yetu kwenu nyinyi ila tu ni kukufikishieni yale tuliyo pewa jukumu la kuyafikisha kwenu nyinyi kwa uwazi usio na uficho wala utatizi/mkanganyo.

Msomaji mwema-Allah akurehemu-wewe hushindwi kuona kwamba Mitume hawakuukabili usafihi wa wakaazi wa mji kwa usafihi mfano wake. Lakini wao waliukabili ukadhibishwa wao kwa mantiki thabiti, jawabu salama na kwa mdahalo wa mtu karimu, timamu wa akili. Lakini wakaazi wale wa mji hawakukinaishwa na mantiki salama hii, wakawarudi Mitume kwa jibu baya mno kuliko lile la mwanzo, kiasi cha kuwaambia: Hakika sisi tumepatwa ukorofi kwa ajili yenu na tumefikwa na madhara pale tulipo ziona nyuso zenu. Sasa kama hamtatuacha na mambo yetu, mkaenda zenu, basi bila ya shaka tutakupopoeni kwa mawe na ikupateni adhabu kali, iliyo chungu kutoka kwetu.

Lakini Mitume watukufu bado walivikabili vitisho vikali hivi, kwa uimara na kwa jibu la kishujaa lililo shehenezwa busara, wakawaambia: Suala haliko kama mnavyo sema nyinyi ya kwamba uwepo wetu pamoja nanyi ndio sababu ya nyinyi kukorofika. Lakini ilivyo haki ni kwamba ukorofi wenu mnao nyinyi wenyewe. Kwa sababu nyinyi ni watu ambao ada yenu ni kutopea katika ukafiri, ufasiki na uasi.

Kisha baada ya hapo, Allah-utakati wa mawi ni wake-akabainisha ya kwamba wakaazi wa mji ule, walijiwa na mtu miongoni mwao akiwanasihi ya kwamba wawafuate Mitume na wawatii. Lakini wao hawakumtia maanani na hilo lisitoshe bali wakamuua. Hapo sasa ndipo Allah akawaadhibu adhabu ya Mshindi, Mwenye nguvu.

Na katika jumla ya mazingatio na mawaidha tunayo yapata kutoka katika aya hizi na zile zilizo tangulia. Ni kwamba watu wapevu wa akili katika midahalo yao na watu wengine, hutumia miundo busara, adabu tukufu, subira njema, rejezo kinaishi, kusimama imara juu ya haki na muelekeo salama. Ama watu masafihi na majaahili, wao silaha yao katika mijadala na midahalo ni: Ghururi fedheheshi, mantiki mbaya, na vitisho kwa yule anaye pingana nao. Na mwisho wao ni kula khasara na kuangamia.

Hii ni mifano miwili ya majadiliano mengi yaliyo jiri baina ya Mitume na kaumu zao kwa sura ya jumla. Ama yale majadiliano yaliyo jiri baina ya kila Mtume na kaumu yake, ni mengi mno. Lakini hapa sisi tutatosheka kutaja baadhi yake ili iwe ni mfano kwa hayo mengine ambayo hatukuyataja.

Huyu hapa ni Mtume Nuhu-Amani imshukie-Allah alimtuma kwa watu wanao abudu masanamu. Basi akakaa miongoni mwao kwa kipindi cha miaka elfu ila khamsini (950), akiwaamrisha kumuabudu Allah Ataadhamiaye peke yake na akiwakataza kuabudu chochote/yeyote asiye Yeye. Na yalijiri baina yake na wao majadiliano/midahalo mingi. Na Qur-ani Tukufu ikasimulia sehemu ya majadiliano hayo katika sura zake (Qur-ani) nyingi, miongoni mwake ni Surat Al-A’araaf, Yunus, Huud, Muuminuna, As-shu’araa, As-swafaat na Nuhu. Na huu hapa ukujiao ni mdahalo ulio jiri baina ya Nuhu na kaumu yake, kama unavyo simuliwa na Qur-ani Tukufu:

Kaumu yake walimwambia pale alipo watolea wito wa kumuabudu Allah peke yake na waache kuabudu asiye Yeye: “...HAKIKA SISI TUNAKUONA WEWE UMO KATIKA UPOTOFU ULIO DHAAHIRI”. Basi je, yeye aliwajibu nini? Aliwajibu kwa kusema: “...ENYI WATU WANGU! MIMI SIMO KATIKA UPOTOFU, LAKINI MIMI NI MTUME NITOKAYE KWA MOLA MLEZI WA VIUMBE VYOTE. NAKUFIKISHIENI UJUMBE WA MOLA MLEZI WANGU, NA NINAKUNASIHINI; NA NINAYAJUA KWA ALLAH MSIYO YAJUA NYINYI. JE, MNASTAAJABU KUKUJIENI MAWAIDHA YANAYO TOKA KWA MOLA MLEZI WENU KWA NJIA YA MTU ALIYE MMOJA KATIKA NYINYI, ILI AKUONYENI NA ILI MUMCHEMNGU, NA ILI MPATE KUREHEMEWA?” [07:60-63]

Yaani: Mtume Nuhu-Amani imshukie-aliwaambia viongozi katika kaumu yake, ambao walimpa wasifu wa upotofu na kuwa mbali na njia nyoofu: Enyi watu wangu nyie! Mimi sina hata chembe ya upotofu, hakika si vinginevyo mimi ni Mtume kwenu nitokaye kwa Muumba watu wote, ili nipate kukufikishieni ujumbe alio nifunulia. Na ili nizipapie nasaha zenu ambazo ndani yake umo utengenevu wenu na Allah Ataadhamiaye amekwisha nipa elimu ambayo nyinyi hamjapewa. Na ikiwa mmestaajabu mimi kupewa utume, eti kwa kuwa mimi ni mwenzenu (mwanaadamu kama nyinyi). Na ameniamrisha ya kwamba Yeye-utakati wa mawi ni wake-ndiye anaye stahiki kuabudiwa. Basi tambueni ya kwamba mshangao wenu huo, ni mshangao pogo ulio wekwa mahala usipo stahiki.

Ndugu msomaji mwema-Allah akurehemu-unaona kupitia aya na maelezo yake haya, kwamba Mtume Nuhu-Amani imshukie-aliwarudi wale walio mpa wasifu wa upotofu na mkengeuko wa kuiacha haki. Aliwarudi kwa mtindo mzuri usio na kauli chafu, kiasi kwamba aliipa nafsi yake sifa nne; sifa ya utume, sifa ya ufikishaji ujumbe, sifa ya kutoa nasaha na sifa ya elimu inayo zishinda elimu zao. Kisha akayakanusha mastaajabu yao ya yeye kuchaguliwa akapewa utume na Allah Atukukiaye na wakaachwa kupewa wao.

Na mahala pengine tunawaona wakimwambia Mtume wao, kama walivyo nukuliwa na Qur-ani Tukufu: “NA WAKASEMA WAKUU WALIO KUFURU KATIKA KAUMU YAKE: HATUKUONI WEWE ILA NI MTU TU KAMA SISI, WALA HATUKUONI WAMEKUFUATA ILA WALE WALIO KUWA KWETU WATU DUNI, WASIO KUWA NA AKILI. WALA HATUKUONENI KUWA MNA UBORA WOWOTE KUTUSHINDA SISI. BALI TUNA HAKIKA NYINYI NI WAONGO”. [11:27]

Yaani: Kwamba viongozi wa kaumu ya Mtume Nuhu-Amani imshukie-walimwambia kwa namna ya kebehi: Ewe Nuhu wee! Kwetu sisi wewe ni mtu tu kama sisi na wala huna lolote la ziada la kutushinda linalo kustahikisha kupewa utume, tukaachwa sisi. Hawa kwa ujaahili wao na upogo wao wa kufahamu, walifahamu ya kwamba utume unakinzana na ubinadaamu; yaani binaadamu hawezi kuwa Mtume. Na hawakukomea hapo, bali waliongeza kusema: Na hatuoni umekubaliwa na kufuatwa ila na wale mafakiri na wasio na thamani miongoni mwetu, tena wenye kudharauliwa. Nao wamekufuata kibubusa tu bila ya kuthibitisha ukweli wa madai yako. Au wamekufuata kwa dhaahiri tu na ilhali wakiukana utume wako huo kwa baatini (sirini).

Kisha wakaongeza juu ya yale madai yao ya mwanzo, madai mengine, wakasema: Na wala hatuoni kwako na wafuasi wako lolote mnalo tushinda katika utajiri, elimu au akili. Si hivyo tu, bali tunalo liitakidi sisi ni kwamba wewe na wao (hao wafuasi wako) ni miongoni mwa wale walio waongo katika maneno na matendo yao.

Hivi ndivyo makafiri wa kaumu ya Mtume Nuhu-Amani imshukie-walivyo anza nae mdahalo, kwa kumvika yeye na walio waumini, wasifu wa hali duni/twevu, kutokuwa na thamani, udhaifu wa akili na urongo katika maneno na matendo!!

Basi je, Mtume Nuhu-Amani imshukie-aliwajibu nini? Hakika aliwarudi kwa jawabu lililo sheheni hekima, linalo iondosha batili yao na linalo mkinaisha kila mwenye siha ya akili, ya kwamba yeye na walio muamini wako katika haki. Na Qur-ani Tukufu imetusimulia jawabu hiyo kupitia kauli yake Allah Ataadhamiaye: “AKASEMA: ENYI WATU WANGU! HEBU FIKIRINI! IKIWA MIMI NINAYO HOJA WAZI ILIYO TOKA KWA MOLA WANGU MLEZI, NA AMENIPA REHEMA KUTOKA KWAKE, NAYO IKAKUFICHIKIENI; JE, TUKULAZIMISHENI KUKUBALI HALI NYINYI MNAICHUKIA? NA ENYI WATU WANGU! MIMI SIKUOMBENI MALI KWA AJILI YA HAYA. MIMI SINA UJIRA ILA KWA ALLAH; NA MIMI SITAWAFUKUZA WALIO AMINI. HAKIKA WAO WATAKUTANA NA MOLA WAO MLEZI, LAKINI MIMI NAKUONENI MNAFANYA UJINGA. NA ENYI WATU WANGU! NI NANI ATAKAYE NISAIDIA KWA ALLAH NIKIWAFUKUZA HAWA? BASI JE, HAMFIKIRI? WALA SIKWAMBIINI KUWA NINA KHAZINA ZA ALLAH; WALA KUWA MIMI NAJUA MAMBO YA GHAIBU; WALA SISEMI: MIMI NI MALAIKA. WALA SIWASEMI WALE AMBAO YANAWADHARAU MACHO YENU KUWA ALLAH HATAWAPA KHERI – ALLAH ANAJUA YALIYOMO KATIKA NAFSI ZAO – HAPO BILA YA SHAKA NINGEKUWA MIONGONI MWA WENYE KUDHULUMU”. [11:28-31]

Yaani: Alisema Mtume Nuhu-Amani imshukie-katika kuwarudi kwake wale makafiri katika kaumu yake: Hebu nipeni khabari, ikiwa mimi nina uoni/ujuzi juu ya suala langu hili na nina hoja iliyo wazi niliyo ongozwa kwayo na Mola wangu Mlezi ambaye amenitunukia utume. Na kukafichikana kwenu kunufaika na uwongofu wa utume huo. Basi je, hivi mimi naweza kuzibadilisha akili zenu na kukulazimisheni kufuata rai yangu mimi?! Katika mambo yasiyo kuwa na shaka, ni mimi kutoliweza hilo kwa hakika.

Kisha akawaelekezea wito wa pili, akawaambia: Enyi watu wangu nyie! Mimi sikutakeni ujira kwa kuwaiteni kuifuata haki, hakika si vinginevyo mimi ninataka ujira wangu kutoka kwa Muumba wangu peke yake. na tieni fahamuni kwamba mimi sitowafukuza wale walio uamini wito wangu, wawe ni matajiri au masikini. Kwa sababu Allah Ataadhamiaye ndiye Muhisabu wa wote na ndiye Muumba wa wote. Lakini pamoja na bayana yote hii iliyo wazi, bado nakuoneni nyinyi ni watu mnao jingikiwa na kitu kilicho wazi.

Kisha akawaelekezea wito wa tatu, akawaambia humo: Enyi watu wangu nyie! Ni nani miongoni mwenu anaye weza kuniokoa na adhabu ya Allah Atukukiaye, iwapo nitawafukuza katika baraza yangu, hawa waumini masikini!! Hivi nyinyi hamuuzingatii muongozo huu ulio sheheni hekima?!

Baada ya miito yote hiyo, hapo sasa ndipo Mtume Nuhu-Amani imshukie-akaanza kuzibomoa shubuhaati (mikanganyo) za kaumu yake, moja baada ya nyingine, akawaambia: Na mimi mbali na yote hayo, sikwambieni kwamba mimi ndiye mmiliki wa hazina za riziki na wala sithubutu kukwambieni ya kwamba mimi ninayajua mambo ya ghaibu. Na wala sijasiri kukwambieni ya kwamba mimi ni mmoja wa malaika. Na hakika si vinginevyo, mimi ni mtu kama nyinyi, ila tu ni kwamba Allah Atukukiaye amenipa utume ambao hajakupeni nyinyi. Na wala sikwambieni pia katika suala la wale mnao wadharau kwa sababu ya ufakiri wao, ya kwamba Allah Ataadhamiaye hatowapa kheri maridhawa katika fadhila na ukarimu wake. Kwani ni Yeye pekee-utakati wa mawi ni wake-ndiye ayajuaye yaliyomo ndani ya nafsi zao; kheri au shari. Na lau mimi nitakwambieni lolote katika hilo, basi ningeli kuwa miongoni mwa madhaalimu wa nafsi zao.

Additional information