KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

SIFA STAHIKI ZA MTUME WA ALLAH (saw) Sehemu ya mwisho

Ama  unyenyekevu wake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie–pamoja na makamu yake  matukufu na daraja yake tukufu. Basi alikuwa ni mwingi mno kuliko watu wote  kwa unyenyekevu na mchache mno  kwa kiburi. Na ikutoshe tu kwamba yeye alipewa khiyari  baina ya kuwa nabii mfalme [kama nabii Suleiman] au nabii mja, basi akachagua kuwa nabii mja. Siku moja Bwana Mtume aliwatokea maswahaba wake akiwa ametegemea fimbo, wakamuinukia, akasema: “Msiinuke kama wanavyo inuka wasio Waarabu, wakiadhimishana wao kwa wao”. Na akaendelea kusema: “Hakika si vinginevyo, mimi ni mja [mtumwa wa Allah] ninakula kama anavyo kula mja na ninakaa kama anavyo kaa mja”.

 

Na alikuwa akipanda punda na akimpakiza mtu nyuma yake, akiwatembelea masikini, akikaa pamoja na mafakiri na akiitika mwaliko wa mja. Na akikaa hali ya kuchanganyika baina ya maswahaba wake akikaa pale inapo komelea baraza. Na amesema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie: “Msinisifu kama manaswara walivyo msifu mwana wa Mariam [kuwa ni Mungu/mwana wa mungu], hakika si vinginevyo, mimi ni mja, basi semeni [niiteni] mja wa Allah na Mtume  wake”.

 

Na Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alihiji kwa kupanda kipando [mnyama] kilicho choka [kwa uzee] kilicho tandikwa guo chakavu lisilo na thamani hata ya dirham nne, akasema: “Ewe Mola wa haki! Ijaalie Hijah hii kuwa ni Hijah isiyo ni riyaa ndani yake wala majisifu”. Hivi ndivyo alivyo kuwa, alikunjuliwa ardhi, na akachinja  wanyama wa sadaka katika Hijah yake hii, ngamia mia moja. Na Allah alipom fungulia  na kumpa ushindi wa mji wa Makah, ukawa chini ya amri yake, akaingia humo na majeshi  ya waislamu. Alikiinamisha chini kichwa chake akiwa amempanda mnyama, akinyenyekea kwa ajili ya Allah Ataadhimiaye. Na wala hakuingia akiwa kifua mbele kwa matambo na kiburi, la hasha. Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi:  “Niliingia sokoni pamoja na Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-akanunua pajama na akamwambia mpimaji katika mizani  pima na uzidishe kidogo. Halafu akasema [Abu Hurayrah] mtu yule akaurukia mkono wa Mtume wa Allah  akaubusu, Mtume akauvuta na akasema: “Haya wanayafanya wasio Waarabu kwa wafalme wao na mimi  sio mfalme, hakika si vinginevyo  mimi ni mtu miongoni  mwenu”. Halafu akaichukua pajama yake, nikaenda kuichukua niibebe mimi, akasema: “Mwenye kitu chake ana haki zaidi ya kukichukua/kukibeba kitu chake kuliko mwingineo”.

 

Ama uadilifu wake, uaminifu, usamehevu na ukweli wa lahaja yake Mtume–Rehema  na Amani zimshukie-basi yeye alikuwa ni muaminifu mno kuliko watu wote na mkweli wao kwa kauli tangu alipo umbwa. Waliikubali na kuikiri sifa hiyo kwake hata maadui zake na kabla ya kupewa utume  aliitwa “AL-AMIYN”-muaminifu.

 

Na imekuja katika hadithi: “Mkono wake–Rehema na Amani zimshukie-haukupata katu kuugusa mkono wa mwanamke asiye imiliki shingo yake”. Amesema Abul–Abbas Al-Mubarrad-Allah amuwiye radhi: “[Mfalme] Kisraa alizigawa siku zake, akasema: Siku ya upepo inafaa kwa kulala, na siku ya mawingu ni siku ya kuwinda. Siku ya mvua ni siku ya pumbao na kunywa na siku ya  jua ni siku ya  kutafuta haja [maisha]; yaani ni siku ya kuhangaika”. Lakini Mtume wetu-Rehema na Amani zimshukie-aliugawa mchana wake sehemu tatu; sehemu ya Allah, sehemu ya ahli zake na sehemu ya nafsi yake. Kisha tena akaigawa  ile sehemu yake baina ya watu, basi akawa akitaka msaada  kwa kilicho chake juu ya kukidhi haja za watu na akisema: “Nifikishieni haja/shida ya yule  asiye weza kunifikishia, kwani hakika mwenye kuifikisha haja ya asiye weza  kuifikisha mwenyewe, Allah atampa amani  katika siku ya fazaa kubwa. Na alikuwa Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–hamuadhibu mtu  kwa dhambi/kosa la mtu mwingine”.

 

Na ama utulivu wake, ukimya, murua na uongofu wake Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Basi alikuwa Mtume wa Allah ni mtulivu mno kuliko watu wote katika majilisi yake, hainyooshi miguu yake. Na  alikuwa alipo kaa hukaa kwa mtindo wa kuikamata miundi yake kwa mikono na huu mara nyingi ndio ulio kuwa  mkao  wake katika baraza. Na alikuwa ni mwingi wa kinyamao, hazungumzi pasipo na haja iliyo jitokeza na maneno yake yalikuwa ni ya kituo  na si ufedhuli wala  upunguani. Majilisi [baraza ] yake ilikuwa ni majilisi iliyo  pambwa na kushehenezwa na upole, haya ,kheri na uaminifu, hazinyanyuliwi hapo sauti na wala haivunjwi heshima ya mtu. Anapo zungumza, huinamisha  vichwa vyao wakazi wa baraza yake  kama kwamba ndege ametua  juu ya vichwa vyao. Amesema Ibn Abi Haalah-Allah amuwiye radhi: “Kutulia kwake Mtume–Rehema na Amani zimshukie–kulikuwa juu ya mambo  manne; upole, hadhari, heshima na tafakuri”. Na amesema Bi. Aysha –Allah amuwiye radhi: “Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akizungumza maneno ambayo lau atayahesabu  muhisabuji angeli yadhibiti”. Na alikuwa akipenda manukato  na riha [harufu]nzuri na akiyatumia  mara nyingi  na akiwahimiza watu kuyatumia. Na katika jumla ya murua  wake Mtume, ni kule kukataza kwake  kupuiliza chakula/kinywaji na kuamrisha kula katika sehemu  inayo muelekea mtu. Na kuamrisha kupiga mswaki  na kusafisha maungio  ya vidole kwa nje na ndani ya kitanga.

 

Ama upaji mgongo wake wa dunia–Rehema na Amani zimshukie-tumeisha tangulia kukueleza mengi yenye kutosha katika masomo yaliyo tangulia.  Na inakutosha kuwa dalili/ushahidi juu ya kuichukulia  kwake dunia uchache na kuzipa nyongo starehe zake na ilhali  akiwa amepewa funguo zake. Kwamba Mtume alikufa  huku akiwa ameiacha diraya [nguo ya vita] yake ikiwa rehani  kwa muyahudi kwa ajili ya chakula cha aila [familia]yake alicho kopa. Amesema Bi. Aysha Allah-amuwiye radhi: “Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–hakupata kushiba siku tatu  pishi ya mkate mpaka anashika njia yake [anakufa]”. Na akasema: “Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–hakuacha hata dirham[ moja] wala dinari wala mbuzi [hata mmoja] wala ngamia. Hakika alikufa ilhali nyumbani kwangu hakuna chochote anacho weza kukila  mwenye ini [aliye hai] ila shayiri kidogo zilizokuwa katika  rafu yangu”. Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-alisikika akisema: “Hakika mimi nilionyeshwa  kufanyiwa mabonde yote ya Makah kuwa dhahabu, nikasema hapana  ewe Mola Mlezi wangu! Nipate njaa siku moja, nile siku moja. Basi ama ile siku  nitakayo shikwa na njaa ndani yake, nitanyenyekea kwako na kukuomba. Na ama ile siku ambayo nitakayo shiba ndani yake, basi nitakuhimidi na kukusifu”.

 

Amsema Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi: “Hakika sisi tulikuwa watu wa Muhammad, kwa yakini tunakaa mwezi mmoja hatuwashi moto [nyumbani kwa kutokuwa na cha kupika]. Hakikuwa (chakula chetu] ila ni tende na maji”. Na imekuja katika hadithi ya Bi. Aysha: “Godoro la Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–nyumbani kwake lilikuwa la manyoya magumu  tukilikunja  mara mbili  ndio akilalia. Usiku mmoja tukalikunja mara nne [ili liwe na uzito] alipo amka akasema: Ulinitandikia nini? Tukamtajia  tulicho kifanya, akasema: Lirudisheni kwa mali yake kwani uzito wake  umenizuia kuswali usiku wa leo”. Na amesema Bi. Aysha: “Tumbo la Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–halikupata kujaa  kwa shibe na wala hakumshitakia mtu njaa. Na ufakiri ulikuwa ukipendwa mno  nae kuliko utajiri. Mara nyingine nilikuwa nikilia kwa kumuonea huruma kutokana na hali  niliyo muona nayo. Nikimpangusa tumbo lake kwa mkono wangu  kutokana na hali ya njaa  niliyo muona nayo na nikimwambia: Nakufidia nafsi yangu, lau ungejisaidia katika dunia  kiasi cha kupata chakula chako tu. Basi huniambia: Ewe Aysha! Nina nini mimi  na dunia! Ndugu zangu katika mitume wenye stahamala kubwa, walisubiria  magumu  kuliko hili [la njaa yangu] wakaishi na hali yao hiyo. Wakafika kwa Bwana Mlezi wao [wakafa], basi akayakirimu  marejeo yao [kwake]na akazifanya  nyingi thawabu zao. Kwa ajili hii basi, mimi ninajikuta naona haya ikiwa nitaishi  maisha ya anasa, kesho [akhera] nikapewa ujira mdogo nyuma yao. Na hapana chochote kinacho pendeza mno kwangu  kuliko kukutana na [hao] ndugu zangu  na mabui wangu”. Anaendelea kusema Bi. Aysha: “Basi baada ya hapo Mtume hakukaa ila miezi kadhaa, akafa-Rehema na Amani zimshukie”.

 

Ama hofu na twaa yake  kwa Bwana Mlezi  wake na ukubwa wa kumuabudu  kwake, kulikuwa ni kwa kadiri  ya elimu yake. Ni kwa ajili hii alisema: “Lau mngeli yajua  yale niyajuayo mimi, mngeli cheka kidogo na  mngelilia sana, ninaona msiyo yaona na ninasikia msiyo yasikia. Ilitoa sauti mbingu  na ilikua na haki  ya kufanya hivyo, hapana ndani yake mahala  pa vidole vinne  ila kuna malaika aliye weka paji lake  hali ya kumsujudia Allah. Wallah lau mngeli yajua yale niyajuayo mimi mngelicheka kidogo na mngelilia sana. Na  msingeli waonea ladha wanawake juu ya vitanda  na mngelitoka  kwenda kwenye nyanda za juu mkimkimbilia Allah-Ataadhamiaye”. Na Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiswali mpaka miguu yake ikivimba, akaambiwa: Unajikalifisha kiasi hiki na ilhali Allah  amekwisha kusamehe dhambi zako zilizo tangulia na zijazo? Akasema: “Basi je, nisiwe mja mwenye shukrani nyingi!” Amesema Bi. Aysha–Allah amuwiye radhi: “Amali za Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–zilikuwa ni za kudumu, ni yupi miongoni mwenu anaweza aliyokuwa  akiyaweza yeye?” Akaendelea  kusema: “Alikuwa akifunga mpaka tukisema hafungui na akila mchana mpaka tunasema hafungi tena”.

 

Amesema Auf Ibn Maalik-Allah amuwiye ardhi: “Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-usiku mmoja, akapiga mswaki, halafu akatawadha kisha akainuka kuswali.  Nami nikasimama [kuswali] pamoja nae, basi akafungua [swala] kwa Suratil-Baqarah. Basi hakuipitia aya ya rehema  ila  alisimama [alisita] na akaomba  na wala hakuipitia aya ya adhabu  ila alisita na kujilinda  kwa Allah. Halafu akarukuu, akakaa [katika rukuu] kadri ya kisimamo  chake, akisema: SUB-HAANA DHIL-JABARUUT WAL-MALAKUUT WAL-KIBRIYAAI WAL-ADHWAMAH. Halafu akasujudu na kusema maneno  kama hayo, halafu akasoma Surat Aali Imraan [katika rakaa ya pili]. Halafu akaendelea  kusoma sura baada ya nyingine, akifanya kama hivyo”.

 

Na amesema mmoja wa maswahaba: “Nilimuendea Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–ilhali akiswali  na tumbo lake likiunguruma kama mtokoto wa sufuria  ichemkayo [kutokana na njaa kali”. Na katika wasifu wa Abu Haalah, kumetajwa: “Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-alikuwa mwenye muendelezo wa huzuni, mdaima wa fikra asiye na raha yoyote”. Na imepokewa kutoka  kwa Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-nilimuuliza Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-juu ya sunah yake, akasema: “Maarifa [elimu] ndiyo raslimali yangu, akili ndiyo shina la  dini yangu, huba [upendo] ndio msingi wangu na shauku ndio kipando changu. Dhikri ya Allah ndio hazina yangu, huzuni  ndio mwenza wangu, elimu ndio silaha yangu na subira ndio nguo yangu. Kuridhia ndio ngawira yangu, ajizi ndio fakhari yangu, kuipa mgongo dunia ndio taaluma yangu, yakini ndio nguvu yangu na ukweli ndio mwombezi wangu [mbele ya Allah]. Twaa [utiifu kwa Allah] ni tosha yangu, jihadi ndio khulka yangu, tuo la jicho langu limo ndani ya swala, tunda la moyo wangu liko katika  kumshukuru Allah. Na upofu wangu ni kwa ajili ya umati wangu na shauku yangu ni kwa Bwana Mlezi wangu”.

 

Allah amjaze kheri Mtume kwa niaba ya umati wake  na amrehemu mja aliye zizingatia sifa hizi maumbile tukufu na mambo mazuri haya. Akashikamana nayo na akamfuata Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie-ili aihodhi  shufaa yake katika siku yenye fadhaa kubwa na Allah  amridhie.

Mpendwa ndugu katika imani-Allah  akuzidishie imani–mpaka hapa  kwa auni na taufiq ya Allah  tutakuwa tumekomelea  kutaja Sira ya mbora wa viumbe. Tunataraji kwa  msaada wa Allah  utakuwa  umestafidi na kujifunza mengi kutoka katika maisha ya mja mwema huyu. Tukutane juma lijalo katika Sira ya makhalifa wake waongofu, Inshallah.

Additional information