KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

MAZUNGUMZO JUU YA UPWEKE WA ALLAH...Inaendelea

NNE: Katika jumla ya miundo fikishi na hoja ambazo zilizo tumiwa na Qur-ani Tukufu ili kuzikinaisha akili ya kwamba mwenye kustahiki kuabudiwa na kutiiwa, ni Allah Ataadhamiaye peke yake, ni kupiga mifano.

Na hakika si vinginevyo, mifano hupigwa kwa ajili ya kuweka wazi maana iliyo jificha na kukisogeza kilicho akilini kuwa chenye kuhisiwa na milango ya fahamu. Na kukionyesha kitu cha ghaibu katika taswira ya kitu chenye kuonekana, basi hapo huwa ile maana iliyo pigiwa mfano ni yenye kutuka mno nyoyoni na yenye kuthibiti mno nafsini. Na amesema kweli Allah Atukukiaye pale alipo sema: “NA HIYO NI MIFANO TUNAWAPIGIA WATU, NA HAWAIFAHAMU ILA WENYE ILIMU”. [29:43]

 

Na katika aya nyingine: “...NA HIYO MIFANO TUNAWAPIGIA WATU ILI WAIFIKIRI”. [59:21]

Na mahala pengine: “...NA ALLAH HUWAPIGIA WATU MIFANO ILI WAPATE KUKUMBUKA”. [14:25]

Na miongoni mwa mifano iliyo pigwa na Allah Atukukiaye ili kubainisha ya kwamba Yeye-utakati wa mawi ni wake-hapana muabudiwa kwa haki zaidi yake Yeye, ni kauli yake: “ALLAH ANAPIGA MFANO WA MTUMWA ALIYE MILIKIWA, ASIYE WEZA KITU, NA MWINGINE TULIYE MRUZUKU RIZIKI NJEMA INAYO TOKA KWETU, NAYE AKAWA ANATOA KATIKA RIZIKI HIYO KWA SIRI NA DHAAHIRI. JE, HAO WATAKUWA SAWA? ALHAMDU LILLAAHI! KUHIMIDIWA KOTE NI KWA ALLAH, LAKINI WENGI WAO HAWAJUI”. [16:75]

Yaani: Enyi watu! Allah Ataadhamiaye amekutajieni hali za watu wawili hao, ili mpate kuwaidhika, mtafakari na mumtakasie ibada Mola Muumba wenu. Mmoja wa wawili hao, ni mtumwa wa mwingine na mtumwa huyo hajimudu kwa chochote hata kama kitakuwa ni kidogo. Na yule wa pili pia ni mtumwa aliye huru, anayamiliki mambo yake yeye mwenyewe. Na Allah akamruzuku mali ya halali nyingi, yenye kutosha, basi naye huitoa mali hiyo kwa njia ya siri na dhaahiri kuwapa masikini na wahitaji.

Hizo ndizo pande mbili zinazo kabiliana katika mfano huu, na tofauti iliyoko baina yao iko wazi, tena ni kubwa kwa kila mkomavu wa akili. Ni kwa ajili hiyo ndio likaja baada yao ulizo kanushi umbuzi, nalo ni lile neno lake Allah: “JE, HAO WATAKUWA SAWA?”, Yaani: Je, katika uelewa wenu au uelewa wa kila mwenye akili timamu, huyu mtumwa mmilikiwa, asiye jiweza kwa lolote analingana sawa na huyu mtu huru, mmiliki mtumwa ambaye Allah Ataadhamiaye amemruzuku riziki halali ya wasaa! Huyu akamshukuru Allah kwa neema alizo mneemesha kwa kutoa sehemu yake kwa siri na kwa dhaahiri kuwapa waja wa Allah, hawa watalingana sawa?! Hakika ni jambo lisilo na chembe ya shaka kwamba wawili hawa, katu hawalingani sawa hata kwa mtazamo wa mwenye akili kidogo kabisa. Kama hivyo ndivyo ilivyo, basi ni vipi enyi washirikina majahili mmelinganisha sawa katika ibada baina ya Muumbaji, Mwenye kuruzuku ambaye anamiliki vyote na wote. Mmemlinganisha sawa na miungu mingine ya batili ambayo haisikii, haioni, haifahamu na wala haileti manufaa na haiondoshi madhara!!

Na kauli yake Allah Atukukiaye: “...ALHAMDULILLAAHI! KUHIMIDIWA KOTE NI KWA ALLAH...”, ni sifa anayo jisifia Yeye mwenyewe pale alipo iswaga (ileta) mifano hii iliyo wazi ili kutofautisha baina ya haki na batili. Yaani: Ewe mtu muumini, mwenye akili, sema kuhimidiwa kote ni kwake Allah Ataadhamiaye kwa kuwaongoza kwake waja wake waumini na kuwafundisha namna ya kuitupa haki yao juu ya batili ya adui yao, tahamaki hiyo batili ni yenye kuondoka.

Kisha Allah-utakati wa mawi ni wake-akaitamatisha aya hii tukufu kwa kauli yake: “...LAKINI WENGI WAO HAWAJUI”. Yaani: Lakini wengi wa washirikina hao hawajui namna ya kuitofautisha haki na batili kwa sababu ya kupofua kwa uoni wao na kutawaliwa na upingaji, hasadi na ujahili. Na akasema Allah-utakati wa mawi ni wake: “...LAKINI WENGI WAO...” ili kuleta hisia kwamba wako wachache miongoni mwa washirikina wale wanaijua haki vilivyo, lakini matamanio ya nafsi, ghururi na uigaji wa kibubusa vimekingama baina yao na kuifuata haki hiyo.

Huu ndio mfano wa kwanza ambao Allah Ataadhamiaye ameutaja ili kutoa dalili juu ya ubatili wa kufanya sawa baina ya ibada ya Allah Muumba wa kila kitu, Mmiliki wa kila kitu. Na ibada ya visivyo kuwa Yeye; yaani masanamu na vitu vigogofu ambavyo haviwezi kuumba chochote, havidhuru na wala havinufaishi.

Lakini je, Qur-ani Tukufu iliishia hapa kwa kupiga mfano huu wa wazi katika kutenganisha baina ya haki na batili? La hasha, baada ya mfano huo Qur-ani Tukufu ilipiga mfano mwingine ulio wazi zaidi katika kutoa dalili juu ya wajibu wa kumtakasia ibada Allah, aliye Mmoja, Mtenza nguvu, akasema Atukukiaye: “NA ALLAH ANAPIGA MFANO WA WATU WAWILI. MMOJA WAO NI BUBU, HAWEZI CHOCHOTE, NAYE NI MZIGO KWA BWANA WAKE. POPOTE ANAPO MUELEKEZA HALETI KHERI. JE! HUYO ANAWEZA KUWA SAWA NA YULE ANAYE AMRISHA UADILIFU, NAYE YUKO JUU YA NJIA ILIYO NYOOKA?” [16:76]

Yaani: Enyi watu! Allah Atukukiaye amekupigieni mfano mwingine wa watu wawili; mmoja wao ni bubu, asiye weza kuzungumza neno lolote na wala hawezi kutenda lolote. Naye wakati huo huo ni: “...MZIGO KWA BWANA WAKE...” Yaani: Twika nzito na dhiki kubwa kwa Bwana wake ambaye anayatawalia mambo yake yote, kuanzia chakula, maji na vinginevyo. Zaidi ya yote hayo, hakika mtu huyu bubu, asiye na uwezo wa chochote, popote anapo elekezwa na Bwana Mlezi wake kufanya jambo lolote, hurejea patupu kwa ajizi yake, udhaifu wa nguvu zake na kuondoka kwa utambuzi wake.

Utaona ewe msomaji wetu-Allah akupe fahamu-kwamba Allah Atukukiaye-amemsifia mtu huyu kwa sifa nne zinazo fahamisha ufahamu wake mbovu, uchache wa nguvu zake na kufungika kwa njia za kheri mbele yake. Hiyo ndio janibu ya kwanza ya mfano huu.

Ama janibu yake ya pili inadhihirika kupitia kauli yake Allah Atukukiaye: “...JE! HUYO ANAWEZA KUWA SAWA NA YULE ANAYE AMRISHA UADILIFU. NAYE YUKO JUU YA NJIA ILIYO NYOOKA?” Yaani: Je, huyu mtu bubu, asiye jiweza kwa lolote anaweza kulingana sawa na mtu mwingine anaye waamrisha wenzake uadilifu na yeye mwenyewe anaifuata njia iliyo nyooka. Na anajipamba na tabia nzuri na akili salama kwa kuwa yeye binafsi yake ni mwema na ni manufaa kwa wengine. Hapana shaka kwamba watu wawili hawa hawalingani sawa katika mizani ya mwenye akili pevu ionayo mbali. Kwa maana kwamba mmoja wa wawili hawa ni bubu asiye jiweza kwa lolote, mrejea patupu. Na mwingine ni mtu fasaha na wakati huo huo anawanufaisha wenzake na amezihodhi tabia na mambo mazuri. Maadam suala liko hivi, basi ni vipi enyi washirikina wapotofu mmefanya sawa katika ibada baina ya Allah aliye Mmoja, Mtenza nguvu na hao miungu wa bandia walio viziwi na mabubu wasio weza kujilinda wao wenyewe, seuze hao wanao waabudu?!

Kwa maelezo haya basi, tunaona kwamba aya mbili hizi zimeleta mifano iliyo wazi ili kubainisha tofauti kubwa mno baina ya dhati ya Allah Atukukiaye, Muumba aliye Mjuzi mno, Mwenye kuruzuku aliye Mkarimu. Na wale miungu wa batili ambao washirikina wamewashirikisha katika ibada ya Allah. Au baina ya muumini ambaye ana ujuzi/elimu ya dini yake na kafiri ambaye ameupenda upotofu kuliko uwongofu. Au baina ya haki katika uwazi wake, uzuri wake na utukufu wake na batili katika kiza chake, ubaya wake na udhalili wake.

Additional information