KARIBU KATIKA MTANDAO WA UISLAMU

"Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliye umba, Amemuumba binaadamu kwa tone la damu, Soma! Na Mola wako Mlezi ni Karimu kushinda wote! Ambaye amefundisha kwa kalamu. Kamfundisha mtu aliyo kuwa hayajui...." 96:1-5

SUNNA ZA KULALA MUZDALIFA

Mahujaji watakapo fika Muzdalifah (na tayari umekwisha jua kwamba kulala hapo ni WAJIBU, kwa sura ya kuwepo hapo walau kwa dakika moja baada ya nusu ya usiku). Kumesuniwa kwao kuchunga mambo yafuatayo:

    i.            Kubakia hapo Muzdalifah mpaka adhana ya alfajiri, kiasi ambacho wataswali swala ya Sub-hi katika wakati wake wa mwanzo.

 

  ii.            Kuelekea Minaa baada ya kuchukua hapo Muzdalifah vijiwe vya kutupia vinara; vijiwe saba kila kimoja kiwe kikubwa kuliko harage. Imepokewa kutoka kwa Al-Fadhli Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia asubuhi ya siku ya kuchinja: “Niokotee vijiwe”. Anasema nikamuokotea vijiwe mithili ya vipande vya vigae. Nasaai & Al-Baihaqiy-Allah awarehemu.

 iii.            Kusimama Al-Mash-aril-Haraam” – nalo ni jabali dogo lililo mwisho wa Muzdalifah – watakapo fika hapo. Na waombe dua huko mpaka zama za jua kupiga umanjano pamoja na kukithirisha kusema: “RABBANAA AATINAA FID-DUNYAA HASANATAN WAFIL-AAKHIRATI HASANATAN, WAQINAA ‘ADHAABAN-NAAR”. Na hili ni kwa mujibu wa fumbulizo la kauli yake Allah: “...MTAJENI ALLAH PENYE MASH’ARIL-HARAM. NA MKUMBUKENI KAMA ALIVYO KUONGOENI, IJAPO KUWA ZAMANI MLIKUWA MIONGONI MWA WALIO POTEA”. [2:198] Kisha wataendelea na msafara kuelekea Minaa, nembo na alama yao ikiwa ni “talbiyah” na dhikri, kiasi kwamba wafike huko baada ya kuchomoza kwa jua.

 

SABA: SUNAH KATIKA KUMPIGA MAWE SHETANI.

 

         Kumesuniwa katika kukipopoa mawe kinara cha “Aqabah”, kuchunga adabu/taratibu zifuatazo:

    i.            Atakapo fika Minaa asianze kufanya cho chote kabla ya kupopoa kinara, kwani hayo ndio maamkizi ya Minaa katika siku hiyo.

  ii.            Akate talbiyah wakati atakapo anza kutupa mawe, kwani Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliendelea kuleta talbiyah mpaka anapo anza kutupa mawe, huzikata (huacha kuzileta) na badala yake huleta takbira.

 iii.            Apige takbira pamoja na mtupo wa kila kijiwe na atupe kwa kutumia mkono wake wa kulia ilhali akiuinua mpaka uonekane weupe wa kwapa zake. Ama mwanamke yeye asiunyanyue mkono wake.

Na kunasuniwa katika kuvitupia mawe vinara ndani ya masiku ya kuanika nyama, kufuata yafuatayo:

                         i.            Atupie vinara mawe pale jua litakapo pinduka na kabla ya kuswali Adhuhuri, ila kutakapo kuwa na msongamano mkubwa sana, hapo hakuna kizuizi cha kuakhirisha.

                        ii.            Asimame kwenye kinara cha kwanza na kile cha pili msimamo utakao muwezesha kuelekea Qiblah. Kisha ndipo avitupie mawe vinara, kimoja baada ya kingine kwa namna/mtindo ule ule tulio utaja katika kinara cha Aqabah.

                      iii.            Achepuke pembeni kidogo baada ya kutupa mawe kwa kiasi ambacho vijiwe vitupwavyo na watu wengine haviwezi kumpata. Kinara kiwe nyuma yake nae aelekee Qiblah na amuombe Allah kwa kila akitakacho yeye binafsi na ndugu zake. Na kunasuniwa kuirefusha dua kiasi cha mtu kusoma Suratil-Baqarah yote. Na atakapo fika katika kinara cha pili, afanye mithili ya haya na aombe dua baada ya kutupa mawe bila ya tofauti yo yote baina ya vinara viwili hivyo. Mpaka atakapo kifikia kinara cha Aqabah – nacho ndicho kile alicho tangulia kukipopoa katika siku ya kuchinja (mwezi 10). Na wala hataomba dua baada ya hapo na dalili/ushahidi wa yote haya ni utendaji wake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kama ilivyo sihi katika hadithi sahihi.

 

           ii.          Namna ya kufungukana na Hijjah:

         Umesha jifunza katika darasa zilizo tangulia kwamba kitendo cha kuingia katika ibada za Hijjah, kinamlazimisha muingiaji huyo (Haji) kuvaana na malazimiko maalumu. Na uharamu wa kuvaana kwake na baadhi ya matendo ambayo tayari tumetangulia kuyabainisha, kwa hivyo ni dhahiri kuwa unayakumbuka. Sasa je, ni lini Haji anafungukana na Hijjah pamoja na malazimu yake na hilo hufikiwaje?

Wakati wa kufungukana na Hijjah huanza baada ya kupita nusu ya usiku wa kuamkia siku ya kuchinja. Wakati ambapo Haji anakuwa kesha ondoka Arafah na akalala mlalo wa wajibu Muzdalifah na akaelekea hali ya kurejea Minaa. Hapo zitakuwa mbele yake zikimngojea amali tatu muhimu miongoni mwa amali za ibada ya Hijjah, ambazo ni:

1)        Kukipopoa mawe kinara cha Aqabah.

2)        Kunyoa na

3)        Kutufu.

Haji atakapo zitekeleza mbili miongoni mwa amali tatu hizi, hapo atakuwa amefungukana na Hijjah mfunguko wa kwanza. Na kwa mfunguko huu, kutamjuzia yeye kufanya mambo yote kumi yaliyo kuwa yamemuharimikia kwa sababu ya Ihramu. Ila wanawake; kwa kuingilia, kubashiriana na kufunga ndoa; yaani sasa anaweza kuvaa nguo zake za kawaida, kujitia manukato, kukata kucha na... na.... Na Haji atakapo itekeleza amali ya tatu miongoni mwa amali tatu hizo zilizo mlazimu, hapo sasa atakuwa amefungukana na Hijjah mfunguko kamili. Na mfunguko huu ndio utakao mjuzishia wanawake na vifuatizi/viandamizi vyake. Na dalili ya haya, imepokewa kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Mtakapo popoa vinara mawe na mkanyoa, basi kwa yakini yamekuhalalikieni manukato na kila kitu ila wanawake”. Ahmad & Abu Daawoud-Allah awarehemu.

Additional information