KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA ZA KIYAMA: MTU KUUZA DINI YAKE KWA MASLAHI DUNI YA KIDUNIA

 

Dhiki, hali ngumu ya kimaisha ni dudu baya na zimwi lililo yatamalaki maisha ya walio wengi ulimwenguni kote. Dhiki na hali ngumu hiyo imemfikisha mwanaadamu kufanya lolote pasina kujali linamridhi au linamchukiza Mola Muumba wake, ili tu apate kujinasua kutoka katika dhiki na hali ngumu hiyo. Kimaumbile mwanaadamu ni kiumbe asiye na ujasiri wa kustahamilia dhiki na hali ngumu, kwa maumbile yake hayo basi yuko tayari kutoa gharama yoyote ile ili tu kujitoa katika hali hiyo.

 

 

Dhiki na hali ngumu ya kimaisha ni vitu vyenye sehemu kubwa sana katika kuishusha/kuipunguza au hata kuiondoa kabisa Imani/dini ya mtu. Ni vema tukatia akilini ya kwamba Imani/dini ni kitu chenye thamani isiyo na bei (kisicho nunulika). Lakini wakati wa dhiki/hali ngumu muumini anaweza kuteleza, akayaweka kando mafundisho ya dini yake, akamkhalifu Mola wake, akatenda lililo la haramu ili kupata hali nzuri ya kimaisha. Kutokana na dhiki muumini anaweza kufanya kazi kama mkemia mathalan katika kiwanda cha kuzalisha pombe, ili tu mkono uende kinywani. Anaweza kutumia mifumo ya uchumi inayo endeshwa kwa njia za riba, anaweza kunasa katika mtego wa michezo ya bahati nasibu na baya kabisa anaweza hata kubadili dini yake, ili tu apate hali nzuri ya kimaisha.

 

Kuielekea hali hiyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia katika Hadithi yake ndefu ambayo katika jumla ya yaliyomo ni: “...(zama hizo) atapambaukiwa (atafikiwa na asubuhi) mtu hali ya kuwa ni muumini na atachwewa (atafikiwa na jioni) hali ya kuwa ni kafiri. Na atachwewa hali ya kuwa ni muumini na atapambaukiwa hali ya kuwa ni kafiri, mmojawao atauza dini yake kwa maslahi duni ya Dunia. Mwenye kushikamana na dini yake (wakati huo) ni kama yule aliye kamata kaa la moto”. Ahmad [18:255]-Allah amrehemu.

 

Haya ndugu mwana-jukwaa, sasa sote tujiulize hawapo miongoni mwetu Waislamu wanao ritadi kwa sababu ya maslahi ya kidunia?! Wengi tu. Hawapo Waislamu wanao tenda ya haramu hali ya kuwa wanajua wamekatazwa na Mola wao, ili tu kupata hali nzuri za kimaisha?! Wapo, hakuna wa kupinga wala kukanusha, Kiyama hichooo kimekaribia. Tafakari, chukua hatua, shikamana na dini yako kwa hali na mazingira yoyote yawayo ili upate amani na salama katika siku hiyo ngumu ijayo. Stahamilia dhiki na hali ngumu hii ya mpito ili usalimike na ile dhiki na hali ngumu ya milele.

 

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

 

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

 

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

 

Ewe Mola Mlezi wa walimwengu wote! Ewe uliye umba ardhi na ukaibarikia! Tunakuomba utubarikie vizazi vyetu, zibariki nyumba zetu, zibariki kazi zetu, yabariki matendo na kauli zetu, yabariki maisha yetu yote na utubarikie katika dini yako. Hakika hakuna mwenye kubariki ila Wewe. Yaa Allah tutakabalie duaa!

 

Aamina!

 


 

Kwa juma hili, hilo ndilo jukwaa letu na hayo ndio tuliyo wafikiwa kukumbushana, tumuombe Mola wetu Mkarimu kupitia ukarimu wake atubarikie ufahamu wetu ili tupate kufahamu na kukumbuka na wala asitujaalie kuwa kama wale ambao: “...wana nyoyo lakini hawafahamu kwazo. Na wana macho, lakini hawaoni kwayo. Na wana masikio, lakini hawasikii kwayo...”.

 

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kujifunza alama nyinginezo za Kiyama kama zilivyo elezwa na Yule Mkweli Muaminifu ambaye:

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ ٱلۡهَوَىٰٓ ٣ إِنۡ هُوَ إِلَّا وَحۡيٞ يُوحَىٰ ٤

 

Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya (ayatamkayo) ila ni ufunuo (wahyi) ulio funuliwa”. An-Najmi [53]:03-04

 

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

 

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

 

                              

 

Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema. Na wasio muitikia, hata wangeli kuwa navyo vyote viliomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangeli vitoa kujikombolea! Hao watapata hisabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni mahala pabaya mno!”. Ar-ra’ad [13]:18

 


 


 


 


 


 


 


 


 


 

Additional information