KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

UFUMBULIZO, UWAZI KWA UTAKASIFU WA NIA...Inaendelea/7

Ama kadhia ya pili ambayo kumekithiri kujadiliwa kwake na watu wakakhitalifiana ikhtilafu pana katika hukumu ya sheria juu ya kadhia hiyo. Ni hii kadhia ya “uzazi wa mpango”. Kadhia hii tutaielezea kwa mukhtasari kama ifuatavyo: Hakika mas-ala ya uzazi wa mpango ni miongoni mwa mas-ala yanayo shughulikiwa kwa umuhimu mkubwa na baadhi ya nchi na mashirika mbali mbali ya kikanda na yale ya kimataifa. Na zimeandikwa tafiti na makala nyingi kuhusiana na mas-ala haya yanayo onekana kuzishughulisha mno bongo za wanaadamu hivi leo.

 

 

Ndugu mwema-Allah akurehemu-kabla hatujaingia kuyaelezea mas-ala haya kwa upande wa kidini, tunapenda kuwafikiana na ukweli halisia ufuatao. Kwa sababu uainisho wa mahala pa mzozo/makindano, kama wasemavyo wanazuoni wa fani ya “Usuulul-Fiq-hi” – Misingi ya Fiq-hi, unasaidia juu ya ukinaishi mzuri. Na kweli halisia hizo, ni hizi zifuatazo:

 

             1.     Hakika sheria ya mbinguni aliyo iteremsha Allah Ataadhamiaye kwa mitume wake-Rehema na Amani ziwashukie-makusudio/malengo yake ya msingi, ni kuwaongoza watu kuelekea kwenye njia iliyo nyooka. Na kuwarasimia njia ya mafanikio na kupanda maana za tabia tukufu nyoyoni mwao. Allah Atukukiaye amesema: “ALIF LAM RA (A.L.R.) HICHI NI KITABU TULICHO KITEREMSHA KWAKO ILI UWATOE WATU KWENYE GIZA UWAPELEKE KWENYE MUWANGAZA, KWA IDHINI YA MOLA WAKO MLEZI, UWAFIKISHE KWENYE NJIA YA MWENYE NGUVU, MSIFIWA”. [14:01]

 

             2.     Hakika kuzungumzia mas-ala ya kidini kwa namna maalumu, ya pekee na kuzungumzia masuala mengine yaliyo na sura ya kidini, ni wajibu mazungumzo yake yawe yamejengwa juu ya elimu sahihi, ufahamu ulio salimika na mapungufu. Na utakasifu wa nia (Ikhlaasi) katika kuifikia haki na kuuliza mambo yaliyo fichikana, kwani Allah Atukukiaye anasema: “NA KABLA YAKO HATUKUWATUMA ILA WATU WANAUME TULIO WAPA WAHYI (ufunuo). BASI WAULIZENI WENYE ILIMU IKIWA NYINYI HAMJUI”. [21:07]

 

Imepokewa kutoka kwa Abdullah Bin Amrou-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Hakika Allah haiondoshi ilimu kutoka mioyoni mwa waja, lakini huiondosha ilimu kwa kuwaondosha (kuwafisha) wanachuoni. Mpaka itakapo kuwa hakubakia mwanachuoni, hapo watu watawafanya watu majahili kuwa ndio viongozi, basi wataulizwa (hao majahili) nao watatoa fat-wa pasina ilimu, hapo watapotea (wao) na watawapoteza (watu)”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

 

             3.     Hakika kukhitilafiana katika mambo yanayo kubali Ijitihadi, si jambo baya na wala halina madhara, muda wa kuwa makusudio ya ikhtilafu hizo ni kuifikia haki. Na muda wa kuwa zinaambatana na nia njema, maneno mazuri na majadiliano tulivu yanayo pambwa na adabu na tabia njema.

 

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliituza Ijitihadi ya namna hii na akawapa bishara njema maswahaba wake ya kwamba wao wanalipwa ujira wakipatia au wakikosea. Imekuja katika hadithi sahihi: “Atakapo hukumu hakimu, akajitahidi na akapatia, basi atapata ujira mara mbili. Na atakapo hukumu, akafanya ijitihadi na akakosea, basi atapata ujira mara moja”.

 

             4.     Hakika watoto ndio tunda la moyo wa mzazi na ndio mojawapo ya mapambo mawili ya maisha ya Dunia hii. Na watu wote, hata mitume wanatamani kupata watoto. Lakini hapo hapo, watoto ni amana iliyomo mikononi mwa wazazi wao na kumewawajibikia wazazi hawa kuilinda ipasavyo amana hii waliyo pewa. Kwa kuwapa malezi bora ya kidini (kiroho), kimwili, kielimu na kitabia na wawape uangalizi wanao uhitaji wa kimaada na kimaana. Kwani imepokewa katika hadithi sahihi: “Nyote nyinyi ni wachunga na nyote nyinyi mtaulizwa juu ya uchunga wenu...”.

 

             5.     Hakika ulimwengu huu, Allah Ataadhamiaye ameusimamisha juu ya mpango maalumu, timilifu toshelezi, kwa kuwa kila kitu kilichomo humo kinakwenda kwa kufuata mpango fanisi na utaratibu maalumu. Ndio maana jua huchomoza na kuzama katika wakati maalumu, kama lilivyo hilo kwa mwezi, usiku na mchana. Hivyo ndivyo asemavyo-utakati wa mawi ni wake: “HALIWI JUA KUUFIKIA MWEZI, WALA USIKU KUUPITA MCHANA. NA VYOTE VINAOGELEA KATIKA NJIA ZAO”. [36:40]

 

Na kama alivyo sema: “...HUONI TAFAUTI YOYOTE KATIKA UUMBAJI WA MWINGI WA REHEMA...” [67:03]

 

Yaani: Huwezi kuona kitu katika uumbaji wa Mwingi wa rehema, mgongano wowote wala mapungufu yoyote. Na mtu mwenye akili, ni yule anaye ufanya utaratibu/mpango kuwa ndio nembo yake katika matendo yake yote. Na huo utaratibu/mpango hauwi katika jambo lolote ila utalipamba na haukosekani katika jambo ila utalitia doa (kasoro). Na amesema kweli Allah Ataadhamiaye: “NA HAKUNA CHOCHOTE ILA ASILI YAKE INATOKANA NA SISI, WALA HATUKITEREMSHI ILA KWA KIPIMO MAALUMU”. [15:21]

 

             6.     Hakika sisi tunaishi katika zama ambazo mataifa hayashindani kwa wingi wa watu wake, wala kwa ukubwa wa eneo lake. Bali tumo na tunaishi ndani ya zama ambamo mataifa yanashindana kwa ugunduzi/uvumbuzi, wingi wa uzalishaji na maendeleo ya kielimu kwa sura na aina zake mbali mbali.

 

Ni maendeleo haya ndio yanayo wafanya wengine kukuhitajia wewe zaidi kuliko wewe unavyo wahitajia wao. Leo tunaona mataifa/nchi zenye idadi ndogo ya watu ukizilinganisha na nchi nyingine. Lakini nchi hizo pamoja na uchache wao zina nguvu kubwa ya kiuchumi na ni tajiri kuliko hizo nchi nyingine zenye idadi kubwa ya watu. Na hili linaonekana na kufahamika na kila mmoja wetu kiasi cha kutohitajia ushahidi.

 

             7.     Hakika katika jumla ya faida za sheria ya Uislamu, ni kwamba yale masuala/mambo ambayo maslahi yaliyomo ndani yake hayatofautiki (hayabadiliki) kwa utofauti wa zama, mazingira na mazingatio. Haya yametolewa hukumu kwa nassi (nukuu) yenye kutinda isiyo toa jukwaa ka Ijitihadi na maoni/rai. Hayo ni kama vile wajibu wa kujipamba na matukufu na kujiepusha na machafu/mabaya.

 

Ama yale mambo ambayo maslahi yaliyomo humo yanatii (yanafuata) mazingira na hali mbali mbali, haya hakika sheria ya Uislamu inaitegemeza hukumu yake kwa wadau wa uoni, Ijitihadi na ujuzi ambao hao ni wanazuoni walio bobea katika elimu na uchaMngu. Na miongoni mwa mambo hayo, ni kadhia ya uzazi wa mpango, kwani kadhia hii ni miongoni mwa mas-ala ambayo hutofautika (hubadilika) hukumu yake kulingana na utofauti wa kila kaya/familia, kila nchi na imkani zake. Kwa mfano ziko nchi ambazo zinahitajia ongezeko la watu, kwa kuwa njia zake za uzalishaji na maendeleo zinauhitajia wingi huu wenye nguvu, uzalishao. Nchi kama hizi huambiwa: Karibu kwa wingi huu, uaminio, wenye nguvu na akili. Hali kadhalika ziko nchi ambazo zisizo hitajia wingi wa watu, kwa sababu tayari zina idadi kubwa ya watu ambayo sehemu yake kubwa inaishi kwa kutegemea juhudi/nguvu za wachache. Na kwa sababu pamoja na wingi wake zinaagiza sehemu kubwa ya mahitaji yake kutoka nje. Nchi kama hizi, suala la uzazi wa mpango huwa kwao ni jambo linalo pendelewa na kutakiwa, likienda sanjari na njia nyingine zitakazo pelekea kwenye maendeleo yake. Njia hizo ni pamoja na kuongeza uzalishaji, kuendeleza kilimo, ufundi na mengineyo. Na wananchi wake wawe na hima ya kutekeleza wajibu wao kwa tija na ufanisi, huku wakimuogopa Allah Ataadhamiaye.

Kwa mara nyingine tena tunakariri: Kwamba idadi kubwa ya watu, walio wema, wazalishao, inakaribishwa. Ama idadi kubwa ya watu, walio dhaifu katika dini yao na maadili na katika utekelezaji wa majukumu yao kwa Mola Muumba wao na kwa nchi yao. Na wenye kutegemea sehemu kubwa ya mahitaji yao ya lazima kutoka kwa nchi nyingine, ile idadi ndogo ya watu ni bora kuliko idadi kubwa hii.

Additional information