KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UZAZI WA MPANGO

Baada ya kuelezea kweli halisia hizi ambazo tunataraji kuwa ndio ziwe mahala pa maafikiano/kongamano. Sasa tunapenda kuingia katika maudhui ya “UZAZI WA MPANGO”, kwa mtindo wa swali na jawabu kama ifuatavyo:

Mosi: Nini maana ya uzazi wa mpango? Na je, kuna tofauti baina ya uzazi wa mpango na kuzuia uzazi, kuhasi (vasectomy) na utoaji mimba?

 

JIBU: Hakika maana ya uzazi wa mpango kwa lugha nyepesi; isiyo tanza wala kutatiza: Ni mke na mume kwa hiari zao na ukinaifu wao, kutumia njia ambazo wanaziona zinafaa kutoa mwanya baina ya mimba na nyingine. Au ni kusitisha utungaji wa mimba kwa muda/kipindi maalumu watakacho kubaliana wao wenyewe bila ya kulazimishwa. Na pamoja na kukubali kusiko na shaka kwamba ziko dharura zinazo pelekea hilo ambazo zinakubaliwa na sheria ya Uislamu. Na kwamba lile alilo likadiria Allah Ataadhamiaye, hapana budi liwe/litokee na wao hakika si vinginevyo wanafanya sababu tu. Na sababu hizo kama zilivyo na imkani ya kufaulu, ndivyo pia zina imkani ya kushindwa (kufeli).

Na makusudio ya hilo la uzazi wa mpango: Ni kupunguza idadi ya wana familia kwa sura ambayo itawafanya wazazi kuweza kuwalea na kuwatunza watoto wao. Malezi na matunzo kamili bila ya uzito au kuwatia makosani kwa kushindwa kuwalea kunako pelekea kuwaharibia mustakabali wao.

Na kuna tofauti kubwa baina ya uzazi huu wa mpango tulio utaja hapa na uzuiaji wa uzazi, kujihasi na utoaji wa mimba. Kwa sababu uzuiaji uzazi kwa maana ya kuzuia kabisa kwa hali yoyote, hilo ni HARAMU katika sheria, limekatazwa. Na mfano wa hili, ni uhasi (vasectomy) ambao maana yake ni kuua kabisa sababu/njia za kupatia watoto.

Ama utoaji mimba, nao pia ni HARAMU na umekatazwa na sheria ILA itakapo patikana dharura inayo lazimisha hilo. Hivyo ni kama daktari bingwa wa masuala ya uzazi, mwenye sifa ya ukweli, kusema: Hakika kuendelea kubakia kwa mwana mimba tumboni mwa mama yake, ama kutapelekea kifo cha mama mja mzito au kutamsababishia madhara makubwa. Na hali zote zinazo zungumziwa kuhusu utoaji wa mimba, zina mazingira na sababu zake na zina hukumu zake zinazo tolewa na wadau wake, miongoni mwa mafaqihi (wataalamu wa fani ya Fiq-hi) na matabibu.

Hapawezi kusemwa katika Fiq-hi timamu na akili nyoofu: Kwamba utoaji mimba ni halali kwa hali yoyote au ni haramu kabisa kwa hali yoyote iwayo. Hakika kila hali inayo hukumu yake inayo chukuzana nayo ambayo inatolewa na Mafaqihi na matabibu. Hivyo ni pamoja na kuchunga kwamba asili/msingi katika sheria ya Uislamu, ni mjamzito kumchunga/kumlinda mtoto wake kikamilifu tangu ile siku ya kwanza anapo hisi kuwa yu mjamzito mpaka siku ya kujifungua kwake. Na kuendelea kumtunza baada ya kumzaa. Na wala asikimbilie kutoa mimba ila kwa dharura lazimishi inayo kubaliwa na Mafaqihi na matabibu kuwa ni dharura halalishi na si vinginevyo.

 

Pili: Je, uzazi wa mpango kwa maana hii iliyo tangulia kubainishwa, ni jaizi kwa upande wa kidini?

JIBU: Bila ya shaka uzazi wa mpango kwa sura/namna tuliyo kwisha ibainisha, Mafaqihi wengi wamesema inajuzu (imeruhusiwa na sheria), rejea vitabu vya Fiq-hi utayaona mas-ala hayo yametajwa kwa ukunjufu wa kukinaisha.

Na kunaruhusiwa kuzuia uzazi katika hali ambayo mwanaume atakapo kuwa na kizazi kingi na hamudu kuwapa watoto anao wazaa malezi bora stahiki. Na hali kadhalika mwanamke atakapo kuwa dhaifu au akawa anabeba mimba mfululizo (kwa kufuatana), pia kunajuzu kuzuia uzazi. Ni katika hali kama hizo, ndimo kunaruhusiwa kuzuia uzazi.

 

Tatu: Je, kuna maslahi serikali kuwawekea sheria ya uzazi wa mpango raia wake?

JIBU: Sisi tunaona hilo halina maslahi, kwa sababu suala la uzazi wa mpango ni miongoni mwa masuala binafsi ambayo yanawahusu wanandoa (mke/mume) peke yao. Na ni masuala yanayo tofautiana baina ya kaya (familia) na kaya nyingine, kwa mujibu wa mazingira na hali zao. Na masuala yanayo fungamana na mke na mume, hayatengenezwi na kanuni/sheria za dola. Bila ya shaka njia bora ya kupanga familia, ni kuifahamu vema dini na kuueneza ufahamu huo sahihi wa dini miongoni mwa wananchi/waumini. Nasi tunaona kwamba sababu ya msingi iliyo wafanya baadhi ya watu kupuuzia suala zima la uzazi wa mpango, ni kutokuwa kwao na ufahamu sahihi wa hukumu za dini na zile za masuala ya Dunia na kuyadogesha majukumu yao kwa watoto wao.

 

Nne: Je, wito wa uzazi wa mpango unapingana na kauli yake Allah Ataadhamiaye: “MALI NA WANA NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA...” [18:46] Au na kauli yake-utakasifu wa mawi ni wake: “WALA MSIWAUWE WANA WENU KWA KUOGOPA UMASIKINI. SISI TUNAWARUZUKU WAO NA NYINYI...” [17:31] Au na kauli ya Mshindi Mtukuka: “NA HAKUNA MNYAMA YOYOTE KATIKA ARDHI ILA RIZIKI YAKE IKO KWA ALLAH...” [11:06] Au na kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Oaneni mzaaneni ili mpate kuwa wengi, kwani mimi nitajifakharisha kwa nyumati nyingine siku ya Kiyama kwa ajili (ya wingi) yenu”.

JIBU: Wito wa uzazi wa mpango haupingani na nukuu hizi tukufu pale nukuu hizo zitakapo pata (kutana na) ufahamu sahihi wa kidini. Wito wa uzazi wa mpango haukinzani na kauli yake Allah Ataadhamiaye: “MALI NA WANA NI PAMBO LA MAISHA YA DUNIA...” Kwa sababu hapana yeyote mwenye akili timamu anaye pinga kuwa mali ni halali (kuichuma na kuimiliki) na kizazi chema kwamba viwili hivi ni pambo la maisha ya Dunia. Mpingaji wa hilo hayupo, ila tu ni kwamba watoto kama hatukuwapa matunzo na malezi mazuri wanayo stahiki, wanaweza kuwa fitina kama alivyo sema Allah-utakati wa mawi ni wake: “HAKIKA MALI YENU NA WATOTO WENU NI FITINA (jaribio/mtihani)...” [64:15] Na pia wanaweza kuwa adui kama inavyo bainishwa na kauli yake Atukukiaye: “ENYI MLIO AMINI! HAKIKA MIONGONI MWA WAKE ZENU NA WATOTO WENU WAMO MAADUI ZENU. BASI TAHADHARINI NAO...” [64:14]

Twendapo na nukuu hizi basi, tunaona kwamba watoto wanaweza kuwa ama ni pambo kama ambavyo wanavyo weza kuwa fitina/jaribio na maadui. Na uzazi wa mpango pale unapo ambatana na nia njema na makusudi/malengo matukufu, huwa ni msaada unao msaidia mzazi kuwafanya watoto kuwa ni tuzo la jicho.

Na wala wito wa uzazi wa mpango haupingani na kauli ya Allah: “WALA MSIWAUWE WANA WENU KWA KUOGOPA UMASIKINI. SISI TUNAWARUZUKU WAO NA NYINYI...” Kwa sababu hajasema asiye mlemavu wa akili kwamba uzazi wa mpango ni uuaji wa watoto. Ila huo uzazi wa mpango hakika ni himaya/hifadhi/ulinzi wao hao watoto kidini, kiafya, kibinafsi na kijamii. Na aya hii tukufu na nyinginezo zinakataza kuwaua watoto kabla na baada ya kuzaliwa kwao, kama watu wa zama za jahilia walivyo kuwa wakiwatendea watoto wadogo wa kike. Allah Ataadhamiaye analielezea hili: “NA MSICHANA ALIYE ZIKWA HAI ATAKAPO ULIZWA, KWA KOSA GANI ALIULIWA?” [81:08-09]

Na wala uzazi wa mpango haupingani na kauli yake Allah: “NA HAKUNA MNYAMA YOYOTE KATIKA ARDHI ILA RIZIKI YAKE IKO KWA ALLAH...” Kwa sababu kila mtu hawi mkamilifu wa imani ila kwa kuitakidi itikadi ya kutinda, kwamba kila kitambaacho ardhini; yaani wanaadamu, wanyama na vingine, vyote hivyo riziki yao iko kwa Allah peke yake. Lakini itikadi hii haikatazi kufanya sababu na kuhangaika ili kuipata riziki hiyo. Kwa sababu riziki hiyo Allah ameiwekea njia za kuipatia, atakaye zifuata ndiye atakaye fanikiwa na atakaye zipuuza atakula hasara. Ni vipi basi isiwe hivyo na ilhali Yeye ndiye asemaye katika aya nyingine: “YEYE NDIYE ALIYE IDHALILISHA ARDHI KWA FAIDA YENU, BASI TEMBEENI KATIKA PANDE ZAKE, NA KULENI KATIKA RIZIKI ZAKE. NA KWAKE YEYE NDIO KUFUFULIWA”. [67:15]

Na imekuja kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika hadithi: “Lau mngeli mtegemea Allah ukweli wa kumtegemea, basi angeli kuruzukuni kama anavyo waruzuku ndege; wanadamka wakiwa matumbo matupu na wanarudi jioni matumbo yakiwa ndii (yamejaa)”.

Na katika jumla ya kauli za Sayyidna Umar Bin Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-alipata kusema: “Asibweteke mmoja wenu kutafuta riziki, kisha aseme: Ewe Mola wa haki! Niruzuku! Na ilhali yeye anajua fika kwamba mbingu haileti mvua ya dhahabu wala fedha”.

Baada ya haya, tunajiuliza kwa masikitiko: Hivi watu kwa ujumla wao, wanaiamini aya hiyo (nukuliwa) kwa imani ya kiamalia (kiutendaji) kama wanavyo itamka kwa vinywa?

Jibu: Ni kwamba uhalisia wao wa kiamalia tuuonao unapingana na kauli zao kwa ushahidi wa ukatikati tunao uona na kujidhalilisha kwa mtu ili amsaidie kuwapatia kazi watoto wake au awaingize chuoni kwa njia zinazo kinzana na utukufu wa uwanaadamu unao mlingania mtu ya kwamba utegemezi wake uwe ni kwa Allah pekee.

Na wala uzazi wa mpango haupingani na ile hadithi tukufu isemayo: “Oaneni mzaaneni ili mpate kuwa wengi...” Kwa sababu sisi tunaona lililo na nguvu ni kwamba makusudio ya hadithi hii ni wingi wenye imani, ulio mwema na wenye nguvu katika dini yake na katika kutekeleza yale yanayo upasa. Na ilhali Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshuki-alikwisha usema vibaya wingi ulio dhaifu katika imani yake, mwenendo na maadili yake, alisema: “Yanakurubia mataifa kuitana dhidi yenu kama ambavyo walaji wanavyo itana kwenye sinia lao. Wakauliza (maswahaba): Hilo ni kwa sababu ya uchache wetu zama hizo, ewe Mtume wa Allah? Akajibu: Bali nyinyi wakati huo mtakuwa wengi, lakini wingi wenu utakuwa kama povu la mumbwi...” Kwa ushahidi huu ulio wazi basi, utaona kwamba wingi ulio mwema na wenye nguvu ndio utakiwao na Uislamu na wala sio wingi ulio muovu na dhaifu.

 

Tano: Je, uzazi wa mpango unapingana na ile imani ya hukumu na qadari ya Allah?

JIBU: Hakuna mwenye siha ya akili hata mmoja aliye pata kusema kwamba uzazi wa mpango kwa maana hii tuliyo itaja unapingana na ile imani ya kuamini hukumu na qadari ya Allah. Tunasema hivi kwa sababu haukuwa uzazi wa mpango ila ni aina ya kuvaana na sababu ambazo Allah Ataadhamiaye ametuamrisha kuzitenda ili kuyaratibu maisha yetu. Na sababu hizi tunazo zifanya, wakati mwingine hufanikiwa na mara nyingine hufeli, kwani mwanamke huweza kutumia njia ya kuzuia mimba kwa kipindi maalumu, pamoja na hivyo bado mimba ikatunga. Kama hivyo mfano wa mgonjwa anaweza kwenda kwa daktari, akapewa tiba, tiba hiyo inaweza kupelekea kupona na inaweza pia isimfikishe huko kwenye kupona. Na sisi kama Waislamu tunatakiwa kidini na kiakili kuvaana na sababu alizo tuwekea Allah Ataadhamiaye kwa ajili ya mafanikio yetu katika maisha. Tufanye hivyo huku tukiamini kwamba yale aliyo yakadiria na kuyahukumu Allah, hapana budi yatakuwa, hakuna wa kuyazuia kwa namna yoyote ile. Lakini tu ni kwamba sisi hatuyajui na wala hatuyafahamu hayo aliyo yahukumu na kuyakadiria Allah, kwa sababu marejeo ya hayo yako kwake Yeye peke yake katika elimu yake ya azali.

Kwa maelezo haya basi, uzazi wa mpango haupingani kabisa na imani ya kuamini qadari na hukumu za Allah, kwa kuwa sisi hatuyajui yale aliyo kwisha yahukumu Allah katika elimu yake ya azali. Hakika si vinginevyo, tunacho fanya sisi ni kuvaana (kutenda) na zile sababu za kuyafikia mambo tuyatakayo, alizo ziweka Allah Atukukiaye. Kisha tena baada ya kuzifanya sababu hizo, ndipo Allah atatupeleka akutakako Yeye: “...FAHAMUNI! KUUMBA NA AMRI NI ZAKE. AMETUKUKA KABISA ALLAH, MOLA MLEZI WA VIUMBE VYOTE”. [07:54]

Huu ndio mukhtasari kuhusiana na mas-ala ya uzazi wa mpango kwa upande wa kidini.

Additional information