KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

SIFA STAHIKI ZA MTUME WA ALLAH REHMA NA AMANI ZIMSHUKIE

Allah Ataadhamiaye amempa Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-katika sifa kamilifu za dunia na akhera, kiasi ambacho hakumpa yeyote miongoni mwa wa kabla na baada yake. Katika sura hii tutakuletea sehemu kidogo ya sifa zake njema na adabu zake tukufu ili ziwe kwako mfano utakao ufuata mpaka uwe katika wanao zifuata nyayo za Mtume wao. Kwa kufanya kwako hivyo ukawa umestahiki kupata sifa njema Duniani na mbeko (akiba) nono Akhera.

 

Fahamu ewe ndugu mwema-Allah atuongoze kwenye njia ya sawa-kwamba mambo ya utukufu na ukamilifu kwa mwanaadamu ni ya aina mbili:

 

1)             Mambo ya dharura ya kidunia yanayo pelekewa na umbile la asili na dharura za maisha.

 

2)             Mambo chumo la dini, nayo ndio husifiwa mtendaji wake na humkurubisha karibu na Allah.

 

Haya na tuanze kuyaangalia mambo haya kwa uchambuzi na ufafanuzi kidogo. Ama aina ya kwanza; mambo ya dharura, haya ni yale ambayo mtu hana khiari ndani yake ya ama kutenda ama kutokutenda. Hali kadhalika hayana kuchumwa kutokana na malezi/maadili ya kidini anayo lelewa mtu ndani yake. Mfano wa yale yaliyo kuwa katika umbile asili la Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-yaani ukamilifu wake wa umbo, uzuri wa sura. Nguvu ya akili, sifa ya ufahamu, fasaha ya ulimi, nguvu ya hisia na viungo, ukatikati wa harakati (matendo), utukufu wa nasabu na wa ardhi (mahala alipo zaliwa). Na yanaambatishwa na haya, yale yanayo pelekewa na dharura/lazima za maisha; yaani ulaji, ulalaji, uvaaji, maskani, mali na cheo/daraja.

 

Ama mambo ya chumo la kiakhera, basi haya ni baki ya  tabia zote tukufu na adabu zinazo tokana na malezi/mafunzo/maadili ya dini, elimu, upole, subira, shukurani, uadilifu, uchaMngu na unyenyekevu. Usamehevu, muepuko wa machafu/maovu, ukarimu, ushujaa, soni (haya), murua, ukimya, utuvu, umakini, huruma, adabu na tangamano jema na mengineyo kama haya ambayo yanajumuishwa na tabia/hulka njema. Basi utakapo yachunguza mamo ya ukamilifu ambayo hayo si yale yatokanayo na chumo na yako katika asili ya umbile (finyango) la mwanaadamu. Utamkuta Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ameyahodhi yote, ameyazunguka mazuri yake tapanyi.

 

Ama sura yake na uzuri wa sura yake hiyo na mnasibikiano wa viungo vyake, hakika zimekuja athari/hadithi sahihi na mashuhuri nyingi katika kulieleza hilo. Ya kwamba yeye Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa mng’avu wa rangi, mweusi wa mboni, mkubwa wa macho, katika weupe wa macho yake kuna wekundu. Mwingi wa kope, mwenye uso mng’aro, mnyoofu wa pua, mwenye mwanya upendezao, mwenye uso wa duara, mpana wa paji (la uso), mwingi wa ndevu. Msawasawa wa tumbo, mpana wa kifua na mabega, mkatikati wa kimo (si mrefu si mfupi) na baki ya sifa maumbile nyingine alizo pambwa nazo na Mola Muumba wake.

 

Amesema Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi: “Sikupata kuona kitu ambacho hicho ni kizuri mno kumshinda Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Kama kwamba jua linajiri usoni kwake (kutokana na ung’avu/mng’aro wake). Na anapo cheka humeta katika viambaza”. Na imepokewa katika hadithi ya Abu Haalah-Allah amuwiye radhi: “Unang’ara uso wake mng’aro wa mwezi kumi na tano (Laylatul-Badri)”. Na amesema Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-katika mwisho wa wasifu wa Mtume alio utaja: “Atakaye muona kwa mara ya kwanza, humuogopa (hutishwa nae kutokana na haiba yake). Na atakaye changanyika nae kwa kumjua (daraja/cheo chake), atampenda”. Anasema mwenye kumsifia: “Sijapata kuona kabla yake wala sitaona baada yake mfano wake Mtume-Rehema na Amani zimshukie”.

 

Ama unadhifu/usafi wa mwili wake, riha (harufu) yake nzuri na riha ya jasho lake na muepukano wake na uchafu na utupu wa mwili. Kwa yakini Allah Atukukiaye alikuwa amemkhusu katika hilo kwa khususi ambazo hazikupatikaniwa kwa mwingine asiye yeye. Kisha tena Allah akayatimiza hayo kwa kumpa nadhafa/usafi wa sheria. Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Dini imejengwa juu ya unadhifu”. Na amesema Anas-Allah amuwiye radhi: “Sikupata katu kunusa ambari wala miski wala kitu chochote chenye harufu nzuri mno kuliko riha ya Mtume wa Allah”. Na imepokewa kutoka kwa Jaabir-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alilipangusa shavu lake. Anasema (Jaabir): Basi wallah nikaukuta mkono wake ni baridi na una riha nzuri kama kwamba ameutoa kwenye kifuko cha manukato”. Na wamesema wengineo: Humpa mkono mtu, basi hushinda kutwa nzima akiisikia harufu yake. Humshika mtoto kichwani, basi mtoto atajulikana baina ya watoto wenzake kwa sababu ya harufu nzuri ya mkono wake”. Na imepokewa na Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-[katika TAARIKHUL-KABEER yake] kutoka kwa Jaabir: “Hakuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akipita katika njia, kisha akaifuata njia hiyo mtu yeyote. Ila atajua tu kwamba Mtume amepita katika njia hiyo kutokana na manukato yake”.

 

Ama wingi wa akili yake Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na utambuzi/welevu wa kokwa ya akili yake na nguvu ya hisia zake, fasaha ya ulimi wake. Na ukatikati wa harakati (matendo) zake na uzuri wa sifa zake, hapana chembe ya shaka kwamba yeye alikuwa na akili kushinda watu wote na mwerevu wao. Na alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anapo simama katika swala huona nyuma yake kama anavyo ona mbele yake. Na kwa hilo ndivyo ilivyo fasiriwa kauli yake Allah Ataadhamiaye: “...NA MAGEUKO YAKO KATI YA WANAO SUJUDU”. [26:219] Amesema Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiona gizani kama anavyo ona mwangazani”.

 

Na katika sifa zake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwamba uchekaji wake ulikuwa ni tabasamu. Anapo geuka hugeuka mzima na anapo tembea huwa kama anadondoka kutokana na mwinamo (wa unyenyekevu).

 

Ama fasaha ya ulimi na utoshefu wa kauli, kwa upande huu alikuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika nafasi bora kabisa. Inayo chunga salama ya tabia, upeo wa ubingwa, ushindani wa kutinda, fasaha ya matamshi, ukubwa wa kauli, usahihi wa maana na uchache wa taklifu. Alipewa mkusanyo wa maneno, akaweza kusema neno moja likabeba maana na tafsiri nyingi adida na alikhusishwa kwa kupewa busara/hekima pevu na ujuzi wa lahaja za Waarabu. Basi akawa anazungumza na kila uma miongoni mwa Waarabu kwa lahaja yake na akiwasemesha kwa lugha yao. Mpaka wakawa wengi miongoni mwa maswahaba wake wakimuuliza katika mahala pengi juu ya ufafanuzi wa maneno yake na tafsiri ya kauli zake. Atakaye zichunguza hadithi zake na muundo wake atalijua na kulithibitisha hilo. Na hayakuwa maneno (mazungumzo) yake anapo kuwa pamoja na Makureishi wenzake ni kama maneno yake pamoja na Aqyaal wa Hadharamaut (mji katika Yemen). Na wafalme wa Yemen na viongozi wa Najid, bali hutumia kwa kila kabila maneno wayapendayo na muundo wa fasaha walio jiundia. Alifanya hivyo ili apate kuwabainishia watu yale yaliyo teremshwa kwao na azungumze na watu kwa lugha waijuayo.

 

Ama maneno yake ya kawaida, ufasaha wake ujulikanao na mkusanyiko wa maneno yake, kwa yakini watu wametunga madiwani katika hayo. Na vimekusanywa katika matamshi na maana zake vitabu, na miongoni mwake ziko ambazo haziwezi kupimwa na fasaha wala balagha yoyote, kama vile kauli yake:

 

“Waislamu zinalingana sawa damu zao, na anaichukua dhima yao wa chini yao kabisa, nao ni mkono (msaada) kwa asiye wao”. Na kauli yake: “Watu ni kama mfano wa meno ya chanuo na mtu yu pamoja na ampendaye. Na wala hapana kheri katika kusuhubiana na yule asiye kuona kama umuonavyo wewe”. Na kauli yake: “Watu ni madini, na hakuangamia mtu aliye ijua kadiri yake na mtakwa ushauri ni muaminiwa. Allah amrehemu mja aliye sema kheri akapata faida au akanyamaza akasalimika”. Na kauli yake: “Silimu utasalimika (ingia Uislamuni, utapata amani). Silimu, Allah atakupa ujira wako mara mbili. Na hakika apendezaye zaidi kwangu katika nyinyi na mkaribu wenu mno kwangu kimakazi siku ya Kiyama, ni mwema wenu mno wa tabia. Wenye kuteremsha mabawa ambao wao wanawazoea watu na watu huwazoea wao”. Na kauli yake: “Huenda yeye alikuwa anazungumza yasiyo muhusu au alikuwa akiyafanyia ubakhili yasiyo mtajirisha”. Na kauli yake: “Mwenye nyajihi (nyuso) mbili (ndumilakuwili), hatakuwa na wajihi (heshima) mbele ya Allah”. Na kauli yake: “Mche (muogope) Allah popote pale ulipo, na lifuatishie ovu (ulilo litenda) jema litakalo lifuta. Na tangamana na watu kwa tabia njema. Na bora ya mambo ni ukati na kati”. Na kauli yake: “Mpende mpenzi wako kwa kiasi fulani, huenda akawa mchukivu (adui) wako siku yoyote...”

 

Na nyinginezo miongoni mwa kauli zilizo pokewa katika minasaba, mihadhara, khutba, dua mazungumzo na mikataba yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Maswahaba wake-Allah awawiye radhi-wamepata kumwambia: Hatujapata kumuona mtu aliye fasaha kuliko wewe. Mtume akasema: “Kipi kinanizuia (nisiwe hivyo) na hakika si vinginevyo Qur-ani imeshushwa kwa lugha yangu; lugha ya Kiarabu iliyo wazi”.

Ama sharafu ya nasabu yake, na utukufu wa mji alipo zaliwa na makuzi yake, ni miongoni mwa ambayo yasiyo hitaji kusimamishiwa dalili/hoja juu yake. Wala kubainisha mushkeli wala lililo jificha katika hayo. Hakika yeye ni mteule wa Baniy (ukoo) Hashim, mteule wa Makuraishi na mtakasifu wao. Na ni mtukufu wa Waarabu wote kwa pande zake zote mbili; kwa baba na mama yake. Na kwa watu wa Makah; mtukufu wa miji ya Allah mbele ya Allah na kwa waja wake. Na hapana shaka kwamba awali kabisa ya somo hili la Sira, tumeeleza ya kutosha katika wigo huu.

Additional information