KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

SHARTI ZA KUFUNGAMANA YAMINI

Ili Yamini iweze kufungamana, kumeshurutizwa kuthibitika na kupatikana kwa mambo yafuatayo:

a)      Muapaji awe mtu mzima mwenye akili timamu:

         Ushurutizo huu ni kwa ajili ya kuondoshwa kupata dhambi na kuadhibiwa kwa asiye baleghe (mtoto) na asiye na akili (mwendawazimu). Ushahidi wa hili: Imepokewa kutoka kwa Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Kalamu imeondoshwa kwa watu watatu; aliye lala mpaka aamke, mtoto mdogo mpaka abaleghe na mwendawazimu mpaka arejewe na akili”. Abu Daawoud [4403] & wengineo-Allah awarehemu.

 

b)      Yamini isiwe puo:

         Yamini puo ni mfano wa kauli zao Waarabu: “BALAA WALLAAH”, “WALAA WALLAAH” na mfano wa ibara hizi zinazo pita katika ndimi za watu pasina kukusudia.

c)      Kiapo kiwe kwa mojawapo ya vifuatavyo:

1)        DHATI YA ALLAH MTUKUFU: Kama kauli yake mtu: “Naapa kwa dhati ya Allah”, au “Naapa kwa Allah”.

2)        MOJAWAPO YA MAJINA YAKE TAALA: Kama kauli yake msemaji: “Naapa kwa Bwana Mlezi wa viumbe vyote”, au “Naapa kwa Mfalme wa siku ya Kiyama” au “Naapa kwa Mwingi wa rehema”.

3)        MOJAWAPO YA SIFA ZAKE: Mfano wa kauli yake mtu “Naapa kwa utukufu wa Allah”, au “Naapa kwa uwezo wa Allah”.

         Na asili/msingi katika yote haya yaliyo tajwa ni hadithi iliyo pokewa kutoka kwa Mtume wa Allah: Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibn Umar-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimkuta Umar Ibn Al-Khatwaab katika msafara akiapa kwa haki ya baba yake. Mtume akasema: “Ehee zindukeni! Hakika Allah anakukatazeni kuapa kwa baba zenu, mwenye kutaka kuapa na aape kwa (jina la) Allah au anyamaze”. Bukhaariy [6270] & Muslim [1646]-Allah awarehemu.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Yamini ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ilikuwa “LAA WAMUQALLIBIL-QULUUB”. Bukhaariy [6253]-Allah amrehemu.

Na imethibiti katika hadithi nyingi mbele za Imamu Bukhaariy na wapokezi wengine wa hadithi-Allah awarehemu wote. Kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akisema katika kiapo chake: “Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu i mkononi mwake”, “Namuapia yule ambaye nafsi ya Muhammad i mikononi mwake”.

Basi lau mtu ataapa kinyume na hivi ilivyo tajwa, Yamini yake haitafungamana kwa sababu mbili hizi:

1)        Hadithi ya Mtume wa Allah: “...mwenye kutaka kuapa basi na aape kwa (jina la ) Allah au anyamaze”.

2)        Kukosekana kwa ukamilifu wa utukufu katika ambavyo havikutajwa katika sharti za kufungamana kwa Yamini. Na muumini amekatazwa kumuadhimisha taadhima ya dhati asiye Allah.

 

SOMO LA PILI.

 

                  i.          Yamini Swarihi (fumbulizi) na Yamini Kinaya (fumbo):

         Naam, Yamini inagawanyika katika mafungu mawili; Swarihi (fumbulizi) na Kinaya (fumbo). Haya tuanze na kuijuvya:

1)        SWARIHI: Yamini Swarihi ni kila kiapo ambacho mtu ameapa kwa kutumia aidha mojawapo ya majina yake Allah yenye kumkhusu yeye pekee, mithili ya kauli ya msemaji: “Naapa kwa Allah”, au “Naapa kwa Bwana Mlezi wa viumbe vyote”.

2)        KINAYA: Yamini Kinaya ni mtu kuapa kwa kutumia tamko ambalo moja kwa moja linaelekea kwa Allah linapo achiliwa huru. Mfano wake ni mtu kusema: “Naapa kwa Muumbaji”. “Naapa kwa Mruzukuji” au “Naapa kwa Bwana Mlezi”. Au kuapa kwa kutumia ibara itumikayo kuielezea dhati ya Allah na asiye yeye kwa upeo sawa, mithili ya kauli ya msemaji: “Naapa kwa aliye Mjuzi”, “Naapa kwa aliyepo” au “Naapa kwa aliye hai”. Au mtu kuapa kwa kutumia mojawapo ya sifa za Allah kama uwezo, elimu au maneno yake Taala.

 

         ii.            Hukumu za Yamini; Swarihi na Kinaya:

         Baada ya kuona aina za Yamini, hebu sasa na tujifunze hukumu zake, tukianza na:

1)        HUKUMU YA YAMINI SWARIHI:

         Yamini Swarihi hutimia kufungamana kwake kwa utupu wa kuitamka tu na wala kauli ya muapaji atakapo dai “sikukusudia Yamini kwa tamko hilo”, haitakubaliwa. Hivi ni kwa sababu matamko haya hayabebi maana nyingine zaidi ya Yamini.

 

2)        HUKUMU YA YAMINI KINAYA:

         Yamini Kinaya haifungamani ila kwa kuambatana na nia na kusudi, hapa hukubaliwa kauli ya muapaji atakapo sema: “sikukusudia Yamini”.

Angalia, iwapo atasema: “Naapa kwa Muumbaji au Mruzukuji au Bwana Mlezi”, Yamini yake imefungamana. Ila iwapo hakuikusudia dhati ya Allah kwa matamko hayo, hapo itapondokea kwenye maana aliyo ikusudia na wala maneno yake hayo wakati huo hayafungamani kuwa Yamini. Kwa sababu maneno hayo mara nyingine hutumiwa kwa asiye  Allah kwa kufungwa, Allah Taala amesema: “HAKIKA NYINYI MNAABUDU MASANAMU BADALA YA ALLAH, NA MNAUMBA (mnazua) UZUSHI...” [29:17] – Yaani mnasema uwongo, mnayatengeneza masanamu kwa mikono yenu wenyewe, kisha mnayaita miungu. Katika aya hii mwanadamu amepewa sifa ya “kuumba” kwa maana ya kuzua. Na akasema Taala: “NA WAKATI WA KUGAWANYA WAKIHUDHURIA JAMAA NA MAYATIMA, WARUZUKUNI (wapeni) KATIKA HAYO MALI YA URITHI...’ [4:07] Hapa pia mwanadamu amepewa sifa ya “kuruzuku” kwa maana ya kutoa. Na akasema Taala: “...BASI MJUMBE ALIPO MJIA YUSUF AKASEMA: REJEA KWA BWANA MLEZI WAKO...” [12:50] Hapa mfalme kaitwa “Bwana Mlezi”.

Na mtu akisema: “Naapa kwa aliye hai”, “Naapa kwa aliyepo”, au “Naapa kwa aliye Mjuzi”, maneno yake hayo hayafungamani kuwa Yamini kwa matamshi haya, ila atakapo nuia kwayo dhati ya Allah. Hii ni kwa sababu ya matumizi ya maneno hayo kwa dhati ya Allah na viumbe wake kwa kiwango sawa, hayatamaanisha Yamini ila kwa nia.

Additional information