KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

ALAMA ZA KIYAMA: WANACHUONI WATAKAPOITUMIA ELIMU YAO KUPATA MASLAHI YA KIDUNIA

 

Katika jumla ya mambo ambayo ni vitambulishi vya kukaribia kwa Kiyama kama yalivyo elezwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ni pale tutakapo waona au kuwasikia Wanachuoni wetu wakiitumia elimu waliyo tunukiwa na Allah kama nyenzo ya kupatia maslahi ya kidunia. Badala ya kuitumia elimu hiyo waliyo teuliwa wakapewa wao na wakanyimwa wenziwao katika kuwabainishia waja wa Allah makatazo na maamrisho ya Mola wao. Wao wanaitumia kama daraja la kuwavusha ili kuwafikisha kwenye ng’ambo ya matajiri na wenye madaraka/mamlaka miongoni mwa waja wa Allah. Na kwa kuwa kimaumbile mwanaadamu ni mtumwa wa ihsani, wanashindwa kuwakemea wahisani wao; matajiri na wenye mamlaka, pale wanapo potoka na kukengeuka. Wanachelea kuwabainishia haki ili wasije wakaizuia ihsani yao kwao, wakakosa maslahi duni ya kidunia wanayo yapata kutoka kwao.

 

 

Ni mara ngapi ama tumeona au kusikia Wanazuoni wetu, tena wale wanao tegemewa na umma, wakizitumia aya au hadithi tukufu, wakazipotoa tafsiri na maelezo yake ili tu kukidhi matakwa na matashi ya wafadhili wao?! Tena wanafanya hivyo kwa ujasiri mkubwa pasina kupepesa macho wala kuingiwa na khofu ya Allah Mwenye Qur-ani yake! Hapo ndipo walipo fikia Wanazuoni wetu leo ila wale wachache kabisa walio tunukiwa na Mola wao shahada ya juu ya uchaMngu, hao ndio walio salimika.

 

Na hivi ndivyo Mkweli Muaminifu anavyo ielezea hali ya Wanazuoni wetu hao walio wengi kama kitambulishi na kielelezo kinacho elezea kukaribia mno kwa Kiyama, tumpe sikio sikizi na moyo zingativu, anasema: “Pale itakapo fikia Wanazuoni wenu wanajifunza elimu ili wapatie kwayo Dinari na Dirhamu (Dola/Shilingi) zenu, nanyi mkaifanya Qur-ani kuwa ni biashara, (hapo tambueni ya kwamba Kiyama ki karibu mno)”. Dailamiy-Allah amrehemu.

 

Hapana wa kuukanusha wala kuukadhibisha utabiri huu wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ambaye karne kumi na tano zilizo pita, aliiona hali ya Wanazuoni wetu wa zama hizi. Kwa kuwepo leo na Wanazuoni wenye sifa hizo, utabiri wa Bwana unakuwa umekamilika na hivyo kuthibitisha kwamba yeye ni Mkweli na ni Muaminifu. Na kwa kutimia utabiri wake huo, umma leo hauna unacho kisubiri zaidi ya kujiwa ghafla na Kiyama na mwenye akili leo ni yule anaye fanya maandalizi ya kukutana na Mola wake akiwa ameridhiwa naye. Tafakari, chukua hatua sasa ili usalimike na kuokoka.

 

Haya sasa ni wakati wa kulihitimisha somo letu hili la leo, tumuelekee Mola wetu aliye Mwingi wa vipawa kwa kuinua mikono ya unyenyekevu na ndimi dhalili tumuombe katika fadhila zake. Tuombe:

 

رَبَّنَا ٱغۡفِرۡ لِي وَلِوَٰلِدَيَّ وَلِلۡمُؤۡمِنِينَ يَوۡمَ يَقُومُ ٱلۡحِسَابُ ٤١

 

Mola wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu”. Ibrahim [14]:41

 

Ewe Mola Muumba wetu! Ewe uliye mpa mwanaadamu macho mawili, ulimi na midomo miwili! Tunakuomba utujaalie kuwa waongofu na sababu ya kuongoka kwa wengine na wala usitujaalie kuwa wapotofu na sababu ya kuwapotoa wengine. Hakika Wewe unatutosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru. Yaa Allah tutakabalie duaa!

 

Aamina!

 

Jukwaa letu la leo linakomelea hapa huku tukitaraji kwa msaada wake Mola utakuwa tayari umesha zijua nyingi miongoni mwa Alama za Kiyama na kwamba kujua huko kumekukurubisha zaidi na matendo mema ili ukakutane vema na Mola wako Mwema ukiwa katika hali njema inayo ridhiwa na Mola.

 

Juma lijalo kwa uweza wake Allah tutaendelea kujifunza alama nyinginezo za Kiyama kama zilivyo elezwa na Yule Mkweli Muaminifu ambaye:

 

وَمَا يَنطِقُ عَنِ ٱلۡهَوَىٰٓ ٣ إِنۡ هُوَ إِلَّا وَحۡيٞ يُوحَىٰ ٤

 

Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya (ayatamkayo) ila ni ufunuo (wahyi) ulio funuliwa”. An-Najmi [53]:03-04

 

Allah ndiye Muwezeshaji Wetu Mkuu.

 

Wakati tukiendelea kumshukuru Mola wetu Mtukufu kwa kutuwezesha kukutana katika jukwaa letu juma hili na huku tukizidi kumuomba atukutanishe tena juma lijalo. Ndugu mwana jukwaa, hebu tuyatafakari kwa pamoja maneno haya matukufu ya Mola wetu Mtukufu yaliyo teremshwa kwa Mtume Mtukufu na kunukuliwa ndani ya kitabu kitukufu, haya tusome, tutafakari na tuzingatie pamoja ili nasi tuupate utukufu:

 

۞وَسَارِعُوٓاْ إِلَىٰ مَغۡفِرَةٖ مِّن رَّبِّكُمۡ وَجَنَّةٍ عَرۡضُهَا ٱلسَّمَٰوَٰتُ وَٱلۡأَرۡضُ أُعِدَّتۡ لِلۡمُتَّقِينَ ١٣٣ ٱلَّذِينَ يُنفِقُونَ فِي ٱلسَّرَّآءِ وَٱلضَّرَّآءِ وَٱلۡكَٰظِمِينَ ٱلۡغَيۡظَ وَٱلۡعَافِينَ عَنِ ٱلنَّاسِۗ وَٱللَّهُ يُحِبُّ ٱلۡمُحۡسِنِينَ ١٣٤

 

Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachaMngu. Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapo kuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu na wasamehevu kwa watu, na Allah huwapenda wafanyao wema”. Aali Imraan [03]:133-134

 


 


 


 


 


 

Additional information