KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA ZA KIYAMA: KUFUATA MWENENDO WA MAYAHUDI NA MANASWARA

Leo umma wa Kiislamu umekuwa kama mtoto yatima asiye na baba wala mama, mtoto asiye na wa kumlea kimwili, kiroho na kimaadili. Umma wa Kiislamu leo umekuwa kama mtoto wa mtaani, anaye pita akiokota na kuchukua kila kilicho mbele yake, pasina kufikiri wala kujali athari; hasara au faida, yeye anacho kijua ni kuokota tu. Matokeo au athari ya anacho kiokota hayana nafasi kwake. Hiyo ndio hali ya umma wetu leo, umma umekuwa na mmomonyoko kama sio mbomoko hasa katika utamaduni (mila na desturi), uchumi, vyombo vya habari, siasa, elimu na malezi na baki ya nyanja nyingine za maisha ya kijamii.

 

Leo Waislamu wamekuwa ni watu wa kuiga na kufuata kila kiingiacho mjini, kwa sababu wameiweka kando dini yao, dini iliyo sheheni na kuzienea nyanja zote za maisha yao. Dini yenye hazina kubwa katika nyanja za utamaduni, uchumi, siasa, elimu na malezi na kila nyanja inayo yagusa maisha ya mwanaadamu ya kila siku bali ya umri wake wote. Waislamu leo wameutupa utamaduni wao, utamaduni na ustaarabu walio rasimiwa na Mola Muumba wao na badala yake wameukumbatia utamaduni na ustaarabu wa kimagharibi ulio wekwa na wanaadamu wenziwao. Na natija ya hilo ndio huu mbomoko wa kimaadili tunao uona leo katika jamii zetu, kiasi cha kuonekana ushoga ni kitu cha kawaida bali hata ndoa za jinsia moja. Yote hayo yanatukumba kwa sababu ya kuiga kibubusa kila kiingiacho mjini na kubwa zaidi ni kule kuupa kisogo utamaduni wa dini yetu.

Angalia leo uvaaji wa watoto wetu si wa kike wala si wale wa kiume, wote mavazi yao yanakiuka maadili, ni mavazi yasiyo ipa stara miili yao, ni mavazi yenye kuchochea na kuamsha shahawa, jambo ambalo limepelekea kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti katika jamii zetu. Hayo ni matunda ya kosa kubwa la kukidharau cha kwetu tulicho pewa na Muumba na tukakithamini cha wenzetu kinacho tokana na matashi ya kibinaadamu. Hilo la uvaaji halikuwasaza hata watu wazima bali hata wake na waume za watu nao wamekumbwa na mkumbo huo, tena wengine ni wasomi wa ngazi za juu lakini elimu yao hiyo haiwasaidii kupambanua kizuri na kibaya.  Hayo ni machache tu kutaja miongoni mwa mengi.

Hili la kutupa mila na utamaduni wa Uislamu na badala yake kuiga kibubusa na kufuata kila kitu pasina kutafakari athari zake, tayari lilisha tajwa na mwanaadamu mwenye uoni wa mbali karne kumi na tano nyuma. Aliliona hilo na hivi ndivyo alivyo lizungumza, tumsikilize na kisha tutafakari na halafu tuchukue hatua: “Kabisa, kabisa! Mtafuata, mtafuata nyenendo (mila, tamaduni, desturi na ustaarabu) za walio kuwa kabla yenu, shubiri kwa shubiri, dhiraa kwa dhiraa (hatua kwa hatua/nyayo kwa nyayo). Hata kama wataingia kwenye shimo la kenge yuru nanyi bila ya shaka mtaingia”. Pakaulizwa: Ewe Mtume wa Allah! Je, ni Mayahudi na Manaswara? Akajibu: Basi ni nani (wengine kama si wao)?” Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Ndugu mwana-jukwaa letu-Allah akurehemu-hili lililo tajwa na Mtume wa Allah lipo na linaishi pamoja nasi katika majumba yetu, mitaa yetu, mahala petu pa kazi, katika vyombo vyetu vya usafiri na kila tulipo, yupo mkanushaji?! Wavaa uchi, mashoga na mfano wao wamejaa majumbani mwetu, mitaani kwetu na hata makazini kwetu. Ikiwa hiyo ndio hali, unasubiri nani aje akuambie kuwa Kiyama hichoo kimeshabisha hodi?! Tafakari, chukua hatua usiige na kufuata kila kiingiacho mjini bali uangalie muongozo wa Mola wako katika kila kipengele cha maisha yako juu ya mgongo huu wa ardhi, ili ukapate salama ndani ya tumbo la ardhi na pale utakapo fufuliwa na kusimamishwa mbele ya Mola wako kwa ajili ya hisabu na jazaa.

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

“Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

Ewe Mola wa haki! Ewe Mwenye kuwaongoza wale walio amini katika njia iliyo nyooka! Tunakuomba utuongoze kutenda yale ambayo unayo yapenda na kuyaridhia. Utufungulie milango ya riziki zako za halali kutokana na ukunjufu wa fadhila zako, utukinge na riziki ya haramu. Na kwa fadhila zako ututoshee na asiye kuwa Wewe, utuepushe na mitihani na fitina za dhaahiri na za siri. Yaa Rabbi tutakabalie dua!

Aamina!

Hapa ndipo linapo tamatia Jukwaa letu juma hili ili kumpa fursa ya kutafakari kila mwenye moyo wa kukumbuka, akumbuke na awaidhike na kisha achukue hatua kwa kujiandaa na siku iliyo ahidiwa ya Kiyama.

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kujifunza alama nyinginezo za Kiyama kama zilivyo elezwa na Yule Mkweli Muaminifu ambaye:

وَمَا يَنطِقُ عَنِ ٱلۡهَوَىٰٓ ٣  إِنۡ هُوَ إِلَّا وَحۡيٞ يُوحَىٰ ٤

“Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya (ayatamkayo) ila ni ufunuo (wahyi) ulio funuliwa”.            An-Najmi [53]:03-04

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

وَمَاٱلۡحَيَوٰةُٱلدُّنۡيَآ إِلَّا لَعِبٞ وَلَهۡوٞۖ وَلَلدَّارُ ٱلۡأٓخِرَةُ خَيۡرٞ لِّلَّذِينَ يَتَّقُونَۚ أَفَلَا تَعۡقِلُونَ ٣٢

“Na maisha ya Dunia si chochote ila ni mchezo na pumbao tu. Na hakika nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wanao mcha Mungu. Basi je, hamtii akilini?”. Al-An’aam [06]:32

 

Additional information